Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji hivi karibuni alikutana na waandishi wa habari kuzungumzia uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai kuiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhusu Jimbo la Mbunge Tundu Lissu kuwa wazi. Tumenukuu sehemu ya maelezo hayo hapa.

Hadi tunapozungumza (na waandishi wa habari) ikiwa ni siku tatu tangu Spika alipotangaza uamuzi wake Chadema ambacho ndicho chama chenye udhamini wa ubunge wa Lissu hakina taarifa yoyote rasmi juu ya uamuzi huo.

Imekuwaje Spika hajachukua uamuzi kama huo bila kutuuliza wadhamini wa Lissu au kwa nini amechukua uamuzi huo bila hata kututaarifu? Tunaamini kuwa (Spika) hajafanya kwa bahati mbaya kwa sababu hii ni mara ya pili sasa anafanya uamuzi wa namna hiyo.

Tumezitafakari sababu ambazo Spika amezitumia kufikia uamuzi wake huo. Amedai kuwa hajui Lissu yuko wapi. Sababu hii ina ukakasi mkubwa.

Spika Ndugai mwenyewe amewahi kuthibitisha namna alivyoshiriki katika kuokoa uhai wa Lissu, kwa kufika hospitalini siku ile ile aliyoshambuliwa kwa lengo la kuuawa. Akashiriki katika uamuzi wa kuhakikisha anasafirishwa kwenda kutibiwa nje ya nchi. Amewahi kunukuliwa akisema atakwenda kumuona hospitalini Nairobi au kokote atakakopelekwa kutibiwa, ingawa hajawahi kufanya hvyo, Nairobi, Kenya wala Ubelgiji. Chadema tunazo taarifa za mawasiliano rasmi ya kiserikali kupitia nyaraka, kati ya Ofisi ya Katibu wa Bunge na familia ya Lissu kuhusu matibabu ya Lissu. Mawasiliano hayo yalinakiliwa kwa Lissu pia akiwa katika matibabu huko Ubelgiji ambako anaendelea hadi sasa, katika Hospitali ya Uz Leuven. Hapa Spika anataka kuwaambia Watanzania kuwa Ofisi ya Katibu wa Bunge na Ofisi ya Spika na Spika mwenyewe hawana mawasiliano ya kikazi kiasi Katibu wa Bunge anajua Lissu aliko lakini Spika hajui.

Kwa muda wote ambao Spika anadai hajui Lissu aliko na kuwa ni mtoro, Bunge limekuwa likimlipa mshahata na posho zake kama mtumishi wa muhimili huo. Ni jambo la ajabu kuwa muhimili huo ulikuwa ukimlipa stahiki zake zote kwa takriban miaka miwili sasa akiwa hahudhurii mkutano wala kikao cha Bunge, lakini haujui mtumishi wake you wapi na kwa sababu gani? Watanzania wote wanajuana dunia iliona, Makamu wa Rais Samia Suluh Hassan alikwenda kumsalimia Lissu akiwa hospitalini Nairobi ambaye alisema ametumwa na Rais John Magufuli kupeleka salamu zake kwa mgonjwa. Akiwa Ubelgiji, serikali imekuwa ikitambua kuwa Lissu ni mgonjwa na ametembelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji.

Aidha, muhimili wa Mahakama unatambua kuwa Lissu ni mgonjwa na yuko kwenye matibabu nje ya nchi na hata Jamhuri walipopeleka ombi mahakamani Kisutu kuomba Lissu afutiwe dhamana yake kwa hoja kuwa hajulikani alipo, Mahakama ilikataa ombi hilo la Jamhuri kwa kuwa inatambua kuwa Lissu ni mgonjwa na anaendelea na matibabu.

Lakini pia Spika amedai kuwa Lissu hajajaza fomu za maadili ya utumishi wa umma. Ukakasi wa suala hili ni mkubwa sana na unaibua suala kubwa la kisheria kuhusu kutoingiliana kwa mihimili ya serikali. Kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, mamlaka yenye wajibu wa kusimamia sheria ya maadili ya viongozi wa umma ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma. Watu wote wanaotajwa na sheria husika kuwa wanawajibika kwa mujibu wa sheria kujaza fomu hizo hufanya hivyo na kuziwasilisha Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Umma. Sekretarieti hiyo ina mamlaka makubwa ya kimahakama. Inao uwezo wa kuwaita, kuwahoji, kuwasikiliza na kuchukua hatua dhidi ya watu wote ambao wamekiuka taratibu zinazosimamia maadili ya viongozi wa umma ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu fomu za tamko la rasilimali na madeni. Swali hapa ni je, lini Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imempelekea wito wa kumtaka Lissu afike kuhojiwa au kusikilizwa kabla ya kuchukuliwa hatua kama akibainika amekiuka sheria hiyo kama ambavyo Spika anataka watu wamuamini?

Chadema tumebaini lengo la uamuzi huo wa Spika ukiachwa kama ulivyo madhara yake yako kwenye Katiba ibara ya 39 (1) ambayo inaweka masharti ya mtu ambaye hatastahili kuchaguliwa kushika kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania, kipengele kidogo cha (d) kinaeleza kuwa mtu hatastahili kugombea na kuwa Rais wa nchi anapokuwa hana sifa za kumwezsha kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, kifungu hicho kikisomwa pamoja na kifungu cha (d) cha ibara ya 67 (2) na 71 (1) ambacho kinaweka masharti ya mbunge kukoma ubunge wake kuwa ni pamoja na iwapo mbunge atathibitika kwamba amevunja masharti ya sheria ya maadili ya viongozi wa umma.

By Jamhuri