Siku za karibuni kuanzia wakati ule wa Sensa ya Watu na Makazi, neno UDINI limekua na linasikika mara kwa mara. Katika baadhi ya magazeti kama JAMHURI, kuna mfululizo wa makala za udini, mathalani makala za Ndugu Angalieni Mpendu – FASIHI FASAHA.

Kumekuwa na mfululizo wa makala “Serikali isipuuze, udini upo, iudhibiti”. Zipo makala nyingine kwenye ukurasa wa JAMHURI YA WAUNGWANA – kichwa cha habari kinasema “Tuamke, tatizo la udini ni kubwa”. Kwenye gazeti la Mtanzania ndiko hasa kumetolewa ukurasa wa mbele kabisa – “UDINI WAMTISHA JK” (Mtanzania toleo 7209 la Alhamisi tarehe 24 Januari, 2013).

 

Aidha, nimewahi kutumiwa DVD kutoka kwa watu kadhaa nizione. Moja inasema, “Unafiki wa Sensa Tanzania”. Nyingine inasema, “Kongamano la Katiba na kadhia ya Muungano Zanzibar”, na ya mwisho niliyoletewa ina picha za masheikh -Sheikh Farid, Sheikh Hussein, Sheikh Issa Ponda na Mohamed. Kichwa cha DVD hii kinasema, “Majumuisho ya makongamano ya Waislamu dhidi ya Wakristo”.


Basi, nikawa hoi! Sasa ninajiuliza hili suala la “UDINI” nani wanalikuza hivi hata kuwa nongwa katika nchi yetu? Nani anayefaidika na huo mtafaruku kati ya Watanzania weusi, Wabantu wa makabila zaidi ya 120 ya hapa nchini kwa mtafaruku namna hiyo?

 

Siamini kama mwananchi mweusi kama mimi au Msukuma au Mgogo asilia wa Taifa hili, atafaidika na mvurugano huo. Kwanza, hii DVD ya majumuisho ya makongamano ya Waislamu, wasemaji wakuu ni wageni wenye asili ya mbari ya Kiarabu, mathalani Sheikh Farid si Mtanzania, ni wa kutoka Yemen au Oman inavyosemekana.

 

Je, atakuwa na uchungu akiona Wanyamwezi, Waha, Wagogo wale Tiputipu aliokuwa anawatwika mizigo ya pembe za ndovu, wanasambaratika baada ya nchi yao kuwa huru, huyu, ataona uchungu kweli?


Ukristo ni imani ya baadhi ya wakazi wa Jamhuri hii ya Tanzania. Uislamu ni imani ya baadhi ya wakazi wa Jamhuri hii ya Tanzania. Sasa tatizo liko wapi? Waislamu na Wakristo wanaoana, wanazaa watoto wa Tanzania. Je, hawa ndiyo tunataka tuwalee katika utamaduni wa kuchukiana?

 

Inaanzia wapi fikra namna hii? Mpaka leo sielewi nani atafaidika ikiwa Juma Njalamoto na Joseph Njalamoto wataanza kuchukiana ingawa ni watoto wa baba na mama yule yule! Chuki kati yao lazima itakolezwa na nguvu kutoka nje ya damu yao. Kweli wamezaliwa kwa baba na mama wale wale, leo Juma aseme wewe John kafiri! Haiyamkini. Lakini kinachotokea hivi sasa ni uchochezi kutoka mbari zisizokuwa za kibantu, hamlioni hilo?

 

Sasa haya ya Geita ndiyo mapya. Mtafaruku umetokea juu ya neno “Halali kuchinja”. Mbona Wasukuma wamekuwa wanachinja ng’ombe na kula nyama za ng’ombe kabla hata wageni Wazungu au Waarabu hawajafika kule Nyehunge Usukumani? Miaka yote hii hawakuwa wanachinja mbuzi au kondoo au ng’ombe wao kwa kitoweo hadi siku hiyo alipotembelea RC wa Mwanza, ndipo waone jambo hilo? Si kweli hata kidogo.

 

Jambo hili linamsumbua hata mkuu wa nchi. Anatuma Waziri kutoka Dar es Salaam kwenda Geita kwa ndege – tena kwa gharama ya fedha za walipa kodi wakristu na waislamu – eti kwenda kusuluhisha mtafaruku uliotokea juu ya neno “Uhalali wa kuchinja ng’ombe?”

 

Hapa mimi nimerudishwa nyuma mbali kifikra kwenye enzi za mzee AESOPO yule Myunani mwenye kibyongo, aliyetunga hadithi nyingi tulizokuwa tukisoma tukiwa shule za msingi. Moja ya hadithi zake na bado naikumbuka ni ile ya Kisa cha Mbwa Mwitu na Mwanakondoo. Labda nifikishe ujumbe ule kwa usahihi kwa wasomaji vijana.

 

Hadithi ile ilisema hivi; hapo kale mbwa mwitu na mwanakondoo walikutana kwenye kijito wote wakiwa na kiu ya maji. Mbwa mwitu alikuwa akinywa maji upande wa juu wa kijito yanakotoka maji, mwanakondoo akinywa maji upande wa chini wa kijito yanakotiririkia bondeni. Mbwa mwitu kule kumwona tu yule mwanakondoo tu, akawa na tamaa ya kupata mlo wa siku ile, akadhamiria amkamate amtafune. Akaanza vitimbwi ili mradi apate sababu za kumtafuna.

 

Mbwa mwitu kwa ukali akamwambia mwanakondoo, “Wee kwa nini unatibua maji wakati unaniona mimi huku nakunywa?” Mwanakondoo kwa woga na hofu akajibu, “Bwana mkubwa mbona maji yanatiririka toka huko juu unakokunywa wewe ndipo yanifikie mimi huku bondeni nitayatibuaje?” Mbwa mwitu akaona amerufai, hakuwa na sababu.

 

Kwa hasira sasa akasema, “Mbona unanijibu kifedhuli na jeuri hivyo? Wewe si ndiye yule aliyenitukana mwaka jana? Mwanakondoo sasa hofu ikawa kubwa, lakini akajikaza akajibu, “Bwana mkubwa mimi nisingeweza kukutukana, huo mwaka jana mbona nilikuwa sijazaliwa bado wakati huo? Mbwa mwitu kuona hakuwa na sababu za kumsakama mwanakondoo mdogo yule, lakini njaa na akisukumwa na silika yake ya mabavu, akasema, “Potelea mbali kama ulikuwa hujazaliwa labda alikuwa mzazi wako ndiye aliyenitukana, wewe nitakuadhibu tu badala ya mzazi wako”. Akamrukia akamkamata akamla.

 

AESOPO anasema “waovu daima watatafuta sababu ya kuhalalisha huo uovu wao” (the wicked will always find an excuse for their wickedness). Hivyo basi, huu udini katika nchi yetu hautokani na imani zetu kwa Mungu aliyetuumba. Mimi naona hapa nchini udini unakuzwa kutokana na tamaduni za kigeni tu zenye asili ya ugomvi na chuki baina yao. Zile chuki za Waarabu (Waislamu) kwa Wazungu (Wakristo) za tangu zamani, ndizo bado zinaonekana kujitokeza hapa kwa visingizo na vitimbwi kadha wa kadha.

 

Nchi yetu Tanzania tangu enzi za ukoloni imekuwa inawalea raia zake kindugu, ndiyo maana amani imeendelea hadi leo hii. Wilaya kama Tunduru, Kondoa-Irangi, Kigoma-Ujiji, Tanga, Mikindani, Kilwa hata Tabora wakazi wengi wana imani ya Kiislamu. Wapo Wakristu wachache, lakini hakujasikika msuguano wa kuchinja wanyama kwa kitoweo kwa miaka nenda miaka rudi. Sasa mwaka huu wa 2013 kunasikika matukio ya ajabu kabisa kama haya ya kuhalalisha kuchinja. Ni kweli Waislamu wamegutuka mwaka huu? Vitimbwi na madai mengi sasa yanaibuka kwa kisingizio hiki au kile ilimradi amani itoweke.

 

Labda nitoe hadithi yangu binafsi. Mimi nina binamu Waislamu. Mjomba wangu alikuwa Mwislamu na wala sijafarakana na binamu zangu. Kule Tunduru ninakoishi asilimia 98 ya wakazi ni Waislamu. Mheshimiwa hayati Juma Akukweti, mwanafunzi wa Songea Boys nilikofundisha mimi ameoa msichana kutoka kijijini kwangu Nakayaya, pale kwa Mzee Mfaume Pelekamoyo, ambaye ni baba yangu mdogo, lakini sikuwahi kuona tofauti ya kimaisha na hao Waislamu.

 

Nikiwa Tabora St. Mary’s nilikuwa na rafiki yangu Mhehe mmoja pale Tabora School. Tumekuwa marafiki tangu mwaka 1950 hadi leo hii anaishi Mtaa wa Ruvuma, Temeke. Huyu alifaulu vizuri mtihani wa Cambridge mwaka 1951 na akaenda Makerere, mimi sikwenda Makerere maana sikupata “credit” katika Kiingereza kama yeye.

 

Hatimaye sote tumekuja fundisha Songea Boys na mpaka leo tungali marafiki na tumeelewana. Sijamsikia huyu Alhaj akinilaumu kuwa wewe Mkristo mnatukandamiza sana sisi Waislamu kwa kitu siku hizi kiitwacho “MFUMO KRISTU”. Kila tukikutana huwa “namjoki” kwa utani wazo la kukandamizwa nyinyi Waislamu linazuka kwa msingi upi? Mbona wewe ulinipita na ukaenda Makerere?

 

Lakini nilichogundua ni kuwa Waislamu wasomi hawana upuuzi wa kunung’unika wala kulaumu Ukristo. Bali, wana kitu au tabia inayojulikana kama INFERIORITY COMPLEX. Ni hali ya kujifikiria daima wanaonewa! Ugonjwa namna hii daima unasikika kati ya Waislamu, lakini sijaona sababu au kisa cha wao kuegemeza dhana yao potofu hii. Siyo kweli kwamba Waislamu hamkusoma. Mbona wapo madaktari chungu mzima – walipataje huo udaktari au uprofesa?

 

Basi, kwanza wajitambue wao ni Watanzania wazalendo. Dini ya Uislamu haiwafanyi kuwa chini ya Watanzania Wakristo. Kuna masheikh waliosomea dini kule Cairo, Alexandria, Islamabad, Tripoli, Riadh, Teheran, Baghdad na kadhalika. Misikitini wanahubiri dini kwa ufasaha kweli. Huwa naangalia kipindi cha dini ya Kiislamu Ijumaa. Basi, Januari 18, 2013 nilimwona sheikh kijana kabisa akihubiri kwa ufasaha msikitini. Moja ya maswali yake, alisema namnukuu; “Leo mwezi 18 Januari yupo Mwislamu humu ndani aliyetenda tendo jema la ukarimu walau akampa maji mhitaji nyumbani kwake?”

 

Hakuna aliyejitokeza kusema mimi hapa! Akasema mnaona ndugu zangu Waislamu? Mtume alikuwa anatenda mema kwa wahitaji. Sheikh yule alisema hapa leo hakuna hata mmoja wetu aliyeiga matendo mema ya Mtume! Hakugusia Ukristo wala ukafiri wala kumchamba Nabii Issa katika mahubiri yake yote kipindi kile.

 

Kwa watu namna hiyo kweli watakuwa na nafasi ya kuongelea uhalali wa kuchinja nyama kweli? Au kuwasema Wakristo? Hawa wasomi wanaongelea mambo ya imani ya dini (issues), kamwe hawaongei eti yule kavaa shati lenye msalaba au huyu kakatazwa kuvaa hijabu au huyu hastahili kuchinja kuku kwa kitoweo. Hivi ni vitu vya kitamaduni si vya IMANI YA KIDINI.


Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


 

1231 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!