Makala iliyopita nilijaribu kujadili athari zinazoweza kutupata – tukiwa Taifa – kwa kuruhusu masuala ya kiimani kutawala sehemu zinazotoa huduma kwa jamii nzima. Bila hofu, nilitoa mfano wa Kituo cha Mafuta Victoria, na kituo chake dada kilichopo Barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam. Nilisema kwenye vituo hivyo wafanyakazi wanalazimika kuvaa sare zenye maneno ya kumtukuza Yesu.

Wakristo wanaamini kwamba Yesu ni Mungu! Imani hii haipo kwa Waislamu ambao kwao Yesu (Nabii Issa bin Mariam) ni nabii tu! Nikasema kwamba katika jamii inayotaka kuishi kwa umoja na mshikamano, suala hili la kiimani katika maeneo yanayotoa huduma kwa watu wa imani tofauti linaweza kutuletea matatizo.


Matatizo ninayoyaona hapa si yale ya mtu kuitangaza imani yake kama huyu mmiliki wa Victoria anavyomtangaza Yesu, bali shida kubwa inakuwa kwenye suala la ajira kwa watu wasioamini kama “Yesu ni Mungu”.


Kuwataka wafanyakazi wavae nguo zenye maandishi hayo kunawafanya wasiokuwa na imani hiyo kukosa nafasi ya ajira hapo kituoni. Kwa maneno mengine, kilichopo hapo ni kama vile mmiliki kasema, “Wanaoajiriwa hapa ni Wakristo tu”.


Lakini akapuuza ukweli kwamba huduma ya mafuta inatakiwa kwa Wakristo, Waislamu, Wahindu na wale wasioamini katika hizi dini za kimapokeo. Kusema kwangu maneno haya hakumaanishi kuwa najaribu kushusha hadhi ya Yesu kwa Wakristo, la hasha! Kama Mungu ni mmoja, naamini sisi hatuna sababu wala maudhui ya kutufanya tufarakanike.


Baada ya makala yangu hiyo nilipata simu na ujumbe mfupi wa maandishi kutoka kwa wasomaji wengi. Wapo waliofurahi. Wapo walionuna, na kwa kweli wapo waliodiriki kuniombea mabaya kwa sababu tu kwamba “mimi Mkristo nahamasisha kuuvuruga Ukristo.” Sidhani laana ya namna hii inaweza kumpata mtu kwa sababu tu anataka kuona jamii nzima ikiishi kwa amani ambako ni moja ya njia za kumpendezesha Mungu. Baadhi ya sms zilizoletwa kwangu zinasema:


*Habari ndugu yangu, nimesoma makala yako na nimekuelewa sana, hivyo tatizo pale Victoria ni uniform. Je, vipi Oilcom pale ukiwa mkristo hupati kazi, na ndiyo maana wameweka na misikiti kwenye vituo vyao, unasemaje kuhusu hilo?

…………


*Karibu Mwanza uone mkuu wa mkoa anapohalalisha Muislamu achinje na Mkristo akamatwe akichinja. Katiba iliyopo haijatamka ni nani ana uhalali wa kuchinja mnyama. Tumwelewe vipi huyu mkuu wa mkoa wa Mwanza. Aliyasema hayo Nyehunge, Sengerema mbele ya wananchi.


*Afadhali huyu ana sheli (kituo cha mafuta) na mafuta (?) yanaingia kwenye magari yetu. Je, huyu mwenye bidhaa zilizoandikwa Kiarabu na nembo za msikiti…Hizi bidhaa tunazinywa na kupikika hatujui maana ya maneno ya Kiarabu yaliyoandikwa. Je, zingekuwa zinatengenezwa na Wakristo wakaweka msalaba tu Waislamu wangetulia?


*Habari. Nimesoma makala yako ya “Jamhuri ya Waungwana” kuhusu Sare za Yesu. Inapendeza, lakini balansi upande wa pili kwa toleo lijalo kuna baadhi ya wamiliki wa petrol station wamejenga misikiti midogo katika hivyo vituo na stafu wao wote wanalazimishwa kuswali muda wa swala unapowakuta kazini. Ebu fuatilia hili kwanza uone, kisha utapata ‘tip’ ya baadhi ya viwanda na makampuni yanayojihusisha na udini kwa kujenga nyumba za ibada katika maeneo hayo.


*Uchambuzi wa makala yako naona umeegemea upande unaotaka. Mbona juisi ya embe na malta pamoja na Azam Cola zina alama ya msikiti? Na ukienda kwenye viwanda vyake kuna misikiti. Je, huo si udini? Je, anazalisha kwa ajili ya Waislamu wenzake au kwa Watanzania wote? Kwanini aweke nembo zinazoshabihiana na imani yake?


*Ujumbe wako ni mzuri. Unajaribu kutukumbusha kuhusu umoja, upendo, lakini kuna makampuni binafsi ili upate kazi lazima usilimu. Huo siyo udini? Kwa mfano, Bakhresa juisi zake kuna nembo ya msikiti na maneno yanayosema “Halal”. Nini maana yake? Ili upate kazi kwa Waarabu ya kufungua geti, kazi za ndani lazima usilimu. Huo siyo udini? Ndani ya viwanda kuna misikiti, ukikataa (kusali?) hakuna kazi. Kuvaa t-shirt yenye nembo ya kumsifu Yesu unakwazikaje? Kusilimishwa ili upate kazi si zaidi ya udini?


*Manyerere, hapo kwenye makala yako juu ya mmiliki wa Kituo cha Victoria kuwavalisha wafanyakazi wake nguo zinazomtangaza Yesu umepotoka. Ni vizuri ungefanya utafiti kabla ya kutuhumu.


*Sare za Yesu napongeza. Anahubiri Victoria. Maandiko yanasema enendeni ulimwenguni mkatangaze injili kwa watu wote. Misikiti vipaza sauti na sala alfajili-zile siyo kero? Hii mada siyo, inazaa maswali. Tafuta mada nyingine.


*Kaka habari, nimesoma makala yako kwenye gazeti la Jamhuri, naomba nikupe hongera kwa makala yako nzuri na yenye kujenga kwa mtu mwenye fikra. Endelea hivyo.


*Mmiliki wa kituo cha mafuta ni mtu binafsi. Hakuna tatizo. Umelikwepa tatizo. Tatizo la Tanzania ni Serikali kudanganya raia kwamba haina dini. Haiwezekani Serikali kutokuwa na dini.


*Manyerere, kwa hiyo una mpango wa kukwamisha injili? Hilo hutaliweza kamwe hata kama wafadhili wako ndiyo hao uliosema (Waislamu).


Ndugu zangu, ukisoma ujumbe huu unaona tuna tatizo kubwa sana la uelewa. Kwa maneno mengine, wanachosema baadhi ya wasomaji hapa ni kwamba endapo mmoja anafanya upuuzi, basi na wewe fanya! Au kwa maneno mengine ndiyo ule usemi wa, “Akimwaga ugali, wewe mwaga ugali”.  Misimamo ya aina hii inaliharibu Taifa letu.


Hapa kuna msomaji kazungumza Halal na misikiti kwenye juisi (sharbati) zinazotengenezwa na Azam. Maneno “halal” nimeyaona. Sijauona msikiti. Pengine nitafute aina nyingine ya juisi.


Neno “halal, hii si mara ya kwanza. Kote duniani ambako kuna jamii ya Waislamu, neno “halal” lipo. Ni neno la Kiarabu lenye maana ya “halali”. Waislamu mnyama anapochinjwa na muislamu mwenzao, nyama hiyo ni halali! Inapochinjwa na asiye muislamu, ni haramu.

 

Hiyo ni imani yao. Miaka yote Wakristo wamekula nyama iliyochinjwa na Waislamu. Hakuna aliyedhurika kiimani au kiafya kwa jambo hilo. Ukristo, kama ulivyo Uislamu, unafundisha kuvumiliana. Kwa hili la kuchinja, Wakristo wanapaswa kuwavumilia wenzao.

 

Kama ilivyokuwa kwenye siku ya upigaji kura (Jumapili) Wakristo wanapaswa kuwa wavumilivu kwa wenzao kama Waislamu walivyokubali siku za Ijumaa wawe kazini. Tukisema kila mmoja atendewe anavyotaka, hakutakuwapo siku ya kazi, maana kila mmoja-hata mpagani, ana siku yake!


Madai kwamba kuna misikiti katika vituo vya mafuta, sioni tatizo. Hata pale Victoria kuna kanisa. Tatizo ni kama wafanyakazi wanalazimishwa kuingia misikitini au kanisani.

 

Nihitimishe kwa kusema tuna tatizo la udini. Tunapaswa kupambana nalo hadi ushindi upatikane. Haya yaliyosemwa na baadhi ya wasomaji yanaashiria kuwapo kwa hisia za hatari katika jamii yetu. Bado naamini suala la kiimani kwenye maeneo yanayohudumia jamii yenye imani tofauti, halifai.

 

Ni kama kuwa na hoteli ambayo wachinja kuku, ng’ombe na mbuzi ni wakristo. Ni wazi kwamba kwa kufanya hivyo, hoteli hiyo itakuwa imetangazwa kuwa ni kwa wakristo pekee.

1531 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!