Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uchumi wa nchi unaendelea kukua kwa kasi pamoja na kuwapo changamoto zinazotokana na kudorora kwa hali ya uchumi wa dunia ambazo zimesababisha kuyumba kwa biashara na uwekezaji duniani.

Katika toleo la hivi karibuni la Muhtasari wa Tamko la Sera ya Fedha, BoT inasema uchumi wa Tanzania ulikuwa madhubuti katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha ambacho ni kipindi cha miezi sita kati ya Julai na Disemba mwaka 2019 kama ilivyokuwa kwa miezi yote 12 ya mwaka jana.

Chapisho hilo la mwezi Februari ambalo linatoa tathmini ya hali ya uchumi wa nchi na dunia nzima kwa ujumla pia linasema uchumi wa taifa utaendelea kukua vizuri kati ya Januari na Juni mwaka huu, ambayo ni miezi sita iliyobaki ya mwaka wa fedha wa 2019/20.

“Uchumi unakadiriwa kuendelea kukua kwa kasi katika nusu ya pili ya mwaka 2019/20, licha ya changamoto zilizopo za ukuaji mdogo wa uchumi wa dunia,” Benki Kuu inasema kwenye tamko hilo ambalo pia linatathmini hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa sera ya fedha katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu wa fedha.

BoT inasema ukuaji wa uchumi wa Tanzania mwaka 2019 ulichochewa zaidi na uwekezaji wa serikali katika miundombinu, kuimarika kwa shughuli za sekta binafsi, kuimarika kwa mahitaji ya bidhaa, huduma, ukuaji wa mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi. Shughuli zilizochangia sehemu kubwa ya ukuaji huo ni ujenzi, kilimo na usafirishaji.

“Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua kwa kasi. Katika kipindi cha robo tatu za mwanzo za mwaka 2019 uchumi ulikua kwa wastani wa asilimia 6.9 kama ilivyokuwa mwaka 2018. 

“Viashiria vya ukuaji wa uchumi vinaonyesha kuwa uchumi katika robo ya nne ya mwaka 2019 umeendelea kuimarika, hivyo inakadiriwa kuwa uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia saba mwaka 2019 na zaidi ya asilimia saba kwa mwaka 2020,” tamko la taasisi hiyo ya fedha linasema.

Kulingana na taarifa ya mwelekeo wa hali ya uchumi wa dunia iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) mwezi Januari mwaka 2020, ukuaji wa uchumi wa dunia ulipungua na kufikia asilimia 2.9 mwaka 2019, ikilinganishwa na asilimia 3.6 mwaka 2018.

BoT inasema hali hii ilichangiwa na mgogoro wa kibiashara kati ya China na Marekani, mivutano baina ya mataifa ya Mashariki ya Kati, na changamoto za kisera duniani, hususan hatua ya Uingereza kujitoa Jumuiya ya Ulaya (Brexit).

Sababu nyingine za kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa dunia ni migogoro ya kijamii katika baadhi ya nchi, majanga yatokanayo na mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi za Caribbean na Australia, na tatizo la ukame katika eneo la kusini mwa Afrika.

IMF inakadiria kuimarika kwa ukuaji wa uchumi wa dunia kuanzia mwaka huu kutokana na kuanza kukua kwa biashara na uwekezaji sehemu mbalimbali duniani. Shirika hilo linakadiria uchumi wa dunia utakua kwa asilimia 3.3 mwaka 2020 na asilimia 3.4 mwaka 2021.

By Jamhuri