Tunazuia sukari kutoka nje kwa maslahi ya nani?

Februari 18, mwaka huu Rais John Magufuli alitangaza kupigwa marufuku kwa uagizaji wa sukari kutoka nje. Akasema kama kuna haja ya kutoa kibali, basi ni yeye ndiye atakayetoa.

Alisema sababu ya hatua hiyo ni kuwa kuna maofisa wa Serikali ambao wanatoa vibali hivyo hata kama nchi ina akiba ya kutosha ya sukari ghalani. Kwa kawaida vibali hutolewa na Bodi ya Sukari (SBT), kwa hiyo bila shaka alikuwa anazungumzia maofisa wa Bodi hiyo.

Nikajiuliza, kweli tutafika iwapo kazi ya SBT itakuwa inafanywa na mkuu wa nchi? Kwanini maofisa wahusika wasichukuliwe hatua za kinidhamu na za kisheria? Kama ni jipu kwanini lisitumbuliwe?

Lakini tatizo siyo tu kuagiza sukari kutoka nje wakati tunayo ya kutosha viwandani. Tatizo kubwa zaidi ni sukari kuingizwa nchini bila kulipia kodi na ushuru. Hili ni jipu kubwa, kwani magendo haya yanaingizwa kwa ushirikiano wa maofisa mbalimbali, kuanzia SBT na Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA) hadi polisi na bandari.

Magendo ya sukari humu nchini ni ya aina mbili. Kuna sukari ambayo inaingizwa kwa kisingizio kuwa ni ya nchi jirani, yaani inapitia bandari zetu na kupelekwa nchi hizo. Inateremshwa bandarini na kabla ya kufika hata Chalinze inauzwa kwa msambazaji wa ndani na kisha inaonekana sokoni. Nyaraka zinagushiwa zikionesha kuwa shehena hiyo imevuka mpakani na kuingia nchi jirani, kumbe imeishia hapa hapa nchini. Hii imekuwa ikifanyika miaka nenda miaka rudi.

Ndiyo maana hata TRA imesema sukari ya magendo imekuwa ikiingia nchini kupitia bandari bubu ya Bagamoyo bila kulipiwa kodi. Nyingine huteremshwa maeneo yaMbweni, Kunduchi, Kigamboni na Mlingotini nje ya Dar es Salaam. Haya ni magendo ya aina ya pili.

Sukari hii hutoka nchi kadha, zikiwemo India na Brazil. Tunaambiwa Serikali inapoteza takriban Sh bilioni 86 kila mwaka kutokana na uingizaji wa sukari ya magendo nchini. Hizi ni habari kutoka TRA. Si habari za leo wala jana, ni za muda mrefu. Tumechukua hatua gani, licha ya kupiga domo tu?

Kama TRA walielewa yote haya kwa nini washindwe kuzuia? Kama maofisa wachache walishirikiana na hawa waagizaji haramu, kwanini wasiweze kuwabana? Walibaki kulalamika tu? Wanamlalamikia nani? Jipu hilo.

Hili sakata la sukari kutoka nje limekuwapo siku nyingi, wenye viwanda wakilalamikia sukari rahisi inayoingizwa nchini. Kwa mfano, Juni 2012 iliripotiwa kuwa Serikali iliongeza muda wa mwezi mmoja kwa vibali vilivyokuwa vimemalizika mwezi uliotangulia. Hivyo kampuni ziliruhusiwa kuingiza tani karibu 20,000 katika mwezi mmoja.

Labda ni vizuri tukajua ni kina nani hawa waliokuwa wakipewa hivi vibali maalumu vya kuagiza sukari. Nao ni wafuatao: Tanzania Commodities Trading Co. LTD (tani 26), TPM  LTD (tani 12), Matunda B.C. LTD (tani 12), East Coast Oils and Fats Ltd (tani 1,292) na New Tradeco Investment  Ltd.

Wengine ni, Mohamed Enterprises (T) LTD (tani 8), Decent Investment Ltd (2,116), Rubab Investment Ltd (tani 12), Multi Modal Transport Africa (tani 2), Trade Logistics (EA) Ltd (tani 12), Ngawaiya Stores (tani 100), DRTC Trading Company Ltd (tani 2,522) na Market Makers (T) Ltd (tani 480).

Wengine ni Supermarket (tani 910), Power Roads (tani 1,170), A. O. K. Investment (tani 500), B. F. K. Company Ltd (tani 500), Kigwaza Holdings (tani 500), Sofia International (tani 500), Conti Africa Ltd (tani 260), Masooma Supermarket (tani 208), BAKWATA (tani 2,500), Saddique Supper Service Station (tani 1,700) OLAM Tanzania Ltd (tani 832), United Youth Shipping Co. Ltd (tani 494) na EDISABA General Supplies Ltd (tani 1,000).

Inawezekana wengi kati ya hawa ni wafanyabiashara wa sukari, isipokuwa Bakwata. Mimi sina hakika kama wao pia wanafanya biashara ya kuagiza na kuuza sukari. Labda wahusika watatueleza.

Tukibaki katika hiyo hiyo Awamu ya Nne, aliyekuwa Waziri wa Kilimo wakati huo, Christopher Chiza aliwahi kutamka kuwa wafanyabiashara hawataruhusiwa kuagiza sukari kwa sababu wanaagiza kwa wingi, hasa kutoka Malawi na hivyo kuinyima Serikali ushuru. Kwa hiyo alisema kanuni za viwanda vya sukari (Sugar Industry Regulations)zitarekebishwa ili sukari iagizwe kwa ujumla kwa njia ya zabuni kama inavyofanyika katika sekta ya mafuta.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa SBT, Henry Semwaza alisema kanuni mpya pia itazuia magendo ya sukari inayodaiwa inakwenda nchi jirani kisha inaishia katika soko la ndani. Akaongeza kuwa chini ya mpango mpya, umoja wa wenye viwanda vya sukari na wafanyabiashara utaanzishwa na kupewa jukumu la kuagiza sukari kwa wingi mara moja au mbili kila mwaka.

Je, haya yaliyoahidiwa na Waziri na SBT yametimizwa au ilikuwa ahadi hewa? Kama yalitimizwa, mbona sasa tena Rais Magufuli analazimika kutumbua jipu la sukari?

Ila ni vizuri tujiulize, kwa nini tuagize sukari kutoka nje wakati tuna viwanda vikubwa vya sukari nchini? Ni kwa sababu soko la sukari hapa nchini linahitaji tani 420,000 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na tani 170,000 kwa matumizi ya viwandani. Kwa hivyo nchi inahitaji tani 590,000. Tuna viwanda vinne nchini  – Kagera, Kilombero, Mtibwa na TPC. Tatizo ni kuwa viwanda hivi vina uwezo wa kuzalisha tani kama 300,000; yaani kuna upungufu wa tani 290,000 kwa sukari ya kawaida na ya viwandani.

Viwanda hivi vilibinafsishwa kati ya mwaka 1998 na mwaka 2000 kwa sababu tunaambiwa eti chini ya umiliki wa umma vilikuwa vimeshindwa kujiendesha. Sasa wanadai wameongeza uzalishaji baada ya kubinafsishwa. Kama ni hivyo, kwanini basi tunalazimika kuagiza sukari kutoka nje?

Mimi nilitarajia kuwa tangu mwaka 2000 tungeongeza idadi ya viwanda badala ya kubaki na vilevile vinne vya enzi ya Mwalimu au enzi ya mkoloni.

Hata hivyo, Jakaya Kikwete, alipokuwa Rais, aliwahi kusema kuwa Tanzania itahitaji angalao viwanda vingine 10 ifikapo mwaka 2030. Ni kwa sababu mahitaji yetu yatakuwa tani milioni 1.5 kwa vile nchi itakuwa na watu milioni 72 wakati viwanda vyetu ni hivi vinne tu.

Hii si rahisi, kwani tutahitaji uwekezaji wa dola bilioni 3 za Marekani. Inaonekana wawekezaji hawapendi kuwekeza katika uzalishaji wa sukari, kwani kwa muda wa miaka 40 hatujafungua kiwanda kipya hata kimoja.  Walichofanya ni “kununua” kwa bei ya che viwanda vya umma na sasa wanataka walindwe na Serikali kutokana na ushindani wa kimataifa.

Ukweli ni kuwa kama hali hii itaendelea, basi sukari kutoka nje itaongezeka hadi kufikia tani milioni 1.1 ifikapo mwaka 2030.  Huo ndio uchumi tegemezi. Na sasa Rais Magufuli anazungumzia kuzuia uagizaji wa sukari.  

Kuna wanaoshauri kuwa badala ya kupiga marufuku sukari ya nje ni vizuri kuwezesha viwanda vyetu viingie katika ushindani wa kimataifa kwa kuzalisha sukari kwa wingi na kwa bei nafuu. Hii ni njia bora kuliko kuiomba Serikali iwalinde kwa kuzuia sukari rahisi kutoka nje. Kuna wazalishaji wengi humu nchini ambao wanalazimishwa kushindana na wazalishaji wa nje. Kama wao hawalindwi na Serikali kwa nini tuvilinde viwanda vya sukari? Na mpaka lini?

Kwa njia hii ya kushindana na wazalishaji wenzao viwanda vyetu vya sukari vitalazimika kupunguza gharama za uzalishaji na kuzalisha sukari kwa bei nafuu. La sivyo tutakuwa tunawabebesha wananchi wetu gharama kubwa za uzalishaji.   

Kwa mfano, tunaambiwa tangu Rais Magufuli apige marufuku sukari ya nje, tayari bei imepanda. Kiroba cha kilo 25 kilichokuwa kikiuzwa kwa Sh 45,000 sasa ni Sh 47,000. Kilo moja iliyokuwa Sh 1,900 hadi Sh 2,000 sasa ni Sh 2,100 hadi Sh 2,200.

Katika mtandao mwananchi mmoja anasema: “Hii imenipa shida sana kujua kama tamko lile la Rais lilikuwa na lengo la kutusaidia sisi wananchi wa kawaida au lilikuwa ni kuwasaidia wafanyabiashara, hususani wenye viwanda ili wauze hiyo sukari yao kwa bei wanayopanga wao?

“Kama nia ya dhati ni kusaidia wananchi wenye hali ya chini, basi Serikali itoe bei elekezi ambayo itakuwa chini ya ile ya sukari kutoka nje. Tofauti na hivyo tutaelewa wazi kuwa mpango unaofanyika ni kuwanufaisha wafanyabiashara wakubwa na wenye viwanda vya sukari.”

Kwa upande mwingine, watetezi na waumini wa kile wanachokiita soko huria wanakumbushwa kuwa viwanda vya sukari huko nje vinapewa ruzuku na serikali zao ili waweze kuuza kwa bei nafuu. Kwa njia hii wazalishaji hao wanaweza kuuza sukari katika masoko ya kimataifa kwa bei iliyo chini ya gharama yao halisi ya uzalishaji.

Hii ina maana hakuna soko huria kama wanavyodai. Mzalishaji wa nje anayepewa ruzuku huwezi kumpambanisha na yule anayejitegemea kama huyu wa Kilombero. Ndio maana tunasema katika biashara ya kimataifa hakuna usawa wanaouzungumzia.

Kuna faida nyingine ya kuongeza uzalishaji wetu wenyewe. Ukiachia ajira inayotolewa na kodi inayolipwa, kuna pia nishati ya umeme inayozalishwa kutokana na makapi ya miwa. Viwanda vyetu vya sukari vinajizalishia umeme wao wenyewe na hata kuingiza ziada katika gridi ya kimataifa. Wakati huo huo maelfu ya wakulima wa miwa watakuwa wanapata soko la karibu.

Lakini kama tulivyosema, kama wamiliki wa viwanda vyetu vya sukari wanataka Serikali iwalinde, basi wakubali pia bei elekezi na masharti mengine. La sivyo tutakuwa tunawatajirisha mabepari  hao na kuwakandamiza wananchi.