Sakata la vyeti feki linalomuhusisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda lina sura nyingi, uchunguzi wa JAMHURI umebaini.

 

Pamba Sekondari

JAMHURI limefika katika Shule ya Sekondari ya Pamba, iliyoko jijiji Mwanza na kufanya mahojiano na Mkuu wa Shule hiyo, Phares Byekwaso, ambaye amegoma kuzungumzia suala hilo akidai yeye ni mgeni shuleni hapo na kwamba suala hilo lipo nje ya uwezo wake.

Mwalimu Byekwaso amelitaka JAMHURI kuwasiliana na Baraza la Mitihani la Taifa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ndiyo wenye uwezo wa kufafanua sakata hilo.

“Baraza la Mitihani wanaweza kukusaidia zaidi maana wanayo matokeo ya kila mwanafunzi nchini, ikiwa ni pamoja na shule aliyosoma. Hapa kwangu itakuwa ni kunionea tu,” amesema Byekwaso.

Hata hivyo, chanzo cha habari kutoka Pamba Sekondari kimelieleza JAMHURI kuwa, Paul Makonda, hakuwahi kuwa mwanafunzi wa shule hiyo na wala jina lake halimo katika orodha ya wanafunzi waliowahi kusajiliwa na shule hiyo tangu kuanzishwa kwake.

“Ukweli ni kwamba Makonda hajawahi kusoma katika shule hii, na hata katika matokeo ya mwaka 2001 ambao unasemekana alimaliza shule jina lake halipo. Hapo ndipo utakapouona ukweli wake, nimekuwa katika shule hii kwa miaka mingi, lakini hatujawahi kuwa na mwanafunzi mwenye jina la Paul Makonda au Daud Bashite,” anasema mtoa taarifa wetu.

Chanzo hicho kimesema Makonda alikuwa anasoma masomo ya jioni katika Sekondari ya Pamba ikiwa ni moja ya vituo vya elimu huku akifahamika kwa jina la Daud Bashite.

Masomo hayo yalikuwa yakitolewa na Idara ya Elimu ya Watu Wazima ambayo hayahusiana na shule hiyo, na kwamba pamoja na kusoma masomo hayo hakumaliza bali aliondoka mwaka wa pili ambapo walisikia kuwa kahamia Shule ya Sekondari ya Lake.

 

 Lake Sekondari

JAMHURI limefika Shule ya Sekondari Lake na kufanya mahojiano na Mkuu wa Shule, Deus Shigelele, ambaye amesema shule hiyo haina Kituo cha Elimu ya Watu Wazima, hivyo ni vigumu kuwa mwanafunzi huyo alopokelewa shuleni hapo.

“Haya mambo mie nayasoma kwenye magazeti, na wapo ambao waliwahi kuuliza kuhusu hili. Mimi hapa hajawahi kufika huyo Paul wala Daudi. Shule hii haijawahi kuwa na mwanafunzi huyo, labda aulizwe vizuri atawaeleza,” amesema Shigelele.

Amesema katika shule hiyo hakuna kumbukumbu yoyote ya shule inayoonyesha kuwa aliwahi hata kuomba kusoma shule hiyo.

 

 Mzee Khamesse

 Kutokana na kuwepo kwa taarifa za Paul Makonda kulelewa katika familia ya aliyekuwa Meya wa Jiji la Mwanza, Seleman Khamesse, JAMHURI limefika nyumbani kwa Mzee Khamesse, katika eneo la Nyamanoro, jijini Mwanza na kufanya mahojiano;

 JAMHURI; Kuna taarifa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewahi kuishi nyumbani kwako. Je, ni kweli?

KHAMESSE; Ni kweli Daudi alikuja kwangu akiwa darasa la tano akitokea kijijini kwao, Koromije na kisha kuishi hapa na familia yangu.

JAMHURI; Mbona unasema uliishi na Daudi wakati nimekuuliza kuhusu Paul Makonda?

KHAMESSE; Ni kweli nimesema Daudi kwa sababu namfahamu kwa jina hilo. Amekuja kwangu akitokea kwa wazazi wake waliokuwa wakiishi Koromije, na jina lake ni Daudi Albert Bashite.

Wakati shangazi yake ambaye ni mke wangu mdogo (Mama Khamesse) anamleta hapa alikuwa akitumia jina hilo na hata alipopelekwa shule alikuwa akitumia jina la Daudi Bashite wakati anasoma Shule ya Msingi Nyanza.

Hata wakati anakwenda kuanza shule Pamba Sekondari alienda kwa jina la Daudi Bashite.

JAMHURI; Una uhusiano gani na Daudi?

KHAMESSE; Daudi ana uhusiano na mke wangu mdogo Bernadeta maarufu kama Mama Khamesse. Mama ndiye aliyemleta hapa kwani ni shangazi yake anaweza kukwambia zaidi kuhusu hilo.

JAMHURI; Tangu alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni na kisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam mmekuwa mkiwasiliana?

KHAMESSE; Hatuna mawasiliano kwani tangu ateuliwe amewahi kufika nyumbani kwangu hapa tulipo mara mbili tu, tena alikuja usiku.

Mara ya kwanza alikuja saa saba usiku, hakuingia ndani aliishia nje akaongea na vijana wenzie akaondoka. Mwaka jana mwezi wa Ramadhan alikuja saa tano usiku akiwa amesindikizwa na vijana wawili hakuingia ndani aliishia nje akaongea na vijana wenzie, kwa vile nilikuwa sijalala tulisalimiana akanipatia mawasiliano yake kisha akaondoka.

Ukweli ni kwamba hatuna mawasiliano, kutokana na kwamba haoneshi kuhitaji kuwasiliana kwani namba alizonipatia nikipiga hapokei, hata nilipotuma ujumbe hakukuwa na majibu.

Ila wasiliana na shangazi yake anaweza kukueleza zaidi maana mie sikukaa naye sana kutokana na majukumu yangu yaliyokuwa yakinikabiri wakati huo. Pamoja na kwamba alikuwa akiishi nyumbani kwangu.

 

 Ramadhani Khamesse

 Ramadhani ni mtoto wa Mzee Khamesse, ambaye alikuwa akisoma shule moja na Paul Makonda, amesema kwamba amesoma na kuishi na Makonda katika kipindi chote alichokuwa nyumbani kwao.

“Tulikuwa naye shule moja ya Nyanza, na jina lake ni Daud Albert Bashite. Dada yangu, mimi, huyu Daudi tulikuwa tunalala naye chumba kimoja hivyo namfahamu. Pia tulikuwa rika moja hivyo hata michezo yetu ilifanana ingawa tulikuwa tunatofautiana baadhi ya tabia,” amesema Ramadhan.

Akimuelezea Makonda amesema anajua kuishi na watu pale anapohitaji jambo lake lifanikiwe kwani alikuwa anajua kunyenyekea kwa walimu ingawa alikuwa na tabia ya kubagua marafiki hasa wale ambao familia zao zilikuwa duni. “Alikuwa ni rafiki wa wenye uwezo,” amesema.

Pia ameeleza kwamba baada ya kujiunga na masomo ya jioni Pamba Sekondari alihamia kwa ndugu yake mwingine anayefahamika kwa jina la Mwana Zakhia.

Kuhusu mawasiliano kati yao, amesema ingawa wamekua pamoja hakuna mawasiliano yoyote kati yao kutokana na Makonda kumpatia namba ambazo hata akipiga simu hazipolewi.

“Alikuja hapa mara mbili usiku tukazungumza mambo mengi ikiwa ni pamoja na kukumbushana maisha tuliyoishi. Zaidi ya hapo hatuna mawasiliano kabisa zaidi ya kumsikia na kumuona kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii,” amesema Ramadhani.

 

Mama Khamesse

JAMHURI lilifika nyumbani kwa Mama Khamesse Lumara na kufanya mahojiano;

JAMHURI: Una uhusiano gani na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam?

MAMA KHAMESSE: Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ni ndugu yangu kwani baba yake, Mzee Albert Bashite ni binamu yangu. Kwa hiyo Daudi ananiita mimi shangazi.

JAMHURI: Unaweza kunisaidia jila lake ni Daudi au Paul Makonda?

MAMA KHAMESSE: Mimi ninamfahamu kwa jina la Daudi Albert Bashite. Na hata wakati nampeleka kuanza shule katika shule ya mshingi Nyanza aliandikishwa kwa jina la Daudi Bashite.

JAMHURI: Ilikuwaje ukaanza kuishi naye?

MAMA KHAMESSE: Mama yake alikuja kuniomba mtoto wake aje kuishi na kusomea kwangu. Ukweli sikuona sababu za kumkatalia. Nilimkubaliana na kumpokea kisha ‘kumfanyia mpango wa kujiunga’ na shule ya Nyanza ambapo aliingia darasa la tano mpaka alipomaliza darasa la saba.

JAMHURI: Alipomaliza darasa la saba matokeo yake yalikuwaje?

MAMA KHAMESSE: Ukweli ni kwamba hakubahatika kufaulu ili kujiunga na kidato cha kwanza hivyo alilazimika kuanza kusoma masomo ya jioni katika shule ya sekondari ya Pamba.

Lakini hakuweza kukaa nyumbani kwangu kwa kipindi kirefu baada ya kuanza kusoma Pamba kutokana na sababu ambazo siwezi kukuelezea, kwani nilimuita mama yake tukazungumza kisha akamchukua na kumuhamishia kwa ndugu mwingine ambaye ni baba yake mdogo na Daudi.

Hata hivyo, wakati shangazi yake akigoma kutaja chanzo cha Makonda kuondoka kwa Mzee Khamesse, habari za uhakika ambazo familia ya Khamesse haikuthibitisha wala kukanusha zinasema Makonda alikuwa anachezea bunduki ya Mzee Khamesse risasi ikafyatuka na kupasua paa.

“Mzee Khamesse alisema huyu mtoto andoke haraka. Alisema kama amechezea bunduki yake kuna hatari anaweza akaua watoto wake kwa risasi kupitia michezo yake isiyokubalika,” kinasema chanzo chetu.

Mtu aliyeko karibu na Makonda amekiri lilitokea tukio hilo, ila akasema: “Hiyo ilikuwa michezo ya watoto. Mbona wengi tumemwaga uji wa mgonjwa? Ni hawa watu wa dawa za kulevya tu wanaochochea hata hayo mambo madogo.”

JAMHURI: Je, alimaliza masomo yake ya sekondari na kuhitimu?

MAMA KHAMESSE: Mh! Hapo kwenye kumaliza sekondari siwezi kukueleza lolote maana ni kautata kidogo kwani sikumbuki kitu kama hicho.

Ila ninachofahamu ni kwamba alianza kufanya kazi ya ukondakta wa daladala kwenye mabasi ya baba yake mdogo ambaye kwa sasa ni marehemu anayefahamika kwa jina la Mabina.

Baada ya muda kupita nilisikia kuwa amejiunga na Chuo cha Uvuvi Nyegezi, jijini Mwanza, na baadaye nikasikia yuko chuo huko Mbegani, Bagamoyo anasoma.

Lakini muda haukupita sana ndipo nikasikia kuwa amekuwa muhubiri hivyo alikuwa akihubiri injili na alikuwa akisafiri sana.

JAMHURI: Katika kipindi chote hicho uliwahi kusikia kuwa amebadili jina na kuitwa Paul?

MAMA KHAMESSE: Hapana nilikuwa sijawahi kusikia akiitwa jina zaidi ya tunalolifahamu wanafamilia la Daud Bashite. Na siku zote namfahamu kwa jina hilo hilo ingawa nilikuja kushangaa kuona kwenye luninga wakati yuko Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) alipotambulishwa kwa jina la Paul Makonda.

Nilishangaa jina nikadhani wamekosea, lakini kila siku zinavyokwenda niliendelea kumuona kwenye luninga akitambulishwa kwa jina la Paul Makonda huku akiwa ni Daud Bashite ninayemfahamu.

JAMHURI: Hili jina la Makonda unadhani amelitoa wapi?

MAMA KHAMESSE: Jina hili la Makonda ni jina ambalo lipo katika ukoo, upande wa babu na bibi zake, hivyo sio jina jipya katika ukoo. Lakini suala la yeye kuanza kuitwa hivyo labda yeye binafsi au wazazi wake wanaweza kulisema hilo.

Ndugu

Mmoja wa ndugu zake wa karibu (jina linahifadhiwa) amesema kwamba Daudi alishindwa kuendelea kuishi nyumbani kwa shangazi yake (Mama Khamesse) kutokana na tabia ya kupenda kuwa karibu na marafiki wenye uwezo mkubwa jambo lililokuwa linamnyima uhuru kwani alikuwa na tabia ya kuhamia huko na kutorudi nyumbani.

“Daudi alikuwa anaweza kutoka nyumbani kwao Nyamanoro akahamia nyumbani kwa rafiki zake baada ya siku kadhaa akarudi nyumbani tena kwa shangazi yake. Tabia hii ilimkera Mama Khamesse ikamlazimu kuwasiliana na wazazi wake ambao walimuondoa hapo na kumpeleka kwa ndugu mwingine,” amesema.

Amesema Mzee Albert Bashite alibahatika kuzaa watoto wawili tu ambao ni Daudi na mdogo wake wa kike ambaye hata hivyo alifariki akiwa mdogo, hivyo Daudi ni mtoto wa pekee wa Mzee Daudi Bashite na Susan Daud Malagila. Jina la Daudi alilithi kutoka kwa babu yake mzaa mama.

 

Shule ya Msingi Nyanza

JAMHURI lilifika Shule ya Msingi Nyanza na kukutana na Mwalimu Mkuu ambaye alikataa kujitambulisha kwa jina kwa madai kuwa hawezi kuzungumza chchote mpaka atakapopata kibali kutoka kwa wakubwa wake.

JAMHURI: Mimi ni Mwandishi wa Habari kutoka Gazeti la JAMHURI. Nimefika kwako kupata ufafanuzi kuhusiana na taarifa za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kusoma katika shule yako ya Nyanza.

Mwalimu Mkuu: Siwezi kuzungumzia suala lolote linalohusu jambo hilo. Unatakiwa kuwa na kibali kutoka Ofisi ya Mkoa, nenda kwa RAS (Katibu Tawala wa Mkoa), RAS akishatoa kibali kitatakiwa kuthibitishwa na DAS (Katibu Tawala wa Wilaya), kisha utakipeleka kwa Afisa Elimu Wilaya, ambaye naye atakithibitisha na kukuelekeza kwa Mkurugenzi wa Wilaya ambaye atakupatia kibali cha kuja nacho hapa shuleni niweze kukujibu maswali yako.

Hapa unataka data (takwimu), na taratibu za kupata data unazifahamu. Hivyo siwezi kabisa kukusaidia chochote. Karibu tena.

JAMHURI limefanya mahojiano na mmoja wa walimu shuleni hapo (jina linahifadhiwa) ambaye amethibitisha Daudi Bashite kusoma katika shule ya Nyanza.

“Nashangaa hili jambo kukuzwa kiasi hiki! Hili suala lipo wazi kabisa, Daudi au Makonda kama anavyoitwa alisoma hapa na huyo Mwalimu Mkuu wa Nyanza, Jovenary anaweza kuwa anafahamiana naye kama hakumtangulia darasa kwani naye alisoma hapa hapa. Picha unayoiona kwenye mitandao Daudi aliipigia palee kwenye ngazi,” amesema Mwalimu huyo.

 Chuo cha Uvuvi Nyegezi

JAMHURI limefika katika Chuo cha Uvuvi Nyegezi na kufanya mahojiano na Kaimu Mkuu wa Chuo, Mwalimu Mukama Ndaro, ambaye amesema ni vigumu kwake kutoa ufafanuzi kuhusiana na mwanafunzi huyo kusoma katika chuo hicho kwani yeye si msemaji wa chuo.

“Mimi ninakaimu tu hapa, na suala hili linahitaji data (takwimu). Hivyo ni vigumu kwangu kuweza kukusaidia, labda usubiri mpaka Mkuu mwenyewe atakaporudi. Lakini pia zipo taratibu za kuweza kupata taarifa ambazo zimewekwa na serikali,” amesema Ndaro.

Hata hivyo, vyanzo vya kuaminika vimelithibitishia JAMHURI kuwa mwaka 2001 alijiunga chuoni hapo kwa jina la Paul Christian.

 Shule ya Msingi Koromije

JAMHURI limefika Wiyala ya Misungwi katika Shule ya Koromije, shule ambayo inaelezwa kuwa Makonda alisoma kisha kukutana na Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Antusa Marandu.

JAMHURI: Naomba kufahamu iwapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alisoma hapa.

Mwl. MARANDU: Mh! Swali lako lipo kimtego sana, kwani huyo Mkuu wa Mkoa anaitwa nani?

JAMHURI: Paul Makonda.

Mwl. MARANDU: Sijawahi kusikia kama amewahi kusoma hapa. Labda kwa vile mimi sio mwenyeji sana.

JAMHURI: Je, mmewahi kuwa na mwanafunzi anayefahamika kwa jina la Daudi Bashite?

Mwl. MARANDU: Ndiyo, Daudi Albert Bashite alikuwa mwanafunzi wa hapa kabla hajahamia mkoani Mwanza.

JAMHURI: Daudi alianza shule mwaka gani na alihama katika shule hii mwaka gani? Pia naomba kufahamu sababu za kuhama.

Mwl. MARANDU: Katika kitabu cha kumbukumbu cha usajili inaonyesha kuwa alijiunga darasa la kwanza mwaka 1989 na kuondoka shuleni hapa kati ya mwaka 1994 akiwa darasa la nne (Miaka 6 madarasa manne. Alirudia?).

Aliondoka na kwenda katika shule ya Msingi Nyanza huko Mwanza. Kuhusu sababu za kuondoka kwake sijui nadhani alihama.

Samahani siwezi kukwambia zaidi kwani zipo taratibu zilizowekwa ili kuweza kuongelea masuala haya. Unatakiwa kuja na kibali ambacho kinatolewa ofisi ya Wilaya.

Wameshakuja watu wengi hapa nawafahamisha utaratibu wa kibali. Siwezi kukujibu maswali yako haya mengi bila kibali naomba unielewe.

Taarifa kutoka shuleni hapo zinaonyesha kuwa vyombo vya dola vimechukua daftari la usajili wa wanafunzi kwa kipindi abacho Daudi Bashite/Paul Makonda alisoma kutoka shuleni Koromije na kulipeleka wilayani.

 Kijijini Koromije

Mmoja wa ndugu wa Makonda (jina linahifadhiwa) amesema kuwa wao kama familia siku zote wanamfahamu kwa jina la Daudi ambalo alipatiwa na wazazi wake.

Pia hata pindi anapokuja kijijini hapo hutumia jina hilo la Daudi. Mwaka juzi alifika kijijini hapo kusalimia ndugu zake pamoja na kuwa wazazi wake walishahamia Igoma, jijini Mwanza.

“Ngoja nikwambie kitu. Hapo shuleni Koromije Mwalimu Mkuu ni ndugu yake, ameolewa kwao na Daudi. Wale ni ndugu anamjua vizuri sana kabla hata hajapata vyeo. Hata hapo kwao Iromelo, Koromije ndipo alipozaliwa na kukulia,” amesema ndugu yake Makonda.

 

Wazazi wa Makonda

JAMHURI limefika nyumbani kwao Makonda Igoma, jijini Mwanza na kukutana na mama yake mzazi Susan Malagila.

Baada ya mwandishi kujitambulisha, Mama Makonda alikataa kuzungumza kwa madai kuwa amechoka na hataki.

“Sitaki kusema, sisemi chochote. Kwanza mimi unanijua? Umefikaje hapa kwangu? Kikombe kimejaa sisemi… sisemi kitu samahani,” amesema Mama Makonda.

Mwandishi alitaka kufahamu sababu za kukataa kuzungumza wakati Mama Makonda hajafahamu sababu za ujio wake, lakini alikataa kwa madai kuwa hayuko tayari kufanya mahojiano yoyote yale na kumtaka mwandishi kuondoka nyumbani kwake.

Chanzo cha habari kutoka shule ya Koromije kimelieleza JAMHURI kuwa mwalimu Mkuu wa Shule hiyo anajikuta katika wakati mgumu kutokana na kupewa maagizo kutoka kwa wakubwa wake kutotoa taarifa zinazomuhusu Makonda.

Pia imeelezwa kuwa nyaraka zote zilizotumika kumsajili Makonda katika shule hiyo zimechukuliwa na maafisa kutoka wilayani jambo lisilo la kawaida.

“Unajua huyu Mwalimu Marandu ameshaitwa na kuambiwa mambo mengi na makubwa zake, na tangu aitwe huko amebadilika sijui aliambiwa nini kinachomfanya kuwa hivi. Kitabu cha usajili wa wanafunzi kilichotumika kumsajili Daudi hapa shule kimeshachukuliwa. Hapa tunapokea wageni wengi tangu hili suala limeibuka, ila ukweli unajulikana nashindwa kuelewa kwanini Daudi hataki kuusema,” anasema mtoa taarifa.

Amesema Daudi alisoma shule hiyo kwa miaka sita tangu 1989 mpaka 1994, lakini katika kipindi cha miaka hiyo sita aliishia darasa la nne kutokana na uwezo wake darasani.

JAMHURI limemtafuta Mzee Bashite zaidi ya mara saba. Kila JAMHURI lilipokwenda nyumbani kwake Igoma, lilijulishwa kuwa amekwenda Kanisani. Kanisa hilo ni la AIC Igoma. JAMHURI limekwenda kanisani mara kadhaa, ambapo wazee wa Kanisa walikiri kuwa ni muumini wao, ila kwa bahati mbaya kila mwandishi anapofika anakuta ametoka.

 

 Mahojiano na Paul Christian Kagenzi

 JAMHURI limefunga safari na kwenda hadi mkoani Tabora, ambako mtu anayetajwa na kudaiwa kuwa jina lake ndilo lilitumiwa na Makonda kuingia katika vyuo mbalimbali anafanya kazi. Paul Christian anafanya kazi katika Radio ya Voice of Tabora. Mahojiano yalikuwa hivi:

JAMHURI: Naomba kufahamu jina lako kamili.

PAUL: Jina langu naitwa Paul Pierre Christian Kagenzi, lakini siku zote tangu shuleni na vyeti vyangu vyote nimesajiliwa kwa jina la Paul Perre Christian. Kagenzi ni jina la ukoo ambalo katika familia yetu tumekuwa hatulitumii.

JAMHURI: Unaweza kunifahamisha kuhusu elimu yako?

PAUL: Nimesoma Shule ya Msingi Rukajange, kisha nikachaguliwa kujiunga na Shule ya Sekondari Bugene, zote hizi zipo Mkoa wa Kagera Wilaya ya Karagwe. Nyumbani kwetu ni Kishao ingawa sikuishi sana hapo.

Bugene Sekondari nilisoma miaka miwili tu, kisha nikahamia shule nyingine Mkoani Mwanza ambako ni kwa mama yangu. Nilimaliza kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Mwanza mwaka 1998.

Kama utakumbuka mtihani huo ulifutwa nchi nzima hivyo mwaka 1999 mwanzoni wahitimu wote tulilazimika kufanya upya mtihani ambapo nilifaulu na kupata daraja la kwanza. Mwaka huo huo mwezi wa saba nikajiunga na Shule ya Sekondari ya Tabora kisha kumaliza kidato cha sita mwaka 2001.

JAMHURI: Katika familia yenu unaye mdogo wako anayeitwa Christina?

PAUL: Hapana, sina mdogo wangu yeyote mwenye jina hilo. Hili suala nimekuwa nikilisikia kwenye mitandao ya jamii na hata kwenye baadhi ya magazeti.

Katika familia yetu, kwa mama tumezaliwa watoto sita tu. Watatu kati yao walishatangulia mbele za haki tumebaki watatu tu ambapo mimi ndiye kaka yao. Hao wengine ni wa kike wenye familia zao.

Agnes Christian, Fidelis Christian na Peter Christian ndio hatuko nao tena. Cafren Christian huyu kwa sasa anaishi Kahama, Rhoda Christian yuko Karagwe kwa sasa na mimi Paul Christian niliyeko hapa Tabora. Wote hawa tulisoma Rukajange kisha Bugene Sekondari.

JAMHURI: Umewahi kusikia vyeti vyako vikitumiwa na mtu yeyote?

PAUL: Kwanza naomba ifahamike, mimi sijawahi kumsaidia [mtu] wala kuibiwa vyeti vyangu. Na pia sijawahi kusikia kuwa vinatumiwa na mtu mwingine zaidi yangu mpaka sasa.

Kumekuwa na taarifa za kunihusisha na Mkuu wa Mkoa na Dar es Salaam. Taarifa hizi kuwa anatumia vyeti vyangu ni za kukera kwani mimi shule nilisoma masomo ya sayansi na nikapata alama A. Ni vigumu kwa mtu wanayesema alipata 0 kuweza kutumia vyeti hivyo.

JAMHURI: Unafahamiana na Makonda?

PAUL: Ndiyo tunafahamiana tangu mwaka 2010.

JAMHURI: Ilikuwaje hasa mpaka mkaanza kufahamiana?

PAUL: Nimemfahamu Paul Makonda mwaka 2010 nilipomkuta nyumbani kwa Marehemu Samweli Sitta. Mimi nilikuwa miongoni mwa waandishi wa habari 10 waliopata mwaliko kwenda bungeni, wakati huo akiwa Spika wa Bunge.

Baada ya ziara ya bungeni, alitualika kula chakula cha usiku nyumbani kwake. Tulipofika nyumbani kwa Spika Sitta ndiyo nikakutana na Makonda ambaye alikuwa pale.

Kwenye utambulisho ndipo tukajikuta tunafahamiana kutokana na majina yetu ya Paul, pia Katibu wa Sitta naye alikuwa anaitwa Paul. Tukajikuta tupo kina Paul watatu ambao wote tulikuwa hatutumii kilevi chochote, tukakaa pamoja na kuanza kuzungumza mambo mbalimbali.

Tulibadilishana namba za simu, tukaendelea kuwasiliana baada ya hapo. Nafikiri wakati huo alikuwa anasoma chuo.

Mara ya pili tulionana wakati wa uzinduzi wa jengo la Ofisi ya Spika Sitta jimboni Urambo. Na kuna kipindi nilipokuwa nakwenda Dar es Salaam yeye akiwa likizo tulikuwa tunaonana.

Mara ya tatu tulionana Tabora kwenye msiba. Wakati huo Mzee Sitta akiwa Waziri wa Afrika Mashariki. Alikuja kwenye msafara wa Sitta Kijiji cha Itetemya Makao Makuu ya Ukoo wa Kichifu wa Fundikila. Makonda alikuja pia na tukazungumza.

Makonda alikuwa ameshaanza kuwa maarufu akiwa Umoja wa Vijana Cha Cha MapinduI (UVCCM). Watu walipoona naongea naye waliniuliza kama tunafahamiana kutokana na umaarufu wake, nikasema ndiyo.

JAMHURI: Baada ya kukutana kwa kipindi hicho mmeendelea kuwa na mawasiliano?

PAUL: Ndiyo tumeendelea kuwa na mawasiliano ila hatujaweza kuonana tena. Lakini tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa sijaweza kuwasiliana naye kutokana na namba niliyokuwa nayo pindi nilipokuwa nikiipiga inaita bila kupokewa.

Hivyo hatuna tena mawasiliano kama hapo awali.

JAMHURI: Kumekuwa na taarifa kuwa alitumia cheti chako cha shule kujiunga na chuo ambacho alipewa na ndugu yako wa kike aliyekuwa na uhusiano naye. Unaweza kufafanua kuhusu hili?

PAUL: Mimi nimemaliza form four nimepata division one, nimesoma masomo ya sayansi, alafu anakuja mtu kutumia cheti chako wakati yeye kapata 0 aliwezaje kukimudu cheti cha division one?

Pia ukiangalia ni kama vile nimemtangulia shule. Yeye alikuwa nyuma yangu na hakuna mahali ambapo tumewahi kukutana hapo awali, si mimi wala ndugu zangu ambao hakuna mwenye jina la Christina.

Mimi nimeishi Mwanza, lakini ndugu zangu hawajawahi kuishi Mwanza zaidi ya kwenda ujombani kusalimia wajomba na kuondoka.

JAMHURI: Suala hili la Makonda kudaiwa kutumia vyeti vyako umelichukuliaje?

PAUL: Kwangu mimi limenipatia shida kubwa. Sina amani wala utulivu wa moyo. Usalama wangu uko shakani, maana sijui adui yangu ni nani.

Kama mtu anaibuka na kusema nimemuuzia Makonda cheti na serikali inafanya uchunguzi hilo sina tatizo kwani hakuna ukweli wowote, lakini wasiwasi wangu mkubwa ni maadui wa Makonda wanaweza kunidhuru ili ionekane kuwa Makonda ndiye aliyenidhuru kuficha ukweli.

Hili jambo kuna watu wameligeuza mtaji wanalitafutia fedha. Vyeti vyangu vinatafutwa kwa mamilioni. Hivi karibuni nilipata taarifa kuwa cheti changu kimoja tu kinatafutwa kwa Sh 500,000 mpaka 1,000,000. Na hasa hicho kinachodaiwa kutumiwa na Makonda.

JAMHURI: Baada ya kuona hayo yote, ni hatua zipi umechukua? Umekwenda kutoa taarifa polisi?

PAUL: Hapana sijaenda kutoa taarifa polisi, ila niliwasiliana na mwajili wangu na kumweleza shaka yangu. Mazingira yalivyo ikiwa ni pamoja na watu wangu wa karibu wanavyotumika. Nashukuru alinielewa na alikuwa mtu wa kwanza kutoa ushauri ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua baada ya kujiridhisha na maelezo yangu.

Isipokuwa jambo hili limenifundisha kuchukua tahadhari zaidi katika maisha yangu.

 JAMHURI: Wewe ni mwandishi wa habari, na jambo hili limeibuka kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari, unalichukuliaje?

PAUL: Kwanza nimesikitishwa na hali ya vyombo vya habari na waandishi wa habari kutochukua hatua za kupata ukweli wa jambo hili zaidi ya kutumia mitandao ya jamii kama vyanzo vya habari.

Nashukuru Gazeti la JAMHURI kwa kuweza kufika Tabora na kuonana nami ana kwa ana ili kupata undani wake, ni hatua kubwa na inayofaa kuigwa na vyombo vyote vya habari na wanahabari kwa ujumla.

Jambo hili lina public interest, waandishi (si wa JAMHURI) wameshindwa kutimiza wajibu wao na kujiandikia tu bila kujali madhara yake. Hii ni aibu kwa vyombo vyetu (vilivyoandika bila kumhoji na si JAMHURI), pia imenisikitisha na kuniumiza.

JAMHURI: Tangu kuibuka kwa sakata hili umewasiliana na Makonda?

PAUL: Hapana sijawasiliana naye kutokana na kutokuwa na mawasiliano yake, pia hata yeye binafsi hajanitafuta.

Lakini pia sijaweza kufikiria kuwasiliana naye kwani hofu yangu ni kuhusu kuibuka kwa hizi tuhuma wakati huu alipoanzisha kazi ya kupambana na dawa za kulevya. Sijui hata yeye anafikiria nini mpaka sasa.

JAMHURI: Unadhani suala hilo na Makonda kutumia vyeti visivyo vyake lina ukweli wowote?

PAUL: Hata watu wengi wanaoongelea suala hili sidhani kama wanalifahamu kwani wamekuwa wakishindwa kueleza kwa mtiririko unaoeleweka. Mimi juzi nilikuwa nasikiliza clip ya Mchungaji Gwajima, nilishindwa kuelewa usahihi wa jambo hili kwani nimebatizwa majina yasiyo yangu.

Kuna mahali naitwa Paul Kagenzi, Paul C. Muyenjwa na anasema ana cheti change pia. Huu ni uongo. Kama watu wana jambo ni vyema wakalifanyia uchunguzi ili kujiridhisha pia kuvisaidia vyombo vya dola.

JAMHURI limepata taarifa kuwa Paul Chirstian amehojiwa zaidi ya mara mbili na vyombo vya dola kuhusiana na suala hilo.

Alipoulizwa kuhusu matokeo ya kidato cha sita, bila kutaja masomo aliyosoma, ameliambia JAMHURI alipata daraja la pili. Alipoulizwa baada ya hapo alisoma kozi gani? Amesema alisoma cheti cha uandishi wa habari, katika Chuo cha Nyegezi (Ambayo sasa ni Chuo Cha Mtakatifu Augustin-SAUT) kwa miaka miwili.

Vyanzo vya habari kutoka Nyegezi, vinasema cheti cha kozi ya uandishi wa habari kinasomewa kwa mwaka mmoja.

 

SUA wazungumza

Katika kufuatilia sakata la vyeti vya Makonda, JAMHURI limewasiliana na Chuo Kikuu cha Sokoine ambacho alidaiwa kuomba udahili mwaka 2005 akawa hakuchaguliwa.

Msajili wa wanafunzi Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA), Prof. George Mwamengele, amesema: “Ngoja nikwambie. Kwanza yaani, yaani ilibidi utafute msemaji halisi wa chuo. Kwa sababu hili ni mambo ya kichuo sasa. Lakini kabla hatujafika huko, nikusaidie mahali pazuri pa kupata hiyo habari.

“Huyu alisoma MUCCOBS, si ndiyo kinachoandikwa?… kile Chuo cha Biashara cha Moshi, ambacho sasa hivi kinaitwa MoCU kule ndiko taarifa zake zipo, ambapo Chuo cha MoCU kimekuwa chuo kikuu mwaka jana, ambapo kabla ya hapo kwa miaka saba, nane, kumi hivi, kimekuwa chini ya SUA.

“Wewe unavyoona SUA, maana yake ni MUCCOBS. Vyeti vyao hawa vina nembbo ya SUA lakini hawakuwahi hawa kuandikishwa hapa kwetu, ilikuwa ni Colleage for Business. Hawaandikishwi huku, hawafanyi mitihani huku, wala hatufanyi chochote.

“Tulikuwa tunalea chuo. Tunakilea kianze kujitegemea. Walikuwa na Baraza lao, na Management yao, wana kila kitu chao. Kwa hiyo huku, huwezi kukuta taarifa za huyu mwanafunzi, hata moja. Kama kuna mtu wenu yuko Moshi, anatakiwa kwenda pale Moshi.

“Na kama ana cheti cha kuhitimu, kitakuwa kina nembo ya SUA. Kwa maana ya kwamba, kile chuko kilikuwa chini ya SUA, kama ambavyo Mkwawa, iko chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, maana yake wanafunzi wa Mkwawa watakuwa na cheti chenye nembo ya University of Dar es Salaam, haina maana kwamba ni mwanafunzi wa Dar es Salaam.

“SUA hapo inaingia kwa sababu alikuwa kama kuku ameatamia vifaranga. Makonda ni mtoto wa kifaranga… hata sisi sasa hivi wanavyohakiki vyeti hapa, Cheti ni cha SUA, lakini mtu alisoma Moshi. Wakileta vyeti waajiri hapa, sisi hatuhakiki hapa, tunavipeleka Moshi,” amesema Prof. Mwamengele.

Amesema wanaokihusisha SUA labda wameangalia vyeti vyake wakaona vina nembo ya SUA wakadhani amesoma hapo, kumbe hajawahi kujiunga na SUA.

 

Makonda kwenye ‘Inspirational Speech’

 Katika kumbukumbu rasmi, Paul Makonda, akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, mwaka 2015 alizungumzia maisha yake kwa ufupi, huku akijinasibisha na Mungu, tangu kuzaliwa kwake miaka 35 iliyopita.

Makonda amesema, kwenye familia ya mzee Christian Makonda walizaliwa watoto wawili, yeye Paul, pamoja na dada yake, ambaye hata hivyo miaka miwili baadaye alifariki.

“Tulizaliwa wawili, mimi pamoja na mdogo wangu wa kike. Bahati mbaya mdogo wangu alipofikisha miaka miwili alifariki. Hata kuzaliwa kwangu kulikuwa kwa maagano na Mungu. Ndiyo maaa sitaacha kumtumikia Mungu,” amesema Makonda, katika mazungumzo yake na vijana.

Amesisitiza zaidi kwamba katika familia yake, Mama kwao ndiye amefanikiwa: “Amemaliza darasa la saba, baba hakuwahi hata kukanyaga darasa la kwanza. Mimi nimekuwa naishi kwa kusudi la Mungu, bila kujua kwamba ninaishi katika kusudi hilo.

“Hakuna kazi ya hovyo ambayo sijaifanya mimi, 2000/2001 Nimefanya kazi za hovyo kweli, 2000 nimekata mkaa na kubeba mchanga hapa Mbezi Louis, jijini Dar es Salaam.

“Mwaka 1999, mimi nimekuwa kondakta Mwanza. Ili uwe kondakta inabidi uhitimu kutoka kwenye utingo. Kazi yangu kama tingo ilikuwa ni kubeba magunia na mizigo, kwa hiyo kazi mimi nimeifanya.

“Shauku yangu ilikuwa ni kupata degree (shahada) moja tu. Nikawa natamani kuvunja laana kweli. Maana msomi nyumbani kwetu ni mama yangu tu, ambaye alihitimu darasa la saba.

“Mungu alikuwa mwaninifu, niliwatumia watu waliokaa pembeni yangu…the next people who are sitting with you is your capital of tomorrow (Mtu liyekaa jirani nawe ni mtaji wako wa kesho), don’t take things for granted (msichukulie kwamba haya mambo lazima yatokee tu), hao waliokaa pembeni yako ndio mtaji wako. Watu wanataka washikwe mkono, sikuwahi kushikwa mkono, isipokuwa kuwatumia watu walioko pembeni yangu.”

 

 Baraza la Mitihani lazungumza

JAMHURI limepata taarifa kuwa katika Baraza la Mitihani Tanzania, hakuna jina la Paul Makonda, bali kuna jina la Paul Christian. Kuhakikisha iwapo hilo ni kweli au la, JAMHURI limezungumza na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde kuhusu matokeo ya wawili hao, aliyesema:

“Matokeo ya mtihani ni mali ya Baraza la Mitihani Tanzania na mtahiniwa tu. Si mtu wa tatu…naomba tuishie hapo,” amesema Dk. Msonde. Hakutaka kuendelea na mazungumzo na akasisitiza hana cha kuzungumza zaidi.

 

Prof. Faustine Bee wa MoCU anena

 Akizungumza na JAMHURI, Makamu Mkuu wa Chuo Cha Ushirika Moshi, Prof Faustine Bee, amesema ni kweli kwamba Paul Makonda amesoma chuoni hapo na amehitimu masomo yake vizuri.

“Ninakumbuka kwamba aliwahi kuahirisha mwaka kutokana na tatizo la ada, hayo mengine nadhani nahitaji kupata file lake kwanza ili nijiridhishe,” amesema Prof Bee na kuomba apewe muda kupata taarifa za ziada ikiwa zinahitajika.

Hata hivyo, taarifa za ndani kutoka Chuo Kikuu cha Ushirika  zinasema Paul Makonda anayedaiwa kutumia vyeti visivyo vya kwake, alifuata taratibu zote za udahili zilizokuwa zimewekwa na Chuo kulingana na fani aliyosomea.

 Kuhusu uhalali wa vyeti vyake, chuo wanasema walijiridhisha na vyeti vyake na ndiyo maana aliruhusiwa kusoma.

Chuo pia wanakiri kwamba Makonda hakufaulu masomo yake kwa vipindi viwili tofauti na hata alipochukua CED mwenendo wake wa masomo darasani haukuwa wa kuridhisha kutokana na utoro wa mara kwa mara.

“Kama tunataka kujua sifa ambazo ziliwekwa na chuo sharti yaandikwe maswali yaelekezwe kwa Msajili ambaye anaweza kuyatolea ufafanuzi juu ya sifa zilizokuwa zimewekwa na Chuo kwa kila ngazi ya kozi na kama sifa hizo Makonda alikuwa nazo,” amesema mtoa habari wetu.

 Gwajima alikimbia JAMHURI

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa muda wa wiki tatu sasa amegoma kuzungumza na JAMHURI hasa baada ya gazeti hili kumwomba kuonana naye kupata uthibitisho wa uhalali wa vyeti alivyodai anavyo.

Kati ya maswali ambayo JAMHURI limewasilisha kwa Askofu Gwajima naye akaahidi kuyajibu au kuonana na mwandishi wa JAMHURI bila kutekeleza ahadi hii ni pamoja na alivipataje hivyo vyeti anvyodai anavyo? Ana uhakika gani iwapo vyeti hivyo si vya kughushi na kwa nini Paul Christian anasema hana dada anayeitwa Christina.

Badala yake, JAMHURI limemshuhudia mara kadhaa Askofu Gwajima akitamka na kurudia maelezo ambayo yamesambaa kwenye mitandao ya kijamii, huku akisisitiza kuwa Makonda hana vyeti na ndiyo maana analia akiombwa vyeti.

 

 ‘CV ya Makonda’ inayozunguka

 Katika mitandao ya kijamii kuna andiko linalozunguka likiwa limeandikwa: *CV YA PAUL MAKONDA*, linasomeka hivi:

 1. Alizaliwa tar.15/02/1981 katika Kijiji cha Koromije, Wilaya ya Misungwi, Mkoa wa Mwanza.

2. Majina yake halisi ni *Daudi Albert Bushite*

3. Alianza darasa la kwanza mwaka 1988  katika shule ya msingi Koromije akitumia majina ya *Daudi Albert Bushite*. Mwaka 1991 alifeli darasa la 4, akarudia.

4. Mwaka 1992 alifeli tena na hivyo akahamishiwa Mwanza mjini, ili aweze kusoma na kupata masomo ya jioni (tuition).

5. Mwaka 1996 alihitimu darasa la 7, lakini hakuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari katika shule ya serikali.

6. Mwaka 1997 akajiunga na kidato cha kwanza shule ya sekondari ya Pamba.

7. Mwaka 2000 akahitimu kidato cha 4 na kupata daraja sifuri (division zero).

8. Mwaka 2001 akatumia cheti cha Ndg. Paul Christian Muyenge (chenye div.3 ya points 25) kujiunga na Chuo cha Uvuvi Nyegezi (Nyegezi Fisheries Training Institute) kwa masomo ya Certificate akahitimu mwaka 2002.

9. Mwaka huohuo 2002 akitumia cheti cha *Ndg.Paul Christian Muyenge*, alijiunga na Chuo cha Uvuvi Mbegani Bagamoyo kwa masomo ya Diploma ya uvuvi (ORDINARY DIPLOMA IN MASTER FISHERMAN, NTA LEV.6), na kuhitimu mwaka 2005.

10. Mwaka 2003 alikutana na Ndg. Benjamin Sitta (mtoto wa Marehemu Samwel Sitta, ambaye ni Mayor Kinondoni kwa sasa). Wakawa marafiki.

11. Mwaka 2005 baada ya kuhitimu Stashahada yake ya uvuvi, aliomba admission Chuo cha Kilimo Sokoine kusoma shahada lakini akakosa nafasi.

12. Baada ya kukosa nafasi alienda kuishi nyumbani kwa Marehemu Sitta akiwa kama rafiki wa Ben (mtoto wa Sitta). Kwakuwa alitoka familia duni, Sitta aliahidi kumsomesha elimu ya juu.

13. Mwaka 2006, alipata udahili Chuo cha Ushirika na Biashara Moshi (wakati huo kikiwa Chuo Kikuu Kishiriki cha SUA), kwa kutumia vyeti vyake vya certificate (ya Nyegezi) na diploma (ya Mbegani).

14. Alidahiliwa kwa course ya BA in Cooperate Management &Accounting. Mwaka 2007 alimaliza first year lakini akashindwa kuendelea na 2nd year baada ya kupata Suplementary 6 kati ya Course 8 alizokua akisoma (akawa discontinued).

15. Mwaka huohuo 2007 akaomba Admission upya. Akamaliza first year akiwa na _carries 3_ ambazo alienda nazo 2nd year. Mwaka 2008 akiwa 2nd year akapata supplementary 4 kati ya course 8 alizokua akisoma. Akawa na mzigo wa _carry over_ na _supplementary_. Akaamua kuacha chuo.

16. Mwaka 2008 akaenda kujaribu kuomba udahili chuo kikuu SUA kwa mara nyingine lakini akakosa.

17. Mwaka 2009 akarudi tena MUCCoBS kwa udahili mpya. Akaachana na CMA akachagua Community &Economic Development (CED).

18. Mwaka 20012 akahitimu Shahada ya kwanza ya Community &Economic Development kwa jina la *_Paul C Makonda_* badala ya majina yake halisi ya *_Daudi A Bushite_*

19. Jina *_Makonda_* analitumia baada ya kula kiapo mahakamani kubadili jina. Cheti cha Form four kinasomeka *_Paul C Muyenge_* lakini vyeti vya elimu ya juu vinasomeka *_Paul C Makonda_* baada ya kuapa mahakamani.

20. Ndugu Daudi Albert Bushite ameoa (tangu mwaka 2009), lakini hajabahatika kupata mtoto. Na ndiye mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam kwa sasa.

 

Mwandani wa Makonda azungumza

Akizungumza na JAMHURI, mmoja wa watu wa karibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, amesema Makonda anaandamwa kutokana na uchapa kazi wake.

Amesema Makonda amekuwa anamtafsiri vizuri Rais Magufuli, hivyo amekuwa ‘anashughulikiwa’ na baadhi ya watu ambao wanaona anafifisha uhusiano wao na Rais.

“Unajua Makonda anachapa kazi kweli kweli, uchapakazi wake ndio sasa unasababisha aanze kuwindwa na hao wabaya wake… amekuwa anawakemea hadharani watumishi wazembe, jambo ambalo hata Rais Magufuli amekuwa anamuunga mkono,” kimesema chanzo chetu.

Chanzo hicho kilichoko karibu na Makonda, kimeliambia JAMHURI, Mkuu huyo wa Mkoa katika kipindi cha mwaka mmoja amehakikisha kwamba Jiji la Dar es Salaam linapata zaidi ya Sh bilioni 180 za maendeleo. Kati ya fedha hizo Sh bilioni 162, zimetoka kwa wadau wa maendeleo.

“Amesaidia kujenga vituo vya Polisi, wodi za wazazi… watangulizi wake hawakuyafanya haya. Sasa hapo unaweza kuelewa hata kwa nini hii vita ya Makonda inapiganwa na watu wawili tu.

“Unaweza kuona hata jambo la kituo cha matangazo cha Clouds, hata baadhi ya mawaziri wanaandika kwenye kurasa zao za ‘twitter’, lakini sijasikia hata Makonda akizungumza nao kuhusu tukio hilo wakati yeye ni Mkuu wa Mkoa, ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa,” kimesema chanzo chetu.

JAMHURI lilipomtafuta Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuzungumzia tuhuma ambazo zimekuwa zinamwandama kwenye mitandao ya kijamii, amesema hawezi kusema chochote.

“Ndugu yangu siwezi kusema chochote, wao acha waendelee kusema tu, ukifika wakati nitasema,” amesema Makonda.

Chanzo chetu kimesema, Makonda amekuwa Rais wa TAHLISO, Amegombea uwenyekiti wa UVCCM Taifa, akateuliwa kuwa katibu wa hamasa na chipukizi wa UVCCM, akamshughulikia Edward Lowassa, jinsi Lowassa alivyokuwa na mtandao jambo hilo kama ni kweli Makonda asingebaki salama.

Lakini pia Makonda akateuliwa kuwa miongoni mwa wabunge wa Bunge Maalum la Katiba, baadaye akawa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, tena baada ya kugusa dawa za kulevya ndio haya yote yanaibuka, tufikiri nje ya boksi.

Kuvamia Clouds

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Makonda anadaiwa kuvamia kituo cha matangazo cha redio na TV cha Clouds jijini Dar es Salaam, kwa nia ya kuchukua mkanda ambao haukutangazwa kwa wakati ukihusiana na kashfa ya Askofu Gwajima kuzaa na mwanamke na amatelekeza.

Akizungumza na JAMHURI, mwingine kati ya watu wa karibu wa Makonda, amesema kilichotokea katika kituo cha matangazo cha Clouds, ni jambo la kushangaza kutokana na ukweli kupindishwa kwa makusudi.

“Tulipita pale Clouds tukitokea kwenye ziara ya Mkuu wa Mkoa, tulikwenda kuangalia matatizo ya maji huko Tegeta na Bunju, kwenye ziara hatukuwa na mwakilishi wa kituo hicho, hivyo ikashauriwa tuwapitishie ‘footage’, baada ya hapo tukaondoka.

“Nashangaa maana Makonda alikuwa kwenye kituo hicho cha matangazo siku ya Jumanne, aliondoka pale usiku wa saa tisa, alikuwa hapo kusimamia utengenezwaji wa kipindi maalumu cha mwaka wake mmoja katika wadhifa wake, hilo halijasemwa…wanarusha hizo clip,” kimesema chanzo chetu.

By Jamhuri