Wasomaji wa makala zangu katika Gazeti la JAMHURI wamenisaidia sana mimi kujitambua ninavyoeleweka katika jamii.

Ujumbe mfupi wa naandishi (SMS) nyingi zimenikomaza, zimenipa moyo na zimenijengea hali ya kujiamini kuwa ninatoa ‘material’ kwa somo la URAIA hapa nchini. Wale waliofaidika wamekiri kuelimika na wale wanasiasa wameona mimi ni tishio, hivyo wakanipachika sifa ya “Mfia Itikadi ya CCM”- ni kada kweli kweli. Hilo si kweli, bali mimi ni mzalendo tu.

Sasa mimi nikaona kumbe ukweli kama alivyotueleza Mwalimu Julius Nyerere katika kile kijitabu chake cha “TUJISAHIHISHE toleo la Mei 1962 uk. ule wa 3 ibara ya kwanza, Baba wa Taifa ameandika: “Ukweli una tabia moja nzuri sana. Haujali mkubwa, wala mdogo, haujali adui wala rafiki. Kwake watu wote ni sawa. Pia ukweli unayo tabia ya kujilipiza KISASI kama ulipuuzwa!”

Basi, wapo watu hawajui ukweli na wanajali nafsi – maana yake kwao ukweli ni maoni yao na matakwa yao tu. Kumbe kinachohitajika katika jamii zetu ni kujifunza kusikiliza hoja kisha kuzikubali au kuzikataa bila kujali aliyezitoa ni rafiki au si rafiki. Makosa yetu mengine ni WOGA. Tabia ya woga inamzuia mtu kulaumu au kutetea kadiri haki inavyotaka kutendwa. Basi kwa utangulizi wangu huo naomba tu tukumbushane kutokana na historia ya Taifa letu tangu harakati za kutafuta Uhuru hadi kufikia hapa tulipo leo. Tusije tukasahau historia yetu hii.

Hebu tujikumbushe hasa vyama vya siasa vya UPINZANI. Tunajua fika kuwa wakati nchi inatawaliwa na mkoloni, chama chochote cha siasa cha wananchi kilipewa sifa hiyo ya kuwa “WAPINZANI”. Mkoloni (mzungu) awe Mwingereza au Mfaransa au Mbelgiji au Mreno) Serikali yake ndiyo ikitawala – ndiyo ilikuwa dola, hivyo chama cha siasa cha wananchi kilipewa majina katika nchi mbalimbali kuonesha ni wapingaji wa utawala halali. Kuna vyama watu wake wakiitwa “REBELS”. Waasi wanamuasi nani? Mtawala Mzungu! Hapo mikusanyiko yao yote ilionekana ni uasi “rebellious” – wakataaji amri halali za dola. Mahali pengine watu hao waliitwa “INSTIGATORS”- wachochezi, waleta chokochoko katika utawala halali, wafanya fujo.

Pengine waliitwa “TERRORISTS au BANDITS” – majahili, magaidi au hata maharamia. Na pengine wamepachikwa majina yasiyoeleweka kama vile “HOOLIGANS” yaani wahuni tu wa mitaani wenye njaa na wasio na kazi.

Huo ndio mtazamo wa wakoloni watawala katika makoloni yote. Upinzani haukupokelewa na dola yoyote ile, bali uligandamizwa tu.

Sisi watawaliwa, tulipoanzisha vyama hivi vya upinzani kwa utawala haramu wa wakoloni hao tulivipa majina yetu kama vile vyama vya “UKOMBOZI” (Liberation Movements) au Vyama vya Wazalendo (Patriotic Movements) kumaanisha vina lengo moja tu la KUMKOMBOA MWANANCHI kutoka tawala dhalimu za wageni wakoloni.

Hata baadhi ya wazungu walipotuelewa waliviita vyama vya siasa vya nchi zetu kuwa LIBERATION/PATRIOTIC MOVEMENTS or PARTIES.

Sasa basi, chama cha Tanganyika African Nationa Union (TANU) au kile cha Afro – Shiraz vilipoanzishwa vilikuwa na malengo hayo ya kumkomboa mwananchi kutoka ule utawala wa wageni. Basi viliitwa na wazungu vyama vya UPINZANI “Opposition Parties”- wapinga serikali za kikoloni. Katika mtazamo huo, neno DEMOKRASIA lililodaiwa na wazungu kumaanisha utawala wa wengi katika makoloni, halikuwapo; ndiyo kusema kulikuwa na utawala kandamizi. Tulitawaliwa kimabavu kwa mtutu wa bunduki, haikuwepo Serikali huru ya kidemokrasia, kwa tafsiri sanifu ya neno hili.

Unabaki unajiuliza hawa walimu, mabingwa wa kutetea haki za binadamu na uhuru wa kujitawala, vipi wao walishindwa kutuachia hiyo DEMOKRASIA ambayo leo wanadai nchi za Kiafrika hazina? Walitufundisha misingi ya demokrasia?

Sisi tuliunda vyama vya kudai tujitawale na tukafanikiwa. Leo Wazungu eti wanakuja kuangalia, kama uchaguzi wetu ni wa kidemokrasia! Wanafiki wakubwa hawa! Hawana hata soni katika kujidai wao ndiyo wenye demokrasia safi na lazima tuifuate.

Wakati TANU wakiwa katika upinzani hapa Tanganyika, wakoloni Waingereza walianza kuminya Uhuru tuliokuwa tunaudai kwa njia mbalimbali. Uhuru wa kukutana na kufanya mikutano elimishi katika matawi ya TANU uliminywa. Uhuru wa kutembelea matawi viongozi wa TANU waliminywa na hata kukataliwa kabisa wilayani.

Watumishi wa umma walizuiwa kuingia au kujiunga katika vyama vya siasa. Hapo unaona demokrasia ya Wazungu? Eti bado tunawasikiliza mpaka leo hii.  Wasipotoa ripoti ya uchaguzi Wazungu hao hao waliotunyima uhuru, leo hii sisi tunapiga kelele “uchaguzi wetu haukuwa huru hata wajumbe wa EU (European Community) wametamka mwenye ripoti yao. Jamani, kweli bado tuna kasumba kubwa namna hiyo? Tumetekwa mno na Wazungu. Kisa? FEDHA zao!

 Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi mwenye ung’amuzi na kiona mbali sana. Alipoona hila za wakoloni Waingereza kuzuia TANU- chama cha upinzani- kisifurukute alitoa tahadhari hii.

Namnukuu: “Ndugu wananchi JIHADHARINI. Adui anashindwa. Njia yake ni moja tu, nayo ni kutaka GHASIA ili atumie bunduki. TUSIMPE nafasi hii. MSIMCHOKOZE, mkafanya GHASIA na MATATA. Kaeni kimya na wachangamfu kama kawaida yetu” (SAUTI YA TANU Na. 29 tarehe 27 Mei, 1958).  Maneno haya ya hekima ya Mwalimu yalizima kabisa mori na hasira za wana TANU kule Geita wasifanye vurugu zozote.

Imetokea mara nyingi watu kusumbuliwa na Serikali tawala. Serikali inapokataa kushirikiana na raia, inajiamulia mambo peke yake, ndipo chanzo cha machafuko katika nchi. Hapo hakuna utawala wa amani wala wa kidemokrasia hata kidogo. Hiyo ni historia ya unyanyasaji kwa upinzani. Wapinzani wamekuwa mwiba kwa kila dola.

Mwaka 1958 wakoloni walipotangaza uchaguzi ule wa mseto uliowalazimisha wananchi wachague Mzungu, Mwasia na Mwafrika, ulikuwa mpango wa kubomoa kabisa umoja wa wananchi. Serikali iliweka kwa makusudi kikwazo kikubwa cha masharti ya uchaguzi ili TANU ishindwe. Serikali ilitumaini (anticipated) kuwa upinzani (TANU) ungefanya KOSA la kihistoria KUUSUSIA uchaguzi ule. Lakini tena hekima na busara za kiongozi wetu Mwalimu Nyerere TANU iliamua kushiriki katika uchaguzi ule. Huu ulikuwa ushindi mkubwa mno kwa upinzani. Dawa ya moto ni maji wala si moto kutoka upande wa pili. Hivyo hamaki penye kulipuka kwa hasira haisaidii kulinda amani na utulivu.

Laiti au kama TANU wangesusia uchaguzi ule, Serikali ingepata fursa na sababu ya kutosha kukipiga marufuku chama kile. Tanganyika ingepata Uhuru tunaojivunia leo hii? Sidhani! Sijui vijana wa leo kama wanalijua hili.

Katika mkutano wa Tabora mwaka 1958 wanachama wote wa TANU, mkutano mzima ule ulitaka UAMUZI wa KUSUSIA uchaguzi ule wa MSETO. Ni Mwalimu Nyerere peke yake alisimama kidete kwa utulivu (cool, methodical and convincingly) na kwa busara kubwa alianza kazi ya kuwaelimisha wajumbe. Hakuelimisha tu wajumbe juu ya madhara ambayo TANU wangeyapata, bali aliwaonesha hasa faida ambazo TANU wangepata kwa kushiriki katika uchaguzi ule.

Baada ya uamuzi ule wa kutokususia uchaguzi wa mseto kwa busara ya Mwalimu mkutano ulitulia na kuendelea kujadili ajenda nyinginezo (Tazama Historia ya Mapambano ya Mtanzania uk. 173 – Mapunda H). Haya nimeyanukuu kutaka kuelezea namna hekima na busara ya kiongozi wa upinzani siku zile vilivyoweza kufanikisha malengo ya wapinzani hatimaye wananchi wakapata uhuru na sasa tunaendesha dola. Wazo au dhana ya kususa ni tazamio la watu wengi wa kawaida katika kudai matakwa yao yatekelezwe. Lakini je, mara ngapi njia hii imeleta mafanikio tarajiwa?

3864 Total Views 1 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!