Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama nchini Kenya imeonesha mfano mzuri unaostahili kuigwa hapa Tanzania. Kamati hiyo imetangaza kusudia lake la kuwahoji wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama wa Kenya kuhusu tukio la ugaidi katika jengo la kitega uchumi, Westgate jijini Nairobi.

Kamati hiyo inatarajia kuwahoji viongozi wa vyombo hivyo kutokana na shutuma kwamba vilizembea kuzuia shambulio hilo lililotokea Jumamosi iliyopita na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 60 na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.

 

Hata hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Kenya inasema watu waliouawa katika tukio hilo ni 67. Lakini kundi la Al-Shabaab lenye mtandao wa kigaidi, lenye makao makuu yake nchini Somalia, lililokiri kuhusika moja kwa moja katika shambulio hilo limesema kwamba watu waliouawa ni 137.

 

Pamoja na tuhuma za kuzembea kiasi cha kushindwa kuzuia uvamizi huo wa kigaidi, vyombo vya ulinzi na usalama nchini Kenya vinashutumiwa kuwa vilisababisha kubomoka kwa jengo la Westgate wakati wa shughuli za uokoaji.

 

Hoja zinazotolewa na Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama nchini Kenya ni za msingi. Kwamba tukio la shambulio hilo la kigaidi limegubikwa na mazingira tata yanayodhihirisha ama udhaifu, au uzembe wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini humo.

 

Bunge la Kenya, kama chombo kinachowakilisha wananchi na kutetea maendeleo yao yanayojumuisha suala la usalama wa raia na mali zao, limeona haliwezi kukaa kimya bila kuhoji utendaji wa vyombo vya dola katika kuzuia na kukabili vitendo vya uhalifu, hasa tukio hilo la ugaidi. Pengine linataka kujua chanzo cha uzembe uliotokea na hatua thabiti ya kuchukua usijirudie katika siku za usoni.

 

Hatua hiyo ya Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama nchini Kenya ni mfano mzuri unaostahili kuigwa na Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Ninasema hivyo kwa sababu kumekuwapo na matukio mengi ya uhalifu yanayotokea hapa nchini katika mazingira tatanishi na yanayodhihirisha uzembe wa baadhi ya maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama. Pamoja na matatizo mengine, tumekuwa tukishuhudia na kuona jisnsi maofisa hao wanavyochelewa kufika maeneo ya matukio ya uhalifu.

 

Ufike wakati na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lijiimarishie ujasiri wa kuwahoji viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama Tanzania kuhusu udhaifu unaotokea miongoni mwa maofisa wa vyombo hivyo katika kuzuia na kukabili wahalifu wanaohatarisha usalama wa raia na mali zao.

 

Kamati hiyo haiwezi kukwepa lawama za kushindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo endapo vitendo vya uhalifu vitaendelea kutokea katika mazingira ya kutatanisha hapa Tanzania. Ni jukumu la kamati hiyo kusimama kidete kuhakikisha Watanzania wanaishi na mali zao katika mazingiza salama.

 

Pamoja na mambo mengine, Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama iwajibike kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayovikabili vyombo vya ulinzi na usalama ili kuviimarisha katika masuala ya kuzuia na kukabili vitendo vya uhalifu.

 

Juzi tumesikia taarifa za kikundi cha ugaidi cha Al-Shabaab kikitangaza kwamba kina mpango wa kushambulia pia Tanzania na Uganda. Taarifa hizo siyo za kubeza, hasa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ni jirani na Taifa la Kenya ambalo limeendelea kuandamwa na mashambulio ya kigaidi.

 

Lakini kwa upande mwingine, Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama haipaswi kusubiri matukio ya kigaidi yatokee hapa nchini ndipo ianze kutafuta uzembe uliotokea miongoni mwa vyombo vya ulinzi na usalama. Cha msingi ni kwamba kamati hiyo ijifunze kutokana na tukio la kigaidi huko Westgate Nairobi, Kenya, ianze kuchukua hatua za kubaini na kutafuta ufumbuzi thabiti wa upungufu uliopo ndani ya vyombo vya usalama.

 

Kuviacha vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kujitawala bila kuhojiwa hata pale vinapoonekana wazi kuzembea katika kudhibiti vitendo vya uhalifu ni kuweka rehani usalama wa raia na mali zao, kama si Taifa kwa jumla.

 

Hata hivyo, simaanishi kwamba Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama haijapata kuhoji uzembe katika vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini, la hasha. Ninachosisitiza ni umakini wa kamati hiyo katika kusimamia utendaji unaoridhisha ndani ya vyombo hivyo. Suala la usalama wa raia na Taifa lipewe kipaumbele cha kwanza.

 

Utaratibu wa Bunge kuhoji uzembe katika vyombo vya ulinzi na usalama utasaidia kuimarisha nguvu ya vyombo hivyo kwa manufaa ya Watanzania kwa jumla. Bunge la Kenya limeonesha njia, na huo ni mfano mzuri unaostahili kuigwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

996 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!