POLISI wa Uganda wameitaka Tanzania kuwa makini na kundi la ugaidi la Al-Shabaab kutoka Somalia, baada ya jeshi hilo kuwakamata watu wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya kigaidi.

Tukio hilo limekuja siku chache baada ya Kenya kujihami kwa Polisi wao kumuua kwa risasi mtuhumiwa wa ugaidi katika maeneo ya Bondeni mjini Mombasa.

“Tunataka Polisi Afrika Mashariki, majirani zetu Tanzania na Kenya kuwa makini na watu hawa hatari,” anasema Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Uganda, Kale Kayihura, mara baada ya operesheni iliyofanyika wiki iliyopita.

Kayihura anasema kwamba watu hao walikuwa wakipanga kutekeleza mashambulizi ya mabomu na walifanikiwa kuwakamata kunatokana na njama zao kufahamika mapema kabla ya tukio.

Bosi huyo wa Polisi anasema kwamba taarifa hizo zilitolewa na maofisa wa Ubalozi wa Marekani uliopo nchini Uganda, na mara moja wakaanza msako rasmi na kuwatia nguvuni watuhumiwa.

Kundi hilo linaelezwa kuwa limekwenda huko baada ya vikosi vya Uganda kupambana huko Somalia, katika mapambano ambayo wanausalama waliokuwa wakivisaidia vikosi maalum vya Marekani walimuua Hamed Godane, kiongozi mkuu wa Al-Shabaab katika shambulio la anga.

Kayihura alisema: “Al-Shabaab walipanga kutekeleza mashambulizi ndani ya Jiji la Kampala na katika miji mingine mwishoni mwa juma hili, lakini Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na washirika wake, tumezuia mashambulizi hayo na kubaini milipuko iliyopangwa kulipuliwa.”

“Tumewakamata baadhi ya watuhumiwa na wanahojiwa,” alisema Kayihura, bila ya kutoa maelezo ya kina kuhusiana na idadi ya watuhumiwa waliokamatwa ama malengo ya jeshi hilo katika operesheni hiyo.

Ubalozi wa Marekani umekuwa ukishirikiana na serikali kwa kutoa taarifa na maonyo kwa raia wa Marekani waishio nchini Uganda kubaki majumbani, pia waliwataka kuchukua tahadhari.

“Kwa kushirikiana na mamlaka za Uganda, na ukizingatia ya kuwa hali ya usalama imeimarishwa, tunaamini tishio la hivi sasa la Al-Shabaab litakabiliwa vilivyo,” Ubalozi ulieleza katika maelezo yake.

“Tubaki waangalifu kwani kuna uwezekano mkubwa wa kushambuliwa tena na Al-Shabaab,” alisisitiza na kuongeza: “Al-Shabaab wanaweza kujaribu kulipiza kisasi kwa mlipuko wa anga uliofanywa na Wamarekani uliosababisha kifo cha kamanda wa kikosi cha Al-Shabaab.

“Chukua tahadhari dhidi ya  uwezekano wa mashambulizi ya kigaidi yanayoweza kutokea ndani ya Uganda na Afrika Mashariki,” alisema Kayihura na kusisitiza: “Tumeonya Wamarekani kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya kisasi.”

Uganda ni mshirika mkuu wa AMISOM – Majeshi ya Umoja wa Afrika (AU) ya kupambana na Al-Shabaab ndani ya Somalia. Serikali ya Uganda ilisema ni furaha baada ya kifo cha Godane, na kifo hicho kimetoa utatuzi, utulivu kwa Marekani katika ngome yake.

Wakati wa Kombe la Dunia miaka minne iliyopita, waasi wa Al-Shabaab waliua watu 79 baada ya mabomu waliyoyatega kulipuka katika migahawa miwili jijini Kampala.

Kushambuliwa kwa Godane kulikuja baada ya vikosi vya Umoja wa Afrika (AU) na majeshi ya Serikali ya Somalia kuzindua Operesheni iliyofahamika kwa jina la “Operesheni Bahari ya Hindi,” lengo kuu likiwa ni kupoka ngome zote kuu za Al-Shabaab ambazo ni bandari ili kuua biashara yao ya usafirishaji wa mkaa, ambayo ni moja kati ya vyanzo vyao vikuu vya mapato.

Hasira za kundi la Al-Shabaab zinalipuka zaidi baada ya Polisi wa Kenya nao kuua, ambako Kamanda wa Polisi mjini Mombasa, Robert Kitur, alisema walifanya hivyo baada ya kupata taarifa za kiintelejensia. Mtuhumiwa huyo aliuawa lakini mwenzake alifanikiwa kutoroka.

“Walikuwa wawili. Tulipata taarifa za kiintelejensia juu ya uwepo wa wahalifu wa vitendo vya kigaidi hapa Mombasa. Walikuwa wawili lakini tulifanikiwa kumpata mmoja tu na hivyo tunaendelea kumsaka mmoja aliyetoroka,” anasema.

Kitur aliwaeleza waandishi wa habari kuwa baada ya msako katika nyumba ya watuhumiwa, Polisi walifanikiwa kupata mabomu mawili ya kurushwa kwa mkono. Watuhumiwa wanahusishwa na mauaji ya watalii ndani ya Mombasa.

Kwa mujibu wa Polisi, mtuhumiwa aliyetoroka inasemekana alijiunga na kikundi cha Al-Shabaab akiwa Somalia. Baada ya mafunzo yake alirejea Kenya kupanga na kutekeleza mashambulizi ya kigaidi.

Hata hivyo, wanafamilia wa watuhumiwa hao wamekanusha wawili hao kuhusika na matukio ya kigaidi. Wanasema watuhumiwa hao ni vijana wasio na hatia.

By Jamhuri