Nataka kusisitiza nini: Kwamba sisi ni Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyealikwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani iliyofanyika kitaifa Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Mei Mosi, 1995. Katika hotuba yake, Mwalimu alielezea historia ya vyama vya wafanyakazi duniani. Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa maoni yake kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini pamoja na ushauri kuhusu mambo ambayo wananchi wanapaswa kuzingatia wakati wa Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba mwaka huo, hasa sifa za wagombea nafasi za uongozi kuwa ni pamoja na kila mmoja kujiuliza ataifanyia nini nchi yake baada ya kuchaguliwa na anakwenda kufanya nini Ikulu. Ifuatayo ni hotuba ya Mwalimu.

Ni muhimu kukumbuka kuwa hotuba hii imefuata mlolongo wa mazungumzo ambayo Baba wa Taifa alikuwa nayo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ambako alikuwa anajaribu kuamsha dhamira ya viongozi wetu wa wakati ule. Hotuba hii ni miongoni mwa hotuba ambazo ukweli wa hoja zake ni hazina kubwa kwa vizazi vijavyo vya Watanzania.

 

Taifa changa miongoni mwa mataifa machanga

Taifa hili halijajenga mizizi mirefu ya kuwa Taifa huru kuwakaribia Waingereza. Waingereza wana miaka mingapi? Sijui, labda elfu na zaidi.

 

Katika mataifa machanga duniani, moja ni Marekani. Lakini, Marekani wana miaka mia mbili na zaidi ya kuwa taifa. Vitaifa vingi vya Ulaya vina miaka mingi tu! Mataifa machanga haya lazima yajenge misingi inayowafanya raia wake wajiite ‘sisi’.

Tumejitahidi na ndivyo jitihada zetu zilivyokuwa. Lakini ukijenga nchi moja, unajenga misingi ya umoja ili tuelewane na tujuane kwamba sisi ni wamoja, ni ndugu. Kama tunahangaika kufanya kazi hapa, tunahangaika kwa pamoja. Kama tunahangaikia ulinzi, tunalinda nchi yetu kwa maslahi yetu pamoja.

 

Tunaulizana “nini mahitaji yenu?” Tunajitahidi wote, tunayapata. Kama tunataka elimu, tunasaidiana wote tupate elimu. Siyo tuseme kwamba wengine wapate elimu wengine wasipate. Kama tunataka afya, tunataka kujitahidi wote tuweze kutafuta njia kusudi wote tupate afya, wote tuwe na afya. Siyo wengine wapate afya wengine wasipate. Kama tunataka nyumba nzuri, wote tujitahidi kwa pamoja tuone kwamba tunajenga mazingira wezeshi yatakayohakikisha kuwa kila Mtanzania atakuwa na nyumba nzuri kwa pamoja. Hapo ndipo tunaweza kushirikiana tujenge nchi pamoja.

Azimio la Arusha na Siasa ya TANU ya Ujamaa na Kujitegemea

Tukaweka kitu kimoja hapa kinaitwa Azimio la Arusha. Leo narudia kusoma Azimio la Arusha hata kama hamlitaki. Kama kuna watu Tanzania hawajali, wachukue waanze kulisoma ili waone na waniambie wanachokiona mle kibaya ni nini hasa. Asome tu kwa dhati tu na kisha aseme hiki ni kibaya.

 

Siasa ya Ujamaa

Linasema Azimio la Arusha, kwa msingi kabisa, kwamba “Nchi yetu ni ya Wakulima na Wafañyakazi”. Sasa mnasemaje? Imeacha kuwa ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi? Kwa hiyo, kama tunaijenga nchi hii, tunaijenga kwa faida ya Wakulima na Wafanyakazi. Ndivyo Azimio Ia Arusha linavyosema. Ukweli huo umekwisha? Umefutika? Umefutwa na nani? Nini kimefuta ukweli huo kwamba nchi hii ni ya Wakulima na Wafanyakazi? Ninyi hapa ni Wakulima na Wafanyakazi.

 

Mtaona wafanyabiashara wadogo wadogo, siku hizi wengine wanaitwa Wamachinga. Lakini, hasa hasa, nchi hii bado ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi. Kama tutafanya jitihada za kuijenga nchi hii, tutajenga uchumi wake na huduma zake za umma ambazo lazima ziwafae Wakulima na Wafanyakazi. Hali hiyo imebadilika lini?

Siasa ya Kujitegemea

 

kwamba “Hatuna budi kujenga nchi hii kwa kujitegemea”. Hatuwezi kuwa tunataka maslahi yetu ya Watanzania ya afya bora, maisha bora na elimu nzuri lakini eti tudhani tunaye mjomba huko nje atakuja kutuletea maslahi hayo. HATUNA! Tutajenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe sisi wenyewe.

 

Akipatikana mtu kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine. Msimamo huo tukauita

 

Siasa ya Kujitegemea.

Msingi huo umekufa. Hivi mmeshapata mjomba? Hivi kweli mtawadanganya Wafanyakazi hawa msiwaambie “chapeni kazi kama mnataka maslahi yenu yaboreshwe, tuchape kazi kwa faida yetu!” Tuache kuwaambia wakulima kwamba “kama tunataka maendeleo, tuchape kazi hivyo hivyo”. Hivi mtawaambia hawa kwamba “tumeshapata mjomba msiwe na wasiwasi!” Mjomba huyo ni nani? Mimi nitafurahi kumwona. Nitakwenda kumwona, lakini sitamwuliza lolote. Nitafurahi kumwona.

 

Halafu mkinionesha, “ndiye huyu mjomba”, nitacheeka! Hali ya nchi hii haijabadilika hata kidogo. Tanaweza kujenga nchi kwa maslahi ya Watanzania kwa siasa ya kujitegemea tu, lakini kwa manufaa ya wote. Manufaa ya wote ndicho tulichokiita ujamaa.

Nchi ya Kijamaa

 

“Nchi ya Ujamaa”, tukasema, “ni nchi ambako kila mtu anafanya kazi. Kama ni mkulima, anafanya kazi; kama ni mfanyakazi, anafanya kazi”. Lililokuwa la msingi na linalotawala ni mfanyakazi: maslahi yanatokana na kazi yake na jasho lake. Watu ambao hawana ulazima, kimsingi ya kupata maslahi yao kutokana na jasho lao wenyewe wapo. Watoto wadogo hawana jukumu hilo. Eti chakula chao kitokane na nguvu zao wenyewe? Hao ni wanyonyaji wa haki sawa kwani wanawanyonya mama zao. Ni haki yao. Lakini zee na madevu yake hatulitazamii limnyonye mama yake.

 

Watoto wadogo tu wanayo haki hiyo. Vile vile, kuna watu ambao hawana uwezo wowote ule wa kujifanyia kazi – siyo uwezo wa kutokuwa na kazi! Wako watu hawawezi. Wana vilema fulani ambao hawawezi kufanya kazi wajipatie riziki kwa kazi na kwa nguvu zao wenyewe. Hawa wana haki ya kulishwa na kutunzwa na umma pamoja na jumuiya zote.

Hali kadhalika, wako watu wazima ambao wamefanya kazi zao. Walipofika umri wao wa kushindwa, hawawezi kufanya kazi tena. Ah! basi tena. Hawajiwezi hawa, tuwatunze. Hawa ni haki kuwatunza. Wamo watu wa aina hiyo wanajulikana kila mahala.

 

Nchi ya Kibepari

Hata hivyo, mbali ya makundi hayo, wapo watu wengine ambao wanapata riziki yao kwa kufanya kazi na wengine wanapata riziki yao kwa kufanyiwa kazi. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ya kibepari. Nchi inakubali wengine wafanye kazi na kupata riziki yao kwa jasho kama inavyosema misahafu, wengine wanafanya kazi kwa kunyonya kama watoto wadogo kama vile vilema na vizee. Ni majitu yanakaa na uwezo wao yanatumia wengine kama vyombo.

 

Kwa hiyo, mfanyakazi na randa ni sawa sawa. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ni nchi ya kibepari. Sasa katika dunia ya siku hizi maneno hayo si mazuri sana kuyasema. Na mimi nawakumbusheni tu na wala sijayasema! Mimi sina taabu, nawakumbusheni tu. Hilo Azimio la Arusha, ambalo sasa mnalitemea mate, lilikuwa linasema hivyo na, kutokana nalo, kuna mambo fulani tukaanza kuyapata.

 

Baadhi ya matunda ya Azimio la Arusha

Moja ya mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni la hali yetu mbovu ilivyokuwa kwanza wakati tunajitawala. Nchi tuliyoipokea kutoka kwa wakoloni ilikuwa ni masikini sana. Ilikuwa nyuma kabisa kwa upande wa elimu. Tulipojitawala, tulikuwa na wahandisi wawili. Kijana mmoja aliitwa Mbuya na alifariki katika miaka miwili hivi baada ya kujitawala. Tulikuwa na madaktari kumi na wawili wakati tunajitawala mwaka wa sitini na moja.

 

Kujenga uchumi wa viwanda

Tukaanza shughuli ya kujenga uchumi wetu. Natumaini nitazungumzia hili la viwanda. Nchi zinazoendelea duniani [kama Marekani ya Kaskazini, Marekani yenyewe na Kanada, Ulaya, hasa Ulaya Magharibi na Japani] na maana moja ya kuendelea ni kwamba uchumi wake unategemea viwanda. Viwanda ndivyo vinatengeneza vipaza sauti, kamera zetu tunazotumia sasa na kadhalika.

 

Maana ya maendeleo ya leo ya uchumi wenye nguvu ni maendeleo ya viwanda. Nchi yenye viwanda tunasema ni nchi iliyoendelea. Hata hivyo, tuna maana nyingine ya nchi zilizoendelea ya kuziita ni nchi zenye viwanda. Nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na viwanda vya kisasa.

 

Viwanda vya nguo ndiyo rahisi kuanza navyo:  historia ya utawala wa Waingereza India

Wakati tunajitawala, hatukuwa na viwanda. Tulikuwa tunalima kahawa, mkonge na pamba, lakini tunauza vyote nje. Mimi najua kidogo historia ya Uingereza, ilikuwa ndiyo nchi ya kwanza duniani kuanza maendeleo ya kisasa ya viwanda. Sekta moja ya viwanda walioanza nayo, ambayo ilikuwa rahisi wakati huo na leo ni rahisi zaidi, ilikuwa ya kutengeneza nguo. Waingereza wakaitumia na wakajenga viwanda. Nguo zao zikawa zinatokana na viwanda vyao.

 

Vile vile, walikuwa wana dola kubwa. Walikuwa wanatutawala sisi Afrika, wanawatawala Asia na wanatawala sehemu nyingine za Amerika, lakini hasa Afrika na Asia. Walipoingia India, walikuta Wahindi tayari wanatengeneza nguo zao kwa mashini. Wakawaza “hata Wahindi nao wanatengeneza nguo! Haina maana”.

 

Wakawazuia Wahindi kutengeneza nguo kusudi soko duniani liwe la Waingereza: liwe huru lisizuiwezuiwe. Namna moja ya  kulifanya soko hilo kuwa huru ilikuwa ni kwa kuvitawala vijitu hivi, halafu unauza vitu vyako.

 

Wenyewe ndivyo walivyoanza na viwanda vya nguo na, baadaye, wakaongeza vingine na hatima yake, Waingereza wakawa wakubwa. Wenzao duniani wakaona  “Alaa! hivi Viingereza tunaviachia vinaendelea namna hii kwa nini?” Wakaanza mambo, wakagombanagombana, wakapiganapigana na wakanyang’anyana.

 

Tulipojitawala mwaka sitini na moja tulikuwa tunajua mambo haya, ijapokuwa tulikuwa wachache, kwamba nchi haiwezi kuendelea na kuwa ya kisasa bila viwanda. Mtawachumia pamba wakubwa hawa na kukata miwa. Hiyo ilikuwa sababu moja ya kuleta utumwa ili kuwachukua Waafrika waende Marekani wakachume pamba na wakakate miwa.

 

Baada ya kupata Uhuru tukajiuliza. Leo tunajitawala, tuendelee kuchuma pamba na kukata miwa? Tukaamua: Tuanze kujenga viwanda kwa kuwa sisi tunalima pamba. Kwa hiyo, shughuli ya kwanza kabisa tutakayoanza nayo ni ya kujenga viwanda vya nguo.

 

Nikawaomba wanaojua mambo haya ya viwanda duniani. Wakati huo sisi wenyewe hatukuwa na wataalamu. Nikawaeleza watu hawa maneno haya: Hivi tunajitawala, tuendelee kuuza pamba ghafi nje? Nataka nianze kutengeneza nguo hapa Tanzania.

 

Wakanishauri na wakaniambia Mwalimu, mnaweza kuanza kutengeneza nguo kutoka pamba yenu hapa. Jenga uwezo ili Tanzania iweze kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba inayolimwa Tanzania kutengeneza nguo hapa hapa.

 

Walinishauri nijenge uwezo ndani ya Tanzania wa kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba yetu hapa hapa. Asilimia kumi na tano (15%) ya pamba iliyobaki, ama tunaweza tuitumie wenyewe hapa hapa au tunaweza kuiuza nje. Hiyo ilikuwa safi sana, kwamba tujenge viwanda kwa makusudi kabisa.

 

Wakati ule, hata mimi ningekuwa na sera za kibepari, ningejenga viwanda. Mabepari ndiyo walioanza viwanda na viwanda vyenyewe hivyo havikuwa na sera ya ubepari au ujamaa. Vilikuwa ni viwanda tu! Sasa tukaanza kujenga viwanda vya nguo na sasa sitaki kusema sana juu ya jambo hili.

 

Itaendelea

By Jamhuri