jakaya kikwete
jakaya kikwete
Wakati Bara la Afrika likiwaaga marais wastaafu watatu mwaka jana katika vipindi tofauti, kulikuwa na matarajio kwamba pengine mmoja miongoni mwa marais hao wastaafu angeweza kuondoka na tuzo ya Mo Ibrahim, hali imekuwa kinyume chake.

Marais hao watatu waliostaafu kwa vipindi tofauti mwaka jana ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ambaye alistaafu rasmi Novemba 5, pale kwenye Uwanja wa Taifa, alipoapishwa mrithi wake, Dk John Pombe Magufuli.

Wastaafu wengine ni aliyekuwa Rais wa Msumbiji, Armando Guebuza, aliyerithiwa na Jancinto Nyusi, pamoja na Rais Goodluck Jonathan wa Nigeria ambaye alishindwa katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo na Rais Muhamadu Buhari.

Aliyesimamia kamati ya kupitia na kuchambua Rais mwenye vigezo anayestahili kupewa tuzo hiyo katika mwaka huu, ni Dk Salim Ahmed Salim, waziri mkuu wa zamani wa Tanzania na mwanadiplomasia mbobezi, inahusisha wajumbe wengine ambao ni mabalozi wastaafu, washindi wa tuzo za Nobel, viongozi wa wafanyabiashara pamoja na wanaharakati wa demokrasia.

Mo Ibrahim Foundation ni taasisi ya Kiafrika, iliyoanzishwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Sudan na raia wa Uingereza, Mo Ibrahim. Lengo la kuanzishwa kwa tuzo hiyo kwa viongozi wastaafu katika Bara la Afrika lilikuwa ni kuwatambua wale walioleta maendeleo pamoja na utawala bora pamoja na kuboresha ustawi wa wananchi wao.

Mshindi wa tuzo hiyo hupata kiasi cha Shilingi bilioni 10.

Taasisi hiyo imetangaza Alhamisi iliyopita kwamba hapakuwa na mshindi wa tuzo hiyo kwa mwaka jana. Inaongeza kuwa hakuna Rais ama kiongozi mstaafu wa Bara la Afrika aliyefikia vigezo vilivyokuwa vimewekwa katika tuzo hiyo kwa mwaka 2015, katika mafanikio ya kiutawala.

Kwa kifupi, kutopatikana kwa Rais mstaafu ambaye amekidhi vigezo vilivyowekwa na jopo lililokuwa chini ya Dk Salim Ahmed Salim, kunathibitisha kwamba kumekuwa na dosari katika uongozi kwa nchi nyingi za Kiafrika.

Matarajio ya wachambuzi wa mambo yalikuwa pengine tuzo hiyo ingemwendea Rais mstaafu Jakaya Kikwete, lakini mambo yamekwenda tofauti.

Tuzo hiyo iliyoanzishwa tangu mwaka 2006, imewahi kuwaendea marais wastaafu wanne tu ambao ni Rais mstaafu wa Msumbiji, Joaquim Chissano, ambaye ndiye aliyeshinda tuzo ya kwanza mwaka 2007, na baadaye tuzo hiyo kwenda kwa aliyekuwa Rais wa Botswana, Festus Mogae, mwaka 2011. Tuzo hiyo ilikwenda kwa Rais mstaafu wa Cape Verde, Pedro Pires, wakati tuzo hiyo kwa mwaka 2014 ilikwenda kwa aliyekuwa Rais wa Namibia, Hifikepunye Pohamba.

Kamati maalumu iliyoko chini ya Dk Salim Ahmed Salim imekuwa ikiongozwa na vigezo vitano ili kumpata mshindi wa tuzo hiyo. Vigezo hivyo ni pamoja na kuwa rais mstaafu, awe amestaafu katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, awe alichaguliwa kidemokrasia, aliyetumikia kipindi cha uongozi wake kama ilivyoainishwa katika katiba ya nchi husika, awe aliyeonesha uongozi wa kipekee katika utawala wake.

Wachambuzi wa mambo wanasema, pengine suala la uchaguzi wa Zanzibar pamoja na kiporo cha Katiba, vimekuwa vikwazo vikubwa kwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuweza kunyakua tuzo hiyo ambayo inaheshimika ndani ya Bara la Afrika na duniani.

Katika suala la uchaguzi wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015, matokeo ya uchaguzi yalifutwa. Uchaguzi huo ulijaa mizengwe, huku Chama cha Wananchi (CUF) kupitia kwa mgombea wake na pia Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad, kilijitangazia ushindi kabla ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Salim Jecha, kuufuta uchaguzi wote kwa kile alichosema ni kuwapo kwa kasoro nyingi, hivyo uchaguzi huo kurudiwa Machi, 2016. 

Akizungumza na JAMHURI, mtaalamu wa masuala ya utawala, Nurdin Ramadhan, anahoji demokrasia ya nchi za Afrika kupimwa katika mizania na vigezo vya mfanyabiashara Mo Ibrahim. Anasena kila nchi ina ukomo wa demokrasia yake inayoweza kuimudu.

Anasema tuzo hiyo ya Mo Ibrahim haivutii kwa vigezo wala zawadi inayotolewa, hivyo si kivutio cha kutosha cha viongozi wa Afrika walioko madarakani. Pengine lingekuwa jambo jema kama fedha hizo angezielekeza kwingine ambako kunaweza kuwa na matokeo chanya kuliko kukwepa kuitoa kila mwaka.

“Unajua marupurupu ya Rais wa Kenya au Sudan? Ana haja gani ya kuitafuta tuzo ya Mo Ibrahim? Hapa kikubwa kwa marais wastaafu ni kupimwa kama waliweza kufikia matarajio ya waliowachagua kwenye masanduku ya kupigia kura,” anasema Ramadhan.

Akielezea kuhusu Rais Jakaya Kikwete kuikosa tuzo hiyo kwa kuhusianisha na kutopatikana kwa Katiba mpya, anasema jambo hilo halikuwa agenda mahasusi katika kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuongoza nchi kwa kipindi cha pili. Vyama vyote havikubeba Katiba kama agenda kubwa katika uchaguzi uliopita. 

Anasema dhamana ya kulea na kuongoza nchi na kuikabidhi ikiwa salama kwa Rais mwingine ni jukumu kubwa zaidi kuliko kuhangaika na tuzo, tuzo ya Mo Ibrahim ingekuwa na maana kama angekuwa anamsaidia Rais aliyeko madarakani mwenye mwelekeo kutekeleza miradi ya maendeleo hata kujenga hospitali moja kuliko kumpa fedha rais aliyestaafu.

“Kuilea nchi kwa saa 24, siku7 kwa wiki, wiki 52 kwa mwaka kwa miaka mitano si jambo rahisi hata kidogo. Saa 24 katika nchi ni nyingi sana kama ilivyo dakika moja kwenye mpira wa soka. Uelekeo wa nchi unaweza kubadilika kabisa na hata kuparaganyika ndani ya saa 24 tu,” anasema

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Kitila Mkumbo, anasema bado kuna safari ndefu kwa watawala wa Afrika kufikia vigezo vilivyowekwa ili kupata tuzo hiyo, kutokana na kile anachokiita viongozi wengi kuongozwa na busara zaidi kuliko kuzingatia sheria. 

“Niseme tu kuwa kwa mazingira ya utawala Afrika, ambapo utawala bado unatumia busara zaidi kuliko kuzingatia sheria na misingi ya demokrasia na utawala bora, ni vigumu kupata kiongozi anayeweza kukidhi hivyo.

By Jamhuri