Matokeo mabaya ya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka jana, yameibua mjadala mkubwa nchini kutaka kujua mbichi na mbivu zilizosababisha vijana wengi kufeli vibaya.

Akitangaza matokeo hayo kwa vyombo vya habari nchini, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema yana ufaulu mdogo yakilinganishwa na yale ya mwaka juzi, wakati jumla ya watahiniwa 240,903 kati ya 367,750 waliofanya mtihani huo wa mwaka jana, wamefeli kwa kupata daraja sifuri, wakiwa ni zaidi ya asilimia 60 ya watahiniwa wote.


Matokeo hayo yamemshitua kila mtu kwa kuzingatia kuwa anguko la elimu katika Taifa lolote, ni anguko linaloashiria mustakabali wa Taifa la wajinga, na bila shaka ndiyo sababu iliyomsukuma Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuunda tume ya kuchunguza chanzo na sababu za kutokea kwa kadhia hiyo.


Lengo la makala haya si kutaka kutoa hadidu za rejea zitakazotumika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, la hasha, bali ni kujaribu kuainisha baadhi ya maeneo ambayo yanaweza kuwa yamechangia kutokea kwa zahama hiyo huku yakiwa yanapuuzwa kila yanapotajwa. Ndiyo maana sitaki kushawishika moja kwa moja na baadhi ya hoja zilizotajwa wakati wa kutangaza matokeo hayo, kuwa ndizo zilizosababisha hali hiyo na kwamba utatuzi wake ndiyo utakuwa mwarobaini wa tatizo hilo huku hoja nyingine zenye mashiko zikifumbiwa macho.

 

Tume hiyo itakutana na sababu nyingine nyingi ikiwamo ya utoro wa walimu. Ni kweli, hivi sasa kuna wimbi kubwa la walimu watoro kazini kuliko kwa wanafunzi wenyewe. Kwa hoja hii, tume isiishie hapo tu bali ipate majibu kuntu kujua nini kinachosababisha utoro huo na hicho ndicho kinachotakiwa kufanyiwa kazi.

 

Sambamba na hilo, lipo pia tatizo la walimu wengi kuamua kuachana na ualimu na kwenda kusomea fani nyingine. Tume iwasikilize walimu wenyewe ili kupata majibu sahihi ni kwanini kumekuwa na wimbi hilo kubwa la walimu kuhama fani yao ya awali. Sababu za kuingia na kutoka huko kwa walimu ndizo zinazotakiwa kufanyiwa kazi na kuzipatia majibu yatakayoweza kupata ufumbuzi wa tatizo hilo, ambapo hatima yake ni upungufu mkubwa wa walimu katika shule zetu pamoja na kuwapo kwa wahitimu wengi kila mwaka.

 

Zimetajwa pia sababu za ukosefu wa maabara, upungufu wa vitabu vya kiada na ziada, wazazi na wanafunzi kutokuona kuwa elimu ndiyo kipaumbele namba moja na tatizo la miundombinu ya kufundishia na kujifunzia. Hata hivyo, sababu zote hizo bila kumjengea mwalimu ari ya kufanya kazi kwa kumwongezea mshahara, kumlipa malimbikizo ya madai yake na kumboreshea mazingira ya kazi na ya kuishi, haziwezi kutosha ikiwa kweli tumekereka kutokana na  matokeo hayo na tunayo dhamira ya dhati ya kutaka kurekebisha hali hiyo isitokee tena, kwa kuzingatia kuwa mwalimu ndiyo kiini cha utoaji wa maarifa, stadi na ujuzi kwa mwanafunzi.


Mwalimu wa leo ni wa kidigitali na facebook na si wa kianalogia na S.L.P. kama ilivyokuwa kwa mwalimu wa enzi za Mwalimu, ambapo ualimu ulikuwa ni wito wakati sasa ualimu ni kazi kama kazi nyingine.


Wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 50 tangu nchi yetu ipate Uhuru, zilitolewa takwimu nyingi za kielimu zenye kujinasibu jinsi Taifa letu lilivyopiga hatua hadi kufikia umri huo, kigezo kikubwa kikiwa ni ongezeko la kitakwimu bila kuzingatia ubora wa takwimu hizo na matokeo yake ongezeko hilo limeshindwa kusadifu kutokana na matokeo hayo mabaya ambayo yalikuwa yakitabiriwa hata kabla hayajatokea.


Kwa mantiki hiyo, tume iliyoundwa na Waziri Mkuu Pinda itakuwa na maana ikiwa itawafikia walimu na walimu wenyewe kuwa tayari “kufunguka” bila kupepesa macho wala kutafuna maneno, na kuipa ushirikiano tume hiyo wakiiambia kile kilichowasibu hata wakaamua kuifikisha elimu ya Tanzania katika aibu hiyo, na kuwa gumzo si tu ndani ya nchi bali hata katika anga za mataifa mengine.


Pamoja na kuitakia kila la heri tume hiyo, ni matumaini ya Watanzania walio wengi kuwa matokeo ya tume hiyo yatafanyiwa kazi sambamba na mapendekezo yake, ili kuhakikisha kuwa Taifa letu halipati tena aibu hiyo na iwapo tume hiyo itakuwa kama ilivyowahi kutokea kwa baadhi ya tume zilizoundwa siku za nyuma, na mapendekezo ya tume hizo kubakia kwenye makabrasha, ni dhahiri kuwa dhamira ya walimu kurekebisha dosari hiyo haitaguswa na hivyo uwezekano wa kujirudia kwa matokeo kama hayo au hata mabaya zaidi ya hayo katika miaka ijayo utakuwapo.

0763545355

Swe2respice@yahoo.com

1006 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!