Kampuni ya Trafigura PTE Ltd imeshinda zabuni ya kuleta mafuta hapa nchini mwezi Oktoba, kampuni hiyo imeshinda zabuni hiyo baada ya kushiriki kwa miaka minne bila mafanikio.

Zabuni hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 6,899,208, ilishindaniwa na makampuni manne, yakiwemo Addax Energy SA, Augusta Energy SA, Sahara Energy DMCC pamoja na washindi wa zabuni hiyo Trafigura PTE Ltd.

Zabuni hiyo iliyoko chini ya Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja nchini (PBPA), iliwataka wazabuni kushindana katika bei ya kuleta mafuta ya dizeli, petroli, mafuta ya ndege pamoja na mafuta ya taa.

Akizungumza na JAMHURI, muda mfupi baada ya zoezi hilo la zabuni kukamilika, mwenyekiti wa mchakato huo wa zabuni Ali Ahmed, anasema kumekuwa na tatizo la wazabuni wengi ambao wameshapita kwenye mchujo kutokujitokeza katika kuomba zabuni za uletaji mafuta hapa nchini.

“PBPA hutangaza vigezo, kamati maalum inachuja kwa kuangalia dhamana za walio omba zabuni husika, wale wanaokidhi vigezo wanakuwa ‘pre-qualified’ na hao ndio uhusishwa katika kuomba zabuni za kuleta mafuta chini ya mfumo wa uagizaji mafuta wa pamoja,” anasema Ahmed 

Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Uagizaji Mafuta Pamoja, Ali Ahmed, anasema kampuni ya Trafigura PTE Ltd, imeshinda baada ya kuonekana ina uwezo wa kuleta mafuta kwa bei ya chini zaidi kuliko kampuni nyingine zilizoomba zabuni hiyo.

Anasema, kampuni hiyo italeta mafuta yenye tani za ujazo wa 205,282 za dizeli, 122,029 za petroli, 27,697 za mafuta ya ndege (Jet A 1) na tani 3,750 za mafuta ya taa.

Akizungumzia utaratibu wa zabuni hizo, Kaimu Meneja Ugavi wa Wakala wa Uagizaji Mafuta Pamoja (PBPA), Raymond Lusekelo, alisema mchakato huo umepitia mchujo, ambapo kampuni 30, zilikidhi vigezo, lakini zabuni ilipotangazwa, kampuni nne ndizo zilizoomba.

Katika hatua nyingine, Lusekelo alisema wanatarajia kuanza uagizaji wa gesi ya LPG kwa pamoja kuanzia Oktoba, mwaka huu, baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kukamilisha utaratibu.

Mwakilishi wa Trafigura, Adam Elinewinga, anasema wanayo furaha kupata kazi hiyo kwa kuwa wamekuwa wakiiomba tangu 2012, bila mafanikio.

“Kwa kweli tumefurahi sana…baada ya kuomba kazi hii kwa miaka minne hatimaye tumepata. Katika safari hiyo tumejifunza kutokukata tamaa,” anasema Elinewinga.

Kampuni ya Sahara Energy imeibuka ikiwa ya pili katika mchakato wa zubuni hiyo nyuma ya Trafigura. Kampuni hiyo ilikumbwa na kashfa ya kuleta mafuta yaliyochanganyikana hapa nchini.

2038 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!