Hivi karibuni, niliposoma tangazo la Kampuni ya Umeme Tanzania (TANESCO) kwa umma likiomba ushauri kuhusu uboreshaji wa muundo na utendaji wake, nilishangaa kukuta kwamba Tanesco wanadhani watu bado wana hamu ya kualikwa kwa aina yoyote na Tanesco.

Watu sasa wanaonekana kukinaishwa na katakata ya umeme ya Tanesco kiasi kwamba hawana muda wa kutoa maoni yenye kichwa na miguu. Tazama tangazo hilo, kwa mfano, kwenye ukurasa 1 wa gazeti la JAMHURI la tarehe Oktoba 9-15, 2012. Hata ukiwa mvumilivu kiasi gani, utakuta unajiuliza kama shughuli za Tanesco zinatawaliwa na sheria yoyote, na kama ndiyo, basi sheria gani?

 

Matatizo ambayo yamesababishwa na Tanesco yanamgusa karibu kila mmoja, swali pekee likiwa kama ni kiasi gani. Mtu wa kawaida atakuwa anatembea barabarani, taa zikiwaka, mara anashtukia zimezimika, zinamtumbukiza katika giza nene na katika hatari ya kuvamiwa na vibaka na au kuanguka kwenye mashimo barabarani.

 

Mtu atakuwa nyumbani akiangalia runinga au anapiga pasi, au yuko chooni au anaendesha mafunzo ya ziada kwa watoto wake au anatayarisha makala yake  na kadhalika, na ghafla umeme utakatika na kuyatumbukiza pia maeneo yote ya jirani katika giza.

 

Eti si mgawo ni kukatikakatika kwa umeme kutokana na kubadilisha nguzo zilizozeeka. Mbona kuzeeka kunatabirika na Tanesco ni bingwa wa kutabiri! Mbona June 1, 2011, Mhandisi Mkuu wa Tanesco aliripotiwa kutabiri, “Mitambo hiyo itakamilika Mei au Juni, 2012….mgawo wa umeme utakuwa historia kwa shirika na wananchi”

 

Yale yale yatamkuta mtu kanisani au msikitini. Waumini watakuta hawawezi kusikiliza tena mahubiri au swala kutoka kwenye kipaza sauti kwa sababu umeme umesitika.

 

Katika maofisi, watu huogopa kuingia katika lifti, kutumia kompyuta au kutumia birika za kuchemshia maji. Pia, kuna swali la kuchaji simu za mkononi. Chaji inaweza kukuishia wakati hakuna umeme nyumbani au ofisini. Hayo ni mbali na yanayotokea kwenye ofisi za vinyozi, wachomeleaji, katika hospitali, mahakamani au gerezani. Wengine wana majenereta ambayo wakati mwingine yanaunguruma zaidi ya kiwango kinachoruhusiwa na sheria.

 

Katika tangazo nililorejea hapo juu, kwa nini Tanesco, wakati huo huo, hawakutoa muhtasari wa mafanikio na kutokufanikiwa angalau kwa kipindi chote kutoka tarehe ya kuanza kutumika Sheria ambayo inatawala maswali ya umeme, Na. 18 ya 2008.

 

Labda Tanesco ikumbushwe kwamba katika kifungu 4 (6) na (7) cha sheria hiyo, imetajwa mara tatu kwa kirefu kama “Tanzania Electric Supply Company”, ikiwa na maana kwamba, kabla ya Sheria hiyo kutumika, Tanesco ilikuwapo. Baada ya kutumika sheria hiyo, Tanesco imefanya kazi kuelekea miaka mitano. Sasa, linganisha kipindi hicho na kipindi cha miaka mitano ambayo ikiisha, Rais wa Tanzania anapaswa aondoke madarakani.

 

Sheria hiyo imeandikwa katika Kiingereza, lakini nitatumia uzoefu wangu kama wakili kwa miaka zaidi ya 30 kuitafsiri katika Kiswahili.

 

Sheria hiyo ilitungwa kwa madhumuni yafuatayo: kurahisisha, kuweka taratibu, kupitisha, kutoa na kutumia nguvu za umeme, kuendesha biashara katika umeme ambao unavuka mipaka ya Tanzania, kupanga na kuweka taratibu za kuweka umeme vijijini, na kuhusu kuandaa mambo mengine ambayo yanahusu hayo. Sasa, Tanesco kweli inaamini kwamba umma unaweza kutoa maoni ya kueleweka kuhusu muundo na utendaji wake hadi sasa?

 

Sheria hiyo inataka EWURA kusaidia kuanzisha viwango vya kufaa, vyenye kutegemewa, watu wanavyoweza kuvimudu, kukinga umeme dhidi ya hatari zitokanazo na shughuli za biashara ya umeme, kusimamia afya na usalama wa wafanyakazi katika mazingira ya shughuli za kutoa umeme.

 

Pia EWURA inapaswa kutangaza taarifa zenye kutolewa kwa vipindi kuhusu kutekelezwa wajibu wa leseni, ikiwa ni pamoja na bila kukomea, hali bora, kutegemewa, usalama wa kusambaza na maendeleo ya kuwekeza kwenye umeme, ufanisi wa utendaji na vigezo vingine vya kuhudumia wateja.

 

Vile vile, utoaji wa huduma unataka kwamba, hata ikiwa sheria  inaruhusu kusimamisha kwa muda utoaji wa umeme, kusimamisha huko kuwe kwa muda mfupi inavyowezekana, kuhusu wateja wachache inavyowezekana, na kupunguza kusimamishwa huko kabisa kuhusu wateja ambao sheria imewapa umuhimu wa kwanza.

 

Hawa wameainishwa kuwa ni wateja wenye leseni za shughuli za kusambaza umeme ambao, kwa sababu ya umuhimu wa shughuli zao, wamepewa kipaumbele na EWURA kupokea ugavi wakati mwenye leseni akisitisha kutoa umeme. Na mwenye leseni anatakiwa, nyakati zisizo za dharura, kutoa taarifa mapema ya kusimamisha utoaji wa umeme kulingana na kanuni zilizowekwa na EWURA.

 

Mwenye leseni anatakiwa, miongoni mwa mambo mengine, kutoa kwa usalama na uhakika kwa wateja wengine huduma ambazo zinatokana na shughuli za leseni yake. Analazimika kuajiri idadi ya kutosha ya wafanyakazi wenye sifa zinazostahili na kutimiza masharti ya leseni yake.

 

Pia, kulingana na kanuni zilizowekwa na EWURA, atawajibika kumfidia mteja ambaye anapata hasara ya mali au ya kuumia kimwili inayotokana na mwenye leseni  na kufikia kiasi cha kukata umeme bila halali; kusimamisha utoaji wa umeme bila halali; na utoaji hafifu.

 

Makosa ya jinai ambayo mtu hatakiwi kuyatenda yameainishwa katika vifungu 6(3) (Kazi za EWURA; 8 (5) (Wajibu wa kupata leseni) ; na 15 (8) (Habari na kutoa taarifa). Na katika kifungu 33 (Kutekeleza), EWURA imewezeshwa kuweka kanuni ambazo zinatoa adhabu kuhusu shughuli zikiwamo uzembe, uharibifu na udanganyifu.

 

Hasa kifungu 33(3) kinataja kwamba mtu ambaye kwa udanganyifu, atachomoa, atatumia au kufanyia kazi umeme, atachukuliwa kuwa ametenda wizi; na kwamba kuwapo kwa njia bandia ya kuchomoa umeme kutachukuliwa kuwa ushahidi wa kutosha hadi inakapothibitika vinginevyo, wa kitendo hicho.

 

Sheria ya ufafanuzi wa maneno inatamka kwamba neno “mtu” lina maana pia ya shirika la umma, kampuni, muungano wa watu bila kujali kuwapo kwa madaraka ya pamoja au la.

 

Kwa yote hayo, umma bila shaka, unatarajia kujulishwa na Tanesco kama katika kipindi kutoka mwaka wa sheria hiyo – 2008 hadi leo EWURA imetoa taarifa kwa vipindi kama Sheria ya Umeme inavyotaka; Tanesco imeajiri wafanyakazi wenye sifa zinazostahili; idadi ya watu waliofidiwa na Tanesco kutokana na kusimamishwa kwa huduma za umeme; utoaji mapema wa taarifa za kusimamisha huduma za umeme; makosa yaliyotendwa kinyume cha sheria ya umeme na kadhalika.

 

Taarifa iliyotolewa na Tanesco na kutangazwa katika ukurasa wa nane wa gazeti la Rai la June 20, 2002 ni mfano nzuri wa jinsi Tanesco inavyopaswa kutangaza matatizo yake na kuomba ushauri wa ufumbuzi. Taarifa ilitangazwa katika Kiswahili kwamba walilenga kukusanya madeni yapatayo shilingi bilioni 100 ambazo iliwadai wateja wake, na kuwa asilimia 30 ya wateja hawalipi madeni yao.

 

Ilitaarifu kuwapo kwa waliochezea mita, waliojiunganishia umeme, na vishoka ama mafundi bandia wa umeme. Iliutangazia umma madhumuni ya kudhibiti matumizi yao na iliomba ushirikiano wa umma. Ila, sijui kama zilikusanywa bilioni zote hizo.

 

Kwa kuwa tunazungumzia historia ya Tanesco, nitarejea kichwa cha habari katika Kiingereza kwenye ukurasa wa kwanza wa gazeti la The African la  Mei 28, 2003. Tafsiri yake, “Tanesco inatumia mafuta yenye sumu ya transfoma yaliyoharamishwa”. Tangazo jingine la Agosti 6, 2009, “Ikulu gizani siku 5. Makazi ya Waziri Mkuu Pinda, nayo kuonja adha hiyo. Ofisi ubalozi Afrika Kusini, Nigeria pia kuwa gizani. Ni baada ya kuharibika transfoma kituo cha Masaki.” Je, leo nchini, usalama wa transfoma ukoje?

 

Labda tuwaache Tanesco wanyooshe mambo yao na tujishughulishe na utata wa masharti ya kifungu 47 cha Sheria ya Umeme ambacho katika Kiingereza kinatamka, “No suit, prosecution or other proceeding shall lie against any officer performing in good faith any functions under this Act or purporting to be done in the implementation of this Act. Tafsiri yake: “Hakuna shitaka la madai, shitaka au uendeshaji shitaka mwingine utakaoletwa dhidi ya afisa yeyote katika utendaji kwa nia njema wa majukumu yake yoyote chini ya sheria hii au katika kumaanisha kutekeleza sheria hii.”

 

Utata unajitokeza kwamba neno “officer” (afisa) halijafafanuliwa na Sheria ya Umeme. Na hata hivyo, katika kifungu 9 (2) (e), sheria hiyo inazungumzia “employees” (wafanyakazi). Na katika kifungu 32 (2), sheria hiyo inahusu “authorized representative” (mwakilishi mwenye mamlaka). Kwa hiyo, je, ina maana kwamba “afisa” peke yake ndiye aliyepewa kinga na wala si “mfanyakazi” au “mwakilishi mwenye mamlaka?”

 

Kwa upande mwingine, neno “prosecution” (mashitaka) linahusu mashitaka ya jinai? Maneno, “in good faith” (kwa nia njema) yana maana kwamba kinga ipo hata kama ni kwa uzembe, maelezo yasiyo kweli, kinyume cha miiko ya weledi, na kadhalika? Ushauri ni kwamba yeyote anayetaka kuelewa na kuishitaki Tanesco atafute maelekezo kwa wakili.

 

Hitimisho ni kwamba ushauri wa umma kwa Tanesco labda uwe kwamba, kwa kuwa huu ni msimu wa kuunda tume, kwa mfano zilizochunguza vifo mikononi mwa polisi, Tume ya Maoni ya Katiba (ingawa hatujajulishwa idadi ya watu ambao wana nakala ya Katiba hiyo), timu ya elimu inayopendekezwa na kadhalika, basi Tanesco iunde tume ya wataalamu kuchunguza matatizo ya muundo na utendaji wake ili wapate ufumbuzi.

 

Matumaini yangu ni kwamba Tanesco itawapatia wataalamu hao, kila mmoja nakala iliyothibitishwa ya Sheria ya Umeme, No. 18 ya 2008.

 

Mwandishi wa makala haya, Novatus Rweyemamum ni Wakili Mwandamizi na anapatikana kwa Simu 0784 312623.

 

By Jamhuri