Wiki iliyopita nilizungumzia juu ya maana na sababu za kutaka mabadiliko. Hivi sasa Watanzania na hasa vijana wanataka sana mabadiliko na huku wakinukuu sehemu tu ya hotuba ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyoitoa kwa wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, mwaka 1995 mjini Dodoma.

Leo, nimeamua kuandika hotuba hiyo yote ya Mwalimu Nyerere kwa wajumbe wa mkutano ule. Nia ni kutaka tuangalie sababu za Mwalimu kutamka ‘MABADILIKO’ ni zipi. Na huyo tumtakaye anazo sifa za kuleta mabadiliko? Nanukuu.

“Rais amewaambieni na mimi nasisitiza. Nitamalizia hapo. Sitaki kuchukua muda wenu mrefu. Teuweni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya wananchi. (kofi) Acha matarajio yako wewe mpiga kura. Tupeni mgombea ambaye atakidhi matarajio ya Watanzania. Watanzania wanataka mabadiliko (kofi). Wasipoyaona, wasipoyapata ndani ya CCM, watayapata nje ya CCM.

Watanzania kuna mambo wanataka uongozi wa awamu ya tatu kuyafanya. Mengi tu. Mimi nitataja machache. Mengi tu. Lakini nitataja machache yatawatosheni. La kwanza. Nitataja manne. La kwanza, Watanzania wamechoka na rushwa (kofi).

“Wajumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu ya Taifa watakumbuka nimepigia kelele jambo la rushwa ningali mwenyekiti wao hapa hapa Dodoma. Nilipiga kelele kiasi kwamba, waziri mkuu wa wakati huo, alikwenda kwa rais. Alikuja kwako ndugu rais, kuja kutoa hati yake ya kujiuzulu. Sasa hivi hali ya rushwa ni mbaya zaidi nchini. Wasaidieni wananchi, kudili nayo.

Mgombea mtakayemteua lazima tumtetee; wote tumtetee (kofi). Lakini inatakiwa ukiulizwa swali, huyu atatusaidia kupiga rushwa vita? Jibu litoke ndani ya roho yako, hapana hapa tu (kinywani) kwamba; ndiyo anaweza (kofi), la kwanza.

La pili, nchi yetu maskini. Nchi yetu hii maskini. Wakulima wetu, wafanyakazi wetu maskini. Nchi hii bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi ambao wote ni watu maskini. Nchi hii haijawa ya matajiri. Chama hiki hakijawa chama cha matajiri (kofi). Tunataka tuendelee kushughulikia na umaskini wa watu wetu.

“Tushughulike kwa dhati na matatizo ya wananchi; ya uchumi wao, hali yao ya uchumi; hali yao ya viwandani; hali yao ya mashambani; hali yao ya shuleni; hali yao ya hospitalini. Tunataka kuwa na hakika kwamba mtatuteulia mtu ambaye ukiulizwa swali: huyu anajua kwamba nchi hii bado ni nchi ya maskini, kwamba nchi hii bado ni nchi ya wakulima na wafanyakazi?  Anajua hivyo? Uweze kumjibu yule anayekuuliza kwamba kwa moyo wa dhati kwamba naam! huyu anatambua hivyo (kofi).

“Sasa hivi katika nchi yetu, la tatu, nataja la tatu. Watu wameanza kuzungumzia udini. Tulikuwa hatuzungumzii mambo ya udini udini katika nchi hii hata kidogo.

“Tulikuwa hatujali dini ya mtu. Anaijua mwenyewe dini yake, basi (kofi). Ilikuwa haiji katika akili yetu kwamba tunapompima mtu tumchague huyu tumfanye rais au tumfanye nani, tunauliza dini yake. Tunauliza dini yake. Hata kidogo. Tulikuwa hatuulizi hata kidogo. Dini inatuhusu nini sisi! (kofi).

“Zamani katika kuhesabu watu hapa Tanzania, katika kuhesabu watu wakati wa ukoloni; siku ya sensa swali lilikuwa linauliza dini ya mtu. Tukasema, sisi hatujengi misikiti; hatujengi makanisa; hatujengi mahekalu. Hili swali la udini wa mtu tunaliuliza kwa nini? (kofi).

“Linatuhusu nini! Tunataka kujua umri wa watu kwa sababu hilo lina maana. Tunataka kujua kama watu wanajua kusoma na kuandika hilo lina maana. Tunataka kuuliza mambo ambayo Serikali inayataka. Kama maimamu wanataka kuuliza, wanataka kujua wana Waislamu wangapi watafute wao. Sisi inatuhusu nini!

“Kama maaskofu wanataka kujua wana Wakristo wangapi watafute wao si wanakuja makanisani kuungama wawaulize (kofi). Sisi inatuhusu nini jambo la dini hata tuulize watu wewe dini yako nani, inatuhusu nini sisi? Hiyo ndiyo iliyokuwa Tanzania tunayojaribu kuijenga. Sasa watu wanazungumza udini udini bila haya, bila ya aibu. Wanajitapa kwa udini!

Tunataka mtuchagulie mgombea ambaye atatusaidia kuondoa mawazo haya ya kipumbavu katika nchi yetu (kofi). Na ukiulizwa na wananchi wa Tanzania kwa dhati, mnadhani mgombea huyu analiona hilo kwa uchungu kama mnavyoliona nyinyi. Useme ndiyo. Muweze kujibu kwa dhati kabisa kwamba ndiyo.

La mwisho. Nilisema nitataja manne. Nilikuwa New York mwaka jana. Yuko mwenzenu mmoja Gaterude Mongella sasa hivi ni Katibu wa akinamama kwa Mkutano wa akinamama utakaofanyika Beijing. Gaterude alinikaribisha chakula jioni katika flat yake hapo New York.

“Akakaribisha jamaa wengine nikaonana nao pale. Wakati tunakula, mama mmoja wa Kiganda ambaye anafanyakazi hapo, kanambia mzee mimi nilikuwa nafanya kazi katika Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Wakati nafanya kazi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, sisi watu wa Uganda tulikuwa tunajuana kwa makabila yetu.

Na tunatajana kwa makabila yetu. Watu wa Kenya walikuwa wanajuana kwa makabila yao. Huyu Mkikuyu, huyu Mjaluo, huyu Mluya. Na wanatajana kwa makabila yao. Watu wa Tanzania walikuwa kabisa kabisa hatujui makabila yao (mayowe). 

Nilimwambia yule mama ni wakati huo mama (vicheko). Nilimwambia ni wakati huo siyo sasa. Sasa Watanzania wanaanza kuulizana makabila. Wanafikiri jambo la maana sana kujua kabila la mtu. Mnataka kutambika? (mayowe). Maana faida faida ya makabila iliyobaki ni kutambika tu, basi. Lakini hasa ina maana gani nyingine, katika nchi ya watu wazima kabila lina maana gani.

“Tukifanya matambiko pale Butiama tunafanya. Mimi nipo karibu sana na chaka  letu ambapo mungu wa Butiama, wale wanakaa. Lakini kabila hasa Tanzania ya leo inazungumza kabila!

“Wazungu wale waliotutawala wana mataifa makubwa makubwa, yametawala dunia, leo wanaviona vitaifa vyao ni vidogo mno wanaungana. Waingereza na jeuri yao yote wametawala dunia. Wafaransa na jeuri yao yote wametawala dunia. Wajerumani na jeuri yao yote yameipiga Ulaya. Leo wanaungana kuwa taifa moja (kofi).

“Nyinyi Waswahili vinchi vidogo vidogo hivi vya watu 27 milioni mnazungumza makabila! Mnazungumza lugha ya makabila! Mtuingize katika karne ya 21, mnapanda basi la makabila! Lakini bado kuzungumza ukabila.

“Tunataka mtuchagulie mtu ambaye anajua kwamba huo ni upumbavu na ni hatari huko(mayowe) hatuwezi. Lugha ya ukabila hatuwezi kuzungumza.

“Wenzetu wanatushangaa. Wenzetu majirani. Sisi ndiyo tulikuwa mfano wao mbona wenzetu Tanzania hawazungumzi ukabila. Sisi tunazungumza ukabila. Mfano wao ulikuwa Tanzania. Tunataka kuwaiga majirani zetu katika hilo!

“Tunataka kusema Kenya wanazungumza makabila na sisi tuzungumze ukabila kwa nini? Tunasema Uganda wanazungumza makabila na sisi vilevile tuzungumze ukabila kwa nini? Tunasema Rwanda na Burundi wanazungumza  makabila na sisi tuzungumze  ukabila, tunasema hivyo kwa nini? Tunasema hivyo Watanzania! Bila haya! 

“Kabila si jambo la kuonea haya. Kabila linakuwa ni jambo leo tunaweza kusema katika basi, unajidai unajitapa ukabila! Tunataka mtuteulie kiongozi anayejua hivyo, atusaidie.

“Ndugu wananchi, ndugu mwenyekiti, mimi mliniomba nije kusaidia . Nilikubali kuja kusaidia. Kwa nini? Kwa sababu hiyo hiyo. Tunataka nchi yetu ipate kiongozi safi. Kiongozi safi hawezi kutoka nje ya CCM (kofi). Nyinyi wapiga kura mnaweza kutupatia kiongozi safi kwa kura zenu. Basi tupatieni kiongozi safi kwa kura zenu. Asanteni sana,” (kofi). Mwisho wa kunukuu.

Nashauri wakati tunataka mabadiliko tuzingatie hayo kama kweli Watanzania tunamuenzi Mwalimu Nyerere.

By Jamhuri