Siku za vituo vya runinga ambavyo havijajiunga na mfumo mpya wa dijitali nchini zinahesabika.

Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetangaza kuvinyang’anya leseni vituo hivyo ikiwa vitaendelea kukaidi agizo hilo la Serikali.

“Tumeviandikia barua vituo vya televisheni vya hapa nchini ambavyo havijajiunga kwenye dijitali kuvitaka vijiunge haraka, vinginevyo tutavinyang’anya leseni,” amesema Mhandisi wa Utangazaji wa TCRA, Andrew Kisaka.

 

Katika mahojiano na Jamhuri Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Kisaka amekiri kuwapo kwa vituo kadhaa vya runinga hapa nchini ambavyo havijajiunga na dijitali licha ya TCRA kuvitaka vifanye hivyo kabla ya Januari 1013.


Serikali kupitia TCRA iliwaahidi wananchi kwamba vituo vyote 14 vya runinga vilivyopo nchini vitajiunga na mfumo wa dijitali na vitakuwa vinarusha matangazo yake bure kwenye runinga zenye ving’amuzi.

 

Lakini hadi sasa zaidi ya nusu ya vituo hivyo havijaanza kutekeleza maelekezo ya Serikali ya kurusha matangazo yake bure hapa nchini.

 

Vituo vya runinga ambavyo vimeanza kutekeleza maelekezo hayo ya Serikali ni pamoja na TBC, ITV, Channel Ten, Star TV, EATV 5 na Sibuka.

 

Hata hivyo, Kisaka amesema TCRA ina taarifa kwamba vituo vya runinga vya Mlimani na Tumaini vinaelekea kukamilisha maandalizi ya kujiunga na dijitali.

 

Serikali ilizindua mabadiliko ya kutoka mfumo wa zamani wa anolojia kuingia mfumo mpya wa dijitali Desemba 31, mwaka jana.

1169 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!