Kwa hiyo sekta binafsi endeleeni kujiamini, endeleeni kufanya kazi, mje Tanzania hapa ni mahali salama kwa uwekezaji. Tunawahitaji leo, tuliwahitaji juzi, tutawahitaji keshokutwa, tutawahitaji miaka yote kwa sababu Tanzania iko hapa kwa miaka yote. Tangu leo, kesho, keshokutwa na maisha yote.”

Ifuatayo ni sehemu ya maneno kutoka katika hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, katika uzinduzi wa Kampuni ya huduma za gesi, Taifa Gas. Uzinduzi huo ulifanywa na Rais Magufuli wiki iliyopita, Kigamboni, Dar es Salaam.

Namshukuru Waziri wa Nishati pamoja na Kampuni ya Taifa Gas Tanzania Ltd kunialika kuzindua ghala na mitambo ya kuhifadhi na kusambaza gesi (LPG) au maarufu gesi ya mitungi.

Napenda kuupongeza uongozi wa Taifa Gas kwa kutoa somo zuri kuhusu tofauti ya gesi ya petroli na gesi ya asili ambayo ipo kwa wingi hapa nchini.

Gesi asilia huchimbwa moja kwa moja kutoka ardhini kama ile inayochimbwa hapa Tanzania.

Tofauti kubwa iliyopo ni kwamba, LPG au gesi ya mtungi ni nzito ukilinganisha na gesi ya asilia pamoja na kwamba zote zinaitwa hydrocarbon materials.

Ndugu zangu, nishati ni sekta nyeti na muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani, ni muhimu katika kukuza uchumi na shughuli za uzalishaji, ikiwemo kilimo, viwanda, uvuvi, ufugaji au uchimbaji madini.

Ni muhimu katika kuboresha huduma za jamii ikiwemo afya, elimu na mawasiliano. Lakini pia matumizi ya nishati bora na usalama ni muhimu katika kutunza mazingira na kulinda afya za wananchi.

Kwa kutambua hilo ndugu zangu, Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015 iliahidi kushirikiana na sekta binafsi, iliahidi kwa nguvu zote na kwa kutumia vyanzo mbalimbali upatikanaji wa nishati hii.

Nafarijika kuona kuwa utekelezaji wa ahadi hiyo unaendelea vizuri sana na leo ni ushahidi mkubwa kuja hapa, kuja kuzindua shughuli hii ya gesi ya Taifa Gas Tanzania Limited.

Napenda niipongeze Wizara ya Nishati kwa jitihada kubwa inazofanya za kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini. Siyo siri, hali ya upatikanaji wa nishati nchini kwa sasa inaridhisha, tatizo la kukatika umeme pamoja na kwamba lipo katika maeneo mbalimbali kidogo, lakini limepungua sana.

Na wananchi wengi wameunganishiwa umeme ikiwemo vijijini, kwa sasa nchi yetu inazalisha megawati 1,601 kama ambavyo amezungumza mheshimiwa waziri, hivyo kufanya tuwe na ziada ya megawati 300 kwa siku. Lakini kama alivyozungumza mheshimiwa waziri, vijiji zaidi ya 7,127 vimeunganishiwa nishati ya umeme kutoka vijiji 2018 mwaka 2015.

Sambamba na hayo, miradi mingi ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi, maji, joto la ardhi, jua au upepo pamoja na miradi ya kusafirishia na kusambaza umeme inaendelea kutekelezwa sehemu mbalimbali. Hivyo basi, narudia tena kukupongeza waziri na watendaji wote wa Wizara ya Nishati kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Ndugu zangu nataka niwaahidi kwamba kadiri ya miradi hii inavyoendelea, tutakapoweza hata tukafikia kuzalisha megawati 5,000 hasa katika mradi wa Stiegler’s Gorge utakapokamilika, ambapo utazalisha umeme zaidi ya megawati 2,100 na ule mradi wa Rufiji kule ambao utazalisha megawati 359.

Baada ya hizo hatua zote pamoja na huu tulionao, nina uhakika bei ya umeme kwa Watanzania wote na viwanda vyetu tutaishusha ili wawekezaji wengi wapate faida katika miradi yao watakayokuja kuwekeza katika nchi hii.

Lakini kwa namna ya pekee naipongeza sekta binafsi kwa kuitikia wito na kuungana na serikali katika kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini. Mheshimiwa waziri ameeleza hivi punde kuwa hivi sasa nchi yetu inazo kampuni nane zilizopewa leseni za kuagiza na kusambaza gesi ya mitungi ambayo inatumika kwa wingi majumbani na viwandani.

Hii imesaidia kuongeza matumizi ya gesi nchini kutoka tani 17,000 mwaka 2010 hadi tani 92,500 mwaka 2018, hivyo kusaidia kutunza mazingira hususan misitu yetu kwa kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, nawapongeza sana.

Miongoni mwa kampuni zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi, yaani LPG ni Taifa Gas Limited ambayo zamani ilijulikana kwa jina la Mihan Gas Company. Kampuni hii kama mlivyosikia imewekeza kiasi cha Sh bilioni 150 ikihusisha ujenzi wa maghala na mitambo ya kuhifadhi gesi kwenye mikoa 20.

Mojawapo ya maghala hayo ni hili ninalolizindua leo ambalo lina uwezo wa kuhifadhi tani 7,650 za gesi. Ghala hili ni kubwa mashariki na kusini mwa Afrika, na limeifanya Kampuni ya Taifa Gas kuongoza kwa kuwa na uwezo wa kuhifadhi gesi ya mitungi nchini.

Ghala hili limeongeza uwezo wa nchi yetu kuhifadhi gesi ya mitungi kutoka tani 8,050 kwa mwaka 2016 hadi kufikia tani 15,600 hivi sasa, ninawapongeza sana.

Nimefurahi kumuona mmiliki, na wamiliki wote ambao wanamiliki kampuni hii kwa asilimia 100 ni Watanzania, kwa utekelezaji huu mkubwa mmenipa moyo sana kwamba Watanzania wanaweza hasa tunapoamua.

Kwa hiyo Mheshimiwa Rostam ninakupongeza sana pamoja na Watanzania wengine kwa uwekezaji huu mkubwa ambao mmeufanya, ambao umewezesha kutengeneza ajira za hapa hapa 260, lakini ajira zingine kufikia mpaka 3,000.

Lakini nimeambiwa kuwa mnalipa kodi na tozo mbalimbali, nilikuwa nasikia, kama hivyo ndivyo, ni matumaini yangu haya malipo yatakuwa yanaongezeka kadiri siku zinavyokwenda. Gesi hii inatumika hapa nchini, nyingine wanauza nchi za jirani Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Sudan Kusini, Afrika Kusini na Zambia.

Hii maana yake nchi yetu inapata fedha za kigeni, hivyo basi, narudia tena kuwapongeza na ninapenda niwaahidi kuwa serikali itaendelea kushirikiana nanyi pamoja na kampuni zingine zinazojishughulisha na biashara hii ya gesi ya mitungi.

Lengo letu ni kuona wananchi wetu wanapata nishati kwa uhakika iliyo salama. Kwanza angependa kupata eneo ili kuongeza maghala pamoja na mitambo ya kuweza kuhifadhi tani 12,000 za gesi. Nina imani kwamba mamlaka husika zitashughulikia kwa sababu hatujawahi kufika hatua ya kupungukiwa ardhi.

Hata huku Kigamboni ninajua kuna maeneo fulani ya eka nyingi tu ambazo zimekaa tu, serikali tulilipia zaidi ya bilioni 120 kwa ajili ya kuweka pale wawekezaji nafikiri chini ya mradi wa EPZA lakini mpaka leo hakuna hata mmoja aliyewekeza.

Lakini nina fahamu biashara hii pia huwa inawanufaisha wananchi. Nimefurahi kuona kwamba mnazungumza na wananchi hapa ili kusudi nao wale. Kwa hiyo kama utaendelea kuzungumza na wananchi hawa majirani zako wanakuuzia ardhi na wewe unawalipa, kwa mujibu wa sheria namba 4 ya mwaka 1999, kifungu namba 3(g), hii itakuwa faida pia ya watani zangu Wazaramo kufaidika na kuwepo kwa kiwanda hiki.

Lakini ni matumaini yangu hili suala la ardhi litashughulikiwa na mamlaka zinazohusika. Pili, mmezungumzia kuhusu pendekezo la serikali kutaka kuanzisha utaratibu wa ununuzi wa pamoja wa gesi ya petroli, yaani ‘bulk procurement’.

Hapa sina neno lolote la kuzungumza kwa sababu nimelisikia leo, lakini ni matumaini yangu wizara na wawekezaji ni vema mkakaa, mkakubaliana katika taratibu nzuri za ‘win win situation’, kwa sababu saa zingine upande wa serikali huwa tunakimbilia sana kukusanya na kujifanya tunaweza kudhibiti halafu baadaye tunaharibu.

Lakini pia inawezekana wawekezaji wakawa wanaitumia hii hii njia kwa ajili ya kukwepa na hasa kwa sababu ‘flow meter’ walizonazo serikali haina uwezo wa kwenda kuziangalia kwamba gesi imeingia, ninyi wote mzungumze.

Serikali nayo isijiingize sana kwenye uwekezaji wa sekta binafsi kwa sababu walishindwa kuleta hii gesi, leo wanakimbia haraka haraka kufanya nini? Badala ya kukaa na kukusanya mapato. Kwa hiyo, mambo haya yote lazima tuyaangalie kwa pamoja.

Lakini kikubwa zaidi ni lazima tuangalie pia kazi nzuri inayofanywa kwa kuingiza gesi katika nchi yetu. Ninafahamu siku za nyuma tuliwahi kuchukua uamuzi fulani, huku palikuwa na Kampuni ya Tipper sasa nisingependa kuyaona yakiendelea yale yaliyosababisha Tipper isiwepo, Tipper ambalo lilikuwa ni shirika letu, yasije yakatokea kwenu.

Na hii ndiyo ilikuwa sababu serikali ilichukua uamuzi wa kufuta kodi na tozo mbalimbali kwenye sekta hii, ikiwemo VAT. Napenda kutumia fursa hii ndugu zangu kutoa wito kwa wasambazaji wa gesi ya mitungi kuendelea kupanua huduma zenu.

Nimeambiwa kuwa sasa gesi ya mitungi inapatikana kwenye mikoa 23 ya nchi yetu, aidha, ninyi Taifa Gas Tanzania mmejipanga katika kipindi cha miaka mitano ijayo kuongeza maghala na mitambo kwenye miji na wilaya zote nchini. Hiki ni kitu kizuri na ninapenda niwapongeze, kwa uhakika hili linastahili kupewa pongezi.

Hata hivyo nawasihi mfikishe huduma zenu hadi vijijini, msiishie mijini peke yake, hii itawasaidia kupanua soko lenu lakini pia kusaidia nchi yetu kutunza mazingira. Nasema hivyo kwa sababu idadi kubwa ya Watanzania asilimia 60 wanaishi vijijini na nishati yao kubwa ni kuni na mkaa.

Hivyo ni wazi mkifikisha huduma zenu hadi vijijini mtapata soko kubwa na kusaidia si tu kutunza mazingira yetu, lakini pia kulinda afya za wananchi wetu, matumizi ya kuni na mkaa si mazuri sana kwa afya.

Sambamba na hilo, nahimiza Wizara ya Nishati kupitia shirika lake kuongeza kasi ya kusambaza gesi asilia hususan kwenye maeneo ambako miundombinu hiyo imepita. Kwa sababu bado Wizara ya Nishati ina gesi yake.

Natambua kuwa jitihada zimefanyika ambapo matumizi ya gesi asilia yameongezeka, takriban viwanda karibu 40 na nyumba 500 zimeunganishwa na gesi asilia na zaidi ya magari 200 ninaambiwa hivi sasa yanatumia gesi nchini.

Hii inafanya matumizi ya gesi ya bomba letu la kusafirishia gesi kuongezeka kutoka asilimia tano mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 16 na ukusanyaji wa mapato pia kuongezeka na hili nawapongeza sana. Kwenye mwaka huu wa fedha unaoisha mlipangiwa kulipa Sh bilioni 394, lakini hadi kufikia Mei 2019 mlikuwa mmekusanya Sh bilioni 484. Hongereni sana.

Napenda pia nitumie fursa hii kutoa wito kwa Watanzania hususan wa hapa Dar es Salaam ambako kwa siku wanatumia magunia 40,000 ya mkaa, sawa na asilimia 90 ya mkaa wote nchini.

Matumizi ya gesi mbali na kutunza mazingira na kulinda afya zetu ni nafuu sana, ni takriban nusu ya gharama ya mkaa.

Kwa mfano, kwa wastani familia moja kawaida hutumia magunia mawili ya mkaa kwa mwezi, sifahamu hapa Kigamboni yanauzwa bei gani, lakini kwa maeneo mengi magunia mawili ya mkaa yanaweza kutumia Sh 120,000.

Mtungi mmoja wenye kilo 15 ambao gharama yake ni Sh 47,000 lakini iwe basi mitungi miwili bado itakuwa ni Sh 94,000, bado ni nafuu zaidi kuliko kutumia mkaa. Hivyo basi, mnaweza kujionea wenyewe jinsi gani ilivyo nafuu kutumia gesi.

Lakini nawasihi wasambazaji nanyi punguzeni gharama za mitungi. Nimefurahi kusikia ninyi Taifa Gas mmeanza kutengeneza na kukarabati mitungi yenu ya gesi wenyewe. Hii bila shaka itashusha bei ya mitungi na kuwahamasisha wananchi wengi kutumia gesi.

Tena ikiwezekana fanyeni kama kampuni za soda na bia zinavyofanya, ukinunua soda au bia ukinunua kwao maana yake hulipii kreti lake, unakodisha, mfikiri kitu kama hicho.

Napenda pia kuwahimiza Watanzania na hata wasio Watanzania kuendelea kuwekeza nchini, nchi yetu ina fursa nyingi za uwekezaji. Kwa mfano kwenye sekta hii ya nishati mbali na gesi kuna fursa ya uwekezaji katika kuzalisha umeme wa jua, joto la ardhi, upepo, maji, makaa ya mawe na kadhalika.

Na kwa bahati nzuri tuna sera na pia tumetengeneza sheria na kanuni nzuri zinazoruhusu sekta binafsi kuwekeza kwenye sekta ya nishati. Uwekezaji huu mkubwa uliofanywa na Taifa Gas Tanzania Limited ni uthibitisho kuwa serikali yetu inaipenda sekta binafsi na ipo tayari kushirikiana nanyi.

Kwa hiyo sekta binafsi endeleeni kujiamini, endeleeni kufanya kazi, mje Tanzania hapa ni mahali salama kwa uwekezaji. Tunawahitaji leo, tuliwahitaji juzi, tutawahitaji keshokutwa, tutawahitaji miaka yote kwa sababu Tanzania iko hapa kwa miaka yote. Tangu leo, kesho, keshokutwa na maisha yote.

Kwa hiyo wawekezaji na ninyi tunawahitaji kwa sababu kikubwa serikali ita-collect revenue, lakini mbali ya hivyo Watanzania watapata ajira, kama ambavyo Taifa Gas mlivyoanza.

Ndugu zangu wananchi wa Kigamboni, narudia kuwashukuru, kwa kuiunga mkono serikali katika ukuaji wa uchumi. Natambua kwa mfano hapa Kigamboni tumefanya ukarabati wa vituo viwili vya afya, Kigamboni na Kimbiji na hivi sasa tunamalizia ujenzi wa hospitali yenu ya wilaya pale Gezaulole.

Ujenzi wa barabara ya lami ya Tange hadi Kibada najua unaendelea na kwenye bajeti ya mwaka ujao wa fedha tumepanga kuanza ujenzi wa barabara kutoka Kibada hadi Kimbiji na kutoka Kimbiji kurudi Mjimwema. Sambamba na hiyo, serikali imetoa takriban Sh milioni 48 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya madarasa na kuendelea kutoa elimu bure.

Yale mengine yamezungumzwa na mheshimiwa mkuu wa mkoa pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, tembeeni kifua mbele, serikali ninayoiongoza iko pamoja nanyi. Kigamboni itabadilika na imeshaanza kubadilika.

Tutaitengeneza upya, huu mradi wa barabara wa kilometa nyingi ni mfano pekee wa kuibadilisha Kigamboni, na Kigamboni ndiyo mji wa Dar es Salaam, ndiyo maana daraja hili lilijengwa.  Master Plan ya Jiji la Dar es Salaam iko Kigamboni.

Mimi nilikaa Wizara ya Ardhi miaka yangu miwili na nusu ninafahamu ‘Master Plan’ ya Jiji la Dar es Salaam, mji mzuri mkubwa ‘plan’ yake iko Kigamboni.

Ndugu zangu zipo baadhi ya changamoto za wilaya hii mpya ya Kigamboni ambazo nafikiri siku nitakapopanga ziara rasmi ya kuja kutembelea hapa tutakuwa tumezifanyia kazi vizuri.

Kuna yale majengo ya NSSF yanaitwa Dege, yamekaa pale kwa muda mrefu. Ni majengo ambayo yamekaa wala hayaendelezwi, ni mradi bomu. Ni mradi wa ovyo, wa kifisadi.

Tumeshawaeleza NSSF pamoja na bodi washughulikie, watoe mawazo yao na ninyi wananchi wa Kigamboni na uongozi wa mkoa mtoe mawazo yenu. Kwamba ni kwa namna gani hayo majengo tunaweza tukayatumia katika njia iliyo sahihi.

Kama ni kuyatoa yawe mabweni ya chuo, yawe nyumba za wafanyakazi, au iwe nini, tusubiri huo uchambuzi utakaofanywa katika sehemu zote mbili. Serikali ni moja, hatuwezi tukaiacha ‘investment’ kubwa kama hiyo imekaa na wala hatutoi majibu.

Na mimi nina uhakika watendaji ndani ya serikali hasa wizara inayoshughulikia sera pamoja iko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu itatusaidia katika kutoa majibu, Katibu Mkuu wa Nishati uko hapa utatusaidia ili kusudi tupate majibu kama ule mradi unaendelea au hauendelei.

Kama mradi huo unachukuliwa na serikali tukajenge kitu cha maana tufanye kuliko kutokuamua, kwa hiyo nina uhakika hili nalo tutalifanyia kazi ili tuone nini cha kufanya.

Shughuli ya leo ni uzinduzi. Mheshimiwa Rostam Aziz, mwenyekiti wa kampuni hii, mimi napenda kuwahakikishia nimefurahi sana na hiki ndicho huwa nakitaka. Mimi huwa sipendi wawekezaji wa maneno maneno tu, umeonyesha, hii imenipa nguvu sana.

Tafuta wawekezaji wengine hata kumi tu au ishirini wenye moyo wa namna hii wa kuwekeza, tuje tuwape support serikali, na sisi tutawapa support hawa wawekezaji. Tunahitaji wawekezaji wa ukweli, waje wasisikilize maneno ya wale ambao hawatutakii mema.

Waje wawekeze, tutawasaidia, lakini tunataka wanapowekeza serikali nayo kupitia wananchi wake wapate ndiyo maana tunazungumzia juu ya win win situation. Kwa hiyo ninakushukuru kwenye hili sana tu, na ninaendelea kuwashukuru wawekezaji wengine ambao watakuja kwa moyo wa namna hiyo.

Umeniambia kiwanda cha ngozi cha Mbeya ndani ya miezi mitatu, cha Morogoro ahadi ni deni. Nitakuja huko nikicheki kiwanda cha ngozi na nitakifungua kwa sababu moja ya sehemu kubwa ya tatizo tunalolipata tuna mifugo mingi, ni wa pili au wa tatu katika Afrika lakini hatuna viwanda vya ngozi.

Tunaagiza viatu kutoka nje wakati ng’ombe wetu wapo, tuna ng’ombe zaidi ya milioni 30, ngozi tunaagiza nje! Ile ni ‘poor planning’, kwa hiyo kama kuna muwekezaji anayeweza akaja awekeze kwenye ngozi na afanye mpaka kwenye ‘final product’.

Tutavaa hivi viatu vizuri kutokana na ngozi za wanyama wetu. Kwa hiyo fursa zipo nyingi, nilitaka nichomekee hili, kwa hiyo ndugu zangu ninawashukuru sana, ninawashukuru sana Wizara ya Nishati, ninawashukuru sana wakuu wa wilaya na viongozi wote, ninawashukuru sana wakuu wa majeshi yetu kwa kuendelea kulinda amani ya Watanzania.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki wawekezaji wa Taifa Gas Limited na Mungu awabariki wawekezaji wote, awabariki wana Kigamboni wote.

By Jamhuri