Leo ni Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani. Tunawapongeza wafanyakazi wa Tanzania ambao, licha ya kufanya kazi katika mazingira magumu na kupata ujira mdogo, wameendelea kuwa wavumilivu.

Uvumilivu wao hautokani na woga, bali inawezekana ukawa unasababishwa na namna Watanzania walivyolelewa kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano.

Wafanyakazi wa Tanzania leo wanashiriki sherehe hizi wakiwa na malalamiko mengi, yanayotokana na kulipwa mishahara midogo isiyokidhi mahitaji yao ya msingi ya kibinadamu. Wapo wengi wanaopata mlo mmoja kwa siku, huku wakiwa hawana uhakika wa maisha yao ya baadaye.

Wakati maadhimisho haya yakifanyika nchini kote, sasa ni wakati mwafaka kwa wafanyakazi wote kuungana kupinga vitendo vya wizi, ubadhirifu wa mali za umma na kujilimbikizia mali kunakofanywa na baadhi ya Watanzania waliopewa dhamana ya uongozi.

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2010/2011, imeonyesha jinsi utajiri wa Tanzania unavyowanufaisha viongozi na wafanyabiashara wachache wasio waaminifu. Mali za umma zinauzwa bila huruma.

Utajiri wa nchi umehodhiwa na wageni na wazawa wachache. Tofauti kati ya masikini na tajiri inakua kwa kasi ya kustaajabisha. Huduma za kijamii kwa masikini zimedorora. Rushwa imeota mizizi katika idara zote za Serikali.

Misamaha ya kodi imefikia mabilioni ya shilingi huku Serikali ikitembeza bakuli kuomba misaada kutoka kwa wafadhili. Hii ni aibu kubwa.

Tanzania ina rasilimali ya madini, ardhi, mito, maziwa, bahari, milima, mabonde, ndege, wanyamapori na kila kitu kinachoweza kutumiwa na taifa lolote kujiletea maendeleo. Ni jambo la kushangaza kuona kuwa pamoja na ukwasi wote huo, Tanzania ndiyo nchi inayochechemea kwa umasikini, si Afrika tu, bali duniani.

Wafanyakazi wa Tanzania walianza kufanya kazi kwa moyo mmoja tangu tulipopata Uhuru mwaka 1961. Wamefanya kazi kwa uadilifu na kwa kujituma, lakini miaka kadhaa iliyopita moyo huo wa uzalendo umetoweka.

Baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wahujumu uchumi, wezi na wasiowajibika ipasavyo. Hali hii haikuja yenyewe tu. Imesababishwa na kuwaona viongozi wakuu wakiongoza kulihujumu taifa, kuiba mali za umma, kuendekeza uzembe na kutowajali wananchi wa hali ya chini.

Kama taifa, sote tunapaswa kuketi pamoja kuona ni kwa namna gani dosari hizi zinaweza kuepukwa, ili kuliwezesha taifa letu kusonga mbele kimaendeleo.

Pamoja na dosari zote zilizopo, bado tunaamini kuwa wafanyakazi wana wajibu wa kuchapa kazi kwa moyo mmoja. Uchapakazi wa aina hiyo unapaswa kuwapo serikalini, katika sekta binafsi na kwa mtu mmoja mmoja.

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kusema, “Kazi ni kipimo cha utu”. Hatuna budi kuienzi kauli hiyo kwa vitendo, hasa ikizingatiwa kuwa katika ulimwengu wa leo mtu asiyefanya kazi hawezi kuwa na maisha bora.

Serikali pia iboreshe masilahi ya watumishi wa umma kama njia murua ya kupambana na adui rushwa. Hongera wafanyakazi wa Tanzania.

By Jamhuri