Awali ya yote nianze makala hii kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa rehema zake nyingi anatujalia afya njema na amani katika Taifa letu.
Mei 15, mwaka huu kupitia “dondoo za magazetini” (Radio Tumaini kipindi cha “Hapa na Pale” ilielezwa kwamba kuanzia Julai 2017 matumizi ya mkaa hayataruhusiwa.
Baada ya kusikia maneno hayo nikajiuliza: “hakuna kutumia mkaa-kulikoni?” Naelewa kuwa kwa mamlaka husika (Serikali) kuweza kuchukua hatua kama hiyo kupitia Wizara yenye dhamana ya masuala ya misitu nchini; yawezekana ikawa na nia nzuri ya kuilinda na kuiendeleza misitu ya asili (natural forests & woodlands) isiendelee kuteketea kutokana na matumizi makubwa ya mkaa hasa kwa wakazi wa mijini. Ikiwa hivyo ndivyo, ni sawa, lakini tumejiandaa vipi kuhakikisha dhamira nzuri kama hiyo inazaa matunda yaliyokusudiwa?
Ni rahisi kusema au kutamka, lakini inapofika hatua ya kutekeleza kunazuka mikwara na changamoto kibao kutokana na kutojiandaa vya kutosha. Kwanza tuelewe kuwa nishati itokanayo na misitu au tungamotaka (biomass) inachangia asilimia 90 ya matumizi ya nishati nchini kutokana na vyanzao tulivyo navyo. Hii ina maana kwamba vyanzo vingine vya nishati-umeme, mafuta, gesi na vinginevyo, kwa ujumla wake vinachangia asilimia 10 tu
Ninaposema wahusika wamejiandaa vipi kuitekeleza azma hiyo namaanisha kwamba walio wengi (zaidi ya asilimia 80) wanaoishi mijini wanategemea mkaa kupika chakula chao. Je, wanaotegemea sana mkaa kwa usalama wao wa chakula (food security) wamehakikishiwa vipi kupata nishati mbadala na ya uhakika ili kuendelea na maisha yao ya kila siku bila mahangaiko? Kimsingi, tunaposema usalama wa chakula ni pamoja na kuwepo nishati ya uhakika. Vinginevyo familia zitakuwa na unga au mchele na maji, lakini iwapo nishati ya kupikia haipatikani kwa urahisi hali hiyo itafananishwa na wale wasiokuwa na chakula. Kwanza, ni vizuri kujua tutapataje nishati mbadala yenye kupatikana kirahisi na kwa bei nafuu? Ni kweli sasa gesi inasambazwa kwa wingi, lakini bei yake ni kikwazo kikubwa kwa familia nyingi mijini. Je, Serikali yetu sikivu itatusaidia vipi kwa suala kama hili kwa kutoa ruzuku?
Pili, ni vizuri kufahamu mapema Serikali imejipanga vipi kuhakikisha mkaa hautengenezwi kwa njia yoyote ile, kwa kuweka ulinzi na usimamizi madhubuti kwa maeneo ya misitu kwa kuzingatia ukubwa wa nchi na uwepo wa rasilimali watu na fedha kutosheleza mahitaji?
Nikiwa mmoja wa wataalaam waliohusika katika kuitekeleza Sera ya Taifa ya Misitu na Mazingira, natambua changamoto katika kuisimamia misitu na mazingira. Kwanza, kuna changamoto ya msingi ya kisera kwa maana kwamba sekta ya misitu au maliasili katika ujumla wake: kitaifa misitu haijapewa umuhimu unaostahili kama ilivyo kwa sekta za maji, kilimo, elimu, afya, na miundombinu.
Kwa mantiki hiyo, tunashuhudia misitu ya asili inateketea kila kukicha kwa sababu kitaifa ni kitu “kipo-kipo tu kama shamba la bibi”.
Kwa mfano, Sheria ya Misitu (Sura 323 RE:2002) inazuia kuvuna miti kwenye msitu usio na mpango wa usimamizi, lakini bado miti inavunwa hata kama hakuna huo mpango. Vilevile, sheria hairuhusu kusafirisha mkaa kwenda nje ya nchi. Lakini kutokana na udhaifu katika kusimamia utekelezaji wa sheria, hakuna siri- mkaa unasafirishwa nje ya nchi bila kukamatwa. Kama hivyo ndivyo, uwezo wa kusimamia utekelezaji wa sheria na kuzuia mkaa usiingizwe mijini utatoka wapi?
Usimamizi uliopo ni duni sana. Mfano, msitu wa hifadhi wenye hekta 400,000 unakuta unasimamiwa na watumishi wanne au hawazidi 10 na wengi wao wako makao makuu ya wilaya na hawawezeshwi ipasavyo. Kwa hali kama hiyo tunatarajia nini? Lazima misitu iteketee kwa mapanga na mashoka. Zamani tulikuwa na Kada ya Walizi Misitu-“Forest Rangers” lakini katika harakati za kupunguza ukubwa wa Serikali wakubwa wakaamua kada hiyo ifutwe. Kwa kufuta walinzi misitu sidhani kama tulipunguza ukubwa wa Serikali, bali ni kitendo kilichoambatana na dhana ya kuiona misitu si muhimu kwa maendeleo ya taifa-“itakuwepo tu hata kama hailindwi au kutunzwa”: sasa tunahaha nchi inageka jangwa, vyanzo vya maji vinakauka na kadhalika.
Bila kuwapo usimamizi madhubuti hata kama tukipiga marufuku mkaa bado hali itaendelea kuwa tete na misitu kuzidi kuteketea kutokana na shughuli za kibinadamau zisizodhibitiwa.
Mathalani, kilimo cha kufyeka misitu na baada ya miaka mitatu kuhamia eneo jingine kwa mwendelezo huo huo wa kufyeka misitu ya asili; kuwa na mifugo mingi; kila mara kuichoma moto misitu; makazi ndani ya misitu iliyohifadhiwa kisheria; ukataji misitu hovyo kwa ajili ya magogo na mbao na uchimbaji madini usiodhibitiwa. Misitu imeharibika sana kiasi pia cha kuhatarisha maisha ya wanyamapori na biashara ya utalii. Wanyamapori wanategemea sana rasilimali misitu kwa maisha yao ya kila siku kupata chakula na maji. Hii si dalili nzuri kwa maendeleo ya Taifa letu.
Ili taifa liweze kudhibiti matumizi makubwa ya mkaa nashauri yafuatayo:
(i) Kwanza, badala ya kupiga marufuku matumizi ya mkaa, Serikali ione kuwa utengenezaji na biashara ya mkaa ni fursa ya kusaidia Watanzania kuinua kipato na wakati huo huo kutunza mazingira. Kwa kuwa soko la mkaa ndani na nje ya nchi ni kubwa; na kwa kuwa misitu inaweza kuendelezwa kwa kutumia misitu ya asili iliyopo kwa misingi endelevu na kwa kupanda miti, ni vema kuwapo mpango madhubuti wa kuendeleza na kuisimamia sekta ya misitu nchini kwa faida ya Watanzania.
Nia kubwa iwe ni kuhakikisha misitu ya asili inasimamiwa isiendelee kutumika hovyo. Kwa mantiki hiyo kuwapo na mipango ya usimamizi (management plans) na pia kuwapo rasilimali watu wa kutosha na fedha ili kutekeleza mipango hiyo;
(ii) Pili, Sera ya Taifa ya Nishati ioneshe kuwa nishati ya kupikia (domestic energy) ni kitu muhimu kwa Watanzania (hasa wenye kipato cha kati na cha chini)- mijini na vijijini. Kwa mtazamo huo Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, itenge bajeti ya kusimamia na kuiendeleza nishati ya aina hiyo kwa maslahi ya Watanzania wote kama inavyofanya kwa mafuta, umeme na gesi;
(iii) Tatu, sambamba na hilo, Serikali ifanye kila linalowezekana kuhakikisha matumizi ya gesi hasa kwa wakazi wa mijini yanaongezeka. Kwa sasa bei ya gesi ni kikwazo na kulazimisha baadhi ya familia zinazopenda kutumia gesi zishindwe na badala yake zikimbilie mkaa. Kwa mfano, mtungi mkubwa wa gesi (kilo 30) unauzwa Sh 52,000. Karibu gunia la mkaa (kilo zaidi ya 50) linauzwa kwa bei kama hiyo. Tofauti ni kwamba, ni vigumu kwa wengi kupata Sh 50,000 kwa mara moja kuweza kununua gesi, (ukiachilia mbali bei za vifaa) vya kutumia gesi. Urahisi wa kutumia mkaa ni pale unapopatikana kwa bei nafuu kwa kopo moja Sh 1,500 na kuiwezesha familia kupika kwa siku moja au mbili kulingana na aina ya chakula kinachopikwa na aina ya mkaa. Hii ni njia rahisi ya kumudu maisha kuliko kulazimika kupata Sh 60,0000 kwa mara moja kununua gumia la mkaa. Bei ya gesi ikipungua itakuwa ndiyo “mwarobaini” kwa matumizi makubwa ya mkaa mijini;
(iv) Nne, sekta binafsi, serikali za vijiji, mashirika na Watanzania kwa ujumla tuwekeze kwenye upandaji miti kwa ajili ya mkaa na kuni. Kuwekeza kwenye upandaji miti siyo gharama sana ilimradi unayo ardhi na mvua za kutosha. Gharama halisi zitahusu kuandaa sehemu ya kupanda miti, kutayarisha miche, kuipanda na kuitunza kwa miaka mitatu hadi minne ya mwanzo kwa kuhakikisha miche iliyopandwa haizongwi na magugu. Vilevile, kwa miaka hiyo ya mwanzo unaweza ukapanda mazao ya msimu (mahindi, mtama, uwele na kadhalika) kwenye eneo lililopandwa miti. Hali hiyo itasaidia kurahisisha utunzaji wa miti iliyopandwa kwa kupalilia mazao utakuwa pia umepalilia miti. Miti ikifikia kimo cha mita zaidi ya mbili huwezi kuendelea na  upandaji mazao humo. Itabidi uache miti iendelee kukua. Jambo la msingi ni kuhakikisha moto na mifugo haviingii shambani;
(v) Tano, mkazo pia uwekwe kwenye kutumia teknolojia zenye kutoa mkaa mwingi badala hali ya sasa ya tanuru za udongo (earth moulds) kutumia kuni au miti tani 10 na kupata tani moja ya mkaa. Kwa kutumia teknolojia nzuri kwa kiasi hicho cha kuni/magogo unaweza kupata tani 4-6 za mkaa. Isitoshe, matumizi ya mkaa hasa kwenye sehemu za biashara mfano, maeneo ya vioski, wachoma mihogo na viazi, mishikaki/kuku au mighahawa na wakaanga ‘chips’ na kuku au samaki wanatumia mkaa vibaya. Unakuta mhusika amewasha mkaa mwingi unaendelea kuteketea kwa moto huku akimenya viazi au mihogo au akiandaa kuku au nyama. Kwa maneno mengine wanawasha mkaa kabla hawajawa tayari kuutumia. Kwa kufanya hivyo wanasababisha upotevu mkubwa wa nishati.
Ili kurekebisha hali hiyo ni vema mamlaka za majiji, manispaa na miji zikaweka utaratibu kisheria wa kuwabana wafanyabiashara wa aina hiyo wanaosababisha matumizi mabaya ya mkaa kwa kuwatoza faini kila wakiwabaini wakifanya hivyo.
 
Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) na Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki (mstaafu) katika Wizara ya Maliasiali na Utalii. Anapatikana kupitia namba:
0783 007 400.

1420 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!