Kwa siku za karibuni nchi yetu imegubikwa na mambo mengi ya kuudhi. Taifa linapokuwa na polisi wezi, waporaji na wauaji, usitarajie kwamba litaendelea kuwa salama. Taifa linapokuwa na majaji kama wale tulioambiwa na Mheshimiwa Tundu Lissu, hakika tumekwisha.

Inapotokea watu wamevunja sheria halali za nchi, wamekamatwa, lakini wakaachiwa kwa misingi ya woga wa Serikali, hakika hatuko salama. Labla nianze kwa kifo cha rafiki yeangu Daudi Mwangosi, aliyeuawa na polisi wasiokuwa na huruma.

 

Mimi ni mpigapicha, lakini nikiri kuwa yule mwenzetu aliyeweza kuinasa picha ya tukio lile la kupigwa, kuelekezewe mtutu wa bunduki tumboni hadi kuuawa kwa Mwangosi, anastahili tuzo kubwa. Ameisaidia jamii ya Watanzania na walimwengu kutopata shida ya kuwajua majahiri waliomuua mwanahabari huyu.

 

Picha ile inajieleza. Wanaonekana polisi waliokuwa na huruma ya kumwokoa Mwangosi, lakini pia inawaonyesha wale wenzao wavuta bangi walioamua kummaliza huyo ndugu yetu.

Wakati polisi wakianza kutumia mavazi haya ya “askari wa Kirumi”, niliandika makala nikisema kwamba huo ulikuwa uchuro wa hali ya juu.

 

Nilisema kwamba Tanzania, nchi ambayo haina rekodi za raia kupigana kwa risasi na polisi, haina sababu ya kuwa na polisi wenye mavazi ya kutisha kiasi hiki. Nikasema wazi kwamba kuwaona polisi waliovalia namna hiyo kwenye mikutano ya kisiasa ilikuwa ni kuwatisha wananchi. Mavazi haya yalianza kushamiri kuanzia mwaka 2005.

 

Tena ikumbukwe kuwa kuna kipengele katika Sheria za Uchaguzi kilichopinga polisi wenye bunduki zinazoonekana hadharani kuwapo kwenye mikutano ya vyama vya siasa. Polisi wenye silaha walitakiwa wawe mita kadhaa kutoka eneo la mkutano ili wakihitajika kupambana na wavunjifu wa amani, waweze kufika mara moja. Sheria au kanuni hiyo imeachwa, na sasa tunashuhudia polisi wakivaa ma-guo na vifaa vya kuwatisha wananchi.

 

Nikasema uchuro huu utawafanya wananchi wawe sugu. Kweli, miaka michache tangu mavazi haya yaanze kutumiwa na polisi wetu, tunashuhudia mauaji ya kipuuzi kabisa.

Utawala wowote unaojitahidi kutumia vitisho vya askari ili kuituliza hadhira, hata kama hakuna tishio baya kwa viongozi, utawala huo umepoteza uhalali.

 

Nimejaribu kuwatazama polisi wa Marekani katika mikutano ya Democratic na Republican. Huwezi kuona polisi wakiwa wamevaa kivita kama hawa wa kwetu. Ni wazi kwamba kama zana hizi za kivita wameletewa, lazima wazitumie! Matokeo yake ndiyo haya ya polisi wasio na maadili kuwaua masikini waandishi walioshika kamera tu.

 

Katika siku za karibuni kumeibuka utaratibu miongoni mwa wanafunzi wa kuandamana na kufunga barabara pindi magari yanapowagonga na kuwaua wenzao. Wanafunzi wa shule za msingi wamefanya hivyo mara nyingi katika jiji la Dar es Salaam kama shinikizo la kuwekewa matuta.

 

Kitu kinachoshangaza ni kwamba polisi wanapokwenda maeneo husika wamekuwa wakienda wakiwa wamevalia kana kwamba wanakwenda kupambana na waasi wenye silaha! Wanakwenda na magari na silaha za moto.

 

Fikiria, watoto wa shule ya msingi wanashikiwa mitutu! Hapo tunajenga kizazi cha aina gani? Mabomu ya machozi na bunduki kwa watoto za nini? Kuvaa kama wale askari tunaowaona kwenye sinema wakati wakimsulubu Yesu kunawapa funzo gani watoto hawa? Kwanini zisitumike njia za kisaikolojia kuwatuliza hawa watoto?

 

Wizi. juzi, tumewasikia polisi wengine katika Bandari ya Dar es Salaam wakiiba shaba! Mungu wangu, nchi inakwenda wapi? Lakini hii si mara ya kwanza. Nimepata kuandika katika gazeti hili habari ya kusikitisha na ya kutoa machozi juu ya polisi Mkoa wa Mara waliosimamia wizi wa mitambo na mali zote katika Mgodi wa Dhahabu wa Buhemba.

 

Polisi waliwaalika wezi kutoka hadi Kenya kwenda kuchukua magari, majenereta, mabati, vipuri, mitambo na kila kilichoonekana kinamfaa mwizi. Fikiria, polisi waliopewa dhima ya kulinda usalama wa raia na mali ndiyo wanaokuwa watafutaji wa wezi wa kwenda kuiba mali za umma. Hii ni dalili ya utawala kufikia tamati.

 

Haya yakiwa bado ya moto, juzi tumeshuhudia maandamano ya Waislamu wakienda Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kushinikiza wenzao waliokamatwa kwa kukaidi kuhesabiwa kwenye sensa, waachiwe huru. Kweli, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo akatoa tamko. Akawaamuru wakuu wa polisi wa mikoa yote nchini kuwaachia watuhumiwa hao kwa “dhamana”. Hii dhamana ni gelesha tu. Hapo hakuna kesi tena.

 

Ikumbukwe kuwa watu hao walikamatwa kwa sababu wamevunja sheria ya nchi inayotaka kila mtu ahesabiwe. Kufuata sheria hakuna hiari. Hawa wamevunja, wamekamatwa, na wameachiwa huru! Hii inakumbusja kesi moja ya Dibagula ambaye alihukumiwa na kufungwa kwa kuandika maneno kwenye baiskeli yake akisema, “Yesu si Mungu”.

 

Anasema hivyo wakati kuna watu wanakubali kusurubiwa hadi kufa kwa kuamini kuwa “Yesu ni Mungu”. Nguvu ya Waislamu ikashinda. Akaachiwa huru. Ndugu zangu Waislamu naomba wanielewe katika hili. Nalo ni kwamba imani hii tunayoona inaendelea kuwapo nchini mwetu ni kwa sababu Wakristo na wapagani  wameamua kuwa na busara ya kupuuza haya yote.

 

Lakini ikatokea siku moja wakaibuka kina “Ponda wakristo”, naamini huo ndiyo utakuwa mwisho wa Tanzania kuitwa kisiwa cha amani. Udini sasa ni balaa katika nchi yetu. Tumeanza kubaguana waziwazi. Tunatazama kwa namna ya uvaaji na ufugaji ndevu! Haya yameendekezwa na Serikali na sasa yameshakomaa. Anayesema kwamba Tanzania si nchi ya udini, anajidanganya.

 

Lakini tuyafanye haya tukitambua kuwa Tanzania ni ya Watanzania wote. Yakitokea machafuko, watakaopona ni wale wenye uwezo wa kuikimbia nchi. Masikini wengi watataabikia na kufia hapa hapa. Tuyaepuke haya kwa gharama zozote maana Watanzania tulishafikia hatua ya mkristo kuwa na marafiki walioshibana ambao ni waislamu; vivyo hivyo waislamu wamekuwa na marafiki wa kweli wakristo. Katika familia zetu wengine ni wakristo, wengine ni waislamu lakini tumekuwa tukiishi pamoja.

 

Kwa hali ilivyo sasa tunapaswa kuwa na mjadala wa kitaifa. Mjadala huu ujikite kwa kila dini na kila kabila kuheshimu utawala wa sheria. Kama leo waislamu wameweza kufanikiwa kuwatoa wenzao rumande kwa shinikizo, kesho wakristo nao wakiamua kuwatoa wenzao majambazi waliofungwa magerezani, nchi hii itabaki salama? Wapi tunaipeleka? Haya yote tunayoyana ni matokeo ya kufa kwa maadili katika nchi yetu. Ni matokeo ya kutoweka kwa upendo. Ni matunda ya viongozi walioshindwa kutekeleza wajibu wao.

 

Nchi ya ufisadi na mafisadi, nchi ya wavunja sheria, nchi ya polisi wezi na wauaji, nchi ya ajali za barabarani zisizokoma, nchi ya rushwa, nchi yenye kukaribisha majizi kwa jina uwekezaji, nchi ya kila mmoja kufanya analojisikia kulifanya, nchi yenye viongozi wanaojifanya hawaoni wala kusikia kero zinazoliyumbisha taifa, nchi ya wakubwa kuwaumiza wadogo, nchi yenye viongozi wanaoacha mambo yajimalize yenyewe, nchi yenye kuwaza uchaguzi mmoja baada ya mwingine; nchi yenye watoto wa wakubwa wanaosoma ughaibuni ilhali makabwela wakiishia kwenye kata, nchi ambayo hospitali ya taifa haina mashine ya x-ray.

 

Nchi ambayo majangili yanatazamwa huku yakimaliza wanyamapori, nchi ambayo kila anayetaka anaingia porini kukata miti na kuchoma mkaa, nchi ambayo uvuvi unafanywa kwa mabomu na sumu, nchi ambayo viongozi wanapishana angani kama mbayuwayu wakishindana kusafiri ughaibuni, nchi ambayo daktari akidai malipo manono anapelekwa mahakamani, nchi ambayo mwalimu akitaka alipwe japo kidogo anachodai anashushwa cheo; hakika nchi ya aina hiyo inakuwa ni kama inakata roho! Mwisho wa nchi yenye sifa za aina hii ni mbaya. Tuwe na mjadala wa kitaifa kwa ajili yakuihami nchi yetu.

 

1041 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!