TPA: Bandari ya Mtwara ni fursa mpya kwa nchi za SADC

Katika makala hii tunakuletea maelezo kuhusu Bandari ya Mtwara, ambayo ni miongoni mwa bandari za Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambazo zipo kimkakati katika kuhudumia soko la nchi za SADC.  Bandari hii ya Mtwara inasimamia bandari ndogo ndogo za Lindi na Kilwa.

Kutokana na mikakati mbalimbali inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli ya kuboresha bandari hii na miundombinu ya barabara katika ukanda wa kusini mwa Tanzania, ni dhahiri kwamba Bandari ya Mtwara itakuwa lango kubwa la biashara si tu kwa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma bali pia kwa nchi za SADC, ikiwa ni pamoja na Msumbiji, Malawi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Bandari ya Mtwara ilijengwa mwaka 1950, ikiwa na uwezo wa kuhudumia tani 400,000 kwa mwaka na ina gati lenye urefu wa mita 385 likiwa na kina cha mita 9.5 (chart datum). Kulingana na aina ya meli zilizokuwa zikija Mtwara kipindi hicho, gati liliweza kutumika kuegesha meli tatu (3) kwa pamoja zenye urefu kati ya mita 70 hadi 100 kila moja. Hivi sasa, meli zinazokuja zina urefu kati ya mita 150 hadi 210 kila moja, ambazo huegeshwa moja tu kwa wakati mmoja na nyingine kusubiri.

Lango la kuingilia meli katika bandari hii lina upana wa mita 250 na kina cha mita 20. Meli zinazoruhusiwa kuingia bandarini ni zenye urefu wa mita 175. Hata hivyo kuna meli zenye urefu wa zaidi ya mita 175 zimeshaingia bandarini na kuhudumiwa.

Bandari ya Mtwara kwa kiasi kikubwa inategemea zaidi kuhudumia shehena ya zao la korosho linalolimwa zaidi katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Ruvuma na Wilaya ya Tunduru kupata mapato yake. Katika mwaka 2016/ 2017 bandari ilihudumia shehena ya korosho tani 216,000 na mapato yatokanayo na kuhudumia shehena hiyo yalikuwa ni Sh bilioni 20.266 sawa na asilimia 74 ya mapato kwa mwaka huo ya Sh bilioni 27.549.

Mapato yatokanayo na kuhudumia shehena ya korosho yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 20 kwa mwaka. Ongezeko hilo la mapato limechangiwa na ongezeko la shehena ya korosho inayozalishwa katika mikoa hiyo ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.

Katika kuhakikisha tija inaendelea kuongezeka kuhudumia shehena ya korosho kwa Bandari ya Mtwara mwaka 2017/ 2018, uongozi wa bandari kwa kushirikiana na wadau wake ulifanya maandalizi ya hali ya juu ambayo yalisaidia kufanikisha usafirishaji wa shehena ya korosho kutoka  katika bandari hiyo.

Mipango iliyofanikisha usafirishaji wa shehena hiyo ya korosho ni pamoja na kuhakikisha bandari inafanya kazi saa 24 na siku 7 kwa wiki (24/7) na kufanya vikao vya kufanya tathmini na kupanga utendaji wa shughuli za meli na shehena mara 3 kwa wiki kwa siku za Jumatatu, Jumatano na Ijumaa na kila mahitaji ya dharuraa yalipojitokeza.

Maandalizi mengine yaliyofanywa na bandari ni kuongeza eneo la kufanyia stuffing pamoja na eneo la kuhifadhia makasha. Pia bandari imeongeza eneo la kuegesha meli kutoka mita 285 hadi mita 385 ikilinganishwa na msimu uliopita.

 Aidha, maandalizi mengine yaliyochangia kuongeza tija ni uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo milango ya kupitishia shehena na maeneo ya ukaguzi (checkpoints) kwa lengo la kutumia mageti mawili kupunguza msongamano wa malori.

Hatua nyingine iliyochukuliwa ni ununuzi wa vifaa ili kuboresha utendaji kazi wa karakana, kuimarisha ulinzi na usalama, ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya hujuma kwa bandari na taifa kwa jumla. Pia kuboresha mawasiliano na wadau wa bandari na kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana wakati wote.

Ili kuhakikisha Bandari ya Mtwara inaendelea kufanya kazi kwa ufanisi na kwa mafanikio makubwa kwa ajili ya kuhudumia mikoa ya Kusini, mikoa ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na baadhi ya nchi za SADC, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa kupanua Bandari ya Mtwara kuwa ya kisasa zaidi.

Nia ni kuiwezesha kuhudumia shehena kubwa kwa kujenga gati namba 2. Gati hilo linalojengwa na Kampuni ya China Harbour Engineering, liliwekewa jiwe la msingi Machi 4, 2017 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Ujenzi wa gati hilo ambalo litakuwa na urefu wa mita 350 utakapokamilika utaongeza uwezo wa Bandari ya Mtwara katika kuhudumia shehena kubwa kama vile saruji kutoka Kiwanda cha Dangote, makasha na mafuta kwa kutumia meli kubwa zaidi. Pia kukamilika kwa ujenzi wa gati hilo kutafungua milango ya kiuchumi na hasa kwa nyakati hizi ambazo Tanzania ipo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Ujenzi huo ni moja ya hatua muhimu za Serikali ya Tanzania katika kuboresha na kuimarisha bandari zake nchini kwa kuzijengea uwezo wa kuhimili ushindani wa kibiashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Uboreshaji wa miundombinu ya barabara na reli utachochea matumizi ya Bandari ya Mtwara hususan kuongezeka kwa shehena itakayopita kwenye bandari hiyo. Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutafungua uchumi wa Ukanda wa Mtwara (Mtwara Corridor), hasa ukuaji wa viwanda ambavyo vitapata malighafi ya makaa ya mawe kutoka Mchuchuma kwa ajili ya uzalishaji wa umeme.

 Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara ndio unategemewa kuwa chachu ya uboreshaji na upanuzi wa Bandari ya Mtwara kwa kufungua milango kwa nchi za SADC za Malawi, Zambia, Msumbiji na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa shehena za madini.

Serikali kupitia TPA imedhamiria kuboresha Bandari ya Mtwara kunufaika na fursa kubwa zilizopo za kuhudumia shughuli za watafutaji wa mafuta/gesi, uzalishaji wa gesi asilia, bidhaa zitokanazo na gesi na bidhaa za viwanda vinavyojengwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Pia itahudumia mazao mbalimbali yapatikanayo mikoani humo na maeneo ya jirani pamoja na bidhaa za madini na viwanda mbalimbali katika Ukanda wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) na nchi jirani za Msumbiji, Malawi na Zambia na Kongo.

Endapo unahitaji taarifa ya aina yoyote kutoka TPA unaweza kutuma ujumbe au kupiga simu za bure za TPA kwa namba 0800110032 au 0800110047.