Miaka 44 iliyopita Watanzania wengi tukiwa hatujui chochote kuhusu teknolojia wala televisheni, Sunday Manara, anakwenda Uholanzi kucheza soka la kulipwa.

Baada ya miaka miwili (1978) maisha ya Uholanzi yanamshinda, anaamua kutimkia Marekani kwenye Klabu ya New York Eagles. Mambo bado yanamkataa, mwaka 1981 Manara anajiunga na ligi kuu ya Dubai kucheza katika Klabu ya Al-Nasri kabla ya kurejea nyumbani  mwaka 1984. Anarejea nyumbani baada ya miaka minane ya kuzurura duniani kupambana na fursa katika soka. Anashindwa hapa, anajaribu kule bila kuchoka au kukata tamaa katika kipindi cha miaka minane!

Inasikitisha mno kumuona Shiza Kichuya anarudi Simba akipokewa kwa furaha na Watanzania eti kisa ni kiboko ya Yanga. Shiza anayecheza kwenye ‘smart phone’ mpaka za Sh 80,000, Facebook ya bure, YouTube, televisheni na Instagram zilizozaliwa na teknolojia inayomuwezesha kujifunza chochote anashindwa kucheza soka Misri ndani ya mwaka mmoja tu na kuamua kurudi Tanzania. Basi angalau hata angekwenda Zambia badala ya kurudi nyumbani moja kwa moja.

Kuna maswali unaweza kujiuliza mpaka ukamkufuru Mungu. Kwa mfano, unaweza kujiuliza, aliyemuumba Shaaban Idd Chilunda ni mwingine au ndiye yule yule aliyemuumba Farid Mussa? Kwa nini wanakosa roho ya Thomas Ulimwengu? Ulimwengu ameonyesha ujasiri wa kipekee, kama ule wa Manara. Anashindwa hapa, anajaribu kule. Tangu ameondoka nchini hajaangalia nyuma!

Huyu Mungu ndiye huyu huyu aliyemuumba Mbwana Samatta aliyeanzia TP Mazembe? Ndiye huyu huyu aliyemuumba Ibrahim Ajibu aliyekataa pesa za Moise Katumbi wa TP Mazembe ya Kongo na kuchukua za Mohammed Dewji wa Simba mwenyeji wa Singida?

Chilunda na Farid wote wawili wametoka wamecheza timu moja hapa Tanzania. Wote wawili wakaenda Hispania kucheza soka la kulipwa. Mmoja amerudi yupo Chamanzi muda huu, mwingine amebaki Hispania anapambana.

Katika mfululizo huohuo wa maswali hayo, unamshangaa Kichuya kurudi Tanzania, katikati ya taarifa za Mbwana Samatta kusajiliwa Aston Villa ya Uingereza.

Iceland ina watu 500,000, idadi hii ni mara nne ya watu waliomo kwenye Mkoa wa Morogoro unaokadiriwa kuwa na watu milioni mbili na zaidi. Idadi ya watu kwa nchi yote ya Iceland ni mara kumi ya watu wa Jiji la Dar es Salaam lenye wakazi wanaokadiriwa kufika milioni tano. Idadi ya watu wote wa nchi hiyo ni ndogo kuliko wakazi wa wilaya moja tu ya Jiji la Dar es Salaaam.

Idadi ya watu wote wa nchi ya Iceland ni zaidi ya mara 100 ya Watanzania wote. Pamoja na uchache wao, wamecheza Kombe la Dunia kule Russia na kuibana Argentina yenye Lionel Messi na kufanikiwa kutoa sare ya 1-1.

Wakati Emmanuel Amunike akiwa kocha mkuu wa Taifa Stars, timu yetu ilivunja rekodi ya kuwa na wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya Tanzania. Kati ya wachezaji 23 walioitwa kulikuwa na wachezaji tisa wanaocheza soka nje ya Tanzania. Ingawa si jambo la kujivunia katika nchi yenye watu zaidi ya milioni 55 kuwa na wachezaji tisa wanaocheza nje, lakini si haba, hasa ukizingatia historia yetu katika soka. Halafu tunawapongeza kina Kichuya wanaporudi kirahisi rahisi.

Lazima tuwacheke, tuwazodoe, lazima tuwaseme, tuwanange, ni muhimu pia tuanze kuwadharau na kuwasengenya ili wapate hasira za kutukomoa, ili wahamasike kwenda mbele zaidi. Tusiwapokee kama mashujaa, kwani kufanya hivyo kunatoa somo baya kwa wenzao na hatuwatendei haki kina Simon Msuva, Kelvin John na kina Kibabage wanaovumilia yale yale ambayo wao yamewashinda.

Hawajifunzi kwa Mrisho Ngasa anayelialia mitandaoni kila siku kuhusu pesa zake pale Yanga. Hawajifunzi kwa Haruna Moshi Boban aliyewakimbia ‘Wasweden’ lakini leo yupo Singida United inayopambana isishuke daraja. Inasikitisha sana.

Jambo la ajabu wote tunamsifia Samatta kwenda Aston Villa baada ya kutoka Genk. Hatutatenda haki kumsifia Samatta pasipo kuwakosoa hawa wanaorudi nyuma badala ya kwenda mbele.

Ni kweli maisha yana vipindi tofauti. Kuna kupanda na kushuka. Lakini si kutoka Misri mpaka viwanja vya Bunju na Kariakoo. Vinginevyo mmekuja kuvunja ndoa za kina Stamina tu si kucheza mpira.

Tanzania ina vivutio vingi sana vya utalii. Ukiacha milima na wanyama, vingine vinapatikana kwenye soka. Eti leo unasikia suala la kuwaacha kina Fei Toto na Detram Nchimbi Yanga kwenda kucheza soka Misri ni mjadala, wakati huohuo Madrid wanamuuza Christian Ronaldo kwenda Italia.

0629500908

nnnguzo@gmail.com

489 Total Views 3 Views Today
||||| 1 Unlike! |||||
Sambaza!