BiasharaWakati fulani kule Marekani kulitokea malumbano makali baina ya kampuni mbili kubwa zenye nguvu na ushindani mkali. Kampuni zilizohusika katika sakata hili zilikuwa ni ile ya Brother na nyingine ni Smith Corona.
Kampuni hizi zilijihusisha na utengenezaji wa bidhaa zinazofanana ikiwamo mashine za kudurufu (type writers), ‘keyboards’ za kompyuta, mashine za kusafisha hewa (air-conditioners) pamoja na vifaa lukuki vya kielektroniki.


Chimbuko la malumbano hayo lilikuwa ni ukiukwaji wa sheria inayokataza mrundikano wa bidhaa zisizo na ubora na zinazozidi kiwango cha wingi kisichozingatia mikingo (limitations levels) katika soko. Sheria hii inayofahamika kama Anti-Dumping Law, ilionekana kuvunjwa na kampuni zote mbili.
 Kampuni ya Smith Corona ilituhumiwa kutengeneza skandali hii ya kibiashara ili kusaka uwezekano wa kuimaliza kampuni ya Brother ambayo ilikuwa ni tishio kubwa kwake. Smith Corona ilizichanga kizembe karata zake na kuibuka na hoja nyepesi ya utaifa wa kampuni. Smith Corona ni kampuni iliyoasisiwa nchini Marekani na hata makao yake ya kidunia yapo huko huko Marekani wakati Brother iliasisiwa nje ya Marekani na kuanzisha tawi lake nchini Marekani.


 Fikra za wakurugenzi na wamiliki wa Smith Corona zilidhani kuwa kwa kutumia karata ya uzalendo, tume ya ushindani wa kibiashara ingewahurumia wao na kuwaadhibu washindani wao, Brother, ambao ni wageni wa kutoka nje.
 Smith Corona wakavitumia vyema vyombo vya habari na kujipamba mbele ya Wamarekani kuwa wao ni wazalendo na hivyo wanatakiwa walindwe na kuhurumiwa kwa sababu wao ni ‘wa hapa hapa’. Baada ya Tume ya Ushindani ya Marekani kusikiliza shauri hilo iliamua kuwa Brother haikuwa na kosa lolote na badala yake Smith Corona ndiyo walioonekana na makosa na hivyo wakawajibishwa.


 Pamoja na kuwa Smith Corona walikuwa ni ‘wazalendo’ lakini walipigwa mweleka na ‘wageni’ kiushindani halisi sokoni na katika shauri mbele ya chombo cha kibiashara. Hapo kukapatikana somo moja kubwa katika ulimwengu wa kampuni hasa za kimataifa ya kwamba; suala la msingi siyo “kuwa kampuni ya kizalendo” bali ni “kuwa kampuni inayoshindana katika soko kwa mujibu wa viwango na sheria”
 Moja ya changamoto kubwa zinazozikabili biashara nyingi katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania, ni ushindani mkali kutoka kwa kampuni kubwa kutoka katika mataifa yaliyoimarika kiviwanda. Kampuni hizo za kimataifa ninayoyagusia hapa ni zile ambazo zinaendesha uzalishaji ndani ya nchi mbalimbali duniani, huku zikiwa na makao yake makuu katika nchi mama.


 Ni vema kufahamu kuwa Kiswahili chetu kinachanganya maneno mawili ya Kiingereza – multinational companies na international companies – kwa kuyaweka kwenye neno moja tulilolizoea yaani makampuni ya kimataifa. Ipo tofauti ya kimantiki; tunaposema ‘multinationals’ tunamaanisha yale makampuni ambayo yamefungua matawi katika nchi mbalimbali wakiendesha uzalishaji kamili wa bidhaa katika nchi hizo husika. ‘Internationals’ ni yale makampuni ambayo yanazalisha bidhaa ama huduma katika nchi moja na kisha yanasafirisha bidhaa ama huduma hizo katika mataifa mbalimbali.
Kwa Tanzania tunayo changamoto kubwa, kwani makampuni ambayo ni ‘multinationals’ ni machache mno na hata uwepo wake hauna nguvu kubwa kimataifa. Ingawa miaka ya hivi karibuni kumekuwa na hamasa kubwa sana kwa makampuni ya hapa nchini kujitanua na kuanza kuwa ‘internationals’ ambapo tunashuhudia yakisafirisha bidhaa zao katika mataifa ya jirani na katika nchi za Magharibi na Marekani


Hii ni tofauti sana na wenzetu wa jirani, Kenya, ambao msuli wao kibiashara umetanuka na wanayo makampuni ambayo ni ‘multinationals’ na yanaonesha nguvu ya kibiashara na yanatamba. Upo mfano mzuri kwa benki yao ya Kenya Commercial Bank (KCB Tanzania) ambayo imepenya Tanzania na katika nchi kadhaa za Afrika; wakati huo huo sisi Watanzania tunajikongoja na benki zetu (za Kitanzania) ambazo hata soko la ndani ya nchi tu ni changamoto kubwa mno.
 Katika nchi mama ambapo kampuni inaasisiwa ndiko kunakokuwa kichwa cha kampuni na katika nchi ambako kampuni husika inajisambaza kunakuwa ni mikia. Kuwapo kwa dhana hii ya ‘head and tail’ ndiko kulikoibua mjadala mzito miongoni mwa wanataaluma wa sayansi ya biashara unaohusu utaifa wa kampuni hizi za ‘multinationals’.


 Utaifa kuhusu makampuni haya (multinationals) unaonekana kuwa na mantiki kubwa kutokana na tabia, hulka na mienendo inayooneshwa na makampuni husika. Mengi ya makampuni haya (kama si yote) kimsingi huwa hayana nia za kulinda maslahi ya nchi yanakoingia.
 Kuna mengi ambayo hutiliwa shaka ikiwamo kupendelea kuchukua malighafi za kuzalishia kutoka katika mataifa mama, uonevu kwa makampuni ya nyumbani pamoja na uhatarishi katika mambo ya usalama wa taifa.
 Yapo makampuni ambayo hupewa ruzuku na serikali za nchi zao, mengine huchukua mitaji kutoka mabenki ya nchi mama pamoja na wamiliki kuwa katika nchi mama. Kitendo hiki husababisha makampuni haya kujikuta yakilinda hata maslahi ya kisiasa ya nchi mama. Hii nayo ni hatari kwa sababu taifa husika (host country) huweza kuwa mashakani.


Makampuni mengi ambayo ni ‘multinationals’ yana nguvu kubwa sana kiuchumi na yana faida mororo za kiuzalishaji (economize of scales). ‘Multinationals’ wanapoingia katika nchi husika ni rahisi sana kuyamaliza kiushindani makampuni ya nyumbani na kuyaacha hoi bin taaban. Ujanja mwingine ambao makampuni haya yanatumia ni kuficha ama kuzuia teknolojia na ufundi wa kiugunduzi.
 Kwa mfano, kampuni ya Coca-Cola yenye makao yake makuu kule Atlanta, Marekani, ni kampuni ya kimataifa (multinational) ambayo imefanikiwa kushika masoko ya vinywaji katika mataifa mengi sana ulimwenguni. Kampuni hii ina bidhaa kuu ambayo ni soda ya Coca-Cola lakini hadi leo kanuni (formula) ya kutengeneza unga wa soda hiyo, imebaki kuwa ni siri ya wagunduzi (trade secret).


Siri za kiugunduzi kimsingi hazina makosa kisheria (na ni haki ya mgunduzi kubaki na siri hiyo kwa manufaa yake ya kimaslahi ama kibiashara), lakini zinapochanganyika na nguvu za makampuni haya kibiashara mara zote zimekuwa ni mwiba kwa makampuni madogo ya nyumbani ambayo yanajikongoja.
 Tunaweza kubashiri hili tunapoangalia bidhaa zinazobuniwa katika mataifa haya machanga, zikitaka kushindana na bidhaa zinazotengenezwa na makampuni haya ya ‘multinationals’. Hapa tujikumbushe jambo moja.
 Baadhi yetu tutakuwa tunakumbuka soda maarufu sana ambazo zilikuwa zinatengenezwa mkoani Tanga zikijulikana kama Vimto. Pamoja na kuwa soda hizi zilikuwa nzuri na fahari ya Kitanzania lakini zilishindwa kuhimili ushindani katika soko ambalo tangu wakati huo lilikuwa limetawaliwa na soda tulizozizoea za Pepsi na Coca-Cola. Hii ilisababisha Vimto kujikuta zikijifuta zenyewe.


 Kiharaka haraka mtu anaweza kudhani kuwa wateja wanaendelea kununua bidhaa za makampuni ya kigeni (na kuacha za kizalendo) kwa sababu ya ama kukosa uzalendo ama kuwa na mazoea na bidhaa hizo. Hata hivyo upo ukweli uliofichika ya kwamba, makampuni haya ‘multinationals’ na hata ‘internationals’ yanazo mbinu na uwezo mkubwa sana wa kimasoko ambao ni vigumu mno kufikiwa na makampuni yetu ambayo ama ni machanga, au ni makongwe lakini dhaifu.
 Ni dhahiri kuwa mikia (uzalishaji unaofanyika katika nchi nje ya nchi mama) ya makampuni haya umekuwa ni jinamizi linaloendelea kuua viwanda vingi vya mataifa machanga. Mbali na hiyo pia makampuni makubwa ambayo ni ‘internationals’ yamekuwa yakiingiza bidhaa nyingi na kwa bei ndogo sana katika masoko yetu na kusababisha hali mbaya kwa bidhaa zetu za nyumbani.


 Huwa ninajiuliza, itakuwaje siku moja kampuni ya McDonald’s ikifungua tawi lake Tanzania? MacDonald’s ni kampuni ambayo inauza vyakula karibu vya aina nyingi sana duniani na imesambaa katika nchi nyingi sana duniani. Je, utakuwa wapi usalama wa makampuni ya nyumbani yanayotengeneza biskuti? Tutawasalimishaje mama ntilie wetu na wale wanaotengeneza vitafunwa huko mitaani?
 Ikiwa kampuni kubwa na yenye nguvu kama Smith Corona ilitolewa kamasi na kampuni ya kigeni na kuomba kuhurumiwa na serikali ya nchi mama, je, si zaidi sana kwa makampuni ya kizalendo yaliyopo katika nchi hizi masikini kuhurumiwa na serikali za nchi zao?
Tutafakari, tuendelee kujadili, tuone ni namna gani wazalendo watasaidika. Wazawa wanastahili ushindi kibiashara.

 
1701 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!