Siku za karibuni nchi za Afrika zimetamkiwa na wakubwa matajiri wa nchi za Magharibi kupokea tabia ngeni ya ushoga na ndoa za jinsi moja. Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, amediriki hata kutishia kunyima misaada kutoka Uingereza kwa nchi zile zitakazokataa siasa yake hiyo ya kutambua ndoa za jinsi moja.

Juzi juzi hapa kukasikika tena tamko la Barrack Obama, Rais wa Marekani akitamka kulikubali wazo la ndoa za jinsia moja katika nchi yake. Wakubwa hawa wanataka kuingiza tabia ngeni kabisa ulimwenguni ya kuwa na ndoa za jinsi moja kwa kisingizio cha ustaarabu wa kisasa au wanaheshimu na kutekeleza haki za binadamu kama zilivyotangazwa na Umoja wa Mataifa (UN).

 

Sielewi fikra na azma ya wakubwa hawa wanapotaka mwanadamu wa leo karne ya 21 avunje amri ya Mungu, na atende kinyume kabisa na utaratibu wa Mwenyezi Mungu aliyeumba vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana kwa mpangilio maalumu kadri ya matakwa yake.

 

Hawa Wazungu walipokuja Afrika walijidai kuleta mambo mawili – ustaarabu wa kwao, na ni kutuletea neo la Mungu, ndiyo dini ya Kikristo. Kutekeleza malengo mawili haya walitumia njia mbalimbali. Katika utekelezaji wa malengo hayo walituletea pamoja na mila na desturi za kwao kama vile elimu ya darasani njia za uchumi wa kisasa na hata namna ya kuishi maisha ya kwao Ulaya.

 

Historia inatuelimisha kuwa hapo zamani Wazungu wote wakiishi maisha duni misituni na mapangoni wakiwinda wanyama. Wakati huo au enzi hizo walijulikana kwa majina kama ‘Barbarians’ au ‘Savages’ kumaanisha walikuwa washenzi na wasiostaarabika! Polepole waliboresha maisha yao, wakaanza kujenga viwanda na miji na ustaarabu wa kisasa ukajengeka.

 

Walipofikia hali hiyo wakaanza kwenda nje ya Ulaya kama Marekani na Afrika na Asia kwa nia tofauti. Baadhi wakitafuta maisha bora zaidi, baadhi wakitafuta biashara na baadhi wakieneza neno la Mungu. Bara letu Afrika liliitwa bara jeusi lililogubikwa na giza, basi lilihitaji mwanga wa ustaarabu wa Kizungu.

 

Wale walioleta biashara na kutaka kujipanua waliunda ukoloni na kujidai wanakuja kutustaarabisha (to civilize Africans) na baadhi walikuja kuleta neno la Mungu hawa walikuja kuleta uongofu (to evangelize Africans). Lakini wazungu wote walikuwa na imani ya ukristo!

 

Huku kwetu makundi yote hayo yalituita waafrika washenzi wasiostaarabika, lakini kwa vile hatukuishi kama walivyoishi mababu zao mapangoni na misituni sisi hawakutuita “Barbarians” au “Savages”, bali walituita “natives” maana yake wenyeji wenye aina ya ustaarabu wao, lakini tunahitaji kupakiziwa ustaarabu mpya wa kigeni kutoka Ulaya ndipo tuishi nao.

 

Watanzania tunajua kila kabila liliona kabila jingine ni geni kwake, hivyo kila kabila walikuwa na namna ya kuwaita wageni wasiokuwa wa kabila lao. Mathalani Kagera, usipokuwa Mhaya unaitwa “NYAMAHANGA”, Kilimanjaro usipokuwa Mchaga unaitwa “CHASAKA”, Dodoma usipokuwa Mgogo, basi unaitwa “MKONONGO”.

 

Songea usipokuwa Mngoni wewe ni “MHENJA” na Iringa kama siyo Mhehe utaitwa “MGENZI”, lakini majina yote hayo yanaonyesha ustaarabu wa Mwafrika wa kutokumdhalilisha mgeni kama walivyokuwa wakifanya wazungu Ulaya. Kuitana Barbarian au Savage ni jina la kudharau mtu asiye wa kabila lako.

 

Kwa kuwa wazungu wote walikuwa wa imani moja ya ukristo, basi walituletea na desturi na utamaduni wa kuoana kikristo. Ndoa ya kikristo ni ya muungano wa mume mmoja na mke mmoja kujenga familia ya Mungu yenye watoto na kuwa kaya au jumuiya katika kabila.

 

Kumbe msingi wa ndoa za wazungu umo katika Biblia waliyotuletea kama agizo la Mwenyezi Mungu. Katika sura ya kwanza kabisa kitabu cha Mwanzo tunakuta maneno haya; Mungu akasema, “Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na wanyama na nchi yote pia na kila chenye kutambaa, kitambaacho juu ya nchi”(Mwa. 1:26).

Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimuumba mwanamume na mwanamke aliumba, Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia “zaeni, mkaongezeke mkaijaze nchi na kuitiisha…” (Mw. 1:27 – 28).

Hivi ndiyo Mwenyezi Mungu aliumba watu wa jinsi tofauti mtu mwanamume na mtu mwanamke wenye viungo tofauti ili kutekeleza lile agizo lake la kuzaa na kuijaza nchi. Kwa imani yetu ya dini tunaamini kuwa mtu mume na mtu mke wakioana watatekeleza agizo lile la Mungu kuzaa na kuongeza wanadamu katika dunia hii.

 

Basi, utamaduni wa kikristo ni kuoana mtu mume na mtu mke ndiyo sababu viongozi wa dini walifundisha tusiwe na mitara ndiyo ukristo unavyotaka kimaadili. Mitara ni utamaduni wa kiasili wa kuwa na wake zaidi ya mmoja kumbe agizo la Mungu ni mume na mke, wala si wake!

 

Tulipokuwa tunaelimishwa shuleni elimu dunia, lipo somo la elimu ya viumbe- biolojia.  Huko tulisema viumbe vyenye uhai vinaongezeka kwa kuzaana. Wanyama, wadudu, mimea panakuwapo na jinsi ya kiume na ya kike, zote mbili.

 

Katika mimea sehemu zinazoitwa “stamens” katika maua zinakuwa za jinsi ya kiume- kwa kitaalamu sehemu hii inaitwa “androecium” (neno la Kigiriki – “aner” kiume na “oikos” nyumba). Sehemu hii inatengeneza chembe chembe au unga unaoitwa poleni.

 

Aidha, katika ua kuna sehemu nyingine inaitwa “carpels” ambayo ni mfuko wa uzazi. Sehemu hii ni ya kike, inaitwa kwa kitaalamu “gynoecium” (neno la Kigiriki liitwalo “gyne” maana yake kike)- hapo ndipo yanapotengenezwa mayai.

 

Ili mmea upate kuzaa matunda yenye uhai ndani yake kunahitajika ile “pole” kutoka sehemu ya kiume ije kuungana na yai kutoka sehemu ya kike “gynoecium” na kupatikana uhai katika matunda.  Hapa tunaona maajabu ya Mwenyezi Mungu ambaye kwa utaratibu wake wa busara hata mimea ina jinsi mbili ili kuzaana na kueneza aina ya kiumbe hicho (propagation of species).

 

Maajabu mengine ya Muumba wetu ni pale alipoumba madini ambayo hayana uhai, lakini kadiri ya mpangilio wa Mungu, kaweka upande mmoja nguvu za chanya na upande mwingine nguvu za hasi.  Kwa lugha nyepesi ni nguvu dume na nguvu jike.  Hii wale wote waliosoma “elementary physics” wanaikuta katika somo la “magnetism”.

 

Hapa kuna aina ya chuma (Fe3O4) chenye ncha mbili tofauti- ncha ya chanya (nyekundu) na ncha ya hasi (nyeusi), basi ukikaribisha ncha chana za vyuma viwili vyuma vile vitakimbiana (will repel), lakini ulogwe kukaribisha ncha chanya na ncha hasi mara moja vyuma vitavutana na kuungana (will attract each other).

 

Maajabu haya katika sayansi ya “magnetism” yanathibitisha kuwa Mungu ameumba jinsi mbili ili zivutane na kamwe ncha za nguvu ya aina moja hazitavutana. Basi, kwa mtazamo wangu binafsi nalenga kuonyesha namna dunia kadiri ya maumbile yake Mwenyezi Mungu jinsi moja haiwezi kuelekeana pamoja isipokuwa jinsi zile mbili tofauti alizoumba Mwenyezi Mungu -jinsi ya kiume na jinsi ya kike vina mvutano wa kukaa pamoja.

 

Sasa ndoa ya jinsi moja kuna mvutano gani hapo? Au ni tamaa za kimwili tu? Ni tamaa chafu hiyo isikubaliwe, na isipokewe katika utamaduni wetu wa Kiafrika. Agizo la Mwenyezi Mungu ni kuongezeka na kuijaza nchi. Ili hilo lifanyike, lazima pawepo na jinsi ya kiume na ya kike ndipo kizazi kinaweza kutokea.

 

Nimeeleza kijuujuu sana kujaribu kuonyesha uozo wa ustaarabu wa wazungu kutaka kabisa kumsahihisha Mungu! Wamejaribu kutengeneza kiumbe kwa kupitia chupa (clowning) na wamejaribu kuongeza uhai ili wasife, lakini hayo yote siyo mpango wa Mwenyezi Mungu, hivyo wazungu wameshindwa.

 

Sasa ndiyo wanajaribu kwenda kinyume kabisa cha maumbile kuhalalisha ndoa za jinsi moja. Huku ni kujaribu kumsahihisha Muumbaji wa vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Kanuni asilia za uumbaji (natural phenomenon) hazibadilishwi na viumbe vyovyote vya Mungu isipokuwa Mungu mwenyewe tu.

 

Mwandishi wa Makala hii, Francis Mbenna ni Brigedia Jenerali mstaafu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye makazi yake jijini Dar es Salaam . Anapatikana kwa simu: 0755 806 758; email: fxmbenna@yahoo.com

 

1079 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!