Hivi sasa Taifa letu liko kwenye mjadala mkubwa wa kijamii na kisiasa katika mchakato muhimu wa kuandika upya Katiba yetu. Mchakato huu umeanza kutokana na kuwapo malalamiko kutoka kwa watu kadhaa kuwa Katiba yetu, ambayo imelilea Taifa letu tangu mwaka 1962, imezeeka, imejaa viraka na hivyo iandikwe upya.

Kutokana na kauli ya Rais Jakaya Kikwete, Desemba 2011 kwamba ataanzisha mchakato wa kuandika upya Katiba yetu, Bunge lilitunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura 83 mwaka 2012 na mchakato ukaanza baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kukusanya maoni na kuwasilisha rasimu ya pili ya Katiba bungeni mapema Machi, 2014.

Bunge Maalum la Katiba sasa linaendelea na vikao vyake Dodoma. Mjadala mkali umezuka na unaendelea kuhusu muundo wa Serikali, baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kupendekeza kwenye rasimu ya Katiba kuunda Shirikisho la Serikali Tatu, kinyume cha Katiba ya sasa (Katiba ya mwaka 1977) yenye Serikali Mbili.

Je, Katiba yetu imezeeka na hairekebishiki?

Japo swali hili halina umuhimu tena kwa sasa kwani mchakato wa kuandika Katiba mpya unaendelea, mazingira na mijadala inavyoendelea inatulazimu wadadisi kulirejea swali hili.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliandikwa mwaka 1977, miaka 37 iliyopita. Tangu wakati huo, imefanyiwa marekebisho kwa nyakati na sababu tofauti mara 14.

Katiba hii iliandikwa baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 ambako ilikubaliwa kwamba Katiba ya Jamhuri ya Tanganyika ya mwaka 1962 ifanyiwe marekebisho ili kuipa sura ya Muungano na kuifanya kuwa Katiba ya mpito. Marekebisho hayo yalifanyika mwaka 1965 na hivyo kuifanya Katiba ya mpito hadi mwaka 1977 ilipoandikwa Katiba ya Kudumu inayotumika hadi sasa.

Tanzania, ambayo ni Taifa la Muungano wa nchi mbili — Tanganyika na Zanzibar — ni Taifa changa kwani lina umri wa miaka 50 tu. Ziko nchi zenye umri zaidi ya Taifa letu ambazo zimeendelea kutumia na kurekebisha Katiba zake.

Taifa la Marekani, kwa mfano, linatumia Katiba yenye umri wa miaka zaidi ya 200 na ambayo imefanyiwa marekebisho zaidi ya mara 100.

India, kwa upande wake, iliandika Katiba yake ya Uhuru mwaka 1945, miaka 70 iliyopita. Mwaka 2012 iliifanyia marekebisho Katiba yake, marekebisho ya 94 katika Katiba yake hiyo ya mwaka 1945.

Hivyo, madai kwamba Katiba yetu ya sasa imezeeka na kujaa viraka (kwa kufanyiwa marekebisho mara 14) na hivyo iandikwe upya, ni madai yanayoacha mjadala.

Nini msingi wa malalamiko kuhusu Katiba ya 1977

Kwa mujibu wa taarifa na nyaraka mbalimbali zilizoambatishwa na Rasimu ya Pili ya Katiba ‘mpya’ iliyowasilishwa bungeni na Jaji Joseph Warioba, Machi mwaka huu, madai ya kuandikwa upya kwa Katiba yetu ni kwamba;

Muungano wetu umegubikwa na malalamiko mengi kutoka kila upande, hasa Zanzibar kulalamika kwamba Tanzania Bara inanufaika zaidi kiuchumi kwa kuwa Serikali ya Tanzania Bara ndiyo hiyo hiyo ya Muungano wa Tanzania, na hivyo, Bara ‘imevaa koti la Muungano’.

Madai hayo ya Zanzibar yameufanya upande huo wa Muungano kuwa na majaribio na maombi ya mara kwa mara ya kudai ‘uhuru zaidi’, hasa kwa lengo la upande huo kunufaika zaidi kiuchumi na kijamii na uhusiano ‘wa nje’.

Kwa upande wa Bara, malalamiko machache yaliyopo ni kwamba “upande wa Zanzibar unanufaika zaidi na fursa na faida za Muungano”, wakati huo huo, kutokana na mazingira yake (ya udogo ki-eneo na kwa idadi ya watu), Zanzibar inachangia kidogo au kutochangia kabisa “gharama za Muungano”.

Mabadiliko ya kisiasa na kijamii ambako Katiba ya sasa, licha ya kufanyiwa mabadiliko, kwa mfano, mwaka 1992 kuruhusu Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa, bado Katiba imekuwa kikwazo kwa vyama hivyo kufanya vizuri katika uchaguzi kwa madai kwamba Tume ya Uchaguzi, na vyombo vingine vya demokrasia vimebanwa kikatiba kuegemea upande wa chama tawala, hasa kwa kuwa viongozi wake wanateuliwa na Rais ambaye ndiye kiongozi wa chama tawala.

Kuwapo kwa umaskini mkubwa miongoni mwa Watanzania; umaskini ambao hauendani na utajiri wa Taifa wa maliasili; hali inayoashiria kuwa Katiba ya sasa haijaweka mifumo mizuri ya kusaidia wananchi wanufaike na kuendelezwa na maliasili na utajiri wa asili wa Taifa letu.

Hali hii imeelezewa kusababishwa na mifumo dhaifu ya uwajibikaji wa viongozi; kukosekana kwa dira ya Taifa baada ya Azimio la Arusha kufutwa mwaka 1991 na misingi dhaifu ya haki za binadamu.

Ukweli na uhalali wa sababu au madai ya Katiba Mpya na jinsi madai hayo yalivyozingatiwa Katika Rasimu ya Pili ya Katiba inayojadiliwa bungeni

Kama ilivyoelezwa, msingi mmojawapo wa madai ya kuandikwa upya kwa Katiba yetu ni malalamiko kuhusu ‘manufaa, hasa ya kiuchumi na kijamii’ ya Muungano. Nitalizungumzia zaidi eneo hili kwa sasa.

Maeneo mengine ya ‘uhuru wa Tume ya Uchaguzi na vyombo vingine vya kukuza demokrasia’ pamoja na eneo la ‘udhibiti na usimamizi wa rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi’, nitayazungumzia katika makala zitakazofuata.

Muungano wa Tanzania, na hasa muundo wake, limekuwa ni eneo la mjadala mpana na mkali sana wakati huu wa mjadala wa Rasimu ya Pili kwenye Bunge Maalumu na nje ya Bunge.

Kwa kutambua umuhimu wa Muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano, lilipopitisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, sura 83, katika kifungu 9(2), liliweka maeneo ambayo yanapaswa kulindwa na kuzingatiwa katika mchakato na hatimaye kuandikwa kwa Katiba Mpya. Moja ya maeneo hayo, ni uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika kufanya kazi yake, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilizingatia eneo hilo kwa mtazamo kwamba “linapaswa kulindwa na kuimarishwa”, na hivyo Tume ikajipa uhuru wa “kupendekeza marekebisho” ambayo inaamini yataboresha Jamhuri yetu ya Muungano wa Tanzania.

Kwa utafiti wa aina za Muungano, Tume inasema, Muungano wa nchi zaidi ya moja huleta, ama serikali moja (yaani Muungano uitwao Unitary Union), au serikali mbili au zaidi (katika mfumo wa shirikisho, yaani Federation), au serikali tatu zinazoshirikiana kimkataba (yaani Confederation).

Katika aina zote hizo za muungano, bado uwezekano wa muungano kuvunjika upo (bila kujali idadi ya serikali zinazoundwa baada ya muungano). Kwa maoni ya Tume, uimara wa muungano hautokani na idadi ya serikali zinazoundwa, bali “dhamira ya kisiasa” kusimamia na kumaliza “malalamiko kuhusu muungano yanayotoka kwenye nchi washirika”.

Kwa tafsiri hiyo ya kifungu hicho cha sheria, Tume, kwa kuamini kwamba inaboresha na kwa kuzingati utafiti kadhaa ambao Tume ilifanya na kwa kusikiliza maoni ya wananchi kadhaa kuhusu jambo hilo (la Muungano), na kwa kutambua hatua ambazo zimekuwa zikichukuliwa na upande mmoja wa Muungano, hususani Zanzibar kujitafutia “uhuru zaidi” (hasa kupitia marekebisho ya 10 ya Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 yaliyofanywa mwaka 2010) , ilipendekeza “kuivua Tanzania Bara koti la Muungano”, na hivyo kupendekeza kuwapo kwa serikali ya “kati au ya ushirika au ya washirika wote wawili’, serikali ya tatu, ya shirikisho, sambamba na ile ya Tanganyika inayoanzishwa kutoka Tanzania Bara iliyokuwa ndani ya Muungano.

Utafiti wa Tume kwa nchi mbalimbali zilizoungana, unaonesha kwamba, ipo miungano iliyodumu ya serikali moja, na mingine ya serikali mbili au zaidi (yaani ya Shirikisho), na pia ipo mifano ya nchi zilizokuwa za muungano zilizokuwa za serikali moja na nyingine zaidi ya serikali mbili ambazo miungano yao imevunjika. Hii inathibitisha ukweli kwamba, idadi ya serikali pekee, hailindi muungano.

Nchi za Somalia (Somalia na Somaliland); Ethiopia (Ethiopia na Eritrea), Sudan (Sudan Kusini na Kaskazini) zote zilikuwa na Muungano wa serikali moja (Unitary Union), lakini miungano hiyo imevunjika.

Pia zipo nchi za Shirikisho, kama Urusi (USSR), Chekoslovakia na Yugoslavia zilizokuwa za Shirikisho nazo zimesambaratika! Aidha, zipo nchi zenye mashirikisho (serikali zaidi ya moja) ambazo zinaendelea kudumu kama vile Canada, India, Brazil, Marekani na hata Ujerumani.

Kwa hiyo, kwa maoni ya Tume, dawa ya kulinda Muungano wetu ni kubadilisha muundo wake huo kutoka muundo wa serikali mbili wenye malalamiko lukuki yasiyokoma, na kuunda shirikisho la serikali tatu ambazo mipaka yake ya kiutendaji inaeleweka vizuri.

Kwa Mtazamo wa Tume na baadhi ya watu, kuitenganisha Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Muungano, kutapunguza malalamiko, hasa kutoka upande wa Zanzibar kwamba Tanganyika imevaa koti la Muungano na hivyo kunufaika zaidi kiuchumi na Muungano.

Malalamiko ya Zanzibar, ambayo yamekuwa kichocheo kwa mshirika huyo katika Muungano kuchukua hatua za “kujitafutia uhuru zaidi” na hivyo kunufaika zaidi kiuchumi, yasiporekebishwa yanaweza kusababisha Muungano kuvunjika; jambo ambalo Tume imeagizwa kisheria kwamba iweke mazingira ya kuzuia lisitokee.

Itaendelea…

Mwandishi wa makala haya, Ezekiel Maige, ni Mbunge wa Msalala mkoani Shinyanga. Amewahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anapatikana kupitia simu: 0754 779 907.

1234 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!