Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imesaini mkataba wa mwaka mmoja na kampuni ya usafirishaji ya African Fossils Ltd, ya hapa nchini, kusafirisha petroli yenye lita za ujazo milioni 18 kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkataba ambao gazeti la JAMHURI limeuona, unaonesha tayari lita za ujazo 1,000 zimeshasafirishwa kutoka katika Bandari ya Dar es Salaam kwenda DRC. Lita nyingine za ujazo 2,000 zinatarajiwa kusafirishwa katika kipindi cha mwezi mmoja ujao kuanzia sasa.

Makubaliano hayo yamefikiwa baada ya pande zote kuridhika na kuondolewa kwa vikwazo vilivyokuwa vikilalamikiwa na wafanyabiashara wa mafuta.

Akizungumza na JAMHURI kutoka Lusaka, Zambia, msemaji wa Tazara, Conrad Simuchile, amethibitisha kuwapo makubaliano ya kibiashara kati ya Tazara na kampuni ya African Fossils kutoka nchini Tanzania.

“Ni kweli Tazara imeingia makubaliano ya kusafirisha kiasi hicho cha mafuta, hiyo imetokea baada ya Mamlaka kuboresha na kuimarisha miundombinu yake,” anasema Simuchile.

Anasema Tazara katika mwaka huu wa fedha, inaboresha mazingira ya usafiri wa mizigo ili kuwavutia wateja wengi.

“Ikumbukwe kuwa kabla ya mkataba huu wa sasa tulikuwa na mkataba na Malawi wa kusafirisha lita za ujazo milioni 48 za mafuta ya taa,” anasema Simuchile.

Anasema kwa mwaka mmoja Tazara imeondoa vikwazo vingi vilivyokuwa vinapigiwa kelele na wafanyabiashara wanaotumia Reli ya Tazara.

“Changamoto zote zilizokuwa zikilalamikiwa na wateja wetu tumeziondoa, zoezi hilo (mpango huo) limekwenda sambamba na kuboresha miuondombinu yetu,” anasema Simuchile.

 Matarajio ya Tazara katika mwaka wa fedha utakaoishia Juni 30, mwakani ni kuhakikisha wanasafirisha tani 381,000 kutoka tani 130 walizosafirisha katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016.”

 Kama taasisi, tupo njiani kuhakikisha tunairudisha Tazara na kuanza kuaminika tena kutokana na kushindwa kufikia malengo katika mwaka wa fedha uliomalizika wa 2014/2015 tuliposafirisha lita za ujazo 87,680,” anasema Simuchile.

Simuchile anasema Tazara imejipanga kuzishawishi nchi zote zisizokuwa na bandari katika ukanda huu, kutumia reli yake kusafirisha mizigo kutoka na kwenda Bandari Dar es Salaam.

By Jamhuri