Sehemu ya kwanza, mwandishi wa makala hii alisema katika mkutano wa Tabora mwaka 1958 wanachama wote wa TANU, mkutano mzima ule ulitaka UAMUZI wa KUSUSIA uchaguzi wa MSETO. Ni Mwalimu Nyerere peke yake aliyesimama kidete kwa utulivu (cool, methodical and convincingly) na kwa busara kubwa alianza kazi ya kuwaelimisha wajumbe. Hakuelimisha tu wajumbe juu ya madhara ambayo TANU wangeyapata, bali aliwaonesha hasa faida ambazo TANU wangepata kwa kushiriki katika uchaguzi ule. ENDELEA…

 

Mwalimu Nyerere aliwahi kudhamiria kususia ule uchaguzi, lakini alikaa akafikiri na kusema kama tusiposhiriki uchaguzi huu vyama mbadala vitaingiza watu wao na hapo Serikali itaweza kutunga sheria za ajabu kabisa bila sisi kuwamo humo.

Ni lazima tushiriki ili tukiingia katika Baraza hilo la kutunga sheria hatimaye matakwa yetu yatatambulika na tutashika dola. Na ndivyo ilivyotokea.

Mimi mtazamo wangu kwa historiai ya matukio hayo ya demokrasia ya wakoloni kutukandamiza, tukafanikiwa kupenya na kuingia katika chombo chao cha kutunga sheria, tulifanikiwa sana kubadili mwelekeo wa siasa wa nchi hii hatimaye tukapata Uhuru wetu. Bwana Mungu asifiwe.

Sasa vijana wa leo, tunajifunza nini kutokana na historia ya nchi yetu kutoka upinzani mpaka kushika dola?

Kwa mtazamo wangu ninaona upinzani wa sasa unao wasomi wengi na wenye “talents” nyingi.  Kuna vijana wenye uzalendo na wenye uchungu wa maendeleo ya wananchi. Lakini kwa masikitiko yangu makubwa hawajatulia. Hawana ile hali ya kusema “mkaange samaki kwa mafuta yake mwenyewe”.

Mwalimu Nyerere alitumia uchaguzi wa Kura Tatu au wa Mseto na kumng’oa mkoloni aliyetumia fedha, mabavu ya serikali na hata kuunda chama cha walowezi kilichoitwa UTP chini ya mlowezi Ivor Bayldon na Mtendaji Mkuu Brian Willis kutoka Chama cha Conservative cha Uingereza ili waendeleze dhulma yao.

Lakini sote tunajua walizidiwa kete na Mzanaki wa Butiama, Mara. Aliwakaanga kwa kutumia kanuni zao zile zile za kura ya Mseto.

 Neno kususa kwa sasa haliwezi kabisa kuleta matokeo endelevu katika Taifa letu. Ninaamini wakijikita katika kushiriki vikao watatoa mchango mkubwa na utaitikisa Serikali ya chama tawala. Njia hii ya mapambano (provocative method and confrontation) inaonekana haifai kwa hali ya sasa kwa maneno, Mwalimu alisema Serikali wanatafuta kila chokochoko watumie bunduki. Kwa nini upinzani wasijaribu kuepuka chokochoko ili wasibugudhiwe na hii Serikali ya chama tawala?

Sasa tunaona magari ya kumwagia wananchi maji ya washawasha yanatumika na virungu vinatumika, kwa nini kuwapa mwanya huo Serikali watumie mabavu?  Bado naona hekima ya Mwalimu inaweza kusaidia upinzani wa sasa kunufaika kwa kutumia utulivu na busara katika malengo yao.

Mwalimu alionya hivi: “Fellow – Africans be on your guard. Don’t give the government that chance. Don’t be provoked into violence. Be as calm and as good – humored as you have always been (Nyerere: Uhuru na Umoja uk. 60). Upinzani wamewahi kufikiria namna hiyo?

Suala la kudai maandamano kuwa ni haki ya kila chama ni kaulimbiu iliyopitwa na wakati kwa sasa. Je, tunaelewa udanganyifu wa Wazungu?

Tumewahi kujiuliza kwanini katika kila uchaguzi katika nchi huru za Afrika, Wazungu wanataka kuja kuangalia kama kweli uchaguzi wa Waafrika unakuwa huru au kuna mizengwe?

Shirikisho la Nchi Huru za Afrika (African Unity) kule Addis Ababa wamewahi kupeleka wajumbe wao kutazama uchaguzi katika nchi ya Ulaya au Marekani mara ngapi? Kwaninii waangalizi kutoka AU hawapelekwi? Ni ulofa wetu Waafrika au ni imani yetu kuwa Wazungu hawavurundi au ni ukosefu wa fedha za kuendea huko?

Ina maana moja tu! Ulaya na Marekani wamestarabika sana hata hawawezi kufanya madudu? Ni kweli hiyo? Nchi ya Italia haina kabisa “Stable Governments” lakini Waafrika hatuthubutu kulichunguza hilo. Ureno na  Uhispaniawana Serikali babaishi. Na hao ndiyo Wazungu wa EU wanatoka EU kuja kutuangalia uchaguzi wetu. Sababu kubwa ni Wazungu wanaogopwa na mtu mweusi, kisa? Walitutawala, basi wana demokrasia nzuri! Je, imani namna hii ni sahihi kweli?

Nchi huru za Afrika na hasa niseme za duniani kote kamwe hazihitaji tena mwongozo wa kimawazo kutoka nchi za Magharibi. Wazungu popote na wakati wowote wametumia nguvu zao kubwa hata za kijeshi kuvunja UPINZANI. Sasa wanatumia nguvu zao za uchumi na ushawishi kusimamia nchi maskini za Afrika huru.

Sisi wengine tungali tunakumbuka Urusi wakati ikiitwa USSR (Union of Soviet Socialist Russia) na siasa yao ya umashariki (Eastern Block) enzi za vita baridi walivyotumia mabavu kumpiga DUBCHEC wa Hungary (mwaka 1968) asilete mageuzi katika wananchi kule nchi za Mashariki.

Tunakumbuka Marekani walivyomchukia Saddam Hussein wa Iraq na mpaka wakamng’oa. Leo hii Iraq bado imesambaratika na kusababisha Mashariki ya Kati kuwa kitovu cha mapigano ya mara kwa mara.

Marekani hao hao walimsambaratisha Muammar Gaddafi wa Libya kwa chuki binafsi tu, hadi leo Libya haijapata Serikali kamili kuongoza nchi ile. Rais Barack Obama wa Marekani mwenyewe amekiri kuwa walifanya makosa kumwondoa Gaddafi.

Wafaransa, enzi za mtawala akiitwa General De Gaulle, aliwakandamiza wananchi wa Guinea enzi za Sekou Toure, kisa? Eti hawakumuunga mkono katika ile kura ya maoni ya Septemba 28, 1968.

Tunasoma maneno haya namnukuu: “…For doing so, Guinea was punished by de Gaulle in a way he had implicitly threatened – all economic aid was cut off, all French Staff were withdrawn. This caused a state of confusion and dislocation in the country” (Tazama Africa Today uk. 627 – Independence of Guinea). Hapo tunaona ukandamizaji wa Wazungu kwa maskini Waafrika.

Mwingereza alisambaratisha Argentina wakati ule wa kugombea Visiwa vya Falk Lands kule Amerika ya Kusini kwa namna hata wananchi wa kule wakajikuta wakichapwa bila huruma – mwaka ule wa 1982. Ni tabia ya ubabe tu hiyo kuonea wanyonge.

Hao ndiyo wastaarabu wanaojigamba wasimamizi wa demokrasia duniani – Wamagharibi, hasa niseme Wazungu, wenye kujidai ukinara wa kuangalia demokrasia. Huku kwetu EU wametoa ripoti yao juu ya uchaguzi wa mwaka 2015- Bara na Visiwani.

Katika ripoti yao wanadiriki kukosoa Katiba za nchi zetu huru. Wanataka kupandikiza mawazo yao kati ya wananchi wetu. Kwani walikuja kuangalia namna uchaguzi ulivyokuwa ukiendeshwa au walikuja kufundisha uchaguzi uendeshweje?

Tume za uchaguzi NEC, Bara na ZEC, Unguja walitoa miongozo husika kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.  Lakini ukisoma ripoti yao waliyotoa Mei, 2016 Kiongozi wa EU Bibi Judith Sargentini, amejikita katika kutoa yale wanayofikiria Wazungu kwa mtazamo wao yangepaswa yatekelezwe ndipo wakubali uchaguzi ulikuwa huru.

Huko Ulaya kuna kasoro chungu nzima. Nchi zao katika EU yenyewe bado kuna mitazamo tofauti na ya kibinafsi na ndiyo sababu Uingereza imefanya kura ya maoni ya kujitoa katika EU!

By Jamhuri