Juma lililopita, Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe,  alimwomba Rais Jakaya Kikwete auridhie Muswada wa Marekebisho ya Mabadiliko ya Sheria ya Katiba, kwa lengo la kuepusha vurugu nchini.

Akizungumuza jijni Dar es Salaam, Waziri Chikawe alidai kuwa kelele zinazopigwa na wapinzani kumtaka Rais Kikwete asisaini muswada huo, hazina maana kwa kuwa muswada huo ulipitishwa baada ya taratibu zote kukamilika.

 

Waziri Chikawe aliendelea kusema kwamba kutokana na hali hiyo ya muswada huo kupitishwa baada ya kufuata taratibu zote, atamshangaa Rais Kikwete akisikiliza kelele za wapinzani na kukataa kusaini muswada huo, kwa sababu wapinzani hao walishiriki kupitia kamati  na  hata bungeni kabla ya kupitishwa kwake.

 

Waziri alisema pia kwamba vitendo vya wapinzani kujiunga pamoja na kuanzisha kampeni za kuwahamasisha wananchi ili waukatae muswada huo, hakisaidii lolote kwa sababu sheria zote zinatungwa bungeni na si kwenye Viwanja vya Jangwani wala Ikulu.

 

Basi, Waziri Chikawe anamwomba Rais Kikwete asaini  muswada huo ili kupisha vurugu zinazoweza kujitokeza katika Mkutano wa Bunge unaotazamiwa kuanza Oktoba 29, mwaka huu. Kihistoria ndiyo siku mwaka 1964 nchi yetu ilipoanza kutumia rasmi jina la Tanzania.

 

Tukitaka kusema  kweli na hata lazima tuseme kweli, mambo yanayatokea katika Bunge letu nyakati zetu hizi, yanadhihirisha kwamba wabunge wa pande zote mbili – wa chama tawala na wa vyama vya upinzani – kwa pamoja wamekosa uzalendo na hawaitakii mema Tanzania.

 

Tusidanganyike, hivi sasa kule bungeni hatuna chama cha siasa kinachopigania maslahi ya wananchi na ya Taifa kwa jumla. Kila chama  kinapigania maslahi yake na ya wanachama wake.

 

Kinachofanyika sasa ni kitendo cha ‘mwamba ngoma ngoma huvutia kwake’. Kikubwa zaidi kinachoonekana kwa sasa, kila chama kinaangalia mbele kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

 

Kwa hiyo, kila chama kinafanya kile ambacho kinaweza kufanya sasa katika kuhakikisha kinashinda uchaguzi kwa kupigania ipatikane Katiba itakayosaidia chama husika kushinda uchaguzi huo.

 

Katika hali hiyo, ni ndoto kutazamia kuwa hazitokei tena vurugu bungeni katikati ya mapambano haya ya kila chama kutaka Katiba ya nchi tunayoitafuta ilenge maslahi yake.

 

Kwa upande wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hapana shaka watataka kutumia wingi wao kutuletea Katiba itakayolinda maslahi yao na ya chama chao, kama walivyofanya mwaka 1992 walipopitisha Sheria ya Vyama Vingi.

 

Wakati ule wa mfumo wa chama kimoja hakuna vurugu zilizotokea bungeni. Wote lao lilikuwa moja lakini leo kuna wabunge vyama vya upinzani na hao lao moja. Katika mazingira hayo vurugu zitaishaje?

 

Tutaepuka tu vurugu kwa kutendeana haki kama wabunge wa chama tawala wanaitakia mema nchi yetu, na kama ndiyo hivyo tunavyoamini, basi wasithubutu kutuletea Katiba mbovu inayowabeba. Tusije tukasahau vijana wetu wa miaka hii ni wanamapinduzi kweli kweli.

 

Kwa hiyo, hawatakubali kuwa na Katiba inayoweka mbele maslahi ya chama tawala na ya wanachama wake, hivyo hatutaki wabunge wa chama tawala watuandalie Katiba itakayoleta machafuko ambayo nchi hii haijapata kuyaona.

 

Lakini nao wabunge wa vyama vya upinzani yafaa wachukue tahadhari, kususia vikao vya Bunge hakuwasaidii kwa sababu hakuna sheria ya nchi hii wala kanuni ya Bunge inayowazuia wabunge wa chama tawala kupitisha sheria wabunge wa kambi ya upinzani wanaposusia vikao.

 

Kwa hivyo, nawashauri wabunge wa vyama vya upinzani kufanya vile walivyofanya Mwalimu Julius Nyerere na wenzake wakati wa ukoloni.

 

Mwanzoni mwa mwaka 1958, Tanganyika ilikuwa ikijiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa Baraza la Kutunga Sheria. Wakati ule kulikuwa na chama cha siasa cha Wazungu cha United Tanganyika Party (UTP), ambacho kilikuwa kinaungwa mkono na Gavana wa Tanganyika, Sir Edward Twining.

 

UPT ilikuwa ikipigania Tanganyika ikipata Uhuru itawaliwe na mataifa yote mkuu matatu – Wazungu, Waasia na Wafrika.

Kwa hiyo, Serikali ya Mwingereza Tanganyika iliyoongozwa na Twining ilikuwa imeandaa uchaguzi wa kura tatu, ambapo mpiga kura alitakiwa kupiga kura tatu kwa mpigo ili kuchagua mgombea Mzungu, Muasia na Mwafrika.

 

Baadhi ya wanachama wa TANU walitaka isusie vikao vya Baraza la Kutunga Sheria pia isusie uchaguzi mkuu huo uliokuwa umepangwa kufanyika Septemba 8, 1958. Kwa hiyo, TANU iliitisha Mkutano Mkuu Maalum mkoani Tabora Januari 1958 ili kutafuta suluhu.

 

Katika mkutano ule, Rais wa TANU, Mwalimu Nyerere, alitaka TANU isisusie vikao vya Baraza la Kutunga Sheria wala Uchaguzi Mkuu ule bali wakae kwenye Baraza kuendeleza mapambano.

 

Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa kitendo cha kususia vikao vya Baraza kisingewaathiri wapinzani wao Wazungu, ambao wangeendelea kupitisha pekee yao sheria zinazowapendelea. Lakini kundi la pili la wana-TANU lililoongozwa na Zuberi Mtemvu lilishinikiza TANU isusie vikao vya Baraza na Uchaguzi Mkuu.

 

Kura zilipopigwa kundi la Nyerere lilishinda. Pamoja na uchache wao walipambana katika Baraza la Kutunga Sheria huku hoja zao zikifuatiliwa na wananchi. Ulipofanyika Uchaguzi Mkuu TANU ilishinda viti vyote 30 vilivyogombewa.

 

Uamuzi wa mwisho ni wa wananchi. Basi ni vyema wapinzani wazingatie hilo. Vurugu na kususia vikao vya Bunge ni vitendo ambavyo haviwajengi wapinzani, badala yake vinawabomoa.

By Jamhuri