Tumkumbuke nguli Shakila Binti Said (1)

Ni zaidi ya miaka miwili tangu atutoke Shakila Binti Said aliyekuwa nguli katika miondoko ya muziki wa taarabu humu nchini na Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.

Wakati wa uhai wake, aliweza kuonyesha umahiri wake wa utunzi na uimbaji wa taarabu katika bendi zote alizowahi kuzitumikia.

Shakila alifariki dunia ghafla, ambapo binti yake wa mwisho aitwaye Shani, alisikika kupitia vyombo mbalimbali vya habari akisema kuwa mama yake Bi. Shakila alianguka ghafla alipokuwa akifagia muda mfupi mara baada ya kufanya ibada ya magharibi nyumbani kwake Charambe, jijini Dar es Salaam, Agosti 19, 2016.

Alikuwa na weledi wa kujua jinsi ya upangiliaji wa mashairi na werevu wa kutumia maneno ya lugha adhimu ya Kiswahili katika nyimbo zake zote alizoimba.

Shakila hakutunga nyimbo za mapenzi pekee, aliweza kutunga na kuimba nyimbo zinazoigusa jamii; za siasa na ukombozi.

Bi. Shakila alizaliwa mwaka 1947, wilayani Pangani, Mkoa wa Tanga.

Miaka ya nyuma zao la mkonge lilikuwa na soko kubwa ulimwenguni, Tanganyika wakati huo ikuwa nchi mojawapo iliyokuwa ikizalisha kwa wingi zao hilo.

Wamiliki wa mashamba ya mkonge walikuwa wakiwachukua watu ‘manamba’ kuwapeleka kufanya kazi ya vibarua katika mashamba hayo.

Manamba hao walipofika huko waliamua kuoa wake akiwemo mzee Said Hamis, baba yake, aliyekwenda Tanga akitokea wilayani Kiomboi, mkoani Singida, akifuatana na vijana wenzake kutafuta vibarua katika mashamba ya mkonge.

Mzee huyo alimuoa mama yake aliyekuwa wa kabila la Kizigua kutoka mkoani Tanga. Walizaa mtoto wa kike ambaye ni Shakila.

Shakila alikulia katika malezi mema ya baba na mama yake, alipofikisha umri wa kwenda shule, aliandikishwa kuanza masomo katika Shule ya Msingi Pangani, mkoani Tanga.

Shakila aliolewa na mume wake wa kwanza Khatibu Akida akiwa na umri wa miaka 11, wakafanikiwa kupata mtoto mmoja.

Mume huyo alikuwa mbofya kinanda maarufu, ambaye ndiye aliyemshawishi kuingia katika tasnia hiyo ya muziki wa taarabu.

Shakila alikubali ushauri wa mumewe, akaanza kufanya mazoezi makali ya kutunga na kuimba nyimbo za taarabu.

Baada ya kuonekana kuwa ana uwezo mkubwa, Khatibu alimshawishi kujiunga katika kundi la Kijamvi Taarabu lililokuwepo mjini Pangani, mkoani Tanga.

Hakudumu kipindi kirefu, akalazimika kuhamia mjini Tanga kumfuata mumewe Khatibu Akida.

Alipofika huko alijiunga katika kundi la Al Watan, lakini kwa sababu ambazo hazikuelezwa, Shakila akiwa katika kundi hilo hakupewa nafasi ya kuimba mbele ya kadamnasi.

Kitendo hicho kilisababisha yeye na mumewe baada ya muda mfupi wakahamia katika kundi lililokuwa likimilikiwa na mzee Kiroboto la Young Novelty mwaka 1961.

Ikumbukwe miaka ya 1960 hadi 1980 sinema za Kihindi zilichukua nafasi kubwa katika kumbi nyingi hapa nchini. Katika sinema hizo watu walimshuhudia mwimbaji wa nyimbo za Kihindi aliyekuwa akiitwa Shakila.

Hivyo, wapenzi na mashabiki wa miondoko ya taarabu wa wakati huo walilinganisha na sauti ya Tatu Said kuwa haitofautiani sana na ya Shakila, wakampachika jina hilo.

Shakila Binti Said alikuja kuwa miongoni mwa waanzilishi wa kundi la taarabu la Black Star, ambako alionyesha cheche zake baada ya kuachia tungo yake ya ‘Duniani Nakupenda Wewe’.