Kwa Watanzania wengi Tanzania ni nchi kubwa sana. Kwa Kaskazini inaanzia Ziwa Nyanza (Ziwa Victoria) ikipakana na Kenya na Uganda, na kushuka Kusini hadi Mto Ruvuma inapopakana na nchi ya Msumbiji.

Kwa mashariki inaanzia Ziwa Tanganyika ikipakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), na kuendelea Mashariki hadi inapokutana na Bahari ya Hindi na kufika kwenye visiwa vya Unguja na Pemba. Lakini kwa Watanzania wachache, Tanzania ni Dar es Salaam na Dar es Salaam ni Tanzania.

Kwanza, tuanze na jambo la msingi kabisa. Yapaswa kujiuliza nchi hii itapataje maendeleo iwapo watu wote muhimu watang’ang’ania Dar es Salaam pekee au kwenye miji mikubwa?

Tunafahamu kuwa kuna watumishi wengi wa umma ambao pindi wanapopewa uhamisho kwenda nje ya Dar es Salaam hufanya kila jitihada kuomba mwajiri abatilishe uamuzi huo na kuwaruhusu wabaki walipo kwa kuzusha visingizio vya kila aina, au wahamishiwe Kibaha tu.

Sehemu muhimu ya kuchochea maendeleo katika eneo lolote ni kuwapo mchanganyiko mzuri wa viongozi na wataalamu wazoefu kwa upande mmoja, na wananchi ambao wanahitaji huo utaalamu na uzoefu kwa upande mwingine.

Viongozi na wataalamu wana uzoefu ambao wananchi hawana, lakini ushirikiano kati yao na wananchi unaweza kuleta maendeleo na mabadiliko chanya.

Kwa bahati mbaya Tanzania ya sasa imekuwa ni nchi ya viongozi na wataalamu ambao wanapopelekwa maeneo ambayo hawayapendi (na mara nyingi huwa ni maeneo yaliyo nje ya miji mikubwa), basi hufanya kila jitihada kurudi kule yaliposheheni maendeleo, wakitarajia kuwa kule wanakokimbia atakuja mtu mwingine kuleta hayo maendeleo.

Na mara kwa mara hawa wanaoenda kushika hizo nafasi sehemu zenye maendeleo duni wanakuwa watu ambao hawana utaalamu au uzoefu wa kutosha wa kukabiliana na changamoto zilizopo.

Kubwa zaidi, uwepo wa watu wenye utaalamu na uzoefu miongoni mwa wananchi unasaidia kuleta mawazo mapya ya namna ya kukabili changamoto za kila siku zinazowakabili wananchi. Mtaalamu aliyetoka kwenye masomo hana huo uzoefu, na huyu ndiye pengine angeanzia kwenye maendeleo ya ahuweni akijifunza, na pale anapopata uzoefu awapishe wataalamu wasio na uzoefu ili nao waweze kujifunza na yeye kuhamia kule kwenye mahitaji makubwa zaidi ya taaluma na uzoefu.

Watu wasioishi mijini ingetosha tu kukimbiwa na walimu, wahandisi, wataalamu wa kilimo, wataalamu wa tiba, na kadhalika na kuwafanya wajisikie kama wageni kwenye nchi yao. Lakini hawa hawa hujikuta mara kwa mara wakilazimika kwenda mijini kufuata huduma muhimu. Zipo huduma nyingi ambazo Mtanzania akizihitaji atapaswa kufunga safari kutoka anaokoishi na kuzifuata Dar es Salaam au mji mwingine uliyo mbali naye.

Nitatoa mifano. Mwaka jana nilitaka kukamilisha usajili wangu kusomea shahada mojawapo ya chuo kikuu kimojawapo nchini. Waliopitia mpango huu wanafahamu kuwa maombi yote yanafanyika kupitia kwenye mtandao. Ukikwama wakati wa kujaza maombi zimetolewa namba za simu ambazo unaweza kupiga kupewa maelekezo.

Nilikwama mapema kwa sababu nina stashahada ya nje ya nchi ambayo haitambuliwi na mchakato wa maombi ya usajili. Nilipiga simu hizo kwa muda mrefu, lakini, ama hazikupokelewa, au hazikuwa hewani.

Bahati nzuri nilipata namba nyingine ya Kamisheni ya Vyuo Vikuu (TCU) ambayo nilipiga na kuunganishwa na mhusika. Nilimweleza tatizo langu. Akaniambia kuwa TCU bado haijakamilisha tathmini ya vyeti vya nje na kwa hiyo nilipaswa kupeleka shahada yangu ‘ofisini’ ili ihakikiwe. Nilimwambia kuwa mimi niko Musoma. Akanijibu: “Sasa mimi nifanyeje?” Ilikuwa ni kama vile ananieleza: “Nani kakutuma kuishi bara?”

Sifahamu kama watu wanaopanga taratibu mbovu kama hizi wanatambua kuwa safari kutoka baadhi ya sehemu za Tanzania ni zaidi ya kilomita 1,000 hadi Dar na inagharimu pesa. Hawa wanatoa majibu kama vile Watanzania wote milioni 45 wanaishi Dar. Naamini kuna makumi ya maelfu ya waombaji wa kusoma kwenye vyuo vikuu ambao hawako Dar. Kwanini haiwezekani kuwapo mwakilishi wa Kanda ili mimi niliye Butiama nisilazimike, mathalani, kusafiri hadi Dar kuhakiki cheti changu?

Ingetosha kusafiri hadi Mwanza tu, ingawa wakati mwingine hata Mwanza pia naona ni mbali. Hawa wahakiki wanaweza kuwapo kwenye kila wilaya na gharama zao kujumuishwa kwenye gharama ya maombi. Ongezeko la gharama hii haitazidi gharama za kusafiri kwenda Dar na itakuwa nafuu kubwa kwa muombaji.

Ni jukumu la Serikali kuhakikisha kuwa raia wake wote wanapata huduma kwa haki na usawa ule ule. Ningekuwa na muda (na pesa) ningefungua kesi mahakamani kudai kukiukwa kwa haki zangu za msingi kama raia ambaye anastahili kupata huduma ile ile ya umma kama raia anayeishi Dar es Salaam. Uhakika wa kushinda kesi haupo, lakini ujumbe ungekuwa umefika na labda yangepatikana mabadiliko.

Mfano mwingine unadhihirisha kuwa siyo Serikali pekee ambayo inaweka thamani ndogo kwa watu wasioishi mijini, bali hata kampuni binafsi nazo zina taratibu za aina hiyo. Katika kutatua matatizo yanayohusu matumizi ya simu kuna aina nyingi ya matatizo ambayo yanaweza kumalizwa kwenye simu, lakini baadhi ya watoa huduma za kampuni za simu watakwambia unapaswa kwenda kwenye ofisi zao ili kutatua shida fulani.

Watoa huduma wa Voda wanayo sentensi wanayopenda sana kutumia kumaliza tatizo: “Nenda Voda Shop.” Mimi kwenda Voda Shop iliyo karibu ni kilomita 80 (kwenda na kurudi). Mimi nilifikiri maana ya kuwa na simu ni kupunguza ulazima wa kufunga safari zisizo za lazima, ili kuongeza ufanisi katika kazi. Ukiniambia niende Voda Shop napoteza siku nzima ya kazi bila sababu ya msingi.

Nasema haya siyo kwa kukosoa tu bila sababu ila kwa kutoa hoja kuwa kuna baadhi ya taratibu zinapaswa kupitiwa upya ili kutoa huduma sawa kwa mteja wa Butiama kama ambavyo anafaidika mteja wa Dar. Na hili si tatizo la kampuni ya Voda pekee, lipo kwenye kampuni nyingi tu.

Teknolojia ina manufaa kama itatumiwa vizuri na ingerahisisha sana shughuli za utawala na biashara nchini ingawa bado ziko hitilafu za kurekebisha. La msingi ni kuwa Tanzania ni nchi kubwa na inahitaji mtazamo huo mpana kupanga mipango ya kuhudumia raia na wateja ili sote tujisikie kuwa tunaishi kwenye nchi moja.

By Jamhuri