Mwaka 1958, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alizungumza maneno ya maana sana kuhusu ardhi.

 

Alisema, “Katika nchi kama yetu, ambayo Waafrika ni maskini na wageni ni matajiri, kuna uwezekano mkubwa kwamba Mwafrika akiruhusiwa kuiuza ardhi, katika miaka themanini au miaka mia ijayo, ardhi yote ya Tanganyika itamilikiwa na matajiri wageni, na wenyeji watakuwa watwana. Lakini hata kama wageni wasingekuwa matajiri, litaibuka tabaka la Watanganyika matajiri wajanja. Tukiruhusu ardhi iuzwe kama kanzu, katika muda mchache, kutakuwa na kundi dogo la Waafrika wakiwa na ardhi na walio wengi watakuwa watwana.”

Kitu pekee ambacho Mwalimu hakukilenga vizuri, ni miaka. Alidhani kwamba miaka 80 au 100 hali ndiyo inaweza kuwa mbaya. Sasa ni miaka 54 tangu atoe wosia huo mzito kwa Watanzania. Sioni kama tutafika miaka hiyo aliyoitaja Mwalimu kabla ya Tanzania kuingia kwenye vurugu kubwa za kugombea ardhi.


Mara kadhaa nimehadharisha jambo hili, lakini kama vile tuliologwa, viongozi wetu waandamizi hawaonekani kabisa kuguswa na jambo hili. Wimbo wao ni kwamba ardhi isiuzwe kwa wageni! Wageni si tu kwamba wananunua, bali wanapoka ardhi sana . Lakini matajiri Watanzania nao sasa wanashindana kununua. Maelfu ya ekari yananunuliwa kila uchao. Matajiri wanatumia udhaifu wa wananchi masikini kuhodhi maelfu ya ekari kwa fedha kidogo mno.

 

Hatari hiyo imemfanya Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Ahmed Kipozi, awaangukie wananchi kwa kuwasihi wabakize ardhi kwa ajili ya manufaa yao na kwa vizazi vyao. Sidhani kama kaeleweka.

 

Taarifa zinasema Tanzania inaongoza katika Afrika Mashariki kwa uuzaji ardhi kiholela kwa watu binafsi na kampuni za kimataifa.


Inakadiliwa kuwa ekari milioni 2.2 za Tanzania zimeshaingia mikononi mwa wanaoitwa wawekezaji kutoka ughaibuni. Wanatumia umbumbumbu wa wananchi wetu kujipatia ardhi. Ten basi, wanasaidiwa na kauli kama zile za Waziri Mkuu Mizengo Pinda, za kuwataka wananchi wasione wawekezaji kuwa maadui. Ndiyo maana Pinda anafanikisha mpango kwa kampuni ya Marekani kuhodhi eneo la ukubwa wa karibu nchi nzima katika Mkoa wa Katavi.


Hapa sitaki kabisa kugusa takwimu zilizokwishatolewa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema). Halima ameweza kuorodhesha malefu ya ekari zilizochukuliwa na wageni. Wengi wameingia kwa kisingizio cha uwekezaji. Wametumia ardhi waliotwaa kujipatia mikopo ya mabilioni ya fedha katika benki na vyombo vya fedha vya kimataifa. Dhamana ni ardhi yetu. Uwekezaji walioahidi hauonekani. Mfano mzuri ni wa Kisarawe mkoani Pwani ambako malefu ya ekari alikabidhiwa mwekezaji wa mibono. Hakuna chochote kinachoendelea, na ardhi ni yake. Wananchi wanalia.


Hali ni hiyo hiyo katika mikoa yote nchini. Migogoro ya ardhi inaongezeka. Idadi ya watu inaongezeka. Ajira namba moja ya Watanzania wengi ni kilimo. Ardhi kwa ajili ya mifugo inapungua. Ufugaji wenyewe ni wa kuhamahama. Itakuwaje kama vijana wengi watazaliwa na kukosa ardhi? Je, kwa staili hii na upofu wa Serikali yetu, nini kitaepusha vita ya ardhi miaka ijayo?


Tumeshindwa kabisa kujifunza kwa ndugu zetu Zimbabwe . Mapambano ya ardhi yameiweka pabaya nchi hiyo. Ardhi nzuri imehodhiwa na wazungu wachache. Kenya hali ni kama hiyo.


Ni vema basi, Katiba yetu mpya ikalipa nguvu suala la ardhi ili kuondoa haya mamlaka ya viongozi wa vijiji na Serikali kugawa ardhi ya Tanzania kadri wanavyojisikia. Uelewa wa wananchi wetu, hasa vijijini ni mdogo. Kuwataka wao ndiyo wazungumze na wawekezaji ili wawape ardhi, ni kuiweka rehani nchi yetu Ndiyo maana tumeshuhudia baadhi ya wanaojiita wawekezaji wakinunua ekari moja kwa gharama ya msuli!


Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mohamed (CUF) mnamo Julai 12, mwaka huu, akichangia Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2012/2013 ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alizungumza maneno ya msingi sana kuhusu ardhi. Inawezekana maneno yake yamepuuzwa kwa sababu ni mbunge wa upinzani, au kwa sababu hana jina kubwa. Nilikuwapo bungeni.


Naomba ninukuu maneno yake, alisema, “Mheshimiwa Naibu Spika, Profesa (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anna Tibaijuka) ni mchapakazi na ana uzoefu mzuri kwenye nyumba na maendeleo ya makazi. Tuna imani naye tangu alipokuwa UN-Habitat. Tunakuomba mama uchape kazi, usiangalie nyuma.


“Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kwa dhati Mheshimiwa Naibu Waziri, ni mwelewa, mchapakazi na akiahidi kitu anafanya. Mheshimiwa Naibu Waziri amesaidia sana kurudisha amani katika Kijiji cha Pande B. Naomba atakapofanya majumuisho aelezee mgogoro huo, utatatuliwaje.


“Mheshimiwa Naibu Spika, naandika hili kwa masikitiko makubwa sana . Tanzania bado hakuna udhibiti wa uuzaji/ununuzi wa ardhi, holela. Suala la ununuzi/uuzaji wa ardhi Tanzania liko kiholela sana , tena sana kwa sababu hakuna utaratibu/mfumo wa kisheria unaoeleweka wa kudhibiti hili.


“Mheshimiwa Naibu Spika, watu wenye pesa/mitaji

mikubwa wamekuwa wakiwadanganya/dhulumu wananchi wa chini kwa kununua ardhi yao kwa bei ya chini na kuwaacha masikini. Hata wageni wanatumia fursa hii kwa wananchi wa chini, na mbaya zaidi ni kupitia viongozi wa kijiji, kata na kadhalika.


“Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waziri ukija kufanya majumuisho, uniambie: Je, unafahamu huu uuzwaji/ununuzi wa ardhi kwa wageni kiholela? Je, ni hatua gani Wizara yako inajipanga kuzichukua? Chonde chonde, ardhi yetu inakwisha. Kwa mfano, Tanga, ardhi yetu imenunuliwa sana na Wakenya kwa kupitia Mombasa . Hali inatisha na inasikitisha sana .


“Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapaswa kuwa mlinzi wa ardhi ya wananchi wa chini kwa kuweka utaratibu au mfumo wa kisheria ambao hata walaghai wakiwaendea wananchi, siyo rahisi kuwadanganya au kuwadhulumu. Mbaya zaidi, kinachonichanganya, hata wageni toka nje tena wengi wanatumia mwanya huu wa uuzwaji wa kiholela kununua ardhi kiulaghai kwa sababu wana pesa nyingi.


“Mheshimiwa Naibu Spika, mfano dhahiri, miongoni mwa mifano mingi ni katika Mkoa wa Arusha hasa maeneo ya Sanawari, Mianzini, Ngaramtoni na maeneo ya karibu. Naibu Waziri anafahamu zaidi maana ni Jimbo lake.


“Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri aniambie, hivi anafahamu kweli kama Gerezani yote Kariakoo, imenunuliwa na Wasomali na inaitwa Somali Land ? Mtaa huu wa Gerezani Wasomali wamenunua wote. Ni hatari sana, kwani sijui wametumia utaratibu gani.


“Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuwa Rais ndiye msimamizi mkuu wa ardhi Tanzania na anaweza kufanya maamuzi yoyote juu ya ardhi bila kuhojiwa na kuomba. Mheshimiwa Waziri achukue nafasi hiyo kutufikishia maombi yetu kwa Halmashauri ya Jiji la Tanga, tunayoomba kufutwa kwa hati kumi za mashamba ya mkonge na shughuli za maendeleo.


“Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na usimamizi mdogo wa ardhi, leo hii kuna migogoro mingi sana, mojawapo ni mgogoro baina ya CDA na Manispaa ya Dodoma unaotokana na mkanganyiko huu wa usimamizi wa ardhi. Wakati CDA ina ardhi, Halmashauri ya Manispaa ina ushawishi mkubwa kwa watu kupitia madiwani.


Mara kadhaa hili limepelekea (limesababisha) kuibuka migogoro isiyo ya lazima, na mbaya zaidi ni kucheleweshwa kwa miradi ya maendeleo kutokana na ubishani baina ya taasisi hizi mbili. Mgogoro uliopo ni wa kisheria, maana kimsingi Manispaa ndiyo iliyopaswa kumiliki ardhi na wala siyo CDA.


“Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Waziri ajitahidi kutatua migogoro hii ya ardhi ambayo ni mingi.” Mwisho wa kunukuu.


Ndugu zangu, tufafakari, tuchukue hatua. Ardhi ya Tanzania inachukuliwa na matajiri wa ndani na nje wakati vijana wetu wakiwa ‘bize’ kuendesha bodaboda. Waking’amka hawatakubali. Watashika silaha kutaka kurejesha ardhi yao . Tuanzishe mjadala wa kitaifa ili tupate njia sahihi za kukabiliana na janga hii.


By Jamhuri