Muhongo pasportWafanyabiashara wakubwa duniani kote wamekuwa na kanuni moja ya kuwekeza katika nchi yenye miundombinu rafiki, ambayo itakuwa tija katika kusafirisha bidhaa zao kwa urahisi ili kufikia malendo yao.

Kufuatia kipaumbele hicho katika kukuza uchumi wa nchi yoyote duniani, nchi zote zimekuwa makini katika kuhakikisha zinapanua wigo wa kukuza uchumi na soko la ajira kupitia wawekezaji hawa kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwamo barabara, reli n.k.

Nchi yetu Tanzania pamoja na jirani zetu Uganda, sasa zipo katika hatua za kukamilisha mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi, ambao unatarajiwa kuanzia Ziwa Albert nchini Uganda (kupitia Masaka na Mutukula) na kuingia Tanzania kupitia Bukoba, Biharamulo, Shinyanga na hatimaye kufika bandari ya Tanga.

Kupitia mradi huo, zipo fursa nyingi zinazotarajiwa kujitokeza baada ya mradi huo kumalizika na hata kabla ya kumalizika, ikiwamo utoaji wa huduma za usafi za kudhibiti taka, kandarasi za kujenga na umeme, huduma za mawasiliano na mtandao, ujenzi wa barabara n.k.

Bomba hilo la kusafirisha mafuta lenye urefu wa kilomita 1,403 na kipenyo cha inchi 24, litakuwa na umhimu mkubwa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania hasa kuimarisha matumizi ya bandari ya Tanga na kuongeza mapato katika Serikali kupitia bandari hiyo. 

Katika kukamilisha, mradi huo unatarajiwa kutumia kiasi cha Sh. trilioni 11, pamoja ujenzi wa barabara mpya takribani kilometa 200 na uboreshaji wa barabara kilometa 150 na madaraja katika maeneo linapopita bomba la mafuta.

Hivyo, siku za hivi karibuni maafisa wa Uganda na Tanzania wamefanya mpango wa maendeleo wa mapendekezo wa kusafirisha mafuta hayo yasiyosafishwa (crude oil) kuja bandari ya Tanga. Imeelezwa pia kuwa yatafanyika maboresho ili kuleta tija katika kukamilisha mradi kikamilifu kwani kwa sasa inatunza mizigo tani 700,000 kwa mwaka.  

Taarifa iliyochapishwa katika gazeti la the Monitor la nchini Uganda la Aprili 29 mwaka huu, imebainisha kuwa kumekuwa na makubaliano yakiendelea kati ya nchi hizo mbili yanayolenga hatua mbalimbali za kutekelezwa ili kukamilisha mradi.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa endapo mradi huo utakamilika, utafungua mlango mpana wa maendeleo kwani itakuwa njia ya kuaminika zaidi katika kusafirisha mafuta hayo tofauti na njia nyingine ya usafirishaji na kuleta maendeleo kwa umma.

Kamishna wa Mamlaka ya Mapato nchini Uganda (URA), Dickson Kateshumbwa, kupitia gazeti la the Monitor anasema kuwa Wizara ya Biashara imefuatilia kwa makini bandari ya Tanga, ambayo imeonekana kama chaguo katika utekelezaji ujenzi wa mradi huo wakati Tanzania ilipokwenda katika Bodi ya Biashara nchini Uganda.

Anasema endapo mradi wa bomba utakamilika, kutakuwa na uwezekano mkubwa wa uwekezaji katika kufufua miundombinu ikiwamo reli pamoja na barabara ili kufanya marekebisho ya bomba kama ukiwa na matatizo katika mradi huo.

Afisa Mwandamizi wa Usafirishaji katika Wizara ya Kazi nchini Uganda, Herry Ategeka, anasema kuwa mwaka 2009 viongozi wa Uganda na Tanzania walisaini makubaliano ya kufufua miundombinu ya reli zilizopokuwapo, pamoja na kuendeleza bandari ya Tanga ambayo inahitaji upanuzi mkubwa.

“Katika kipindi cha miezi miwili hadi mitatu, tunapaswa kuwa na rasimu ya waraka kwa Baraza la Mawaziri na tunapaswa kuangalia kisha kuwa tayari kusonga mbele katika kutekeleza ujenzi mradi wa bomba,’’ anasema Ategeka. 

Lakini miongoni mwa sababu zilizofanya bomba hilo kuwa Tanzania badala ya Kenya, ni kwa bandari ya Tanga kuwa na kingo za asili ambazo ni adimu sana kuwapo katika bandari nyingi duniani.

Umuhimu wa kingo hizo ni kuzuia upepo kwani baadhi ya vipindi baharini kunakuwa na upepo mkali, hali inayosababisha meli kushindwa kupakia mzingo bandarini. 

Hivyo, inaonekana ni bora zaidi ikilinganishwa na bandari nyingine Afrika Mashariki kwa kuwa kingo ni za asili (naturally sheltered) na ina kina kirefu, na kufanya kupunguza muda na gharama za ujenzi kwa kuwa uchimbaji wa kuongeza kina hauhitajiki na itakuwa na uwezo wa kupakia mafuta katika kipindi cha mwaka mzima.  

Sanjari na hayo, kisiwa cha Pemba kilichopo upande wa mashariki mwa bandari ya Tanga ambayo inazuia mawimbi kutoka bahari kuu na kuipa Tanga uwezo wa kupata mafuta mengi pamoja na kuleta viashiria vingi vya uchocheaji wa uchumi.

Katika hatua nyingine, wataalamu kutoka nchini Uganda wamekubali na kuamini kuwa Tanzania ina uzoefu mkubwa katika ujenzi wa mabomba ya kusafirisha nishati mbalimbali kama walivyojenga bomba la mafuta kutoka Tanzania hadi Zambia (Tazama), bomba la kusafirisha gesi kutoka Songo Songo hadi Dar es Salaam pamoja na bomba kuu la gesi kutoka mkoani Mtwara hadi jijini Dar es Salaam. 

Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini nchini Uganda, Profesa Justin Ntalikwa, akizungumza na wafanyabiashara wakati wa kikao chake kilichofanya hivi karibuni, alieleza kuwa kabla ya makubaliano hayo, awali kulikuwa na makubaliano kati ya Uganda na Kenya juu kujenga bomba la mafuta, lakini gharama ndogo ya ujenzi kutoka Uganda hadi Tanga ndiyo  miongoni mwa sababu zilizofanya kukubali kujengwa katika bandari ya Tanga. 

Anasema njia zinazopita mradi huo hadi bandari ya Tanga ni bora zaidi kwa upande wa ujenzi wa bomba kwa kuwa haipiti sehemu yenye makazi ya watu wengi, sehemu za hifadhi na haina miinuko mikali; hivyo kupunguza muda wa ujenzi na gharama za ujenzi kwa kampuni. 

Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Tanzania (TNBO), Dkt. Gibeson Kaunda, alisema kuwa wafanyabiashara wamejipanga kikamilifu kunufaika na fursa zilizopo na zitakazojitokeza katika ujenzi wa mradi wa bomba ikiwamo kushindana katika zabuni zitakazotangazwa.

Bandari ya Tanga ni miongoni mwa bandari kongwe Afrika Mashariki baada ya kuanzishwa na wafanyabiashara wa Kireno mwaka 1500 na kuwa na manufaa kwa wafanyabiashara kwa kufanya shughuli za kusafirisha pembe za ndovu na kukuza mji wa Tanga.

Historia inabainisha kuwa mwaka 1960, aliyekuwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, na pamoja na Rais wa Uganda, Milton Obote, walitoa wazo kwa Uganda kukodisha bandari ya Tanga ili kuifanya bandari hiyo kuwa njia mbadala baada ya bandari ya Mombasa iliyopo nchini kenya. 

Hata hivyo, mpango huo ulikufa baada ya kuangushwa kwa Rais Obote mwaka 1971 na Idi Amin na hali hiyo ndiyo iliyosababisha mpango huo kutotekelezwa.

Kwenye mpango huo walikuwa wanatumia miundombinu ya Reli ya Kati katika kusafirisha mizigo kwa kutumia bandari ya Dar es Salaaam kupitia Dodoma, Tabora na hatimaye kufika bandari ya Mwanza katika mwambao wa Ziwa Victoria. 

Kutokana na orodha za kampuni zinazozalisha mafuta nchini Uganda ikiwamo kampuni ya Tullow kutoka Ireland, Total ya Ufaransa pamoja na kampuni ya CNOC kutoka China, hapo baadaye baada ya mafuta kufika katika bandari ya Tanga bila shaka mafuta hayo kuna uwezekano mkubwa wa kusafirishwa kwenda barani Ulaya kwa ajili masoko na kuongeza wigo wa uwekezaji hapa nchini. 

By Jamhuri