Rais Jakaya Kikwete akiwa katika mkutano wa SADC nchini Msumbiji, alimhakikishia Rais Joyce Banda wa Malawi kuwa kamwe Tanzania haitaingia vitani dhidi ya ndugu zao, Malawi.

Akamhakikishia kuwa wanaosema Tanzania inajiandaa kupigana na Malawi ni wapinzani na vyombo vya habari vinavyoshabikia jambo hilo (vita).

Kauli ya Rais wetu ilikuja kutokana na msimamo awali uliooneshwa na Kaimu Kiongozi wa Shughuli za Serikali Bungeni, Samuel Sitta, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, na baadaye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Edward Lowassa.

Membe aliliambia Bunge: “Mheshimiwa Spika, tunazungumzia maisha ya Watanzania wapatao 600,000 wanaoishi kwenye mwambao wa Ziwa Nyasa. Kwao wao, Ziwa Nyasa ni urithi wao – natural heritage. Kwao wao, Ziwa Nyasa ni chanzo cha uzima wao na maendeleo yao. Kwa vyovyote vile Serikali inayo dhamana ya kuwalinda watu hawa kwani ni wananchi wetu.


“Serikali ya Tanzania inapenda kuchukua nafasi hii kuyaonya na kuyataka makampuni yote yanayofanya shughuli za utafiti kwenye eneo la ziwa hilo kusitisha kuanzia sasa – napenda kurudia sehemu hiyo – napenda kuyaonya makampuni yote yanayofanya utafiti kwenye eneo hilo kuanzia {leo Jumatatu} kuacha shughuli za utafiti katika maeneo hayo.

 

Serikali haitaruhusu – narudia – Serikali haitaruhusu utafiti huu kuendelea hadi makubaliano na majadiliano kuhusu mpaka yatakapofikiwa kati ya nchi mbili, yaani Tanzania na Malawi. Let us give diplomacy a chance.


“Mheshimiwa Spika, Serikali inapenda kuwahakikishia wananchi wote wa eneo la Ziwa Nyasa kuendelea na shughuli zao ziwani na nchi kavu kama kawaida, na bila ya wasiwasi wowote kwa sababu serikali yao ipo macho, ipo imara, ipo tayari kulinda mipaka ya nchi yetu kwa gharama yoyote.”


Mzee Sitta yeye hakuwa na mengi, bali alisema, “Tanzania ipo tayari kupambana na aina yoyote ya uvamizi. Wananchi wasiwe na wasiwasi, waendelee na shughuli zao kama kawaida”.

Lowassa, kwa niaba ya Kamati, alisema Tanzania imejiandaa kiakili na kivifaa kuingia vitani kama italazimika kufanya hivyo. Akasema Kamati yake imeridhishwa na maandalizi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).


“Tumepewa maelezo na jeshi letu na tumeridhika kuwa ikibidi kuingia vitani, jeshi letu liko vizuri sana na limejipanga vizuri sana kwa uhakika, kiakili na kivifaa.”


Kabla ya Lowassa kuzungumza na waandishi wa habari, alifanya kikao cha faragha kilichohusisha wajumbe wa Kamati hiyo na makamanda wa JWTZ walipofika bungeni kutoa taarifa kwa Kamati hiyo. Hata hivyo, katika tamko hilo, Lowassa alisema Tanzania inatarajia mgogoro huo utamalizika kwa njia za kidiplomasia kwa sababu Watanzania na Wamalawi ni ndugu wa muda mrefu.


Kwa ujasiri, Lowassa akasema, “Ikibidi kuingia vitani jeshi letu liko vizuri sana na kama ilivyo ahadi yao (JWTZ), wako tayari kulinda mipaka ya nchi yetu hadi tone la mwisho. Tunasali sana tusifike hapo,” alisema Lowassa na kuongeza: “Tunategemea hatutafika huko, lakini kwa heshima ya nchi yetu kama ikibidi kufika huko (vitani) tutafika kulinda mipaka yetu”.


Nimejaribu kurejea kauli za viongozi hawa kuonesha tu namna walivyoweza kuwajenga kiimani wananchi juu ya mzozo huu ambao kama alivyosema Membe, unahatarisha maisha na uchumi wa Watanzania zaidi ya laki sita.


Niseme wazi kuwa naungana na msimamo na kauli madhubuti zilizotolewa na viongozi hawa. Hatuwezi kuwa dhaifu au wapole katika kutetea mipaka ya nchi yetu. Tumekubali madini yetu yaondoke kwa mhuri wa mikataba mibovu. Sasa hatuwezi kukubali tena ardhi (ziwa) nayo ichukuliwe. Malawi ni ndugu zetu wa damu, lakini hata ndugu hupigana pale inapolazimu!

Haiwezekani ndugu wawe na urithi kisha mwingine atake kupoka mali ya mwenzake, na mwisho aachwe hivi hivi tu (scot-free) kwa kigezo cha undugu! Hiyo haipo. Au, haiwezekani ndugu ashike kisu, atake kukutoa roho, wewe uchekelee tu kwa sababu ni ndugu! Ziwa Nyasa ni uhai wa Watanzania maelfu kwa maelfu. Hawawezi kufa kwa kiu na kiuchumi kwa kuwaheshimu tu ndugu zao Wamalawi wanaotaka kujitwalia lote. Kuwakubalia ni uzuzu. Hilo halipo.


Katika diplomasia kuna kitu kinaitwa Gun Boot Diplomacy (Diplomasia ya Vitisho). Aina hii ya diplomasia ingawa si ya kiungwana sana, lakini ina umuhimu wake. Marekani wanaitumia sana kufanikisha mambo yake.


Mara kadhaa wamefanikiwa kwenye mambo yao bila kurusha risasi au bomu. Kwa maneno mengine ni kwamba kwenye diplomasia hii, unazungumza na “mbaya” wako ukiwa umejiweka wazi kwamba msipoafikiana, kitakachofuata ni kitu fulani.


Baada ya kauli hizo za viongozi niliowataja hapo juu, wapo waliojitokeza kuwakejeli. Tukaambiwa kwamba mwenye mamlaka ya kutangaza vita ni mmoja tu, yaani Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete.


Gazeti moja likaenda mbali zaidi na kuandika kwamba JWTZ wamemshushua Lowassa kwa “kutangaza vita”, kwa maelezo kwamba hana mamlaka hayo. Nilijaribu kupitia kauli ya Lowassa. Sikuona ametangaza vita.


Habari ile ilikuwa na kila aina ya vimelea vya “ngwala za kisiasa”. Alichofanya ni cha kawaida. Kwanza, yeye kama kiongozi wa Kamati ya Bunge yenye dhima ya ulinzi na usalama wa nchi, na Bunge kama chombo cha kuisimamia Serikali, alitoa maelezo yaliyogota kwenye wigo wa mamlaka yake. Pili, kama Mtanzania, ni lazima awe na kauli ya kujipa moyo na kuonesha ujasiri ili adui ajue kuwa mpango wake unapingwa.


Sitta alitoa kauli hiyo kulingana na nafasi aliyokuwa nayo bungeni. Kimsingi asingeweza kukaa kimya wakati akiwa Kaimu Waziri Mkuu. Kukaa kimya ni jambo ambalo lisingekuwa la busara. Kwa nafasi aliyokuwa nayo, tusingetarajia kusikia akiwatia hofu wananchi, hasa wa mpakani na Malawi.


Membe alitoa msimamo wa Serikali. Tunatambua kuwa msimamo wa aina hiyo hauwezi kutolewa bila kumhusisha Amiri Jeshi Mkuu.


Sasa kama hivyo ndivyo, ilikuwaje Rais Kikwete, akiwa Msumbiji, kutoa kauli za kuwavunja nguvu viongozi wenzake? Je, alilenga kumhadaa Rais Joyce au kweli alidhamiria kuwashushua Sitta, Membe na Lowassa? Je, ni kweli kwamba Malawi ikitaka kwa namna yoyote kulitwaa ziwa lote, Tanzania haitawahami wananchi wake kwa mtutu?


Tangu Rais Kikwete atoe kauli yake, tena akisema “wanaotaka vita ni wapinzani”, na kwamba jambo hili linakuzwa na vyombo vya habari, tumeona na kusikia msuli wa Malawi ukizidi kuimarika.


Pigo la karibuni ni Rais wa nchi hiyo kuamuru timu yake ya majadiliano ya mgogoro wake na Tanzania kujitoa kwenye mazungumzo. Kisa, eti Tanzania imetoa ramani mpya! Kwa maneno mengine ni kwamba ramani ya Tanzania inayoonesha mipaka ya mikoa na wilaya mpya haikupaswa kuandaliwa na kuzinduliwa hadi hapo mgogoro kati yetu na wao utakapomalizika!

 

Jeuri hii ameipata zaidi baada ya mwenzake kumhakikishia kwamba hapatakuwapo na vita wala matumizi ya nguvu katika kuumaliza mgogoro huu. Sasa tumejiegemeza kwenye Mahakama ya ICJ.


Kwa sheria za kimataifa kuhusu mpaka baina ya nchi zinazotengwa na maji, tunaweza kushinda. Lakini tuna hakika gani tutashinda, hasa ikizingatiwa kuwa Uingereza wana masilahi kwenye mgogoro huu?


Rais Kikwete alivishutumu vyombo vya habari kwa “kuukuza mgogoro”. Huko ni kuvionea vyombo vya habari. Daima, chombo cha habari linapokuja suala la kuitetea nchi kinapaswa kuwa upande wa nchi. Magazeti yanapaswa kuandika, “Tutawapiga…”, “Majeshi yetu”, “Tutashinda…” Hata kama kuna tofauti za kisera na kimtazamo, kwenye suala la kuitetea nchi ni lazima tofauti hizo zizikwe hata kama ni kwa muda.


Nakumbuka tukiwa Moroni, Comoro, Kanali Sukambi Mahela alituambia; “Waandishi wa habari mkifanya kazi yenu, tunaweza tusirushe risasi hata moja.”


Kanali Mahela alitambua kuwa vyombo vya habari vina kazi kubwa ya kumlegeza adui. Hapo nikakumbuka msemo wa Wazanaki unaosema: “Omunwa ndugabo”, yaani mdomo ni uzio. Maneno pekee yakipangiliwa, yanaweza kumfanya adui ashindwe kutekeleza azma yake. Watoto wa mjini wanasema “mkwara”.

 

Umoja ni nguvu. Kwa kulijua hilo, Malawi sasa imekuwa moja dhidi ya “maadui” Tanzania. Wanasiasa na vyombo vya habari wamekuwa na msimamo mmoja –   Ziwa Nyasa (Malawi) lote ni lao! Rais Joyce amewaita viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani. Amejadiliana nao. Amesema suala la mpaka lina masilahi ya Malawi nzima, hivyo hakuna kumtenga yeyote awaye katika mapambano hayo.


Amekutana na viongozi wakuu katika makazi yake ya Sanjika, Blantyre. Walioshiriki ni Kiongozi wa Upinzani, John Tembo (MCP), Dk. George Mtafu na Friday Jumbe (UDF), Kamlepo Kalua (MDP), Gwanda Chakuamba (NRP), Mark Katsonga Phiri (PPM), Kamuzu Chibambo (Petra) na George Nnensa (Mafunde).


Wakati Rais Joyce akiwaunganisha Wamalawi na kuwa kitu kimoja kudai ziwa, sisi Tanzania ni porojo za kukatishana tamaa, kulibeza letu, kuogopa athari zinazotokana na vita na kuonesha kutojali. Huu ni mtaji mzuri sana kwa Malawi.


Sasa ni wakati wa Watanzania na taasisi zote kuungana kukabiliana na mzozo huu ambao wapo wanaodhani kuwa ni mdogo. Wakuu wa vyama vya upinzani wajitokeze kuiunga mkono Serikali. Mjadala wetu ulenge kutufanya Watanzania tuwe kitu kimoja kama wakati wa Vita ya Kagera.


Sisi tunaokuwa na misimamo ya aina hii hatuna maana kwamba tuna asili ya kupenda vita, bali tunasukumwa na moyo wa kulipenda na kulitetea Taifa letu. Shime Watanzania tuungane ili tuhakikishe nusu ya Ziwa Nyasa inabaki kuwa mali halali ya Watanzania.

 

 

 

1352 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!