* Kompyuta za England kwa Italia ovyo

Kung’olewa kwa England katika robo fainali za michuano ya Kombe la Euro 2012 na kukamilisha idadi ya timu nne ambazo zitacheza nusu fainali, kumeziacha Hispania na Ujerumani zikipewa nafasi kubwa zaidi kwa mojawapo kuwa bingwa.

Mashabiki wa kandanda wanaoshuhudia michuano ya Euro 2012 wanatazamiwa kuangalia namna gani washambuliaji wakali wa Hispania akina Xavi Alonso, Fernando Torres, Cesc Fabregas na Jesus Navas na wa Ujerumani kama Mario Gomez, Marco Rues, BenderLas Bender, Miroslav Klose au Lucas Podolski watakavyozisaidia timu zao kunyakua ubingwa huo.

Mbali na Hispania na Ujerumani, timu mbili nyingine zilizotinga hatua hiyo ni Ureno na Italia iliyoing’oa England juzi Jumapili kwa matuta, baada ya kwenda suluhu kwa dakika 120 kwenye Uwanja wa Olympic katika Jiji la Kiev, Ukraine.

Mapambano yajayo ya nusu fainali yanaanza kesho Jumatano wakati Ureno itakapoikabili Hispania, kisha yatamalizika kesho kutwa Alhamisi, kwa Italia kupepetana na Ujerumani huku mechi zote zikianza saa 3.45 usiku kwa saa za Afrika Mashariki.

England iliyokwenda katika fainali hizo huku ikitarajiwa kufika mbali, iling’olewa kwa penalti 4-2 na kuendeleza jinamizi lililoanza baada ya fainali za Kombe la Dunia za mwaka 1966 zilizofanyika nchini mwake.

Italia ilishinda mechi hiyo baada ya Mario Balotelli, Andrea Pirlo, Antonio Nocerino na Allesandro Diamanti kukwamisha penalti zao huku Ricardo Montolivo akipiga mpira nje kabisa ya lango.

Kuendelea kwa jinamizi linaloimaliza England katika michuano ya kimataifa, kulikuja baada ya mkwaju wa mshambuliaji Ashley Young kugonga mtambaa panya, kisha kiki ya beki Ashley Cole nayo kudakwa na kipa mkongwe wa Italia, Gianluigi Buffon.

Katika hatua za makundi, Ujerumani iliyomaliza ikiwa kinara wa Kundi B baada ya kushinda mechi zote dhidi ya Ureno, Denmark na Uholanzi kwa kutikisa nyavu mara tano huku zake zikiguswa mara mbili tu, itaingia uwanjani hapo keshokutwa kupimana ubavu na Italia katika nusu fainali ya pili.

 Timu nyingine zilizokuwa katika kundi hilo ni Ureno iliyoshika nafasi ya pili kwa kushinda mechi mbili na kufungwa moja, hivyo ikakusanya pointi sita ikiwa imefunga mabao matano huku yenyewe ikitandikwa manne.

Imeingia hatua hiyo kwa ushindi mkubwa wa mabao 4-2 dhidi ya Ugiriki, timu iliyomaliza hatua za awali kwa kushika nafasi ya pili katika Kundi A lililoongozwa na Jamhuri ya Czech.

Kutoka kundi hilo, Ugiriki ilipoteza mechi moja, ikatoka sare moja na kufungwa moja na hivyo kuvuka ikiwa na pointi nne, ikafunga mabao matatu na kufungwa pia matatu huku Urusi ikishika nafasi ya nne na wenyeji wenza Poland wakishika mkia kwa pointi zao mbili walizozipata kwa kutoka sare mara mbili na kupoteza mechi moja.

Katika Kundi C zilikotokea Hispania iliyokuwa kinara ikifuatiwa na Italia iliyoshika nafasi ya pili, lilikuwa likiundwa pia na timu za Croatia iliyoshika nafasi ya tatu huku Ireland ikiwa ni ya mwisho. Katika hali hiyo, Kundi D lililokuwa na England iliyoongoza ilifuatiwa na Ufaransa, Ukraine na Sweden iliyofunga tela.

Katika hali hiyo, timu zote nne zilizovuka zimetokea Kundi B na C pekee huku Kundi A na D yakiishia hatua hiyo ya pili baada ya England kufungashwa virago na Italia hapo juzi. Kati ya timu zote zinazocheza nusu fainali, Hispania ndiyo iliyo na rekodi nzuri kuliko zote kwa kufunga mabao manane, lakini yenyewe imefungwa mawili tu baada ya kuingia uwanjani mara nne.

Ikiwa imefunga mabao sita kwenye makundi, timu hiyo iliing’oa Ufaransa katika robo fainali kwa mabao 2-0 na kusababisha winga wake, Samir Nasri, awatukane matusi ya nguoni waandishi wa habari walipomuuliza mtazamo wake kuhusu michuano hiyo mikubwa kuliko yote Ulaya.

Kana kwamba hiyo haitoshi, ingawa Ujerumani ndiyo iliyofunga mabao mengi zaidi hadi sasa kwa kutikisa nyavu za adui zake mara tisa baada ya kuikung’uta Ugiriki mabao 4-2 katika robo fainali, kufungwa kwake mabao manne tangu iende katika michuano hiyo, kunaiweka juu zaidi Hispania kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Mbali na hizo, Italia iliyoing’oa England hapo juzi kwa penalti 4-2 ina mabao manane kama Hispania na kufungwa manne, lakini kwa sababu nusu yake yote imeyapata kwa matuta, kunaufanya mstari wake wa ushambuliaji usiwe tishio kwa mabeki wa Ujerumani hapo keshokutwa.

Ureno iliyotinga robo fainali kwa kuitandika Jamhuri ya Czec bao 1-0 nayo ina mabao sita hadi sasa, lakini imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara tano, rekodi ambayo ni hafifu zaidi kati ya timu zote nne zitakazochuana katika nusu fainali huku ikiikabili Hispania yenye kiwango kikubwa zaidi katika safu zote kuanzia ulinzi, kiungo na washambuliaji wake.

Kabla ya kuondoshwa kwa matuta juzi, kocha wa England, Roy Hodgson alitamba kwamba kikosi chake kimejipanga kisayansi ili kuidhalilisha Italia katika mechi ya robo fainali dhidi yake.

Mikakati hiyo ilikuja baada ya kuifanyia ushushushu mkali na kujua mbinu zake zote, hivyo akaamua kutumia mifumo ya kompyuta ili kutafuta ushindi, mikakati iliyofanikishwa na wataalamu wawili wa sayansi ya vyombo hivyo waliotajwa kwa majina ya Steve O’Brien na Andy Scoulding.

Lakini licha ya hayo yote, mbwembwe na tambo zao zote zimekwenda ovyo kwa kushindwa kufikia lengo, hali iliyomwacha Hodgson akishindwa kufufua matumaini yaliyopotea kwa England tangu mwaka 1966 ilipotwaa Kombe la Dunia kwenye Uwanja wa Wembley, London.

1186 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!