Watanzania, ni watu wa amani, ni watu tunaojaribu sana kuishi kindungu na tuwatulivu. Kwa maana hiyo, nchi yetu imejipatia sifa moja nzuri sana. Tanzania inaitwa kisiwa cha amani humu barani Afrika. 

Ulimwengu unakiri hilo na tunastahili kujivunia hali hiyo. Nchi nyingi wanatuonea gele kwa hilo. Madhari tunajitambulisha kuwa sisi ni Watanzania hapo chati ya heshima mbele ya mataifa mengine inapanda juu. Tujivunie hilo na tumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia utulivu na amani hivyo.  

Onyo lile katika maandiko, matakatifu lisemalo “…. kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke”, (1Wakorintho  10:12) linatuasa tuwe waangalifu (to be watchful) tusijazwe na kiburi cha sisi Taifa la amani, barani Afrika tubweteke – tutajaanguka vibaya. 

Vimetokea viashiria kadha katika taifa letu, tumekumbana na sumu kadhaa katika taifa letu ili mradi tuchukiane tuingie katika machafuko na amani ivunjike.  

Sumu zilizojitokeza dhahiri nchini mwetu na zimesababisha hali ya mitafaruku ya kutokupendana na nusura tusambaratike ni kama hizi 1. Udini 2. Ukabila 3. Elimu na4. Itikadi za siasa. 

Sumu hizo zote zimetokea miongoni mwetu kuanzia kabla ya Uhuru mpaka leo hii. Kila aina ya sumu hizo imekuwa na lengo la kutusambaratisha sisi kama watanzania. Shabaha kubwa tuchukiane, tubaguane na hatimaye tugombane nahata tuuane.

Hayo yote yametokea katika nchi mbalimbali barani Afrika na duniani kote na damu ya watu wasiokuwa na hatia imemwagika.Kila ziliposheheni sumu hizi basi amani imetoweka. 

Mataifa kadha hasa ya wale wakati wa Mwl. Nyerere Tanzania imesaidia kuwahifadhi na kuwapa fursa za mafunzo katika harakati za ukombozi wa nchi zao wanatuona sisi kama taa ya Uhuru wao na wanatamani kuiga umoja na mshikamano wetu.

Ingawa tuko makabila zaidi ya 123 hapa nchini lakini kamwe hatutofautiani kiutamaduni, mwonekano na tuna lugha moja katika utawala. Hilo linawashangaza watu wa mataifa mbalimbali barani Afrika nahata nje ya bara hili.Huwa wanatuuliza nyie watanzania mkoje? Mbona mnapatana namna hiyo?

Athari za sumu zimeonekana katika mataifa kadhaa barani Afrika. Mifano michache tu kuthibitisha hilo jaribu kusoma makala ya yule mwandishi wa kutoka LOME; TOGO (YAHAYA MSANGI) katika RAIA MWEMA Toleo No. 463 la Jumatano tarehe 22 Juni, 2016 uk. 18 

Mwandishi ametoa uzoefu wake huko nchi za Magharibi ya Bara letu. Kule kuna Udini na wananchi wake wanaishi katika vijiji au mikusanyiko vinavyojulikana kitaifa kama zongo. Humo wanaishi watu wa dini moja tu waislamu, siyo ukabila, siyo ukoo bali ni udini, imani ya kiroho. Mtu asiyehusika na imani hiyo kamwe hawezi kukubalika kuishi katika ZONGO.

Pili huko nchi za Afrika Magharibi, kuna ubaguzi wa ukabila, wengi wao wanapenda kuishi kadri ya lugha/kabila zao. Hili wakoloni walifurahishwa nalo, kwa sababu hiyo kule Nigeria Taifa lao   lina Serikali ya Shirikisho (Federal Government) na majimbo yao yaligawanywa kimakabila.

Hivyo Kaskazini kuna Wahausa wengi kuliko makabila mengine. Mashariki kuna Waibo, Kusini na Magharibi ni kwa wa Yoruba. Katikati ya Nigeria kuna wa Fulani na kadhalika.

Kwa misingi ya utawala wa machifu wa makabila yao linchi likubwa lile limewahi kupata taabu hata kukazuka vita vya wenyewe kwa wenyewe. Sisi tulijua kama vita vya Biafra kwa Kanali Ojukwu.

Kwa ubaguzi wa ukabila huko nchi za Magharibi baadhi ya Waghana wakati wa mapinduzi ya kijeshi 1966 yaliyomng’oa mwasisi wa Ghana Hayati Kwame Nkurumah, wananchi wengi  walikimbilia Nigeria kufuata makabila yao – kilugha, kumbe wao ni wakristo. 

Nigeria kuna ukabila na udini – Waghana wale hawakulijua hilo! Kuja kushutukia siku moja kwa ghafla tu Wanigeria wakawatimua wakimbizi wote wa Ghana eti warudi kwao Wanigeriawalikuwa na kauli mbiu “Ghanaians must go” basi maskini wakristo wa Ghana walifukuzwa bila msalie mtume.

Hapo udini ulitumika kubagua watu wa kabila moja.

Kule Ivory Coast, kule wana utamaduni au mapokeo kuwa kila mtawala mpya basi aingie na watu wake. Hivyo mtiririko wa eti utumishi wa Serikali (Civil Service) ubaki kuendeleza utawala haupo.Hakuna mapokeo namna hiyo.

Kila mtawala ataingia na utaratibu wake na watu wake. Kwa mantiki hiyo hakuna mfumo kiutawala hapo kunakuwa na ukabila au udini tu. 

Basi sumu hizo za udini, ukabila, itikadi, mpaka elimu zimeharibu amani na utulivu wa nchi kadhaa barani Afrika. Watanzania tungali tunakumbuka mauaji ya kimbari katika nchi za jirani tunaopakana nao kama Rwanda, Burundi, Congo DRC.

Ni matokeo ya sumu za udini, ukabila na itikadi ya siasa. Watu wa kabila fulani likitawala au wa dini fulani hapo wengine hutolewa bila kujali madaraka au kazi wafanyazo.

Kule Msumbiji, naamini wazee, tunakumbuka sumu za ukabila kati ya Frelimo na Renamo. Aidha Angola kumekuwepo na machafuko kati ya Augustino Neto, siku hizi yupo Rais Jose Eduardo dos Santos wa MPLA na Jonas Savimbi wa UNITA – ni ukabila na itikadi za siasa zimeleta ubaguzi katika nchi hizo. Machafuko yamedumu kwa muda mrefu sana huko. 

Hapa kwetu tumebahatika kabisa kuepukana na machafuko namna hiyo.Lakini chokochoko za sumu za udini, ukabila, elimu na sasa itikadi ya siasa zimekuwa zinajitokeza mara kwa mara.

Lengo kubwa la sumu ni hili la kuvunja umoja na utaifa wetu, Mataifa wanauliza kwa nini Watanzania washikamane namna hii? Watulie bila kuparaganyika?Waendelee kufaidi amani ya Uhuru wao? Hapana! Lazima watomaswe tomaswe hapa na pale hatimaye siku moja watalipuka na hapo ndio utakuwa mwisho wa amani wanayojivunia. 

Sumu inaua, inaweza kutumika kupitia chakula, kinywaji au kuchomwa kwa sindano au kuvuta hewa (gas poisoning) au kugongwa na nyoka.  Na sumu ikishaingia mwilini matokeo yake ni kifo tu! 

Basi kuna sumu ya maneno pia. Hii ndiyo inayozusha magomvi miungoni mwa wanadamu hata ikazua mapigano na kuuana. Sumu hili ya maneno ni mbaya kweli ikipakiwa vizuri inazaa chuki, husuda na kufikia mapigano. Ni sumu inayosambaratisha koo, makabila hata mataifa. 

Nieleze kidogo uzoefu wangu namna sumu hizi zilivyojaribu kuingizwa katika taifa letu hili. Ile sumu ya udini, hii ilianza tangu tunaanza harakati za Uhuru. Wapo akina Lipyoto walioibua dhana ya udini ili mradi tusambatatike na uhuru usipatikane au ucheleweshwe. 

Serikali ya Mwingireza iliweka maliwali waislamu ukanda wote wa Pwani. Huko bara kama Kagera walikuwepo watawala wa wakijadi 

“OMUKAMA” na wasaidizi wao “walangila”. 

Uchagani walikuwa na machifu wa jadi akina Mangi (Mangi Mkuu Thomas Mareale), Chifu Maruma, Chifu Petro Itosi; Iringa palikuwa na Chifu Mkwawa wa Wahehe, Songea kulikuwa na Nkosi Zullu, Nkosi Mbonane Tawete. Bambo Nkulungwa Mbinga na kule Nyasa mwambao wa ziwa alitawala Mzee  Chifu WabuMusa.

Kuanzia Tanga mpaka Mikindani ukanda wote wa Pwani palikuwa na maliwali wa asili ya kiarabu. Ugogoni kulikuwa na Chief Mazengo. Uluguru palikuwa na Chief Kunambi na Usukumani na Unyanyembe walikuwepo watemi wa jadi – akina Chifu Fundikira (Itetemia Tabora) Chifu Kidaha Makwaia Shinyanga. 

Serikali ya mkoloni iliamini Pwani yote wote ni wa dini moja nayo ni Uislamu. Ndiyo maana iliweka maliwali wa kiarabu. Hili lilileta msukosuko wakati wa kudai Uhuru na baada ya kupata Uhuru.

Dhana iliyokuwepo ni ile ya kila mswahili wa Pwani awe Mzaramo, Mndengereko, Mngindo, Mdigo. Mmaraba, Mzigua na kadhalika kuwa muumini wa uislamu. Dhana potofu hii imeleta sumu ya udini hapa Dar es Salaam.

Msomi mmoja alitumia maneno haya namnuku “…. one has to keep in mind that Muslims were a majority in Dar es Salaam and were in control of local politics. Very few Muslims had confidence in mission – educated christians” (Tazama Mohamed Said sura ile ya V uk. 115). Kwa tafsiri yangu ni hivi “ikumbukwe hapa kwamba waislamu ni wengi mjini Dar es Salaam na walikuwa katika siasa za hapa mjini, wachache sana waliwaamini wasomi wakristo”.

Ni jambo la hatari kwa msomi wa kiwango cha Chuo Kikuu kuwa mpotoshaji wa historia kwa ushabiki tu (mere fanatism). Katika kitabu chake (Mohamed Saidi) amethibitisha kuwa waislamu mjini Dar es Salaam waliogopa kuwa Uhuru ukifika wakati ule mwaka 1958 baada ya mkutano wa Tabora, waislamu hawangeambulia kitu katika viti vya ubunge kwa vigezo vile vya elimu.  

Basi aliandika haya, “some of these were people who did not rise up with the political movement. Sheikh Takadirii feared that once in power these mission educated Christians and newcomers in the struggle would strive to maintain the status quo having no obligation to lead the movement to its logical conclusion (Mohamed Said sura ya IX uk. 245). 

Kwa tafsiri yangu isiyokuwa rasmi maneno hayo yalisema, “baadhi ya watu hawa (ambao kwa hofu ya kiongozi wa Chama) Sheikh Takadiri alisema, hawakujishughulisha na harakati za chama, pindi utawala ukipatikana si ajabu wakristo wasomi wataingizwa kuongoza Serikali ingawa hawajashiriki katika hizi harakati za ukombozi”. 

Hofu kuwa waislamu hawangepata nafasi za uongozi Serikalini ilienea miongoni mwa wakazi wa hapa Dar es Salaam. 

By Jamhuri