Kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema na amani tele ndani ya Taifa letu na katika jamii na familia zetu.

Kusema kweli Mwenyezi Mungu ni mwema sana kwetu ndiyo maana tunatakiwa tumshukuru kila wakati na kulisifu jina lake takatifu kwa mema mengi anayotutendea.

Tunaposema kila mwenye pumzi na amsifu Bwana ina maana kwamba sisi binadamu tulivyo tunavuta pumzi au tunapumua kwa kutumia hewa ya oksijeni ambayo tunaipata kwa neema tu ya Mwenyezi Mungu. Hatuigharimii au kuitafuta kwa nguvu zetu, hatuitoleo jasho wala kuinunua.

Vilevile miti au misitu na mimea mingine Mungu aliiumba ili itusaidie na ni chanzo muhimu cha oksijeni.

Baada ya kusema hayo, sasa nirejee kwenye mada: Kwamba Serikali ya awamu ya tano itoe kipaumbele kuhifadhi misitu na mazingira.

Kwa nini nasema hivyo? Kusema kweli hali ya misitu na mazingira kwa jumla ni mbaya sana. Maeneo mengi nchini yamekuwa makame: vijito na mito sehemu mbalimbali Tanzania Bara imekauka na watu wanahangaika kutafuta maji. Sasa tumemaliza uchaguzi na Serikali ya Awamu ya Tano inaanza utawala wake.

Kwa bahati mbaya suala la uhifadhi wa misitu halikuzungumzwa sana katika kampeni za uchaguzi. Kama limezungumzwa, basi ni kwa kiasi kidogo angalau nilisikia, kwa kiasi fulani, suala la kupambana na ujangili. Tunazungumza ujangili mawazo yanakuwa zaidi kwa upande wa wanyamapori, na si katika misitu. Tunasahau kuwa misitu ni tegemeo kubwa la wanyamapori na binadamu. 

Isitoshe, misitu ya asili ni nguzo kubwa kwa vyanzo ya maji kwa maana ya sehemu ambazo chemichemi, vijito na mito huanzia. Misitu ni nguzo muhimu katika kuhifadhi na kuendeleza udongo na kuimarisha rutuba kwa mazao. Tunapozungumza ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kupata asali na nta, tusisahau kuwa nyuki pia wanahitaji uwepo wa misitu kwa mahitaji yao ya msingi: chakula na sehemu za kuweka mizinga.

Nyuki wakiwapo wengi ikolojia nzima ya kuzalisha chakula kutokana na kilimo itakwenda sawa sawa kwa nyuki kutembelea mazao. Katika harakati zao za kupata chakula chao kutoka kwenye maua mbalimbali wanaongeza uwezo wa kupata mazao mengi.

Ukiachilia mbali masuala ya kiikolojia, kutokana na misitu tunapata mazao ya misitu kama mbao, nguzo, fito, kuni, mkaa na kadhalika. Pia kuna faida nyingine nyingi za matunda ya asili kama ubuyu, ukwaju na mengineyo. Vilevile, kuna kupata mboga za kijani za asili kama mnavu; pia kuna uyoga wa asili unaopatikana sehemu zenye misitu ukiachilia wadudu wa aina mbalimbali ambao wengine ni chakula cha binadamu.

Kama nilivyokwishasema, misitu ina uhusiano mkubwa na wanyamapori. Misitu ya asili inawapa wanyamapori hifadhi mahali pa kujiburudisha kwa kupata malisho kutokana na miti yenyewe, lakini pia kwa nyasi nyingi zinazoota sehemu zenye misitu.

Mahali penye misitu hapakosi kuwapo unyevunyevu wa kutosha hivyo kusaidia kuwapo nyasi za kutosha na hivyo kuwafanya wanyamapori waweze kumudu maisha yao kwa kupata chakula na maji. Sehemu ambazo hazina misitu ya asili iliyohifadhiwa na kutunzwa, dalili za kupata unyevu au maji ni hafifu.

Mbuga zetu zikiwa na wanyamapori wa kutosha, Taifa litaweza kupata watalii wengi na hivyo tutuwezesha kuingiza mapato, lakini kiini na kivutio kikubwa kikiwa wanyamapori na mazingira mazuri ya misitu ya asili.

Kwa ufupi, misitu ni hazina kubwa ya Taifa, lakini inatelekezwa sana kiasi kwamba kila mwenye pumzi anafanya anavyotaka katika misitu ya asili. Kibaya zaidi, unapokuta hata watu kutoka nje ya nchi nao wakifanya wanavyotaka kwa sababu misitu mingi inakosa usimamizi wa kutosha.

Ninaposema hakuna usimamizi wa kutosha namaanisha kwamba yeyote anayetaka kupata chochote kutoka kwenye misitu yetu iwe ni kupata mbao, nguzo, mkaa na kadhalika, anajiona yuko huru kufanya hivyo kwa sababu anaingia eneo fulani lenye msitu haoni au kukutana na mlinzi wa msitu huo anayemuuliza: “Vipi ndugu, unaingia katika eneo la msitu uliohifadhiwa kufanya nini?” Vilevile kutoweka kwa misitu ni chanzo kwa mabadiliko ya tabia nchi.

Sababu ya kuanzishwa Wakala wa Huduma za Misitu

Idara ya Misitu na Nyuki katika Wizara ya Maliasili na Utalii ilionekana inashindwa kumudu shughuli za kulinda na kuhifadhi misitu ya asili. Ikaonelewa bora tuibadilishe iwe Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (Tanzania Forest Services-TFS).

Msingi wa kuifanya Serikali ifikie uamuzi huo takribani miaka mitatu iliyopita, ulikuwa ni kuweka mpango mzuri wa kuhifadhi misitu kwa kuisimamia. Ilionekana kuwa kwa kuwapo TFS urasimu kama ulivyo ndani ya Serikali utapungua zaidi na uwezo wa kusimamia misitu utaongezeka.

Kwa kipindi cha miaka mitatu tunaweza kusema sasa TFS imeishajipanga vya kutosha na iko tayari kufanya kazi muhimu ya kuilinda misitu yetu ya asili kwa faida ya Watanzania wote. Bado kumekuwapo kusuasua, lakini hii inatokana na uwezo mdogo wa TF -kwa maana ya walinzi.

Nimekuwa napata malalamiko kutoka kwa wadau kwamba TFS imekuwa mfanyabiashara zaidi kuliko kuilinda misitu. Wadau wanasema inafukuzana na wafanyabiasha wa mazao ya misitu barabarani badala ya kuwazuia wasikate miti bila ya vibali. Ni kweli hiyo ndiyo hali halisi ilivyo sasa, lakini hali hii inatokana na uwezo mdogo wa TFS.

Hata wakati mimi nikiwa katika utumishi wa Serikali nilikuwa nasema kama tumeshindwa kuisimamia miti isikatwe na ikakatwa, basi angalau tusishindwe kuwabana hao wanaokata miti bila kibali kwa kuwakamata na kuwatoza faini na kuwanyang’anya mazao.

Hii ilikuwa kwa dhana kuwa watumishi wachache waliokuwapo na vifaa duni angalau wajipange vizuri katika sehemu za kuyapitishia hayo mazao ya misitu na kuwakamata.

Hata hivyo, kunakuwapo changamoto kwa baadhi ya watumishi kutokuwa na dhamira ya kweli ya kuilinda misitu na badala yake kwa kushirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu wanahujumu nguvu za Taifa za kuilinda misitu.

Naamini TFS watafanya vizuri zaidi kwa kuongezewa nguvu maana kwa taarifa nilizopewa wamepata ruhusa ya kuajili watumishi 500 kwa kipindi cha mwaka 2015/2016.  Hii ni ishara nzuri ya kuweka nguvu kwenye kuhifadhi misitu ya asili. Wakala wa kuisimamia misitu kwa mamlaka waliyopewa kisheria wanatakiwa watunze misitu ambayo ni mali ya Serikali Kuu inayokaribia 600 nchini kote. Hii ni zaidi ya hekta milioni 13 za misitu ya asili iliyohifadhiwa kisheria.

Misitu hiyo imetawanyika maeneo mbalimbali nchini na mingi imevamia na kuharibiwa kwa kiasi kikubwa sana. Kwa TFS kuweza kuirejesha misitu yote hiyo katika hali yake ya kawaida ni kazi kubwa inayohitaji juhudi kubwa na ushirikiano mzuri kutoka vyombo mbalimbali kama Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya na mamlaka mbalimbali.

Mapato yatumike kulinda misitu

Kawaida Serikali huendesha majukumu yake kutokana na makusanyo ya kodi. Hata hivyo, wakoloni walipoanzisha misitu ya hifadhi kwa nguvu ya sheria hatimaye wakaanzisha utaratibu wa kuvuna baadi ya miti iliyokomaa kwa kutoza malipo (royalties). Waliweka utaratibu wa kutoa leseni za kukata miti ambayo imefikisha umri wa kuvunwa.

Kutokana na hali hiyo, viwango vya tozo vilitofautiana kutokana na aina ya miti. Kwa mfano, miti aina ya mipingo (Dalbergia melanoxylon), mivule (Milicia excelsa) au mininga (Pterocarpus angolensis) iliwekewa tozo za juu kuliko aina nyingine za miti. Matumizi ya mkaa kwa wakati huo yalikuwa madogo mno, hivyo ulikuwa hapakuwa na tozo kama ilivyo sasa.

Fedha zilizokusanywa kutokana na mazao ya misitu zilikubaliwa kutumiwa na Idara ya Misitu kutunza na kusimamia misitu. Hakuna hata senti moja iliyopelekwa Hazina kama mapato ya Serikali. Hivyo viwango vya tozo (royalties) vikawa vinatangazwa kupitia Gazeti la Serikali na kupewa namba ya tangazo (Government Notice – GN number). Mathalani, GN Na. kwa tozo za mazao ya misitu kwa wakati huu ni GN Na. 324 ya Agosti 14, 2015. Kwa maana hiyo, tozo za misitu siyo kama kodi nyingine ambazo zinatumika kuipatia mapato Serikali ambazo hutangazwa na Waziri wa Fedha na kuwekwa kisheria.

Tozo kwa mazao ya misitu hutangazwa na Waziri mwenye dhamana ya misitu na kujulikana kama (non-tax base charges). Kimsingi zinatakiwa zitumike kuimarisha utunzaji na usimamizi wa misitu nchini kwa asilimia 100.

Kwa sababu ambazo watoa uamuzi serikalini wanazifahamu wao, waliamua kuzifanya tozo zitokanazo na mazao ya misitu kuwa sehemu ya kodi za Serikali, Hapo ikawa chanzo cha kudorora kwa usimamizi wa misitu nchini.  Idara ya Misitu ikawa haipewi fedha za kuendesha shughuli za kuhifadhi na kuilinda misitu. 

Ikawapo lugha ya “hakuna haja ya kuilinda misitu maana inajiotea yenyewe hata kama ukiikata mingine itaota tu, haitakwisha”. Matokeo yake kada ya walinzi wa misitu ikafutwa katika utumishi wa Serikali.

Kusema kweli hili lilikuwa kosa kubwa maana sasa tunajutia hali ilivyo. Hadi sasa misitu haina ulinzi na mingi imekwisha uhai wake. Vimebaki vichaka tu. Mabwawa ya kuhifadhi maji ya kuzalisha umeme yamejaa tope na udongo. Vina vya maji vimepungua na kusababisha ujazo wa maji wakati wa mvua kuwa mdogo sana kiasi kwamba wakati wa ukame nchi inalazimika kupunguza uzalishaji wa umeme au kufunga kabisa mitambo.

Shughuli za kilimo hasa kupitia umwagiliaji pia nazo zinaathirika kwa kiasi kikubwa. Haya yote na mengineyo kama wanyamapori kuhangaika kupata chakula na maji; ni matokeo ya kushindwa kuitunza na kuisimamia misitu.

Nani alaumie? Hatuwezi kumlaumu Mwenyezi Mungu. Tumlaumu kwa lipi? Ni sisi binadamu tulio waharibifu na kwa kutojali kuyaweka sawa mazingira yetu. Uamuzi mwingine hauzingatii uhai wa Taifa letu na viumbe vyake, tukiwamo wanadamu.

Sasa tutafakali kwa kina na turejee tulikotoka-tuseme: “Kuteleza si kuanguka”. Tuliteleza, lakini hatujaanguka. Bado tumesimama, hivyo tufanye kweli. Serikali ya Awamu ya Tano iweke mkazo kwenye kuitunza na kuisimamia misitu nchini. Misitu ni uhai na nguzo muhimu kwa maendeleo ya Watanzania na pia ni tegemeo kubwa kwa dunia kwa kurekebisha mabadiliko ya tabia nchi.

Kusema kweli tukiitunza misitu, nayo itatutunza. Hakuna mwenye kutia shaka na hilo. Niiombe TFS ifanye kila linalowezekana ijadili suala la tozo kwa mazao ya misitu iendelee kuwa sehemu ya fedha kwa matumizi ya misitu. Isipelekwe Hazina. Kama TFS itaweza kukusanya  Sh bilioni 100 kutokana na tozo mbalimbali kwa mazao ya misitu, fedha hizo zitumike kuihifadhi na kuiendeleza misitu kwa faida ya Taifa letu.

Nchi ipate maji ya kutosha, kuzalishwe umeme unaotokana na maji (maana ni wa gharama nafuu); utalii uendelezwe kwa kuyaboresha mazingira ya wanyamapori na sekta za kilimo na ufugaji zitaneemeka. Uamuzi huo ni muhimu kwa Serikali ya Awamu ya Tano.

Hebu tuiwezeshe TFS ili isimamie rasilimali misitu ipasavyo, na iwapo watazembea, basi itakuwa ni udhaifu wao. Kwa hali ya sasa tutakuwa tunajidanganya kuwa tuliweka Wakala ili kuiponya misitu, kumbe hali si hivyo. Naamini Mwenyezi Mungu atakisikia kilio hiki na kuwawezesha watunga sera na wafanya uamuzi kuwa makini katika suala la kuhifadhi na kuilinda misitu ya asili. Hakuna lisilowezekana, ni kuamini na kutenda na kuongoza njia kwa kufanya uamuzi sahihi.

 

Mwandishi wa makala hii, Dk. Kilahama ni Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki, mstaafu katika Wizara ya Maliasili na Utalii. Anapatikana kupitia simu: 0783 007 400.

1085 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!