Bandari ni lango la biashara kitaifa na kimataifa, hivyo ni muhimu sana kufanya biashara katika bandari zenye usalama na mazingira rafiki na yanayovutia wateja. Kwa hiyo TPA ina wajibu wa kuhakikisha bandari zote nchini ni salama kwa wafanyakazi ili waweze kufanya kazi katika mazingira rafiki na salama kwa lengo la kufanya kazi kwa ufanisi. Pia TPA ina wajibu wa kuweka mazingira ya bandari kuwa rafiki na salama kwa wateja wanaokuja kuchukua mizigo au kusafirisha mizigo yao.

Katika utekelezaji wa shughuli zake za kupakia na kupakua mizigo melini na kuhifadhi shehena zinazosubiri ama kupakiwa au kusafirishwa nje ya Tanzania au kuchukuliwa na wenye shehena au mizigo husika, bandari za Tanzania ikiwemo Bandari Kuu ya Dar es Salaam zimejipanga vilivyo kukabiliana na majanga mbalimbali yakiwemo ya moto na uchafuzi wa mazingira.

Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kupitia idara yake ya zimamoto, usalama, afya na mazingira kwa kila bandari, imejipanga kikamilifu kuhakikisha, usalama, afya na mazingira ya nchi kavu na mazingira ya majini vinasimamiwa kikamilifu kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyowekwa.

Majukumu ya zimamoto, usalama, afya na mazingira kwenye bandari yanasimamiwa na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria namba 17 ya 2004 ya TPA. Sheria hii katika kipengele cha 12 (j), kinaitaka TPA kuhakikisha usalama wa mizigo na wafanyakazi wanafanya kazi katika mazingira salama na rafiki bandarini.

Pia kwa mujibu wa kipengele cha 12 (h), TPA ina wajibu wa kuyazuia au kukabiliana na majanga yoyote endapo yatatokea ndani ya maeneo ya bandari. Maeneo ambayo bandari inayasimamia ni yale yaliyo ndani ya mipaka ya bandari ambayo yapo katika nautical mile 12.

Pamoja na kufanya kazi kwa kufuata sheria za bandari, Idara ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira inafanya kazi kwa kufuata sheria za nchi. Sheria hizo ni pamoja na Sheria ya Mazingira ya mwaka 2004, Sheria ya OSHA ya mwaka 2003, Sheria ya Nguvu za Atomic ya mwaka 2002 na Sheria ya Merchant Shipping ya mwaka 2003.

Sheria nyingine ambazo idara hii inazifuata ni ya Industrial and Consumer Chemicals and Management Control ya mwaka 2003, pia inafanya kazi kwa kufuata sheria za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pamoja na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Kitengo cha Afya kilichopo bandarini.

Pamoja na sheria hizo za nchi, idara hii inafanya kazi kwa kufuata miongozo ya ndani ya nchi na ya kimataifa. Kwa shughuli za majini inafuata miongozo ya Shirika la Kimataifa la Bahari (IMO) ambalo ndilo linalotoa maelekezo na miongozo ya shughuli za majini ambayo bandari inazifuata.

Kwa mfano MARPOL 73/78 ni sheria inayotoa mwongozo wa kusimamia uchafuzi wa bahari ambayo TPA kama taasisi ni lazima isimamie na kutekeleza. Sheria nyingine ni SOLAS 78 ambayo inatoa mwongozo na usimamizi wa vyombo vinavyofanya kazi baharini.

Kwa kuwa bandari inahudumia mizigo mbalimbali ikiwemo mizigo hatarishi. kuna miongozo ya namna ya kushughulikia na kuihudumia mizigo hatarishi. Idara ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira ina wajibu wa kusimamia mizigo inayobainika kuwa ni hatarishi kwa wafanyakazi, kuhakikisha mazingira ya bandari ni salama kwa kusimamia miongozo ya bandari na masharti yanayoandamana na miongozo hiyo.

Mizigo hatarishi imegawanyika katika madaraja tisa. Miongozo inayosimamia mizigo hatarishi imetoa maelekezo kwa kila daraja namna ya kushughulikia au kuhudumia mizigo hiyo. Miongozo hiyo imetolewa ili kuhakikisha kuna usalama kwa wafanyakazi wetu na kulinda afya zao.

Katika utekelezaji wa sheria, miongozo na maelekezo ambayo yameainishwa, kazi za kila siku za idara ni pamoja na kuzuia majanga ya moto kuhakikisha hayatokei katika maeneo ya bandari. Kazi hiyo inafanyika kwa kufanya ukaguzi wa kiusalama wa kuzuia na inapotokea kuna moto bandarini au katika meli zilizopo bandarini, Idara ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira ina wajibu wa kuuzima.

Majukumu makubwa ya idara hii ni kuhakikisha wafanyakazi wanaingia salama kila siku bandarini na kutoka salama. Hilo linafanyika ili waendelee kufanya kazi wakiwa na afya njema katika mazingira salama kwa lengo la kuhakikisha kazi zinafanyika kwa ufanisi mkubwa ili kuongeza tija.

Pia idara ina wajibu wa kusimamia mizigo ambayo ni hatarishi kwa wafanyakazi kwa kuhakikisha mazingira ya bandari yapo salama kulingana na miongozo na maelekezo ya sheria zilizopo. Usimamizi huo unafanyika kwa kusimamia vihatarishi vinavyoweza kuwepo kwenye mizigo inayopita bandarini.

Mizigo hiyo ukaguliwa kwa kutumia vifaa maalumu ili kugundua kama kuna mzigo wowote hatarishi au una kemikali hatarishi. Endapo mizigo ya namna hiyo ikigundulika hutengwa katika sehemu maalumu ili kushughulikiwa inavyopaswa kwa kushirikiana na taasisi husika.

Wafanyakazi wa TPA wanapohudumia mizigo mbalimbali kulingana na miongozo wanatakiwa kuvaa vifaa vya kinga (PPE) kama vile reflector, helmet, overoll, masks, boots. Umuhimu wa kuvaa vifaa kinga ni kuhakikisha mazingira ya kufanyia kazi ni salama na rafiki.

Aidha, idara hii husimamia mazingira yote ya bandari upande wa nchi kavu na upande wa baharini. Kwa upande wa baharini kunaweza kukatokea uchafuzi kama vile kumwagika kwa mafuta, na hilo likitokea idara inajipanga ili kusafisha. Pia idara inasimamia mazingira ndani ya bandari kwa kushughulikia takataka bandarini.

Kwa kuwa TPA inajenga na kuboresha miundombinu katika bandari zake ili kuweza kutoa huduma bora kwa wateja wake, miradi yote huwa inafanyiwa tathmini ya kimazingira. Idara ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira hushiriki michakato yote na kutoa ushauri wa kitaalamu.

Kazi nyingine ya idara hii ni kuzuia ajali bandarini, kwani mfano Bandari ya Dar es Salaam eneo ambalo lina mitambo mikubwa kulingana na shughuli zake, kila siku kuna watu wapatao wafanyakazi na wateja zaidi ya 3,000 na vyombo vingi vya moto vinaingia na kutoka.

Katika hali kama hiyo ajali ni rahisi kutokea, kwa hiyo Idara ya Zimamoto, Usalama, Afya na Mazingira ina wajibu wa kutoa elimu, kuzuia ajali zisitokee na endapo zitatokea kuzishughulikia kwa kushirikiana na taasisi zingine.

TPA kwa kumjali mteja ina Kituo cha Huduma kwa Mteja ambacho kina simu ambazo mteja anaweza kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi (SMS) bure kuuliza swali lolote au kupata ufafanuzi juu ya meli na mizigo ya wateja bandarini kwa saa 24. Namba hizo ni 0800110032 au 0800110047.

By Jamhuri