AZAM, KMC, Simba na Yanga zote zimeanza safari ya ‘kuifuta machozi’ Tanzania Bara katika michuano ya klabu barani Afrika. Matokeo ya mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki kila mtu anajua.

Lakini wakati tunataka timu hizo zipate mafanikio makubwa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, kuna mahali tunajisahau.

Tunataka mafanikio, lakini tunasahau kusaka watoto wenye vipaji huko mitaani na kuwatunza. Hata yule anayewatunza kwa gharama zake, wakati mwingine tunamuona si kitu.

Anatumia kile anachokitenga kwa ajili yake na familia, kwa ajili ya kuwatafuta watoto wenye uwezo, kuwafundisha misingi ya awali ya mchezo, na mwisho wa siku nchi inakuja kuwafahamu wachezaji waliopitia mikononi mwake.

Viwanja anavyotumia katika kuwafundishia mchezo watoto ni duni sana, afya za watoto na zenyewe ni mbaya, shida ni nyingi, lakini mtu anajitolea kwa hali na mali ilimradi tu vijana waje kuwa wachezaji wakubwa miaka kadhaa mbeleni.

Uchumi wa Afrika hauko vizuri, miundombinu ya michezo haina sura ya kuvutia. Urasimu ni tatizo lisilokwisha, mizengwe inayoanzishwa kwa makusudi na wale wenye mamlaka juu ya michezo, inawatajirisha wao na marafiki zao pekee.

Wale wenye kutumia ubunifu wao katika kuwakusanya watoto kila mwaka ili waviendeleze vipaji, wana adui wa kudumu ambaye ni viongozi wenye kuingia moja kwa moja kwenye mikutano mikuu ya mashirikisho ya soka.

Kwa upande wa Tanzania yetu, TFF imejaa aina ya watu ambao ni kikwazo kwa wale wenye kugharimia ukuzaji wa vipaji. Hakujawahi kuonekana ubunifu wa kiwango cha juu kutoka kwa viongozi wengi wa TFF ngazi za mikoa, ambao utakuwa ni kiunganishi kati ya wanaokuza vipaji na wanaofaidika na vipaji hivyo.

Mfano, miaka michache nyuma, Serengeti Boys inakwenda India kucheza mechi za kirafiki na Marekani na India, halafu inaifunga India magoli 3-1 na kutoka sare ya goli 1-1 na Marekani, hayo ni matunda ya kazi ya wale wanaojitolea bila ya kazi yao kuungwa mkono na viongozi wa soka.

Marekani wamekwisha kuwekeza kwenye soka kwa miaka mingi, kwao kushiriki Kombe la Dunia mpaka hatua ya robo fainali si jambo la ajabu. Lakini Marekani wanazo ‘academy’ nyingi zenye ukaribu na uongozi wa soka ngazi mbalimbali.

Kila mwenye taaluma yake kuhusiana na soka anaheshimiwa kwa kupewa uwanja mpana wa kutekeleza majukumu yake. Wamarekani wanaandaa vijana, ambao wanakuja kufika mbali, na wakati huo huo wadogo zao wanaandaliwa kwenye ‘academy’ nyingi.

Kwa Wamarekani kilichopigwa vita kiufasaha ni ile tabia ya wavizia fursa kuwa karibu na watu wanaotumia kila uwezo walionao katika kukuza vipaji vya watoto. Sisi Tanzania tunayo aina ya watu wenye sura mbili kwenye soka.

Anaongea na mwandishi wa habari akiwa na sura ya kiongozi wa soka mwenye mikakati mingi endelevu, halafu kesho anakaa sehemu na kiongozi wa timu nyingine ili wapange matokeo ya mechi.

Mtu wa aina hii hawezi kushindwa kumhujumu mpenda soka wa kweli anayegawa pato lake katika sehemu mbili, sehemu moja kwa ajili ya familia yake na sehemu nyingine kwa ajili ya watoto wenye vipaji anaowafundisha misingi ya soka.

Tumekuwa na watu wengi sana ambao hawasikiki wala hawawezi kupewa sifa, ingawa walipaswa kuwa wa kwanza kabisa katika kusikilizwa kwenye suala la usimamiaji wa soka la watoto.

Badala ya juhudi zao kupewa heshima ili wao waone kwamba wanachokifanya ni kizuri, wanakwazwa mara kwa mara, wanapuuzwa na wajuaji walio ndani ya uongozi wa soka ngazi za mikoa.

Hawa wanaokubali kusimangwa na marafiki zao pamoja na ndugu kwa sababu ya kukubali kutumia muda na fedha zao ili mradi watoto waje kuwa wanasoka wakubwa miaka ijayo, hawajapewa bado heshima wanayoistahili.

Makocha wanaowapa ufundi kadiri wanavyozidi kukua, wamepokea wachezaji ambao wamepewa elimu ya awali na hawa wapenda michezo waliozungukwa na urasimu kutoka kwa wachumia tumbo.

Wizara ya Michezo itafute muundo wa ufanyaji kazi utakaoiweka karibu na hawa wapenda soka waliopo mikoani. Waziri Dk. Harrison Mwakyembe na wasaidizi wake wanayo kila sababu ya kuwafuata wadau hawa huko huko walipo na kuwasikiliza kwa umakini.

Tabaka la wapigaji, wapenda fedha wasiozitolea jasho linaweza kutaka kusimama katikati ya wizara yenye dhamana ya michezo na hawa wadau wanaokuza vipaji. Lengo linakuwa ni moja tu, kuhakikisha masilahi yao yanaendelea kulindwa.

Wizara ya Michezo isikubali kudanganyika kwa kuwaamini viongozi wa TFF ngazi ya taifa na mikoa, kumekwisha kujitokeza ushahidi mwingi wa udhaifu mkubwa ndani ya shirikisho hilo.

Udhaifu huo ndio kila sababu ya wizara kuja na ubunifu wa kuwa na mawasiliano ya moja kwa moja na wapishi halisi wa wachezaji wa Serengeti Boys. Waswahili wanasema usione vyaelea vimeundwa, waundaji wenyewe wa watoto wenye vipaji vya soka ndio hawa ambao hawapendwi na wachumia tumbo waliomo kwenye shirikisho la soka.

Hatutafika katika mafanikio makubwa kama hatutaanza chini na kuwathamini wale wanaowalea watoto kwa kukuza vipaji vyao, pamoja na ugumu wa nyenzo na kutokuwa na ujuzi wa kutosha.

383 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!