url-4Wakati Rais John Magufuli akieleza kuwa uchumi wa nchi umekuwa kwa asilimia 7.9 hadi kufikia robo ya mwaka huu na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya pili baada ya Ivory Coast, Mchumi Mwandamizi na Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, amesema uchumi umekuwa kwa matabaka.

Profesa Ngowi ameieleza JAMHURI, kuwa ukuaji wa uchumi unaoelezwa wakati mzunguko wa fedha umepungua, huku wananchi wakilalamikia hali ngumu za maisha na ukosefu wa ajira kwa wananchi, ni sera zile zile za ukuaji wa uchumi za serikali zilizopita.

“Kukua kwa uchumi kunakoelezwa na Serikali ni kwa matabaka tu. Wenye viwanda wanazalisha bidhaa lakini hawaajiri kutokana na kazi nyingi kufanywa na mashine, hapa uchumi utaongezeka kwao na hawa waliokosa ajira hakuna wanachoambulia hapa tatizo ni ukuaji wa uchumi usiopanua soko la ajira.

Tunaongeza pia kubana matumizi, hali hiyo ni sawa na kuongeza chumvi kwenye kidonda kile kile, hapo hatuwezi kusema kuna mabadiliko yoyote,” anasema Profesa Ngowi.

Akielezea kuhusu ufujaji wa fedha za umma kwa kupitia makundi mbalimbali ikiwamo wanafunzi hewa wa elimu ya juu wanaokuwa wakinufaika na mikopo ya elimu, wanafunzi hewa wa shule za msingi na sekondari, watumishi hewa wa taasisi za Serikali na sasa kaya hewa 42,000, anasema huo ni mgawanyo kwa wasiostahili.

Naye Omary Hassan (38), mkazi wa Sinza kwa Remmy jijini Dar es Salaam, ambaye pia ni mfanyabiashara katika soko la Kariakoo, akielezea kuhusu ukuaji wa uchumi wa nchi anasema kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani, mzunguko wa fedha umepungua sana na maisha yamekuwa magumu.

Hassan anasema pamoja na hali ngumu ya maisha inayoonekana sasa, anaamini kwamba Serikali ina nia njema ya kubana matumizi na kuziba mianya ya watu wachache waliokuwa wakijinufaisha na fedha za umma kwa njia wizi.

“Mimi ni mfanyabiashara mdogo tu, lakini mzunguko wa fedha kwa sasa ni mdogo na kodi tunazolipa ni kubwa mno. Tunaomba Serikali iangalie namna ya kupunguza kodi hizi kwa kuwa hakuna faida tunazopata,” anasema.

Mwingine aliyehojiwa na JAMHURI, ni mtumishi wa Serikali anayefanya kazi Wizara ya Afya (hakutaka jina lake liandikwe gazetini), akielezea kuhusu ukuaji wa uchumi na hali halisi ya maisha ya wananchi, anasema maisha ni magumu kwa watu wote  walioajiriwa na wasiokuwa na ajira wanaoelezwa kwamba walikuwa wanategemea kuishi kwa fedha za dili.

Anasema wanaolalamikia ugumu wa maisha ni watumishi wa Serikali, taasisi za umma na wafanyabiashara tofauti na inavyoelezwa kwamba ni wale waliokosa ajira pekee.

“Ugumu wa maisha ni kwa wananchi wote sasa, kwani hata tulioajiriwa mishahara bado ni midogo, hakuna kilichoongezwa hadi sasa huku bei za bidhaa zikiongezeka kila kukicha.

Serikali pamoja na kubana matumizi inapaswa kuweka nguvu katika udhibiti wa bei za bidhaa mbalimbali badala ya kuwaacha wafanyabiashara kupanga bei kama wanavyotaka kwa kisingizo cha kutozwa kodi kubwa na Serikali,” anasema. 

Akihutubia katika Mahafali ya 31 ya Chuo Kikuu Huria Cha Tanzania (OUT) mwishoni mwa wiki iliyopita, katika Makao Makuu ya chuo hicho, Bungo Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani, Rais Magufuli alisema uchumi wa nchi umeimarika kwani na unatakiwa ukue kwa asilimia 7.2.

Hata hivyo, hadi robo ya mwaka huu umekua kwa asilimia 7.9 na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi ambazo uchumi wake unakua kwa kasi katika nchi za Afrika na kushika nafasi ya pili  baada ya Ivory Coast inayoshika nafasi ya kwanza.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli aliweka bayana hatua yake ya kuitumbua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kuidhinisha Sh bilioni 26 kupelekwa kwenye akaunti maalumu katika benki tofauti za biashara.

Anasema Bodi hiyo iliidhinisha kupelekwa fedha hizo katika benki hizo wakati kuna agizo la Rais la kupiga marufuku kwa taasisi za umma, idara za Serikali, mashirika ya umma, wakala na wizara kuweka fedha zao katika benki za kibiashara badala yake zinatakiwa kufunguliwa akaunti katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Rais Magufuli anasema wanaoweka fedha za umma katika benki hizo za biashara wanafanya hivyo kwa makusudi ili Serikali inapohitaji fedha inakopeshwa tena fedha zake yenyewe kwa riba kubwa, na kwamba benki hizo badala ya kufanya biashara na wananchi zinafanya biashara na Serikali wakati siyo makusudi ya kuanzishwa kwake.

Novemba 20 mwaka huu, Ikulu ilitangaza kwamba Rais Magufuli ameivunja Bodi ya Wakurugenzi ya TRA na kwa muda mchache akateua Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo. Hata hivyo, haikuelezwa sababu za kuvunjwa kwa Bodi hiyo zaidi ya kueleza kwamba Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu, na kuivunja bodi nzima.

Alimteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo kuziba nafasi iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja, baada ya Rais Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Lusekelo Mwaseba.

Wajumbe wa Bodi hiyo waliteuliwa mwaka 2014 na walitakiwa kuwa katika nafasi hiyo hadi mwaka 2017. Wajumbe wa Bodi hiyo ya TRA iliyovunjwa ni Shogholo Msangi (Kamishna Msaidizi wa Sera, Wizara ya Fedha), Khamis Omari (Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Zanzibar) na Dk Philip Mpango (Waziri wa Fedha na Mipango).

Wengine ni Profesa Beno Ndullu (Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania), Assaa Ahmad Rashid (Katibu Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar), Josephat Kandege (Mbunge Kalambo – Mkoa wa Rukwa), Dk John Mduma (Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Utafiti wa Uchumi na Sera Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ), Dk Nsubili Isaga, (Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mzumbe), na Rished Bade (aliyekuwa Kamishna Mkuu TRA). Katibu wa Bodi hiyo, Juma Beleko (TRA).

Akihutubia katika Mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Rais Magufuli alieleza sababu ya kuitumbua bodi hiyo kuwa ni ukiukaji wa taratibu kwa kuidhinisha fedha hizo kuwekwa kwenye benki hizo za biashara ikiwa tofauti na maelekezo yaliyotolewa na Serikali. 

Pamoja na hayo, ameomba wananchi kuwaombea ili waendelee kutumbua majipu kutokana na nchi kufikishwa mahali pabaya, hali inayowapa mwanya watu kuweza kuitisha vikao hata Ulaya. Hivyo kutokana na utumbuaji mapato yameongezeka kutoka trilioni 1.2 hadi kufikia 1.8.

Jumla ya wahitimu 4,027 walihitimu na kutunukiwa shahada mbalimbali na Mkuu wa Chuo Kikuu Huria Tanzania, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

1985 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!