Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) katika kupambana na majangili, mwaka huu wa fedha wa 2013/2014 limepanga kununua ndege mbili za doria na magari 43, Bunge limeelezwa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki, ametoa taarifa hiyo kupitia hotuba yake ya bajeti aliyoisoma bungeni, jana.

 

Pamoja na ndege na magari, TANAPA itajenga nyumba 29 katika hifadhi tisa za Arusha, Katavi, Kilimanjaro, Mikumi, Mkomazi, Ruaha, Rubondo, Serengeti na Udzungwa; na kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 115.

 

“Aidha, ukarabati utafanyika katika barabara zenye jumla ya kilomita 6,526; viwanja 12 vya ndege na kilomita 41.6 za njia za kutembea kwa miguu katika hifadhi za Ruaha na Kilimanjaro. Ili kuboresha huduma katika hifadhi ya Mlima Kilimanjaro, Shirika litajenga mahema kwa ajili ya kulia chakula, vivuli vya kupumzikia na kuboresha malango ya kuingilia…Shirika litanunua excavator, low loader, low bowser, roller compactor, dumper truck, tractor, water bowser kwa ajili ya ujenzi wa barabara,” amesema Kagasheki.

 

Kwa upande wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Waziri Kagasheki alisema mwaka huu wa 2013/2014 itajenga jengo moja la familia sita za wafanyakazi pamoja na kuweka uzio kuzunguka nyumba za wafanyakazi eneo la Kamyn, jengo la mapokezi uwanja wa ndege Ndutu, jiko kwenye kambi ya kulala wageni ya Simba ‘A’ pamoja na nyumba moja ya askari eneo la Lositete.

 

Pia Mamlaka itaendelea na ujenzi wa jengo la kitega uchumi (kwa ubia) lenye ghorofa 10 mjini Arusha.

 

“Kuanzia mwaka 2013/2014, maeneo ya kihistoria na urithi wa kitamaduni ambayo yamo kwenye eneo la hifadhi ya Ngorongoro, yatasimamiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha uwepo wa uwiano wa viwango vya maeneo ambayo yametangazwa kuwa Urithi wa Dunia.

 

“Maeneo hayo ni pamoja na Oldupai, Laetoli, Ziwa Ndutu pamoja na maeneo mengine ya urithi wa utamaduni yaliyopo Ngorongoro. Hata hivyo, maeneo hayo yataendelea kusimamiwa kwa kutumia Sera na Sheria ya Mambo ya Kale.

 

“Mamlaka imepanga kununua mitambo miwili (grader na excavator) ya kutengeneza barabara, magari mawili kwa ajili ya kuimarisha doria, basi moja kwa ajili ya utalii wa ndani, gari moja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa, basi moja la wafanyakazi na gari moja kwa ajili ya kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli kwenye lango la Naabi.

 

“Mamlaka itaendelea kusaidia miradi ya maendeleo ya jamii kwa kujenga jengo kwa ajili ya kuhifadhi na kuchakata asali Endulen, kuendeleza mradi wa wenyeji waliohamishiwa Jema Oldonyosambu, kuchangia gharama za matibabu kwa ajili ya wenyeji Hospitali ya Endulen, pamoja na ujenzi wa majosho na kuboresha mifugo Ngairish,” amesema Kagasheki.

 

1095 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!