Wiki mbili zilizopita, Gazeti hili liliandika habari zinazohusu kukamatwa kwa msaidizi wa Mbunge wa Tunduru Kusini, Mtutura Mtutura, akiwa na bunduki za mbunge huyo zinazohusishwa kwenye matukio ya ujangili. Baada ya taarifa hiyo, Mtutura amejitokeza kukiri kukamatwa kwa bunduki hizo na ukweli wa mambo ulivyokuwa. Ifuatayo ni kauli ya mbunge huyo tunayoichapisha bila kuihariri.

Ndugu Mwandishi wa Habari, ni ukweli usiopingika kwamba taarifa iliyochapishwa kwenye gazeti la JAMHURI la tarehe Mei 28 – Juni 3 2013 imeniathiri sana mimi binafsi, familia yangu na viongozi wa chama changu CCM. Ni vema sana baada ya kuipokea taarifa yangu ya maandishi, ujiridhishe juu ya ukweli wake na uichapishe kwenye ukurasa wa mbele kama ulivyofanya kwa taarifa ya tuhuma kwangu.

 

Nitajibu hoja moja baada ya nyingine kama ilivyojitokeza kwenye gazeti tajwa hapo juu ikibeba kichwa cha habari “Bunduki za mbunge zanaswa kwa ujangili” kama ifuatavyo;

Si kweli kwamba bunduki zangu zimekamatwa zikitumiwa na Katibu wangu NAKALE kufanyia ujangili katika msitu uliotajwa. Aidha, nathibitisha kumiliki bunduki mbili kubwa ambazo ni Rifle 375 yenye namba A181858 na shotgun aina ya MAVERICK yenye namba MV52661R.

 

Rifle niliinunua mwaka 2008, ni bunduki mpya ambayo hadi naandika barua hii haijapiga risasi hata moja. Bunduki hiyo niliikabidhi kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Tunduru na risasi zake tarehe 07 October 2008 saa4:00 asubuhi ili WANITUNZIE. Nililazimika kuwakabidhi Jeshi la Polisi waifadhi kutokana na sababu zifuatazo;

 

Niliinunua bunduki rifle inisaidie kulinda mifugo yangu (ng’ombe na mbuzi) dhidi ya wanyama hatarishi wa porini kama simba na chui ambao kwa historia ya Tunduru, ni Watanzania wachache wasiojua adha ya wanyama kama simba wanavyosumbua katika eneo hilo . Lakini kutokana na mabadiliko ambayo sisi wenyeji tunashindwa hata kuyatolea maelezo, tishio la simba limepungua sana , ndiyo maana sikuona sababu ya kuendelea kuihifadhi silaha ile ndani ya nyumba.

 

Sheria inamtaka kila mmiliki wa silaha kubwa kuihifadhi sehemu madhubuti (AMARY). Kwa vile nilikuwa sijakamilisha ujenzi wa AMARY, niliona ni vema kuipeleka Polisi ambako ni sehemu salama kwa silaha yangu.

 

Kwa kazi yangu ya ubunge, mara nyingi nimekuwa situlii sehemu moja kwani kila mara nahitajika kwenda vijijini, mkoani Dar es Salaam na Dodoma . Hivyo, uamuzi wa kuipeleka Polisi niliona ni sahihi kwa usalama wa silaha isije ikafika mikononi mwa watu wabaya.

 

Bunduki ya pili niliinunua baada ya kuamua kujihusisha na kilimo cha mpunga katika Kijiji cha LIWANGA Kata ya MISECHELA. Nilianza kilimo cha mpunga msimu wa mwaka 2011/2012 kwa shamba la ukubwa wa hekari 100. Msimu huo, shamba lilishambuliwa sana na ndege aina ya kanga, na wenyeji wangu walinishauri kuwa njia bora na ya uhakika ya kuwadhibiti kanga ni kutumia bunduki ya shotgun kwa kutumia risasi za ndege. Niliwasilisha maombi ya kununua bunduki ya shotgun kwa kutoa sababu nilizozieleza nao wakakubali. Nilikabidhi bunduki hiyo mwezi Juni 2012, nikasafiri nayo hadi Dodoma wakati wa vikao vya bajeti. Nilienda nayo Tunduru mwishoni mwa mwezi Octoba 2012 baada ya vikao vya Bunge.

 

Kwa kawaida mpunga ukishaota na kufikia urefu wa nchi 2-3, usumbufu wa kanga hukoma. Kwa sababu hiyo na zile zingine nilizoeleza awali, nililazimika pia na bunduki hiyo kuipeleka Polisi waihifadhi tarehe 10 Januari 2013.

 

Chimbuko la tuhuma hizi juu yangu ni za kisiasa zaidi na chuki kwangu kwa sababu zifuatazo;

 

Hivi inawezekanaje mtu ashikwe na bunduki tatu akiua tembo halafu afungwe kifungo cha nje? Mbona kijana mmoja wa Kijiji cha Lelolelo amehukumiwa kifungo cha miaka 10 jela kwa kukutwa akila ugali na kitoweo cha nyama ya paa, iweje huyu aliyekutwa na bunduki tatu akiua tembo afungwe kifungo cha nje?

 

Haiingii akilini kwa mmiliki wa bunduki tatu zilizokamatwa zikiuwa tembo akaendelea kupumua mitaani. Hivi haikumbukwi miaka ya sabini mwishoni aliyekuwa Mbunge wa Songea alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kwa kujihusisha ujangili? Kwa nini Mtutura tena mtoto wa mkulima wa korosho asifikishwe mahakamani?

 

Historia yangu haina mashaka kwa binadamu yeyote mwenye akili timamu na asiye na chuki na mimi. Kwa wasiojua historia ya maisha yangu, basi si vibaya nikawajuza japo kwa mutasari.

 

Nimezaliwa Kijiji cha Ligoma, Kata ya Ligoma Wilaya ya Tunduru miaka 53 iliyopita. Baada ya kumaliza elimu ya sekondari ya kawaida na ya juu, Mwaka 1985 – 1999 niliajiriwa na TANESCO. Mwaka huohuo nilienda chuo na kurudi tena kazini 1988. Nimekuwa na mwajiri TANESCO kwa miaka 14 na miezi 8 bila onyo la mdomo wala maandishi. Watumishi wenzangu bado wananikimbuka kwa mazuri mengi.

 

Mwaka 1999 niliacha kazi TANESCO baada ya kupata kazi ofisi ya Umoja wa Mataifa chini ya Shirika la Maendeleo ya Umoja Mataifa yaani UNDP. Nimesacha kazi UNDP mwaka 2007 baada ya kufanyakazi miaka 7 ili kwenda kugombea Ubunge Jimboni Tunduru. Nikiwa UNDP, nilikuwa mmoja wa watumishi tuliopata tuzo ya kufanya kazi kwa uadilifu iliyosainiwa mkuu wa UNDP wakati huo Mr MARK MALLOCK BROWN.

Kwa jumla sina rekodi mbaya mahali popote katika anga ya dunia hii.

 

Sijajihusisha na kesi kwa kufanya njama ili Katibu wangu afungwe kifungo cha nje. Hata hivyo, hakuna shitaka lolote alilofunguliwa katibu wangu hadi nitowapo ushuhuda huu. Kilichotokea ni Katibu wangu kufikishwa mbele ya Hakimu na Serikali kumuomba Hakimu airuhusu Serikali wamuweke Katibu wangu chini ya uangalizi kwa miaka miwili na awe anaripoti ofisi ya Polisi kila mwanzo wa mwezi kwa miaka miwili. Hadi leo hakuna kesi iliyofunguliwa, wakati akikamatwa tuhuma zilikuwa kumiliki bunduki ya Mbunge isivyo halali, lakini baada ya akina Tossi kubaini kuwa bunduki wanayomtuhumu Nakale iko Polisi wakambadilishia tuhuma.

 

Ni ukweli usiopingika, Kamanda Tossi alimpotosha Waziri, na Waziri licha ya kufahamishwa hayo bado amejengeka kuamini kile alichopotoshwa. Kilichotokea Tunduru, yalitolewa matangazo kwenye vijiji kwamba watu wote wanaomiliki bunduki wazipeleke polisi ili zikakaguliwe, walipofika, bunduki zilikamatwa na wamiliki wote kufikishwa mahakamani na mahakama kuiruhusu Serikali kuwaweka watu wale chini ya uangalizi wa miaka miwili (sawa na kifungo cha nje) na wakimaliza waombe upya umiliki wa silaha zao. Huu ni ubabe ambao mtu muungwana hawezi kuufumbia macho.

 

Ningefurahi sana kama Waziri angeenda Tunduru kukutana na wadhulumiwa wa mali na ndugu wa waliodhulumiwa uhai. Bado nina majina watu wengine waliouwawa na askari wa maliasili, ni muda ndio ulinifanya nishindwe kuwataja wote bungeni. Aje na Waandishi wa Habari ayaone hayo makaburi na ajiandae kutoa rambirambi.

 

Nakiri kupokea ujumbe wa maandishi kwenye simu yangu siku ya Jumamosi tarehe 25/5/2013 saa 10:18 nikiwa kwenye semina Hotel ya African Dreams Dodoma. Ujumbe ulisema, Mheshimiwa, salaam. Kuna jambo la dharura, naomba tuonane. (jina nalihifadhi),  ujumbe haukuainisha zaidi ni dharura gani ninayohitajika, pia nakili kuona missed call kwa namba hiyohiyo ambayo pia iliingia nikiwa kwenye hiyo semina. Baada ya semina, kwa kweli nilighafirika hasa kutokana na uchovu niliokuwa nao. Naomba radhi kwa hilo .

 

Aidha, nitumie fursa hii tena kuwaasa wanasiasa na wasio wanasiasa wenye tabia ya kupakana matope wakidhani ni mtaji mzuri wa kufanikisha kupata au kuendeleza madaraka waliyonayo waache mara moja. Madaraka hutolewa na MUNGU, kunichafua mimi kwenye vyombo vya habari wakidhani ni tiketi maridhawa ya kuendeleza utawala walionao au tiketi ya kupata uongozi wajuwe wanajidanganya.

 

Hata hivyo, nawathibitishia ya kwamba kama uhai upo, kwa kuzingatia uadilifu wangu, utumishi wangu uliobora na unyenyekevu wangu kwa wapiga kura wangu, SINA SHAKA WATANICHAGUWA TENA KUENDELEA KUWA MBUNGE WAO. NA WAO HAWATAPATA NAFASI HIYO HATA KAMA WATAZIKIRI UCHI.

Ahsante sana

 

Mtutura A. Mtutura

Mbunge wa Tunduru Kusini

1278 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!