Jakarta, Indonesia

Watu zaidi ya 380 wamethibitishwa kufa baada ya tsunami kusababisha tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa Richter 7.5, lililopiga mji wa Jakarta mwishoni mwa wiki.
Upepo mkali ulivuma kutoka Palu katika Kisiwa cha Sulewesi kwa mita tatu. Video inayoonekana kwenye mitandao ya kijamii inaonyesha jinsi watu walivyokuwa wakipiga kelele huku wakikimbia kwa hofu.
Baada ya mshtuko wa tetemeko hilo, maelfu walizimia majumbani mwao huku wengine wakielekea hospitalini, hotelini na kwenye maduka makubwa.
Jitihada za uokoaji zinaendelea ingawa zimepata changamoto ya umeme kukatika. Njia kuu ya Palu imefungwa kutokana na daraja kuu kuvunjika.

Miili mingi imepatikana ufukweni

Mamlaka ya maafa nchini Indonesia inasema watu 384 wamekufa ingawa idadi inategemewa kuongezeka na watu 540 wamejeruhiwa.
Miili mingi ilikutwa ufukweni kwa sababu ya tsunami, lakini idadi yake bado haijafahamika.
Msemaji wa Serikali, Sutopo Purwo Nugroho, ameliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa wakati onyo lilipotolewa, watu waliendelea na shughuli zao ufukweni na hawakuchukua tahadhari ya kukimbia mara moja, hivyo wakawa miongoni mwa wahanga.
Wengine waliokoka kwa kupanda miti ili kukimbia upepo mkali.

Tetemeko hili lilianza kwa kutangulia kwa tetemeko jingine dogo lililoua mtu mmoja na wengine 10 kujeruhiwa, wakiwa katika soko dogo la samaki huko Donggala.
Mjini Palu mamia ya watu walikuwa wanajiandaa kwa ajili ya tamasha lililokuwa linatarajiwa kuanza Ijumaa jioni.
hospitali kuu imeharibiwa na tetemeko la ardhi, hivyo watu wengi imewabidi kupata huduma wakiwa nje.

Palu na Donggala ni miji yenye makazi ya watu zaidi ya 600,000. Rais wa nchi hiyo, Joko Widodo, amesema makundi ya waokoaji yanaendelea kuelekea katika sehemu iliyopata janga ili kutoa msaada zaidi.
Uwanja wa Ndege wa Palu umefungwa kutokana na tsunami ingawa helikopta zitaendelea kufanya kazi. Jeshi la nchi hiyo litatuma ndege za jeshi kutoka mji mkuu wa Jakarta.
Mamlaka ya hali ya hewa ya Indonesia inalaumiwa kwa kuchelewa kutoa angalizo kwa sababu onyo kuhusu tsunami lilitolewa ndani ya saa moja kabla ya tsunami kupiga.
Inakumbukwa kuwa mwaka 2004 tsunami ilisababisha tetemeko la ardhi nchini Indonesia na watu zaidi ya laki mbili walifariki dunia.
Mwaka 2010 pia zaidi ya watu 282 waliuawa kutokana na tsunami iliyosababishwa na tetemeko la ardhi katika pwani ya Sumatra nchini Indonesia.

By Jamhuri