Ni Raila Odinga

Wananchi wa Kenya jana walipiga kumchagua rais wa nchi hiyo, huku kukiwa na matumaini makubwa kwa Waziri Mkuu Raila Odinga kushinda kiti hicho. Wakenya milioni 14.3 walijiandikisha kupiga kura mwaka jana, ingawa wengi hawakuhakiki taarifa za uandikishaji wao mwezi Januari.

Tayari Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imesema hatua hiyo ya kutohakiki taarifa zao haitaathiri uwezo wa kupiga kura. Kenya ilitarajiwa kufanya uchaguzi mkuu jana huku baadhi ya wananchi wakihofia kutokea tena kwa machafuko ya kisiasa.

Machafuko ya kisiasa yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa mwaka 2007, ambapo watu wasiopungua 1,000 walipoteza maisha na wengi kukoseshwa makazi ndani ya nchi yao.

Uchaguzi huo wa kwanza tangu kuundwa kwa Katiba Mpya ya nchi hiyo, unawapa nafasi wagombea wawili kuchukua nafasi hiyo ya juu nchini Kenya.


Wagombea wanane wameshiriki katika kinyang’anyiro hicho – Waziri Mkuu Raila Odinga, Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta, Naibu Waziri Mkuu Musalia Mudavadi, Martha Karua (mbunge).

Wengine ni Waziri Msaidizi wa Mipango, Maendeleo ya Taifa na Dira ya 2030, Peter Kenneth; aliyekuwa Katibu Mkuu wa Elimu, James ole Kiyiapi; aliyekuwa Mbunge, Paul Muite; na mfanyabiashara Mohammed Abduba Dida.


Anayetajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kukalia kiti hicho kinachoachwa wazi na Rais anayemaliza muda wake, Mzee Mwai Kibaki, ni Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Odinga, akifuatiwa na Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta

Tafiti

Wagombe wa urais waliochuana vikali Kenya – Raila Odinga wa Muungano wa Cord na Uhuru Kenyatta wa Jubilee – walikabana koo ikiwa ni siku tano kabla ya Uchaguzi Mkuu wa jana kufanyika.


Tafiti tatu tofauti zilizodhaminiwa na Nation Media Group (NMG), zimeonesha kuwa wagombea hao wanatofautiana kwa asilimia zisizozidi 1.5. Hata hivyo, Odinga alikuwa na nafasi zaidi katika uchaguzi wa marudio.


Matokeo yote hayo yamebainisha kuwa hakutakuwa na mshindi wa moja kwa moja, kwa kuwa wote hawatafikisha nusu ya kura zinazohitajika, huku utafiti ukibainisha kuwa katika mzunguko wa pili utakaofanyika ndani ya wiki tatu tangu kufanyika kwa uchaguzi wa awali, Odinga ana nafasi kubwa ya kushinda.

Matokeo ya Pollster Infotrack

Utafiti wa Kampuni ya Pollster Infotrack, ulionesha Odinga angeongoza kwa asilimia 46, Kenyatta angefuatia akiwa na asilimia 44.6, huku mgombea wa Amani, Musalia Mudavadi akiwafuata kwa mbali baada ya kupata asilimia 4.3.


Kwa mujibu wa matokeo hayo ya kura za mwisho za maoni, wote wawili – Odinga na Kenyatta – wameongeza kura kwa asilimia moja kila mmoja, ikilinganishwa na matokeo ya wiki iliyopita. Kwa mujibu wa sheria za Kenya, si ruhusa kufanya wala kuchapisha kura za maoni siku tano kabla ya uchaguzi.


Kulingana na matokeo ya Infotrack Poll, Odinga anatazamiwa kushinda matokeo ya mzunguko wa pili kwa asilimia 49.2 huku mwenzake akiwa na asilimia 47.2.


Utafiti huo unaonesha kuwa nusu ya wapiga kura wa Mudavadi watahamia kwa Odinga wakati Kenyatta atapata wale waliowapigia kura wagombea wengine – Martha Karua wa Narc, James ole Kiyiapi (Restore and Build Kenya) na Peter Kenneth (Kenya National Social Congress).


Kwa upande wa makundi ya wagombea, Cord inaongoza kwa kuungwa mkono ikiwa na asilimia 45.8 ikifuatiwa na Jubilee (45.6%) na Amani ya Mudavadi ikiwa na asilimia 4.4.

Utafiti wa Consumer Insight

Matokeo ya utafiti wa Consumer Insight yanaonesha kuwa Odinga hivi sasa anaungwa mkono na asilimia 46.8 ya wapigakura dhidi ya mwenzake Kenyatta, aliyepata asilimia 42.9. Mashabiki wa Mudavadi wamepungua kutoka asilimia 5.4 hadi 4.2.


Kampuni ya Consumer Insight imebaini kuwa iwapo uchaguzi utakwenda hadi marudio, Odinga atatangazwa mshindi kwa kufikisha asilimia 50.6 dhidi ya Kenyatta mwenye asilimia 46.3. Utafiti huo pia unaonesha kuwa umaarufu wa Cord uko asilimia 47.8 wakati ule wa Jubilee ni asilimia 44.1.

Utafiti wa Strategic Pollster

Utafiti wa Strategic Pollster unaonesha kuwa Odinga ataibuka mshindi kwa kupata asilimia 45.7 dhidi ya Kenyetta mwenye 43.8. Mudavadi bado ni wa tatu akiwa na asilimia 5.7.


Katika uchaguzi wa marudio, Strategic Pollster inasema Odinga ataibuka kidedea kwa asilimia 51.7 huku mwenzake Kenyetta akisimama kwenye asilimia 45.7. Tafiti hizi zimetumia sampuli ya watu 2,600 wanaowakilisha wananchi 14,337,399 waliojiandikisha kupiga kura.


Wagombea urais walichuana vikali kwa mara ya pili juzi katika mdahalo, ambao ulikuwa fursa ya mwisho kupimwa na wapiga kura kabla ya uchaguzi utakaofanyika Jumatatu ijayo.

Kura ya maoni nchini Kenya inaonesha kuwa Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, ana nafasi kubwa zaidi ya kumshinda Waziri Mkuu Raila Odinga kwenye uchaguzi mkuu ujao ikiwa ataungana na Naibu Waziri Mkuu mwingine, Musalia Mudavadi.

Wagombea katika mdahalo

Mdahalo wa urais wa pili na mwisho wa Kenya ulifanyika Februari 25, mwaka huu. Katika mdahalo huo masuala nyeti kama uadilifu, rushwa, uchumi na uchukuaji wa ardhi, yalijadiliwa.


Wagombea mahasimu katika uchaguzi wa urais wa Machi 4 mwaka huu walishiriki kwenye mdahalo huo, uliooneshwa moja kwa moja na televisheni. Umma wa watu wa Kenya ulikusanyika kuangalia mdahalo wa huo katika maeneo mbalimbalia nchini humo.  Mdahalo huo ulianza saa 1 usiku na ulidumu kwa saa nne.


Wagombea hao ni Waziri Mkuu Odinga; Naibu Waziri Mkuu Kenyatta; Naibu Waziri Mkuu Mudavadi; Martha Karua,(Mbunge);  Waziri Msaidizi wa Mipango, Maendeleo ya Taifa na Dira ya 2030; Peter Kenneth; aliyekuwa Katibu Mkuu wa Elimu James ole Kiyiapi; aliyekuwa Mbunge Paul Muite, na mfanyabiashara Mohammed Abduba Dida — ambaye mwanzoni alisema asingehudhuria akinukuu “mambo mbalimbali ambayo hayakusemwa na yaliyosemwa kwa kusudi” katika mdahalo wa kwanza, hususani kwa kulenga mashitaka yanayomkabili Kenyatta kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai.


Katika mdahalo huo, wagombea walijibu maswali kuhusu namna watakavyoshughulikia mizozo ya ardhi na kuinua uchumi wa Kenya. Hata hivyo hawakutoa ufafanuzi wa kina kuhusu mipango maalumu.


Mkurugenzi Mkuu wa Dira ya 2030 ya Kenya, Mugo Kibati, alisema muda mwingi ulitumika katika kukabiliana na masuala ya ardhi.


Amesema alitegemea wagombea kujadili sera ya kigeni na kuwaambia Wakenya zaidi kuhusu namna wanavyopanga kupata maliasili nyingine kama vile maji, gesi na utafutaji mafuta.


“Nilikatishwa tamaa, viongozi katika ilani za vyama vyao wana mipango yenye nia ya uchumi na maendeleo kwa ajili ya nchi, lakini hakuna aliyeulizwa kuhusu jinsi wanavyodhamiria kukuza uchumi maradufu na kutoa ajira ambazo wamekuwa wakiahidi,” amesema


Mratibu wa Taifa wa Kenya Land Alliance, Lumumba Odenda, kundi lenye ushawishi kuhusu masuala ya ardhi. Aliwakosoa wasimamizi wa mdahalo kwa kushindwa kuuliza maswali yanayofaa ambayo yangeweza kuwalazimisha wagombea kutoa taarifa zaidi ya jinsi ya kushughulikia kabisa masuala ya ardhi.

 

“Wananchi hawakupata nafasi kujua ni ekari ngapi za ardhi wagambea wanamiliki, wanadhamiria vipi kushughulikia maskwata na jinsi serikali yao itakavyosuluhisha migogoro ya ardhi pamoja na jinsi wanavyotaka wananchi watumie ardhi,” amesema.

Unyakuaji wa ardhi

Kenyatta aliulizwa atamke familia yake inamiliki ekari ngapi za ardhi na kama ni kweli “nusu ya ardhi” ya nchi ni mali yake.  Alikana tuhuma hizo za umilikaji wa ardhi, akisema ardhi inayomilikiwa na familia yake ilinunuliwa kupitia njia halali.

 

“Tutahakikisha kwamba ardhi inatumika kama kigezo cha uzalishaji na kwamba Tume ya Ardhi ya Taifa iachwe ili ishughulikie suala la ardhi lenye kuamsha hisia katika nchi hii,” amesema, akikataa kueleza wazi anamiliki ekari ngapi.


Akijibu swali aliloulizwa kuhusu umiliki wa kiwanda cha Molasi kilichopo Kisumu, ambacho awali kilikuwa kinamilikiwa na serikali, Odinga amesema familia yake ilipata kiwanda kupitia mnada wa umma.

Suala la Ardhi limekuwa likiamsha hisia nchini Kenya na mara nyingi kuwa chanzo cha migogoro. Ardhi imekuwa kichocheo vya vurugu za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008.

Uchumi na kiwango cha chini cha ajira

Swali la kwanza ambalo wagombea walikutana nalo, lilikuwa kuhusu uchumi na iwapo wagombea wanaunga mkono kuweka kiwango cha chini cha ujira kwa Wakenya wenye kipato cha chini.

Odinga amesema kulikuwa na uhitaji wa kuwa na uhusiano wa kikazi kati ya vyama vya wafanyakazi, waajiri na serikali, ili kuhakikisha gharama iliyopo ya maisha na matoteo kwa ajili ya siku zijazo kabla ya kupanga kiwango cha chini cha ujira.

 

“Tunahitaji kuwa na mazungumzo na vyama vya wafanyakazi, waajiri na serikali ili tujue gharama za maisha nchini leo zikoje na zitakuwaje.


“Hicho ndicho kitakachoamua kipi ni kiasi cha ujira wa kuishi,” alionya kwamba ujira haupaswi kupangwa kuwa juu sana kwa sababu utazuia ushindani wa Kenya.


Kenyatta amesema kwamba kama atachaguliwa atahakikisha kwamba ujira wa kiwango cha chini unawawezesha watu kufikia maisha yenye heshima.


Amesema kupunguza gharama za bei za chakula na kuwapa watu nyumba nzuri za bei nafuu, ilikuwa ni njia mojawapo ya kushughulikia kupanda kwa gharama za maisha nchini Kenya.


Muite alitoa wito wa kushughulikiwa tofauti ya kodi na kipato kisicholingana, kuwawezesha kupanga kiwango cha ujira endelevu nchini.


Karua alitetea harakati zenye nguvu za wafanyakazi ili kuzungumzia malipo mazuri kwa ajili ya wanachama wao, akiahidi kwamba serikali yake itafanya kazi na harakati hizo kama wabia. Pia aliahidi kupunguza gharama za juu za mzigo wa maisha, kwa kutoa elimu bure katika shule za msingi na sekondari na kwa kutoa huduma ya afya kwa wote.


Mdahalo huo umechochea hisia mchanganyiko kutoka kwa wananchi Jambo jingine ambalo liliibuka katika mdahalo wa kwanza wa wagombea urais, ambao uliendeshwa zaidi kwa Kiingereza, lilikuwa kuhusu matumizi ya lugha nyingine rasmi ya Kenya, Kiswahili.

 

Tofauti na mdahalo wa Februari 11 mwaka huu, amesema mdahalo wa Jumatatu ulikuwa wa kuvutia zaidi na wagombea walionekana wametulia.


Waratibu wa mdahalo pia wamesema tukio hilo lilikuwa la mafanikio na kwamba litawasaidia Wakenya kuwachagua viongozi wao, pamoja na kuweka kitangulizi kinachofanya midahalo ya kisiasa kuwa sehemu ya kalenda ya uchaguzi nchini Kenya.


Mwenyekiti wa Kamati ya Mdahalo huo, Meneja Mwendeshaji wa Royal Media Services, Wachira Waruru, amesema kuwa mdahalo huo uliwapa jukwaa wagombea urais kubadilishana mawazo na kutokukubaliana, lakini bila ya kupigana na wala kunyanyasana.


Kuwaweka wagombea urais katika jukwaa moja ili kuelezea ajenda zao kulitoa fursa ya uvumilivu, kwa vile ilionesha wafuasi wao ambao wangeweza kuonana kama maadui kwamba siasa ni ushindani tu.


“Kama unavyojua, hii ni mara ya kwanza tunafanya aina hizi za mijadala na tulikuwa na matatizo makubwa kadhaa,” Waruru.


“Utaona kuwa na wagombea wanane katika mjadala mmoja kujadiliana masuala, mara nyingine muda huwa hautoshi kwa wao kushughulikia masuala vyema,” amesema.

 

Kwa kuwa uchaguzi wa Kenya umepangwa kufanyika Machi 4 mwaka huu, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka imetangaza wagombea wanane watakaoshindana kushika nafasi hiyo ya katika nchi ya Kenya.

Wasifu wa wagombea

Mohammed Dida alizaliwa mwaka 1975 katika Wilaya ya Wajir. Dida, ni Mwalimu, anagombea urais kupitia Chama cha Muungano kwa ajili ya Mabadiliko Halisi (Alliance for Real Change). Mgombeamweza wake ni Joshua Odongo Onono, pia ni mwalimu.


Dida, hana muda mrefu katika siasa, ameapa kuwa rais ambaye ataawangalia maskini. Amesema elimu inapaswa kuwa bure kwa Wakenya wote, na si kwa kutegemea mfumo wa ruzuku.

 

Dida amesema kwa kujiamini kwa uwezo wake wa kufanya vizuri katika uchaguzi, kama alivyosema chama chake kinaungwa mkono na vijana.

 

Ana shahada ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta na kwa sasa anafanya Shahada ya Uzamili katika masomo ya dini kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.


Amefundisha katika shule kadhaa, ikiwa ni pamoja na kufundisha fasihi ya Kiingereza na dini katika shule ya sekondari ya Daadab katika kambi mchanganyiko ya wakimbizi na baadaye katika shule ya Lenana.

 

Alijiuzulu kufundisha mwaka 2009 na kuanza kazi ya uwakala wa kazi ya muda, lakini amesema mradi haukufanikiwa kwa sababu ya rushwa ya serikali.

Martha Wangari Karua

Martha Karua, mgombea pekee mwanamke, katika kinyang’anyiro cha urais, amezaliwa Septemba 1957 huko Kirinyaga, Jimbo la Kati. Karua, mbunge wa Gichugu, anagombea kupitia National Rainbow Coalition pamoja na aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Bunge la Afrika Mashariki Augustine Lotodo.


Karua ameapa kuwakilisha muungano wa Kenya pamoja na jukwaa la mabadiliko ya uchumi na jamii, ikiwa ni pamoja na huduma za afya kila mahali na kuifanya Kenya kuwa kitovu cha uchumi katika kanda.

 

Amesema atatoa asilimia 10 ya bajeti ya Kenya kuboresha uzalishaji wa kilimo, kuongeza vyanzo vya nishati rejezi na kufanya kazi ili kuwezesha ufikivu wa intaneti kwa asilimia 50 kwa Wakenya katika miaka mitano.

Wakati wa mjadala wa urais, amesema atashughulikia vifo vinavyotokana na uzazi kwa kutoa upatikanaji wa huduma za afya mahali kote.


Karua ana shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Marekani, Nairobi. Kuanzia mwaka 1981 hadi 1987, Karua alifanya kazi mahakamani, alipanda kutoka Hakimu wa Wilaya hadi Hakimu Mkuu Mkazi. Baada ya hapo amekuwa na shirika la uwakili binafsi hadi 2002.  Mwaka 1992, Karua alichaguliwa kuwa mbunge wa Gichugu, kiti ambacho anakishikilia hadi sasa.

 

Mwaka 1997 na 1998 alifanya kazi na kikundi cha Bunge cha Vyama Mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya mfumo wa vyama vingi nchini Kenya.  Mwaka 2008, aliteuliwa kuwa Waziri wa Sheria, mshikamano wa taifa na masuala ya katiba na amekuwa Waziri wa Usimamizi na Maendeleo ya Rasilimali za Maji. Mwaka 2009 alijiuzulu katika nafasi yake ya uwaziri katika serikali ya umoja, akitaja kukatishwa tamaa katika kutekeleza kazi zake.

Peter Kenneth

Peter Kenneth alizaliwa Novemba 1965 huko Bahati, Nairobi. Yeye ni mbunge mwenye taaluma ya masuala ya benki. Anagombea urais chini ya Chama cha Kenya National Congress, pamoja na mgombea mwenza aliyekuwa meneja mwandamizi wa Safaricom, Ronald Osumba.


Kama mgombea, Kenneth amejielekeza katika kuboresha tatizo la ukosefu wa ajira na uhakika wa chakula. Pia alidhamiria kuipa polisi vifaa na kuwalipa vizuri maofisa hao, ili kuwahamasisha kufanya kazi nzuri, na anaamini kwamba maendeleo na elimu katika maeneo yanayokumbwa na uhalifu yatazuia vitendo haramu. Anapanga kulipia programu zake kwa kupunguza matumizi makubwa ya serikali.


Kenneth ana shahada ya kwanza na ya uzamili katika sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, pamoja na kozi ya shahada ya juu kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Programu ya Utendaji kwa ajili ya Maendeleo ya Usimamizi huko Lausanne, Uswisi.


Kama Mkurugenzi wa Benki, Kenneth alianza kufanya kazi na Kampuni ya Fedha ya Nationwide mwaka 1985, kisha akafanya kazi na Prudential Finance na Benki tangu 1986 hadi 1997, ambako alikuwa meneja.


Kuanzia 1997 hadi 2002, alifanya kazi katika Kampuni ya Kukata Bima ya Kenya, wakati huo huo akishika vyeo katika Shirika la Kukata Bima la Afrika na Benki ya Maendeleo ya Viwanda.  Tangu 1998 hadi 2009, alifanya kazi kama mwenyekiti wa Kampuni ya Kukata Bima ya Zep.


Katika maisha yake ya kisiasa, Kenneth alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge wa kiti cha Gatanga mwaka 2002, kiti anachokishikilia hadi sasa. Tangu 2003 hadi 2005, alifanya kazi kama Msaidizi wa Waziri katika Wizara ya Maendeleo ya Ushirika na Masoko, kisha kama msaidizi wa waziri katika Wizara ya Fedha hadi 2007. Tangu 2008, amekuwa Msaidizi wa Waziri katika Wizara ya Mipango, Maendeleo ya Taifa na Dira ya 2030.

Uhuru Muigai Kenyatta

Uhuru Muigai Kenyatta alizaliwa Oktoba 1961. Baba yake ni rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, ambaye aliongoza tangu 1964 hadi 1978.  Ni mgombea wa urais wa chama cha Jubilee Alliance, chama cha muungano kilichoundwa chini ya The National Alliance cha Kenyatta na chama cha United Republican cha William Ruto.


Katika ilani ya muungano wake, Kenyatta ana msimamo wa Kenya iliyoungana “chini ya ndoto moja ya kujenga Kenya bora”.  Amesema atajikita katika suala la umiliki wa ardhi, na anadhamiria kuibadili Kenya kuwa kitovu cha uchumi, akijenga uchumi wa usafirishaji bidhaa nchi za nje. Kenyatta ana shahada ya kwanza katika siasa na uchumi kutoka Chuo cha Amherst huko Marekani.


Baada ya kipindi kifupi cha kufanya biashara, Kenyatta aligombea kiti cha ubunge cha Gatundu Kusini mwaka 1997, lakini alishindwa.  Miaka miwili baadaye, Rais Daniel arap Moi alimteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii ya Kenya, na mwaka 2001, alimteua bungeni.

 

Kenyatta aligombea urais bila ya mafanikio mwaka 2002, lakini alishinda kiti cha ubunge akiwakilisha Gatundu kusini mwaka huohuo. Amegombea urais tena mwaka 2007, lakini alijitoa na kumuunga mkono Rais Mwai Kibaki kwa uchaguzi wake tena.


Kibaki alimteua Kenyatta kuwa Waziri wa Serikali za Mitaa, Januari 2008 kabla ya kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Biashara, Aprili 2008 kama sehemu ya serikali ya umoja iliyopanga kumaliza vurugu baada ya uchaguzi 2007.

 

Amehamishiwa katika Wizara ya Fedha kuanzia mwaka 2009 hadi 2012, wakati akiendelea kuwa Naibu Waziri Mkuu. Ameacha kazi ya uwaziri wa fedha Januari 2012 baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) kumtuhumu kwa kufanya uhalifu kinyume cha ubinadamu kwa wajibu wake katika vurugu za uchaguzi wa 2007-2008.

 

Wote Kenyatta na Ruto walikabiliwa na upinzani wakati wa kampeni za uchaguzi kuhusu kesi zao zilizosimamishwa na ICC, na Kenyatta alijibu maswali kuhusu suala hili wakati wa mdahalo wa urais.

James ole Kiyiapi

James ole Kiyiapi alizaliwa Mei 1961 huko Osupuko, Jimbo la Bonde la Ufa. Katibu Mkuu wa zamani katika wizara mbalimbali, aliacha kazi mwaka 2012 ili kugombania pamoja na mwanamke mfanyabiashara Winnie Kaburu, chini ya Urejeshaji na Kukijenga chama cha Kenya.

 

Kiyiapi anasimamia ilani ya uchaguzi inayokana siasa za kikabila.  Amesema kipaumbele chake cha awali kitakuwa kuzingatia ukosefu wa ajira kwa vijana, ambalo aliita janga la taifa.


Serikali yake, amesema, itashinikiza kazi ya kumaliza migogoro ya ardhi kwa uangalifu wa hali ya juu na uwazi, na itaboresha uzalishaji wa kilimo nchini. Kiyiapi ana shahada ya uzamili kutoka katika Chuo Kikuu cha Moi na Shahada ya Uzamivu kutoka katika Chuo Kikuu cha Toronto nchini Kanada, zote ni kuhusu misitu.


Kuanzia mwaka 1988 hadi 1994, alikuwa mtafiti mwandamizi katika Kitivo cha Utafiti wa Mazingira katika Chuo Kikuu cha York nchini Kanada.  Amefanya kazi kama mhadhiri na Profesa msaidizi katika Chuo Kikuu cha Moi kuanzia mwaka 1994 hadi 2006.  Wakati huo, pia alifanya kazi kama Mkurugenzi wa Programu nchini katika Mfuko wa Wanyamapori Afrika.


Kiyiapi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu katika Wizara ya Mazingira na Maliasili mwaka 2006, Wizara ya Huduma za Tiba mwaka 2008, na Wizara ya Elimu mwaka 2010.

Wycliffe Musalia Mudavadi

Naibu Wairi Mkuu Wycliffe Musalia Mudavadi alizaliwa Septemba 1960 huko Sabatia, Jimbo la Magharibi.  Anagombea kupitia chama cha United Democratic Forum katika Amani Alliance, pamoja na Jeremiah Kioni, mbunge kutoka Jimbo la uchaguzi la Ndaragwa.

 

Mudavadi ameahidi kukuza uchumi wa uhakika nchini Kenya kwa kuzingatia utawala bora na kupunguza umaskini. Amesema atakabiliana na rushwa nchini kwa kupanga upya mfumo wa mahakama, na kuajiri maofisa polisi wengine zaidi ili kuboresha usalama.  Mudavadi ana shahada ya uchumi wa ardhi kutoka katika Chuo Kikuu cha Nairobi.


Baada ya kuhitimu, amefanya kazi katika Shirika la Nyumba la Taifa kabla ya kufanya kazi katika Kampuni ya Tysons Limited, inayohusika na ujenzi na upangishaji wa nyumba.

 

Mudavadi alikuwa mbunge mwaka 1989 wakati alipochaguliwa bila kupingwa, kuchukua kiti cha ubunge wa Sabatia kilichoachwa wazi baada ya kifo cha baba yake, Moses Mudavadi. Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 1992, Mudavadi aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha kwa miaka mitano.

 

Mwaka 1998 aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, kisha Waziri wa Habari, Uchukuzi na Mawasiliano mwaka 1999, na Waziri wa Uchukuzi na Mawasilino mwaka 2001. Kwa kipindi chote hicho alikuwa Mbunge wa Sabatia.

 

Mwaka 2002, Mudavadi alipoteza kiti chake cha ubunge, lakini aliteuliwa na Rais Daniel arap Moi kuwa Makamu wa Rais, na alikaa katika nafasi hiyo kwa miezi miwili. Kisha aligombea bila mafanikio nafasi ya Makamu wa Rais na Mgombea Mwenza Uhuru Kenyatta mwaka 2002.


Baada ya hapo, Mudavadi alisaidia kuanzisha Chama cha Orange Democratic Movement na aligombea kwa nafasi ya rais wa chama mwaka 2007, lakini Raila Odinga alimshinda.


Tangu hapo, alikuwa akifanya kazi kama mjumbe wa Bodi ya Magavana wa Benki ya Dunia na mjumbe wa Kamati ya Bunge iliyochaguliwa kwa ajili ya Mabadiliko ya Katiba. Mwaka 2012, Mudavadi aliondoka katika Chama cha Orange Democratic Movement na kujiunga na Chama cha United Democratic Front.


Kwa muda mfupi alijiunga na chama cha Jubilee Alliance cha Uhuru Kenyatta, lakini aliamua kujitenga Desemba baada ya kutokubaliana kuhusu nani atakayeongoza.

Paul Kibugi Muite

Paul Kibugi Muite alizaliwa Aprili 1945. Ni mbunge wa zamani kutoka Kabete ambaye ni mwanachama muanzilishi na kiongozi wa Chama cha Safina.  Anagombea pamoja na Shem Ochuodho, waziri wa zamani wa nishati na mbunge kutoka Rangwe.


Muite amesema, yeye kama rais atashughulikia ukosefu wa ajira na kuboresha hali za kazi, sehemu moja kwa kupandisha mishahara na kuimarisha sheria za kazi ambazo zinaweka kikomo cha saa siku ya kazi kuwa masaa manane.


Pia ameapa kuzuia ufisadi wa serikali, jambo alilosema kuwa limewapeleka mamilioni ya Wakenya katika umasikini wa milele na mateso. Anaamini kwa umoja wa Wakenya wote, bila ya kujali makabila yao, na atafanyia kazi uboreshaji jamii na uchumi kwa watu wote.

 

Muite amesema Kenya pia inaumizwa na sifa hasi kimataifa kwa ufisadi na rekodi mbaya ya haki za binadamu, jambo ambalo ameahidi kulishughulikia kupitia elimu na masoko. Muite, mwanasheria wa haki za binadamu, alikuwa mtu maarufu wakati wa siku za mwisho za mfumo wa chama kimoja miaka ya 1990, ambayo ilianzishwa na Kenya African National Union (Chama cha Kitaifa cha Waafrika wa Kenya) mwaka 1982.

Alitumikia vipindi vitatu vya miaka mitano mitano kama mbunge wa Kabete, mwaka 1992, 1997 na 2002.

Raila Amollo Odinga

Waziri Mkuu Raila Amollo Odinga alizaliwa Januari 7, 1945 huko Maseno Jimbo la Nyanza, mtoto wa Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga. Anagombea katika chama cha Orange Democratic Movement (Harakati Kidemokrasia za Chungwa) pamoja na Makamu wa Rais Kalonzo Musyoka kama mgombea mwenza.

 

Odinga amejikita katika kuwakomboa vijana kutoka katika umasikini kwenye kampeni zake, akiwaahidi kupata ajira na elimu. Amesema kuwa atatoa fedha taslimu kwa masikini na wazee, na kuanzisha mpango kwa vijana wanaosubiri kuingia chuo kikuu au wanaotafuta kazi kwa kufundisha kwenye shule za msingi.


Kiuchumi, amesema ataanzisha progamu za kusafirisha bidhaa zinazotengenezwa vijijini nchini Kenya, na kusaidia ukuaji wa sekta ya chuma cha pua. Amesema kuwa ataboresha miundombinu na kupanua uwekezaji katika usalama wa chakula kupitia kilimo kilichoboreshwa, ruzuku kwa wakulima na utafiti.


Odinga anayo shahada ya uzamili ya uhandisi mitambo kutoka Chuo cha Magdeburg Cha Tekonolojia ya Juu. Pia ametunukiwa stashahada ya heshima za uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi na Chuo Kikuu cha Kilimo na Ufundi cha Florida huko Tallahassee, Marekani.


Mwaka 1970, alianza kufanyakazi kama mhadhiri kwenye idara uhandisi mtambo katika Chuo Kikuu cha Nairobi. Mwaka 1974, aliondoka wakati alipoteuliwa kama meneja wa viwango katika kikundi kwenye ofisi mpya ya Viwango ya Kenya, ambako alikuwa Naibu Mkurugenzi mwaka 1978.


Mwaka 1982, Oginga Odinga alihusishwa kama mtoa fedha wa jaribio la mapinduzi dhidi ya serikali ya Rais Daniel arap Moi, ambaye alikuwa amezuwia jaribio la Oginga Odinga la kusajili chama cha upinzani.


Raila Odinga alishtakiwa kwa uhaini na kuwekwa kuzuizini kwa muda wa miaka sita bila kesi. Odinga aliachiwa huru mwaka1988, lakini na kutiwa mbaroni tena mwaka mmoja baadaye kwa kuhusika na Harakati za Mapinduzi Kenya, kikundi kilichokuwa kinashinikiza kuwapo kwa demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya.

 

Odinga alikamatwa tena mwaka 1990 na alipoachiwa huru mwaka 1991 aliomba hifadhi huko Norway, kwa madai kwamba serikali ilikuwa inapanga kumuua.

 

Baada ya mfumo wa chama kimoja, Odinga alirejea mwaka 1992 na kujiunga na Jukwaa la Demokrasia (FORD), chama cha siasa kilichokuwa kinaongozwa na baba yake, na kushinda kiti cha ubunge katika eneo la Langata. Mwaka wa 1997, Odinga alishindwa alipogombania urais.


Odinga amekuwa Waziri wa Nishati kutoka mwaka 2001 hadi 2002 na kama Waziri wa Barabara, Kazi za Umma na Nyumba kutoka mwaka 2003 hadi mwaka 2005.


Mwaka 2005, Odinga alianzisha Chama cha Harakati za Kidemokrasia cha Chungwa, ambapo kwa kupitia chama hicho, aligombea uraisi bila mafanikio mwaka 2007.


Baada ya kumalizika kwa vurugu, Odinga akawa waziri mkuu katika makubaliano ya kugawana madaraka.


 

By Jamhuri