OLIMPIKIKwa mara ya mwisho Tanzania kupata medali katika mashindano ya Olimpiki ilikuwa ni mwaka 1980 michezo hiyo ilipofanyika katika nchi ya Urusi ambapo Filbert Bayi na Suleiman Nyambui walipata medali za fedha.

Katika mashindano hayo Bayi alitwaa medali hiyo kutoka katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na Nyambui aliipata baada ya kushiriki mita 5,000.

Tangu kipindi hicho tumekuwa wasindikizaji katika mashindano bila kuwa na mafanikio yoyote, huku viongozi wakikosa akili ya ziada kukabiliana na tatizo hilo.

Mpaka kufikia leo ni miaka minne iliyopita nchi yetu ilipokuwa miongoni mwa nchi zipatazo 204 zilizopata nafasi ya kushiriki michuano ya Olipmpiki katika Jiji la London ambako Tanzania iliambulia patupu pia.

Baada ya kumalizika kwa Olimpiki ya London viongozi wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki (TOC) na wadau wote wa michezo walikuwa wakijua kuwa miaka minne ijayo yaani (2016) kungekuwa na mashindani mengine.

Kwa maana hiyo ulikuwa ni wakati mwafaka kwa Kamati ya Taifa ya Olimpiki kuanza maandalizi ya maana ya mashindano yajayo ya 2016.

Leo hii mashindano ya Rio yanapoanza ni aibu kwa nchi kama Tanzania yenye watu zaidi ya watu milioni 45 kupeleka wachezaji saba.

Hivi kama kweli tunamaanisha tunachokiimba, tulishindwa nini kuanza kuandaa timu ya soka, waogeleaji, wanariadha, kuruka viunzi juu, chini na michezo mingine mingi kwa lengo la kwenda kutoa ushindani na si kwenda kama watalii?

Serikali na wadau wanashindwa nini kujifunza kutoka kwa wenzetu waliopiga hatua na kupata mafanikio katika mashindano haya ya Olimpiki?

Kama taifa kwa nini tunashindwa kutumia mashindano ya Umitashumta na Umiseta kupata wachezaji wapya wachanga wenye viwango?

Kwa mfano mwogeleaji wa China Ye Shiwen aliyetwaa medali mbili za dhahabu na kuvunja rekodi ya dunia ya kuogelea huko London mwaka 2012 alikuwa na miaka 16 tu.

Mifano ipo mingi, lakini huo ni mmoja unaoonyesha jinsi wenzetu walivyo makini katika kugundua vipaji ndani na nje ya nchi zao.

Kwa upande wa Serikali nayo ni kama inaubariki uzembe huu kwa kugeuka watu wa kukabidhi bendera bila hata ya kuhoji mikakati waliyonayo viongozi wa Kamati ya Olimpiki.

Cha ajabu TOC miaka nenda rudi imekuwa ikiwategemea wanamichezo walewale bila ya kuwepo kwa mikakati ya kuibua vipaji vingine vipya.

Tanzania katika mashindano hayo inakwenda kushiriki michezo mitatu tu kati ya 28, ambapo safari hii mchezo wa ngumi umekuwa ukifanya vizuri kimataifa lakini hautakuwa na mwakilishi baada ya kushindwa kufuzu.

Katika michezo ya mwaka huu, Tanzania inawakilishwa na watu 12, huku kati yao saba wakiwa wachezaji na watano ni viongozi. Tayari timu hii imejiandaa kwa staili tofauti tofauti kiasi cha kutia shaka ushiriki wake.

Inatia shaka ushiriki wake kwa sababu timu kama ya waogeleaji hawakuwa na kambi ya pamoja huku kila mmoja akifanya mazoezi kivyake.

Huu ni upuuzi na uzembe wa hali ya juu kwa viongozi kushindwa kupata wachezaji wa masumbwi kwa kigezo cha kushindwa kufikia viwango huku wakibebana viongozi watano kwenda Rio.

Mashindano ya Olimpiki yameanza rasmi Agosti 5, mwaka huu na Tanzania itawakilishwa na wanamichezo hao saba ambapo kati yao wanne ni wanariadha, wawili waogeleaji na mmoja anacheza mchezo wa judo.

Wakati Tanzania ikipeleka wanamichezo saba majirani zetu Kenya wamepeleka kikosi thabiti chenye wanamichezo 50 kitaongozwa kwa mara nyingine na nahodha Ezekiel Kemboi. Kemboi aliingoza Team ya Kenya katika kutwaa taji la dunia mjini Beijing.

Michezo ya Olimpiki ni mashindano makubwa yanayojuisha michezo mbalimbali duniani inayofanyika kila baada ya miaka minne.

Michezoya Olimpiki ni ya kale kwani ilifanyika tangu tarehe isiyojulikana, lakini kwa uhakika kuanzia mwaka 776 KK hadi mwaka 393 BK katika Mtaa wa Mahekalu wa Olimpia kwenye rasi ya Peloponesi nchini Ugiriki, ndiko ilikokuwa ikifanyika.

Michezo ya Olimpiki ya Kisasa ya kwanza ilitokea mwaka 1896 mjini Athens (Ugiriki). Mwazilishi alikuwa Mfaransa Pierre de Coubertin aliyetaka kutumia kielelezo cha michezo ya kale kwa kujenga uhusiano mzuri kati ya vijana wa nchi mbalimbali na kuwapatia nafasi ya kushindana kwenye uwanja wa michezo badala ya uwanja wa vita.

Michezo hii ya kisasa imeendelea kila baada ya miaka minne isipokuwa 1916, 1940 na 1944 kwa sababu ya Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia.

Michezo ya kisasa hufanyika katika mji tofauti kila safari michezo ya 2004 ilifanyika Athens, mwaka 2008 ilifanyika huko Beijing na 2012 jijini London lengo likiwa ni kudumisha michezo duniani.

Ifike wakati viongozi wa Kamati ya Taifa ya Olimpiki Tanzania iache kufanya kazi kwa kutimiza wajibu ili mradi waonekane watu wamekwenda Rio huku wakijua fika kuwa hakuna uhakika wa medali.

By Jamhuri