Uwanja wa Jangwani jijini Dar es Salaam umebeba historia muhimu katika taifa letu. Mikutano kadhaa kipindi kile cha harakati za kudai Uhuru ilifanyika hapo.

Jangwani imeendelea kujizoea umaarufu hata baada ya Uhuru. Mikutano mingi mikubwa imeendeshwa Jangwani. Mikutano ya kisiasa ya vyama mbalimbali imefanyika hapo. Mkutano mkubwa wa Baba Mtakatifu Yohane Paulo II ulifanyika Jangwani kwa sababu ndipo mahali katika Dar es Salaam palipoonekana kuimudu hadhira ile.

Umaarufu wa Jangwani umejulikana pia kwa waumini wa madhehebu mengine. Shughuli nyingi zimefanyika hapo.

Jangwani pia ni mahali ambako makumi kwa mamia ya vijana walikusanyika jioni kufanya mazoezi, hasa kushiriki mchezo wa mpira wa miguu. Tunaweza kutaja mengi, lakini itoshe tu kusema umuhimu wa Jangwani kwa wakazi wa Dar es Salaam hauna kipimo.

Jangwani tuliyoijua miaka ile si Jangwani ya leo. Mambo yamebadilika kabisa. Jangwani imekufa! Kifo cha Jangwani kinaweza kuwa kimesababishwa na kiu ya maendeleo. Serikali ya Awamu ya Nne kwa kutambua tatizo la usafiri katika Jiji la Dar es Salaam, ilileta mradi wa mabasi ya mwendokasi. Ni mradi mkubwa kwa hapa nchini na katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati. Japo unasuasua, faida zake si haba.

Umuhimu wa mradi huo ukawafanya watoa uamuzi watenge eneo la Jangwani kwa ajili ya ujenzi wa ofisi na karakana. Ulikuwa uamuzi mzuri kwa maana ya kile kilicholengwa. Hata hivyo, baada ya mradi huo kukamilika kumeonekana pengine uamuzi wa kuweka majengo yale mahali pale ungeweza kuepukwa.

Majengo yale yamepindua jiografia halisi ya uwanja na Bonde la Msimbazi kwa eneo hilo. Maji yamepoteza mwelekeo, hivyo yamekuwa yakituama.

Kumeibuka madimbwi yanayohifadhi maji, hivyo kustawisha majani na mimea mingine ambayo awali haikuwa tishio katika eneo hilo.

Kwa kuitazama Jangwani ya leo ilivyo, matumaini ya Dar es Salaam kuwa na eneo jingine zuri, kubwa, lililo wazi yanafifia. Tanganyika Parkers pana wenyewe.

Tufanye nini? Hatujachelewa. Maendeleo yana gharama zake. Tuitazame Jangwani kama eneo la urithi kwa wakazi wa Dar es Salaam wa leo na wajao. Tuitazame Jangwani kwa ajili ya manufaa mapana ya kizazi kijacho ambacho kitakuwa na idadi kubwa mno ya watu kuliko ilivyo leo mwaka 2019.

Serikali ina uwezo wa kuifufua Jangwani kwa kuhakikisha inaondoa miundombinu iliyopo na kuacha uwanja kama ilivyokuwa miaka iliyopita. Tena basi, inaweza kuifanya Jangwani ikawa nzuri na ya kisasa kuliko ilivyokuwa awali. Naamini hili haliwezi kuwa jambo la kuitatiza serikali yetu. Uwezo wa kuyafanya haya upo, kinachotakiwa ni utashi tu wa kuyatenda.

Dar es Salaam ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi zaidi duniani. Uwanja wa Taifa uwezo wake ni wa kuhimili watu wasiozidi 60,000. Hii ni idadi ndogo sana. Tumeshashuhudia watu wengi – pengine kuliko walioingia uwanjani – wakibaki nje baada ya kukosa nafasi uwanjani. Haya yametokea kwenye matamasha ya kidini na wakati wa michezo na burudani. Hili pekee linapaswa kutufumbua macho ili kuona umuhimu wa kuwa na maeneo ya wazi kama Jangwani.

Dar es Salaam kunahitajika kuwapo mahali mahususi penye uwezo wa kumeza mkusanyiko wa watu hata 500,000 au zaidi. Hakuna uwanja wa mpira unaoweza kujengwa kuhimili namba hiyo. Tunaweza kuwa na uwanja wa aina hiyo [jambo ambalo ni gumu], lakini kuna hatari za kiusalama.

Kuna faida nyingi za kuwa na ‘Jangwani’ za kutosha katika majiji, miji na vijiji vyote nchini. Miji ya kiungwana kote duniani ina maeneo mengi ya wazi – makubwa kwa madogo. Ukiacha faida za kuhimili idadi kubwa ya watu, maeneo ya wazi yanasaidia mambo mengi hata kwenye masuala ya kiafya.

Najiuliza, ikitokea leo tumepata ugeni mkubwa katika Jiji la Dar es Salaam, wapi tutakusanyika? Tukiwa na mkutano wa kitaifa wenye kuwavuta watu wa kada na itikadi zote, tutaufanyia wapi?

Miundombinu ya mwendokasi iliyopo Jangwani thamani yake ni kubwa, lakini sidhani kama thamani hiyo inazidi faida nyingi ambazo uwanja huo unazitoa kwa Watanzania. Tunaweza kuiondoa miundombinu tukabaki na Jangwani kwa manufaa mapana ya nchi na wananchi. Vijana wanahitaji maeneo ya kukutana kwa michezo, kuimarisha afya na kuchangamana kwa ajili ya kujenga urafiki.

Kuirejesha Jangwani kwenye uhalisia wake ni jambo linalowezekana kwa sababu mafuriko yanayotokea hapo ni jambo la kudumu. Asili imeshathibitisha pasi na shaka kuwa majengo yale pale yalipo si mahali pake.

Mpango huu uwe wa kitaifa. Tuhakikishe kuanzia ngazi za vijiji tuna maeneo ya wazi mengi na makubwa kwa matumizi ya umma. Huu mpango wa wajenzi wa barabara kutumia viwanja vya michezo kutunzia vifusi nao upigwe marufuku. Vijana waachiwe maeneo yao kwa ajili ya michezo.

Tuijenge Tanzania kwa kufikiria miaka 50 au 100 ijayo. Haya yanaonekana katika nchi zilizoendelea. Sioni kwa nini tushindwe. Tutenge maeneo kwa kufikiria ongezeko la watu na mahitaji ya mikusanyiko mikubwa ya kidini, kisiasa, kijamii na kadhalika.

By Jamhuri