Mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom soka Tanzania Bara ulifikia tamati Alhamisi ya wiki iliyopita. Hatua hiyo inatoa nafasi kwa wachezaji na makocha wao kupata mapumziko mafupi, kabla ya kuendelea kwa mzunguko wa pili wa Ligi hiyo hapo Januari 25 mwakani.

Ni wakati wa timu kutumia muda huo kujifanyia tathmini na hatimaye kufanya marekebisho ya hapa na pale, kwa kuzingatia upungufu uliojitokeza katika mzunguko wa kwanza.   Marekebisho haya yataambatana na usajili wa wachezaji katika usajili wa dirisha dogo.

 

Tofauti na ilivyokuwa misimu mingine ya Ligi iliyopita, msimu huu kumekuwa na upinzani mkubwa. Hali hii inaonekana kuchangiwa na baadhi ya timu kuonesha  uwezo wa hali ya juu na hasa pale zilipokuwa zikicheza na vigogo wa soka nchini —   Simba, Yanga na hata Azam FC.

Katika miaka ya nyuma ilikuwa vigumu sana timu kupata ushindi dhidi ya Simba au Yanga pale zinapokuwa zikicheza katika viwanja vyake vya nyumbani na wakati mwingine hata ugenini.

Mwaka huu wapenzi wa soka wameshuhudia timu kama Mbeya City ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu, ikionesha kabumbu la aina yake na kuweza kupunguza kasi ya Simba, Yanga na Azam FC zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi hiyo.  Timu za Kagera Sugar, Coastal Union zimeonyesha ubora. Yanga inaongoza Ligi ikiwa na jumla ya pointi 28, ikifuatiwa na Azam FC na Mbeya City zenye pointi 27 kila moja, Azam inaongoza kwa idadi ya magoli ya kufunga. Wekundu wa Msimbazi Simba wanashikilia nafasi ya nne baada ya kujikusanyia pointi 24. Kagera Sugar iko nafasi ya tano ikiwa na pointi 20.

Timu zinazoshikilia nafasi nne za mkiani ni Mgambo, Prisons, Ashanti na Oljoro.

Kitu kingine ambacho kimeonekana ni ile hali ya wachezaji kutoka nchi za nje kuendelea kuongoza katika ufungaji wa magoli.

Kwa mfano, mshambuliaji wa Simba Amisi Tambwe kutoka Burundi anaogoza safu ya ufungaji kwa kufunga jumla ya mabao 10, Hamis Kiiza, raia wa Uganda anayeichezea Yanga ana mabao manane.

Hali hii inawapa changamoto wachezaji wa hapa nyumbani kufanya jitihada katika mzunguko ujao, ili kukamata usukani katika ufungaji wa mabao.

Historia inaonesha kuwa kwa kipindi cha misimu miwili mfululizo, wafungaji bora wamekuwa ni wachezaji ambao wamesajiliwa kutoka nje ya nchi.

Mbali na msimamo huo, mzunguko wa kwanza umeshuhudia baadhi ya matukio mbalimbali katika viwanja vya soka. Kwa mfano, vurugu za washabiki na uwezo mdogo uliooneshwa na baadhi ya waamuzi baada ya kuonekana dhahiri kuwa walishindwa kumudu baadhi ya mechi.

Pengine tukio la mzunguko huu ambalo lilivuma sana katika masikio ya wapenzi wengi wa soka, linaweza kuwa lile la washabiki wa Simba kung’oa viti katika Uwanja wa Taifa na kusababisha hasara, baada ya timu yao kutoa sare na Kagera Sugar ya Bukoba.

Kutokana na hali ya ushindani ilivyo, kila timu inaonekana kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya msimu ujao, ili kujiweka katika nafasi nzuri, ama ya kuchukua ubingwa  au kubakia katika Ligi Kuu.

Katika hatua hii kuna baadhi ya timu zimeanza kutangaza mipango yake. Kwa mfano, Azam FC tayari wameishamtema kocha wao, benchi la ufundi la Simba liko mguu nje mguu ndani kutokana na kile kinachosemwa kuwa limeshindwa  kutengeneza kikosi cha kufanya vizuri katika mzunguko wa kwanza.

Tathmini zote za mzunguko wa kwanza zinaonesha kuwa kuna timu ambazo zimeshindwa kutandaza soka safi kutokana na usajili mbovu.

Kwa mfano, kuna timu kama Ashanti United ambayo ilionesha dhahiri kuwa wachezaji wake na hasa safu ya mabeki kushindwa kumudu mechi nyingi kwa kuruhusu mabao mengi ya kufungwa.  Timu hiyo imeruhusu magoli 24 katika lango lake, ikifuatiwa na Mgambo ambayo imemaliza mzunguko huo kwa kufungwa jumla ya magoli 23. Timu hizo bado zina nafasi ya kufanya marekebisho na hasa pale zinapodhihirisha kuwa zimegundua upungufu wao.

 

Kwa mfano, Ashanti wameishasema kuwa watatumia muda huu wa mapumziko kuboresha kikosi chao. Mbeya City wamesema kuwa hawategemei kufanya usajili wowote bali kuimarisha kikosi chake. Kwa upande mwingine, timu zinahitaji kutumia muda huu vizuri kuliko kuendekeza malumbano na kufikiria kuwatimua makocha na kuvunja majopo ya ufundi. Tatizo hili limekuwa likitokea kwa timu kubwa na hasa zile zenye sera ya kuwa na wanachama.

Aidha, TFF kupitia kamati yake inayoshughulikia masuala ya Ligi, inahitaji kuufanyia kazi upungufu mdogo mdogo ambao umekuwa ukijitokeza katika mzunguko wa kwanza, bila kusahau lile la waamuzi ambao wameonesha kushindwa kumudu baadhi ya mechi.

Mashabiki nao wanatakiwa kuwa na subira pale wanapoona kuwa timu zao hazitendewi haki, kuliko kufikia hatua ya kujichukulia sheria mkononi, ambayo inaweza kuleta madhara makubwa na picha mbaya.


 

1194 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!