Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), limeanza kuwakera wateja wake jijini Dar es Salaama, hata baada ya uongozi wa wizara husika kutangaza kikomo cha tatizo la mgawo wa nishati hiyo.

Siku hizi imekuwa ni kawaida kwa Tanesco kukata umeme karibu kila siku katika maeneo mengi jijini Dar es Salaam, kitendo ambacho kinakwamisha na kuathiri shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

 

Tanesco mara nyingi imekuwa ikikata umeme kwa zaidi ya saa tano kwa siku na wakati mwingine bila kuwatangazia wananchi katizo la huduma hiyo. Matokeo yake wananchi wengi wameathirika kiuchumi kutokana na shughuli zao mbalimbali zinazotegemea nguvu ya umeme kukwama mara kwa mara.

 

Kero hii imeanza miezi kadhaa iliyopita, ambapo uongozi wa Tanesco umekuwa ukiwatangazia wananchi kuwa utakuwa unalazimika kukata umeme kwa saa kadhaa siku za Jumamosi na Jumapili kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu ya nishati hiyo, lakini kadiri siku zinavyozidi kusonga mbele utaratibu huo haufuatwi na badala yake huduma hiyo inakatwa ovyo Dar es Salaam.

 

Sisi JAMHURI kama mmoja wa waathirika wa tatizo hilo, kwa niaba ya wateja wengine tunaikumbusha Tanesco kutambua umuhimu wa kuwatazama wateja wake kama wafalme. Ihakikishe inawahudumia kwa kiwango kisichokwaza shughuli za uzalishaji mali.

 

Tunasema hivyo tukiamini kwamba kero hii ya kukata umeme ovyo inayozidi kuota mizizi jijini Dar es Salaama na labda kwingineko nchini inaweza kudhibitiwa kama uongozi wa Tanesco utajiimarisha kiutendaji.

 

Tena, Tanesco ikumbuke kwamba uongozi wa wizara husika umekwisha kuwatangazia Watanzania kwamba mgawo wa umeme hauna nafasi tena nchini na wateja wake wengi tunaikumbuka ahadi hiyo.

 

Ni vizuri uongozi wa Tanesco ukatambua kuwa wateja wake hawapendi kuona wanaendelea kupata karaha ya kukatiwa umeme ovyo katika kipindi hiki cha ugumu wa maisha unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na mfumko wa bei ghali za bidhaa mbalimbali usioendana na hali halisi ya kipato cha Watanzania wengi.

 

Tunaweza kuamini kuwa kasumba hii ya kukata umeme ovyo iliyoibuka siku za karibuni inawezekana ina mkono wa watumishi wachache wa Tanesco wanaoanza kulihujumu shirika hilo kwa maslahi yao binafsi.

 

Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ajitahidi kushughulikia mapungufu yanayojitokeza sasa ndani ya Tanesco na kusababisha usumbufu usiyo wa lazima kwa watumiaji wa umeme, kama alivyoahidi baada ya kukabidhiwa uongozi wa wizara hiyo.

 

Matumaini yetu ni kwamba viongozi husika watasikia kilio hiki na kuchukua hatua madhubuti kuwaondolea wateja wa Tanesco kero ya kukatiwa umeme ovyo na kukwaza juhudi zao za kujiletea maendeleo.

 

By Jamhuri