“Mohamed Said, katika ukurasa wa 273 wa kitabu chake kuhusu Uislam anaandika kuwa Aprili, mwaka 1964, ujumbe mkubwa ukiongozwa na Sheikh Hassan Bin Amir, ukijumuisha akina Sheikh Said Omar Abdallah, Tewa Saidi Tewa, Katibu wa EAMWS – Abdul Aziz Khaki na Mzee wa TANU, Mzee Mwinjuma Mwinyikambo walinzisha safari ya kuwasiliana na mataifa ya Kiislamu.

“Makisi Mbwana, Issa Mtambo, Omar Muhaj na Saleh Masasi walianza ziara ya kutembelea mataifa ya Kiislamu kutafuta misaada ya kifedha kwa ajili ya kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiislamu kwa nchi walizokuwa na uhusiano nazo… Hii ilikuwa hatua muhimu katika historia ay Uislamu nchini Tanganyika kwa karibu karne moja, ambapo Tanganyika ilikuwa na uhusiano na nchi za Ulaya na mashirika kadhaa ya Kimisionari. Kwa mara ya kwanza mwaka 1964, baada ya karibu miaka 100 ya ukoloni, nchi ilifungua milango kuwasiliana na dunia ya Waislamu…”

Hebu tujiulize ule utawala wa Waarabu (ukoloni wa Waarabu) tangu mwaka 1824 mpaka siku ya Mapinduzi matukufu kule Zanzibar haikuwa mawasiliano na dunia ya Kiislamu? Kule Kilwa tangu mwaka 957 masultani kibao walitawala, hiyo haikuwa mawasiliano na dunia ya Kiislamu?

Uhusiano ganizaidi ya huu? Dini ya Kiislamu Afrika Mashariki ilingiia tangu walipofika Waarabu. Ukristo uliingia tangu mwaka 1857 pale David Livingstone alipofika Zanzibar na 1868 huku Bara Kijiji cha Bagamoyo, pale Mapadre wa Roman Catholic walipotua Bagamoyo. Ukristo umeleta ustawi wa jamii ndiyo hayo mashule na vituo vya Afya. Wakati utawala wa Waarabu ulileta DINI YA UISLAMU bila kufikiria ustawi wa jamii kwa waliowatala – wabantu weusi wa Pwani.

Kuna wakati Sheikh Kichapiwa Liwale alibomoa shule kule Liwale na kuandika, nanukuu “Nchi hii ya Wamagingo ni ya Kiislamu, wazee wetu walikataa kabisa dini ya Kikristo wala kusikia kengele katika nchi hii”. Hivyo Liwale na Kilwa wakawa hawana shule ya elimu ya dunia. Kwa Mkoa wa Pwani RC mmoja hivi karibuni alipokuwa anahojiwa na Marin Hassan Marin wa TBC1 tarehe 27.02.2012 alijibu hivi, namnukuu…. “Mkoa wa Pwani wenye elimu ni 19.1% wengine wanajiita Al – Shabaab, Boko Haram na Al – Qaeda” (soma SUMU ya UDINI uk. 81 utayakuta mengi hata kwa mikoa ya Lindi na Mtwara). Hili suala la sumu ya elimu lilitikisa sana taifa letu.

Pale Profesa Kigoma Malima alipokuwa Waziri wa Elimu alidhamiria kufumua muundo wote wa elimu na kuujenga upya. Hapa niseme wazi historia hii mbaya ya elimu kwa Waislamu imeanza kurekebishika. Siku hizi baadhi ya wasomi na watu wakweli wasioyumbishwa na kile ninachokiita “FANATISM” ya uislamu wanasema hivi: “Nimekuwa nasikia sisi Waislamu hatupewi madaraka kwa wingi kama ilivyokuwa kwa wenzetu. Jamani, elimu ndiyo msingi wa madaraka. Hakuna kiongozi mwenye upeo akupe madaraka huku hujui kusoma na kuandika. Nilazima tusome elimu zote elimu dunia na ile ya akhera”. (Tazama gazeti la Nyakati la tarehe 25 Sept. – 1 Okt. 2011 uk 5). Hayo yalitamkwa na IGP mstaafu Alhaj Omar Mahita wakati anaweka jiwe la msingi Msikiti mpya BAITUL – MAAMUR – Mtaa wa Kilongo Morogoro.

Labda tukumbushane hapa kuwa katika Baraza la Idi katika Msikiti wa GADDAFI Dodoma tarehe 31.08.2011, mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (wakati huo) alitamka haya, namnukuu “Katika mkutano wangu tarehe 22 Julai, 2011 na Jukwaa la Wakristo suala hili lilijitokeza na nilitoa ufafanuzi ambao napenda nirudie kuuendeleza hapa leo.

“Baba wa Taifa na Rais wa Kwanza wa nchi yetu, Mwalimu Julius Nyerere aliamua kutaifisha shule zote za mashirika ya DINI na JUMUIYA ZA KIJAMIII hasa za Wahindi na Wazungu kwa lengo la kutoa fursa sawa ya kupata elimu kwa watoto wa DINI zote, wasiokuwa na dini, na wana rangi zote bila KUBAGULIWA.

“Kutokana na uamuzi ule hakuna mtoto atakayebaguliwa kupata ELIMU kwa sababu ya rangi yake au DINI YAKE hata wale waliotoka kwenye jamii ambazo DINI zao au rangi zao hawakuwa na shule kabisa au walikuwa nazo kidogo, waliweza kupata nafasi, bora tu wawe na sifa stahili hasa za kufaulu mitihani na nyinginezo.

“Lakini si hivyo tu, ili kujenga USAWA kwa upande wa Sekondari, Mwalimu alikwenda mbali Zaidi. Serikali iligawa sawia nafasi za kwenda Sekondari kwa Mikoa na Wilaya nchini, na siyo hivyo tu kufuata kigezo cha mtu kufaulu mtihani”. (Hotuba ya Rais Dodoma Baraza la Idd Tarehe 31.08.2011)

Nadhani sumu ile ya ELIMU ilimazika hapo. Waislamu na Wakristo wakaridhika, kwa kutegemea vigezo vya SIFA stahiki (proper qualifications). Vyeo pia vimekuwa vinatolewa bila kigezo cha dini ya mtu.

Nilipotoa makala yangu ile ya “UDINI SASA NONGWA”, mwaka 2013 basi kati ya SMS nyingi nilizopokea moja ilisomeka hivi:- “Mzee Mbenna unayafahamu haya? Tazama Rais Mwislamu, Makamu wa Rais Mwislamu, Jaji Mkuu Mwislam, Mkuu wa Usalama wa Taifa Mwislamu, IGP Mwislam, Waziri wa Ulinzi Mwislamu, wakuu wa mikao 19 kati ya 28 Waislamu, matajiri 9 kati ya 10 ni Waislamu. 78% ya wajumbe wa KAMATI KUU YA CCM ni Waislamu. 81% ya wajumbe wa TUME YA KATIBA MPYA ni Waislamu.

“Asilimia 66 ya wakuu wa Wilaya ni Waislamu. Wewe mzee unatetea nini katika makala yako au hujui hayo?” (SMS ya tarehe 19.03.2013 saa 15:0). Wasomaji wa makala zangu, hiyo ni moja ya kukosolewa nilikopata kutoka wasomaji. Basi kwa vile ninapokeaga SMS za kila aina nikajinyamazia.

Sumu ya UDINI na ya ELIMU sasa Taifa letu limevuka zimeshayeyushwa. Kwa sababu hii tungali na AMANI na UTULIVU hadi leo. Kweli bila neema za Mungu nchi hii ingesambaratika siku nyingi.

Sumu nyingine inayotunyemelea wakati huu ni Sumu ya Itikadi ya siasa. Sumu hii imeanza wakati ule wa Bunge la KATIBA. Hapo kulikuwa na mitazamo kinzani ndani ya BUNGE. Chama Tawala na Spika wao Mheshimiwa Samwel Sitta na vyama vya upinzani walitofautiana tafsiri ya kisheria katika Rasimu ile na namna ya kufikia KATIBA MWAFAKA YA TAIFA hili. Kamati ya Jaji Warioba ilishamaliza kazi yake sasa ilibaki Bunge la Katiba kutafuna rasimu ile yote na hatimaye sisi wananchi tumeze kwa kuipigia kura ya NDIYO/HAPANA.

Kutokana na mitazamo hiyo tofauti upinzani waliamua kuunganisha nguvu zao za vyama vyote na wakaja na kitu kinachojulikana leo hii kuwa ni “UKAWA”. Hiki siyo chama kilichoandikishwa kisheria kwa msajili wa vyama ila ni maelewamo ya vyama vinne (4) CHADEMA, CUF, NCCR – MAGEUZI na NLD. UKAWA kina nguvu na kina hoja za kutikisa Bunge.

Kuanzia hapo ukazuka utamaduni wa kususia vikao na kuondoka ndani ya Bunge kama njia ya kutaka sauti zao upinzani zisikike. Juzi juzi hapa wamegundua njia nyingine ya kufikisha ujumbe wao bungeni. Hii ni ile ya kuziba midomo yao kwa makaratasi ya gundi. Macho yanaona, masikio yanasikia lakini ni “bubu” hawaongei.

Ninaita hii ni sumu pia kwa maana ile ile ya kuwagawa watanzania kwa msimamo wa itikadi. Kuna angalizo katika maandiko matakatifu Mtume Paulo aliwaandikiwa Wagalatia hivi:- “Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana” (Gal. 5:15).

Mimi naogopa kuwa sasa Watanzania tuendako tunaelekea kuumana, tukishaumana tutakulana nahii maana yake tutaangamizana pia.

Hii maana yake nini? Itikadi ya siasa imeanza kule Pemba pale Wapemba wana CUF na wana CCM hawashirikiani. Wanashindwa kuzikana katika misiba katika kijiji kimoja. Huko kama si kuumana kutaitwaje hali hiyo? Baada ya uchaguzi wa tarehe 20 Machi 2016 kuna TALAKA zimetokea Unguja Kaskazini na Pemba. Hapo ni mfarakano mkubwa katika familia. Utafika wakati watu watachinjana!

Mwanza na Tanga hayo yameshatokea. Watanzania wamechinjana! Tunauana! Hili ni jambo la kutisha kweli kweli. Tumesikia wenzetu Kenya. Jimbo la Mandera Al Shabab wakiteka BUS, wanawabagua abiria, asiyejua Qur’an au kavaa msalaba basi yu Mkristo si mwenzao, anakula shaba papo hapo.

Nchini Misri sumu hii imeenea katika Chama cha Siasa kiitwacho “Moslim Brotherhood” chama cha Bwana Mohamed Morsi aliyewahi kuwa Rais wa kwanza wa kuchaguliwa baada ya utawala wa kijeshi (tangu enzi za Generali Neghibu 1952 aliyempindua Farao miaka ile) wa zaidi ya miaka 60.

Sasa chama kile (Moslim Brotherhood) kina siasa kali na ya ubaguzi. Kimeenea sana Misri, Syria mpaka Qatar. Itikadi yao na msimamo wa Serikali ya Generali Asisi wamepambana vikali sana na watu wameuawa. Siasa za kuumana, kulana na kuuana sasa zinanyemelea Tanzania.

Sisi tulianza kuona hali si ya kawaida pale Rais wetu (wakati huo) Jakaya Mrisho Kikwete alipokwenda kuzindua Bunge tarehe 18 Novemba 2010 pale Dodoma. Upinzani walitoka nje ya Bunge. Wakasusia hotuba ile ya ufunguzi. Hebu niwarejeshe wasomaji wangu kwenye maneno ya hekima aliyotoa Rais pale Bungeni, namnukuu.

“Mhe. Spika, sura ya tatu ya umoja wa nchi hii ni ile ya wananchi wetu kuwa wamoja, wanapendana, kushirikiana na kushikamana pamoja na changamoto za hapa na pale. Watanzania wameendelea kuwa watu wamoja. Wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, makabila, dini, maeneo wanayotoka na ufuasi wa vyama vya siasa.

“Kubaguana na kuchukiana kwa sababu ya tofauti zao hizo, ni mambo mageni kabisa kwao. Ninafurahi kwamba hata pale waliposhawishiwa, wengi wao walikataa na waliunga mkono kwa wingi sana juhudu za kutafuta suluhu,” (Taz. SUMU YA UDINI uk. 146). Hiyo hotuba sasa inapuuzwa hapa nchini.

Kama ITIKADI YA SIASA inaweza kufikia hatua ya kuandaa mahafali kwa vijana wasomi wa chama cha siasa hapo napo naona pana kasoro. Mahafali kwa mujibu wa kamusi ya Kiswahili Sanifu (uk. 148) maana yake “mkusanyiko mkubwa wa watu kwa ajili ya sherehe fulani”.

Sisi tumezoa kuona sherehe hizo za mahafali (kama graduation) zikilenga elimu yaani kilele cha kuhitimu watu katika chuo/shule na kutunukiwa hati maalum. Kwa maana hii itikadii ya siasa inapoandaa mahafali, tunajiuliza; “ni wahitimu wa nini hao?” kumbe kunaweza kutokea dhana ya U-SISI wa chama fulani.

Kwa mantiki hiyo huo “U-SISI” ni wazi dhana ya matabaka kujitofautisha na wengine wanaoitwa “WAO”. Ni hatari kifikra na ni chanzo kimojawapo cha mgawanyiko katika Taifa. Mgawanyiko ni utengano. 

 

>>ITAENDELEA>>

By Jamhuri