MSUYAWaziri Mkuu mstaafu, Cleopa David Msuya amesema kwamba Tanzania kwa sasa inahitaji Rais mwenye uamuzi mgumu, mwenye kariba ya udikteta.
Waziri Mkuu huyo mwenye rekodi ya aina yake ya kutumikia wadhifa huo kwa marais wawili wa awamu ya kwanza na ya pili, anasema, “Hayo ni mapinduzi yanatakiwa pia yafanyike ndani ya CCM.”
“Rais na mwenyekiti mpya wa CCM anayekuja itakuwa kazi yake ni kupangua msingi wa kubebana. Na kwa upande wa serikali tunahitaji Rais mgumu,” anasema Msuya.


Anasema kwamba haya yote yanatokana na wananchi kuchukia mtu anayehusishwa na rushwa, kula fedha za umma, ufisadi na kwamba manung’uniko hayo yameenea.
Anasema kwamba kwa hali ilivyo sasa, Watanzania hawataki tena mateso na kwamba ipate kiongozi anayeweza kujibu maswali magumu dhidi ya maisha yao.


“We need someone like a dictator person. Anayetafuta majibu kwa haraka. Hii ni kwa sababu, mfumo wa sasa hauleti majibu stahili kwa wakati,” anasema Msuya katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake, Dar es Salaam.
Anasema kwamba kwa sasa Tanzania haihitaji Rais wa kutoa hotuba na badala yake ipate mtu mwenye kuamua na kukabiliana na matatizo kulingana na sasa.


“Sasa tuombe Mungu labda tutapata viongozi wenye zero tolerances ya ufisadi, rushwa na mambo mengimengi. Hata kwenye utendaji wa Serikali mambo kwa sasa sio mazuri hata kidogo. Mpaka ukiona Rais naye analalamika ujue kamba system is not delivered (mfumo haujibu).
Anasema, “Kwa hiyo anayekuja itabidi kweli alitikise hili. Kama huyo Waziri wa Ardhi huyo kijana William Lukuvi, inaelekea ameanza kulitikisa hili. Maana nimemsikia juzi namna anavyopambana na mambo ya ufisadi kwenye ardhi. Kwenye Wizara ya Ardhi unahitaji mtu kama yule,” anasema.
Anasema kwamba wananchi sasa wanatafuta mtu ambaye anaonekana kuwa na mlengo wa kutoa utumishi, “Sio kula. Maana kuna watu wanataka kwenda ikulu ili aite rafiki zake, ili wagawane mali.


“Kusema waende pale wakawahudumie Watanzania wana shida zao. Watu wanatafuta mtu aina ya akina Julius Nyerere hivi. Ni mtu gani huyo? Ahangaike, atuhudumie sisi. Tundokane na shida zetu na matatizo yetu,” anasema.
Anasema sifa nyingine ya kiongozi huyo ni kuwa mjuzi wa masuala ya uchumi kwa sababu utawala wa sasa sio kama enzi zake na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.


“Sasa kuna watu wanaojua mengi na wako wengi. Upate mtu ambaye akikaa mbele ya wasomi, anaweza kusema jambo. Kazi ya kukuza uchumi ni fundamental (muhimu) na kama tukikosa mtu huyo anayeweza kukuza uchumi haraka kwa kuelewa mifumo mbalimbali ya uchumi na kushirikisha njia mbalimbali.
“Rais mwenye uhusiano mzuri wa kimataifa utakaofanya kuwe na marafiki ambao watasaidia mambo mengi kama namna ya kuboresha uchumi na kuondoa matatizo ya kivita nakadhalika.
“Watu wanatafuta watu wa namna hiyo. Msije kuweka mtu jambazi au fisadi. Hii nchi itapasuka. Inaweza kuwa kama Nigeria au Jamhuri ya Kati au Zaire (DRC) wakati wa Mobutu Seseseko.
“Tunataka tupate mtu mwenye mwelekeo wa Kinyererenyerere hivi. Mwadilifu, asiye na ubinafsi, asiye mlaji wa mali na umma, asiye mpendeleo hivi vyote.


Anasema kwamba taifa sasa halina budi kumuomba Mungu asaidie kupata kiongozi wa namna hiyo hasa wakati huu wa mchakato ndani ya vyama.
“Hawa watu wanajua. Viongozi wetu wanajua. Hawa akina Jakaya Kikwete, mheshimiwa Rais wanajua. Naamini watatupatia kiongozi mzuri.
“Wakitupatia mtu tofauti, kwa hizi hisia zinazojengeka vichwani mwa watu na makundi mbalimbali. Itakuwa taabu kwelikweli. Tungojee watakapofanya uamuzi,” anasema.


Anasema hatua madhubuti hazijachukuliwa kupambana na rushwa licha ya kuundwa vyombo na kujenga maofisi makubwa ya Takukuru, lakini dosari iko bado mahakamani.
“Tunahitaji regime (utaratibu) yenye ziro tolerance juu ya ufisadi na rushwa. Kwamba mtu ye yote anayeshughulika na rushwa asihurumiwe na taifa hili.


“Kamata mara moja, ashughulikiwe mara moja kama anahukumiwa…ijulikane. Singapore wako makini katika hili. China wanapiga watu mpaka risasi akipatikana na hatia ya kula rushwa.
“Hapa kwetu tuna vitu vya ajabu sana hapa. Mtu anapatikana na rushwa, tena zilizo wazi badala ya kuchukua hatua, mnaanza kubishana.


“Hapa ilikuwa ifunguliwe hata mahakama ya kijeshi ya kushughulikia masuala haya ya rushwa. Unaweka majenerali hapo. Na kwamba kesi ikiletwa hata isichukue muda, jibu litoke.
“Mtu ana kesi ya kujibu au kutiwa hatiani anachukuliwa hatua na kama mtu hausiki aachiwe. Hapo watu wanaweza kuwa na imani, lakini mahakama zetu hizi za kubishana…


“…Mnabaki mnabishanabishana tu. Mtu anaweza kuhangaikia haki yake miaka nenda rudi. Hakuna kinachofanyika. Sasa hivi shida iliyopo ni kwamba watu wanasema, matatizo yanajulikana, lakini matokeo hawayaoni. Hawaoni hatua dhidi ya wanaokula rushwa. Wanaokamatwa zaidi ni viongozi wa vijiji tu.
“Hawaoni watu wanakamatwa na dawa za kulevya na wanarudi mtaani tu. Watu wanasema wako matajiri hapa. Wanawajua, mnakaa kimya.
“Wakimbizi wanakamatwa Mbeya. Ama kweli hii nchi ya ajabu sana, yaani watu wanavuka Namanga na kukamatwa Mbeya. Wamevukaje hapo katikati? Mtu anapita nchini kwetu, bila kufahamika kweli?” anahoji.
Anasema kwamba uongozi ni kazi ngumu yenye kuhitaji kufanya uamuzi mgumu na kwamba ana imani nchi itapata kiongozi wa kariba ya kuthubutu.


Msuya anasema kama CCM itafanya mzaha kwa kutowatumikia wananchi kwa uthabiti kinaweza kung’oka madarakani hata kama katika uchaguzi wa mwaka huu.
Hata hivyo, amebashiri kwamba chama hicho kikongwe kitaweza kushinda angalau kwa asilimia 51, lakini ana shaka na umakini wa vyama vya upinzani dhidi ya CCM.
Anasema kwamba kwa sasa wananchi wanafanya tathmini juu ya utendaji wa vyama vya siasa kama vinatoa huduma stahiki kwao.
Anasema kwamba vyama ambavyo havionekani kuhudumia watu, vitazidi kuzama katika uchaguzi wa mwaka huu na chaguzi zijazo.


“CCM imejiwekea nafasi ya kubaki, lakini si kwamba chama kingine hakiwezi kuitoa CCM…hata kidogo,” anasema Msuya katika mahojiano maalumu yaliyofanyika nyumbani kwake,  Dar es Salaam.
“CCM inaweza kung’oka,” anasema Msuya aliyepata pia kuwa Makamu wa Rais cheo kilichoendana na wadhifa wa Waziri Mkuu, katika utawala wa awamu ya kwanza na ya pili.


Anasema kwamba ni jukumu la kila chama kutoa huduma kwa raia ili kuvuna kura katika chaguzi mbalimbali na tathmini sasa iko kwa raia ambao wako huru kupima uwezo wa vyama vilivyoko kwa sasa.
“Sasa hivi viko vyama kama 22. Lakini Je, vinatoa njia mbadala ya kuhudumia wananchi? Kwamba mwananchi anajiuliza nikichagua chama hiki nitapata faida hii au nitapata hasara gani, hilo lipo kwa wananchi,” anasema.
Anasema vyama vyote, CCM ikiwa ni sehemu ya kundi hilo hakina budi kujirekebisha kwenye kutoa huduma sahihi ambako wananchi watakuwa wanaona wakifanya hivyo.


Anasema kwamba mfumo wa vyama vingi ulilenga asasi hizo kutoa huduma nzuri na kuwapa nafasi Watanzania kuchagua ni chama gani kinachoweza kuhudumu kwa ubora zaidi kuliko kingine.
“Sasa kwa chama chochote kitakachofanya vizuri kichaguliwe. Ambacho akifanyi vema kitoswe. Hata kama ni CCM, lakini nina shaka kama kuna kinachoweza kuipiku CCM kwa sababu vingi kati ya hivyo, vinalenga kula tu,” anasema Msuya.
Anasema kwamba CCM ingali na sera nzuri ikilinganishwa na vyama vingine sambamba na ‘utajiri’ wa makada wenye uzoefu wanaofaa kuwa viongozi katika ngazi mbalimbali za utendaji kuanzia mawaziri hadi makatibu tarafa.


Anasema licha ya kuwa baadhi ya vyama vina wasemaji wazuri, “lakini bila shaka wananchi wanapata wasiwasi,”  kuwapa dola.
“CCM kuna tatizo kwa baadhi ya viongozi, watendaji ndani ya serikali na ndani ya chama wanaofanya watu wakichukie. Ukiacha hizi sura mbovu za watendaji, CCM bado inakubalika sana kwa watu wengi. Bado wanapenda CCM.
“Nafikiri, Katibu Mkuu wa chama Abdulrahman Kinana amefanya kazi kutembea na kujikosoa hali ambayo imesaidia sana watu kuwa na imani na chama. Watu wanakubali hata ndani ya chama na serikali wanaona kazi yake. Wanaikubali.
“Amekuwa mkali kwa watendaji wabovu hata kwa mawaziri wazito. Ambao hawashughulikii matatizo ya mahindi, sukari na mambo mengine yanayofanya serikali ikasemwa vibaya.


Anataja makosa yanayofanywa na baadhi ya makada wake na viongozi wa serikali, lakini si vema ikahukumiwa na makosa ya mtu mmoja-mmoja.
Anataja makosa kama ya kutolipa wakulima kwa wakati yanaweza kuigharimu CCM kwa namna moja au nyingine kwa sababu “watu wanachoka” kiasi cha kutaka kuchukua mazao yao na kwenda kuuza mahala pengine.


“Umekaa na mzigo wa mtu kwa miezi sita halafu akitaka kuchukua unakataa, haiwezekani. You are making fundamentally wrong (Wanafanya makosa makubwa). Nashukuru sasa wamelipwalipwa wengine, lakini hiyo ni shida,” anasema.
Anasema kosa lingine la CCM ni kuruhusu sukari ya nje kuizamisha ya ndani ambayo sasa haina soko la uhakika na viwanda vilivyoko nchini vinakufa.


“Viwanda vinakufa, vinanunua miwa kutoka kwa wananchi na sukari yao inakaa tu. Sasa kama imefika mahala tunaacha milango wazi, sukari inatoka nje na kuingia ndani na kuua zinasababisha kuua wakulima wetu wadogo na viwanda vyetu. Ni makosa mengine makubwa na hatua lazima zichukuliwe,” anasema.
Waziri huyo Mkuu alirejea ukwapuaji wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuwa ni madoa ambayo ni lazima yachukuliwe hatua.


“Lazima kiongozi achukue hatua kushughulikia matatizo kama haya yanapotokea kwa haraka. Majibu yatoke. Kwa mfano watu kama hawa walioshtakiwa kwa mfano hawa marafiki zangu Basil Mramba, Daniel Yona na Grey Mgonja.
Anasema kwamba haijalishi  kama walioshtaki wana ushahidi au vinginevyo, lakini anasikitika kesi hiyo kuchukua muda mrefu, “Miaka minane kesi haiishi. Nchi ya namna gani hii? Lazima tuwe na vigezo vya utendaji wa utumishi bora. Mtu kama amekosea lazima apelekwe kwenye vyombo vya haki, kesi iendeshwe kwa haraka imalizike. Maisha yaendelee.”


Anasema kwamba CCM na Serikali yake lazima ifanye utumishi bora uliotukuka kwa raia wake na kama kinashindwa ina maana kitakuwa kimeshindwa kuongoza nchi.
Anasema kwamba CCM inahitaji watu wenye akili mpya “reformed minded,” watakaotathmini hali mara kwa mara badala ya kubaki na yaleyale.
“Tunabaki na watumishi wa chama na serikali walewale, that is problem (hilo ni tatizo) kwa hiyo lazima chama hiki kiwe na watu ambao wanasoma na wanajua kutafuta namna ya kuendesha chama kulingana na mabadiliko ya mazingira na kuangalia namna kero za watu zinavyobadilika, “Kutokufanya hivyo. Tutafukuzwa,” anasema.


Anasema kwamba Chama cha Kikomunisti cha Kichina ni kizuri ikilinganishwa na kile cha Sovieti.
“Cha Soviet lilikuwa na mfumo fulani na likashikilia mfumo huohuo, lakini Wachina wamekuwa wakibadilika badilika na ndiyo mafanikio ya China ya sasa,” anasema.


“Tofauti ya Wachina na Warusi wakati ule ilikuwa ni kukubali mabadiliko. Kwa sababu hata sisi wakati tulipokuwa na hali ya uchumi, ilibidi Mwalimu akubali kufungua milango ya kualika watu wenye uwezo waje washirikiane na serikali kutoa huduma kama viwandani, barabarani.
Anasema, “Wachina walifanya hivyo na kwa sasa hivi wako juu kwa kushirikiana na Wajapan na Ujerumani kwenye kutengeneza magari na mambo mengine. Na ndiyo maana wamefanikiwa.”

 

3349 Total Views 2 Views Today
||||| 4 I Like It! |||||
Sambaza!