Rais Uhuru Kenyatta na Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson Ijumaa alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Monica Juma.

Tillerson alipongeza hatua ya rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani Raila Odinga ya kukutana na kufanya mazungumzo, miezi kadhaa baada ya uchaguzi wa urais kusababisha machafuko wakati upinzani ukidai kulikuwapo udanganyifu katika uchaguzi huo.

Rais Uhuru Kenyatta na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga walitangaza Ijumaa kwamba wameanzisha juhudi mpya za kuliunganisha taifa wakati vyama vyao hasimu vimekuwa vinaigawanya nchi kwa misingi ya kikabila.

Akihutubia waandishi wa habari mjini Nairobi, Tillerson alisema kuwa alizungumza na viongozi wa Kenya juu ya hatari zinazoikabili, “Kenya, Afrika na jumuiya ya kitmataifa.”

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Marekani ataenda kutoa heshima siku ya Jumamosi kwa watu waliokufa katika shambulizi la mabomu kwenye ubalozi wa zamani wa Marekani nchini Kenya na Tanzania lililouwa mamia ya watu.

Juma alisema kuwa Tillerson na Kenyatta walifanya mazungumzo ya pamoja mapema siku ya Ijumaa.

Tillerson yuko kwenye ziara ya wiki moja barani Afrika ambayo tayari imempeleka Ethiopia, Djibouti na Kenya. Anatarajiwa kuondoka Nairobi siku ya Jumatatu kuelekea Nigeria na Chad.

By Jamhuri